Saturday 11 July 2020

Waziri Mhagama Azindua Mpango Wa Uendelezaji Wa Viwanda Vidogo Na Vya Kati Jijini Dodoma.

...

NA. MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amezindua Mpango wa Uendelezaji wa Viwanda Vidogo na vya Kati wenye lengo la kutatua changamoto ya upatikanaji wa ujuzi, masoko na mitaji katika miradi midogo na vya kati (SMEs) nchini.

Uzinduzi huo ulifanyika mapema Julai 10, 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage Hazina Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe.

Pia ulihudhuriwa na baadhi ya Wakuu wa Taasisi za SIDO, VETA, NEEC, NSSF na Banki ya AZANIA pamoja na Viongozi na Wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za Sekta binafsi, Wajasiriamali na Wanafunzi kutoka Vyuo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mhagama amesema uwepo wa mpango huo utasaidia kuongeza kasi ya ujenzi na ukuaji wa uchumi kwa kutengeneza mazingira wezeshi na kuandaa mazingira yenye mfumo wa kibiashara yatakayorahisisha kutengeneza uzalishaji wenye tija na kuunda soko la bidhaa utakaoboresha na kuinua maisha ya Watanzania.

“Serikali imetengeneza fursa za kuwezesha wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kujipatia kipato na kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali zinazokabili nguvu kazi ya taifa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa elimu na ujuzi wa kutosha pamoja na ukosefu wa mitaji na masoko ya uhakika wa bidhaa zinazozalishwa”,alisema Waziri Mhagama.

Waziri alifafanua kuwa mpango umejikita katika kuhakikisha kuwa wajasiriamali wanasaidiwa kuongeza ujuzi, kupata uzoefu na kuwawezesha kuhimili ushindani katika masoko ya ndani na nje. Aidha, Mpango huu pia unalenga kuwezesha viwanda kupata vifaa vya kisasa  kama mitambo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji ili uwe na tija, kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kupanua shughuli za uzalishaji pamoja na kuongeza kinga za  hifadhi za jamii kwa wajasiriamali.

“Kupitia mpango huu wenye viwanda na wajasiriamali wamepanuliwa fursa ya kupata mitaji hivyo kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wengi wanaohitimu vyuo katika ngazi mbalimbali,”Alisistiza Waziri

Aliongezea kuwa, Mfumo unajikita kuwafika wananchi wote bila ubaguzi na matabaka ya aina yoyote kwa kuzingatia vigezo na masharti nafuu yaliyopo katika mfumo huu.

“Programu hii inavunja matabaka baina ya makundi mbalimbali katika jamii na kutoa fursa sawa kuanzia mtu binafsi hadi vikundi katika kuwapatia mitaji na ujuzi sawa hivyo tuiunge mkono kwani inawalenga Watanzania wote,” alisema

Aidha alibainisha sekta ya viwanda imeendelea kuwa na tija katika kuchangia ongezeko la Pato la Taifa kwa kuongezeka kwa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ambapo Sekta ya Viwanda katika Pato la Taifa kwa mwaka 2019 ilikuwa asilimia 8.5 ikilinganishwa na asilimia 8.05 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 0.45 na hii ni matokeo ya kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji viwandani katika kipindi hicho pamoja na kasi ya ukuaji wa thamani ya Uzalishaji Bidhaa Viwandani kwa mwaka 2019 ambayo ilikuwa ni Shilingi Trilioni 10.2 ikilinganishwa na Shilingi Trilioni 9.6 mwaka 2018, sawa na kasi ya ukuaji wa asilimia 5.8

Waziri aliendelea kutoa wito kwa taasisi husika kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu fursa zilizopatikana katika program na kuvitumia vyombo vya habari katika kueleimisha umma kwa malengo ya kuwafikiwa wengi pamoja na kuzitaka taasisi za kibenki kutoa mikopo kwa wajasiriamali kwa mifumo rafiki na inayofikika pamoja na kuutaka uongozo wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuwa na program za tathimin utekelezaji wa mpango kwa vipindi mbalimbali.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa alieleza furaha yake ya uwepo wa mpango huo kwani umesadifu mikakakti ya nchi katika uendelezaji viwanda na kusema imekuja wakati mwafaka kwa kuzingatia imelenga sekta zenye tija katika kutoa ajira kwa watanzania wengi kwani imefungamanisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwa ndizo zenye mchango mkubwa katika ajira.

“Ni hakika kuwa, kupitia Mpango huu wa uendelezaji wa viwanda, ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika  mnyororo mzima wa thamani wa sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji zitaongezeka na kupunguza changamoto mbalimbali zinazokabili jamii kutokana na ongezeko la wasio na ajira nchini,”Alisema waziri Bashungwa.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’I Issa alisema, mpango umeainisha namna bora ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwemo la kukuza mitaji na kuimarisha vyanzo vyao vya mapato na kukuza akiba na mikopo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger