Friday 25 March 2016

Marekani, Ulaya Wasusia Kuapishwa Dk. Shein

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Mabalozi kutoka Marekani na Nchi za Umoja wa Ulaya, wameendelea kuonyesha msimamo wao wa kutoridhishwa na uchaguzi wa marudio Zanzibar baada ya jana kususia mwaliko wa kushiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
 
Wanadiplomaasia hao walipewa mwaliko rasmi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), lakini waliiambia kuwa hawatashiriki sherehe hizo.
 
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Zanzibar, Silima Kombo Haji, aliliambia Nipashe kuwa serikali ilitoa mwaliko rasmi kwa Mabalozi wote wa nchi za Afrika na Ulaya kuhudhuria sherehe hizo, lakini Mabalozi wa Umoja wa Ulaya na Marekani walijibu kuwa hawatahudhuria bila kutoa sababu zozote.
 
“Tumewaalika na mialiko imewafikia na kutujibu kuwa hawatahudhuria. Hatukuwa na sababu ya kuwang’ang’ania," alisema Haji.
 
Hata hivyo, alisema licha ya Mabalozi wa Marekani na Umoja wa Ulaya kutohudhuria sherehe hizo, Mabalozi wa nchi nyingine walioalikwa walihudhuria sherehe hizo na wengine kutuma wawakilishi wao.
 
Aliwataja Mabalozi wa nchi waliohudhuria sherehe hizo ambao wengi ni kutoka nchi za Afrika kuwa ni Balozi wa Cuba, Zimbabwe, DRC, Indonesia, Iran, Kenya, Kuwait, Malawi, Msumbiji na Oman.
 
Wengine ni Palestina, Ruwanda, Algeria, Angola, Burundi, China, Japan, Libia, Pakistan, Umoja wa Nchi za Kiarabu, India, Uganda, Uturuki, Urusi na Mratibu Mkaazi wa UN.
 
Nipashe lilipomuuliza Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Roeland van de Geer, endapo walipata mwaliko huo na sababu za kutohudhuria sherehe hizo, alisema ushirika wao usingeakisi dhamira ya tamko lililotolewa na Balozi mbalimbali nchini  Machi 21, mwaka huu.
 
Tamko hilo lilitolewa na Mabalozi na Wawakilishi wa nchi za Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Switzerland,  Uingereza na Marekani.
 
“Tumesikitishwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) wa kuendesha marudio ya uchaguzi uliofanyika 25 Oktoba 2015, bila kuwapo makubaliano ya pamoja baina ya pande kinzani na ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa visiwani humo uliotokana na majadilino baina ya pande husika. 
 
“Ili uwe wa kuaminika na kukubalika ni lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu,” lilisema tamko lao la awali na kuongeza:
 
“Tunarejea wito wetu kwa Serikali ya Tanzania kuonyesha na kuchukua uongozi katika suala la Zanzibar na kujielekeza katika kupatikana kwa ufumbuzi wa mgogoro huu kwa kupitia mazungumzo baina ya pande husika kwa lengo la kudumisha amani na umoja."
 
Mabalozi wamekuwa na msuguano na Serikali ya Zanzibar kwa kupinga kitendo cha Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kufuta uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kwa kile wanachodai kuwa haukuwa na kasoro yoyote na kwamba ulikuwa huru na haki.
 
Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, Oktoba 28, mwaka jana, alifuta uchaguzi mkuu kwa madai kuwa haukuwa huru na haki, lakini waangalizi wa kimataifa wakisema kuwa ulikuwa huru na haki.
 
Wanadiplomasia hao hawakufurahishwa na kitendo cha Mwenyekiti huyo wa Zec kufuta uchaguzi, hivyo kutounga mkono uamuzi wa Zec kurudia uchaguzi ambao ulifanyika Machi 20, mwaka huu na Dk. Shein kushinda kwa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger