Monday, 24 February 2020

Vifo Vya Wajawazito Kipindi Cha Kujifungua Vyapungua Hospitali Ya Rufaa Ya Mkoa Temeke

...
Na. Catherine Sungura - Dar es Salaam
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa temeke imejipanga kuokoa maisha ya wakina mama, wajawazito hususan katika kipindi cha kujifungua, kutimiza lengo hilo imeboresha miundombinu yake, vifaa tiba pamoja na kuimarisha huduma za afya kwenye ngazi za msingi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati wa ziara yake ya kikazi hospitalini hapo, ambako alikwenda kwa lengo la kusikiliza maoni na changamoto kutoka kwa wananchi na watumishi wa hospitali hiyo.

“Mwaka 2018 walikuwa na vifo 19 vya wajawazito na 2019 walikuwa na vifo 8 tu, lakini kwa takwimu za kuanzia Novemba 2019 hadi leo hakuna mwanamke mjamzito aliyekuja hospitalini hapa na kupoteza maisha, niwapongeze madaktari, wauguzi na watoa huduma wote wa hapa kwa hatua hii," amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa jitihada za makusudi, kuwekeza kwenye huduma za afya nchini sambamba na ujenzi wa vituo vya afya na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.

“Sasa hivi hapa temeke kuna huduma za kibingwa za meno ambapo zamani haikuwepo," amesema.

Waziri Ummy amesisitiza Wizara ina mpango pia wa kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinazohitajika zinakuwepo kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa.

Hata hivyo amesema kuwa wanawake 15 kati ya wanawake 100 ndio ambao huhitaji kupelekwa kujifungulia kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa hususan wale wenye changamoto za ujauzito, kwa mfano mtoto amekaa vibaya au viashiria vya uzazi pingamizi.

Kwa upande  wa vipimo waziri huyo amesema kuwa Wizara yake imeongeza vipimo vya utra sound hivi sasa serikali imeboresha vituo vya afya na kwamba vipimo hivyo vinaanza kutolewa kuanzia ngazi za vituo vya afya vya umma na hospitali za wilaya nchini.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma kuanzia ngazi ya msingi na hospitali za rufaa za mikoa ni kwa wagonjwa watakaopata rufaa.

“Kwa yeyeote atakayefanya makusudi kukorofisha vipimo ili watu waende kupima kwenye vutuo binafsi tutawachukulia hatua kwani ni wahujumu uchumi, tunataka vipimo vyote vifanyike ndani ya hospitali ila pale mashine haipo tutaruhusu, lengo letu ni kujitosheleza kwa vipimo vyote kwenye vituo vya afya vya umma," amesisitiza Waziri Ummy.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Yudas Ndungile amesema kuwa kutokana na maboresho ya miundombinu, wataalam na vifaa tiba kwa mkoa huu wameweza kupunguza vifo vipatavyo arobaini kwa mwaka ukilinganisha na vifo186 mwaka 2018 hadi vifo 140 mwaka 2019 na matarajio yao ni kupunguza zaidi.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke Dkt. Meshack Shimwela amesema kuwa  hospitali hiyo imeondoa msongamano wa wajawazito kwa kuwa hivi sasa wananchi wengi wanafuata mfumo wa rufaa.

"Hivyo wakina mama wajawazito wanaofika kwenye hospitali hii ni wale wenye changamoto ya uzazi kwa maana hiyo wengi wanajifungulia kwenye ngazi za chini ambapo huduma za afya nazo zimeboreshwa," amesema.

MWISHO


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger