Friday 3 July 2020

Breaking : MATATANI KWA KUNASWA NA DOTI 600 ZA VITENGE VYENYE NEMBO YA CCM...TAKUKURU SHINYANGA YATOA ONYO KALI

...
NB- Picha haihusiani na habari hapa chini

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga inamshikilia Joseph Jonas Tasia mkazi wa Mwasele Mjini Shinyanga kwa kukutwa na doti 600 za vitenge vyenye namba ya Chama Cha Mapinduzi vinavyodaiwa kuwa vilikuwa vinaandaliwa kutumika katika kufanya ushawishi kwa wapiga kura. 

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Julai 3,2020 na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa,mtuhumiwa alikamatwa na vitenge hivyo nyumbani kwake Juni 29,2020 majira ya saa tatu usiku katika mtaa wa Mwasele B. 

“Tukiwa tunaendelea na ufuatiliaji wa vitendo vya Rushwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa viongozi, Juni 29,2020 majira ya saa tatu usiku nyumbani kwa Joseph Jonas Tasia tulikamata doti 600 za vitenge vyenye nembo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vya kawaida vikiwa vimehifadhiwa nyumbani kwake jambo ambalo linaashiria kuwa vilikuwa vinaandaliwa kutumika katika kufanya ushawishi kwa wapiga kura”,amesema Mkuu huyo wa TAKUKURU. 

Amesema uchunguzi wa TAKUKURU umebaini kuwa Joseph Jonas Tasia ambaye ni mfanyabiashara wa usafiri wa magari madogo TAXI hana duka na wala hafanyi biashara ya kuuza vitenge. 

“Katika mahojiano na maafisa wa TAKUKURU baada ya mtuhumiwa kukamatwa na mzigo huo ameshindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza kuhusiana na vitenge hivyo na hata nyaraka za manunuzi ya mzigo huo alizowasilisha hazijitoshelezi na hivyo kuongeza mashaka juu ya uhalali wa vitenge hivyo”,ameongeza Mussa. 

Amesema uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini iwapo vitenge hivyo vilikuwa ni kwa ajili ya kuhusika na vitendo vya Rushwa katika uchaguzi ujao au ni kwa ajili ya kufanya biashara katika msimu huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa viongozi 2020. 

“TAKUKURU mkoa wa Shinyanga inawaonya watu wote wenye nia ya kutaka kutumia taarifa zozote za uchunguzi zinazofanyiwa kazi na ofisi ya TAKUKURU kwa nia ya kujinufaisha kisiasa na kwamba kitendo hicho ni kuingilia uchunguzi unaoendelea na ni kosa la jinai. Hivyo atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria”,amesema Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger