Tuesday, 16 September 2025
UTEKELEZAJI MRADI WA HEET WAFIKIA ASILIMIA 74.3, SERIKALI YAPONGEZWA

Mratibu wa Mradi, kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Kenneth Hosea, akizungumza wakati wa kumkaribisha Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa kikao cha Mradi wa HEET
.....
UTEKELEZAJI wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) umefikia asilimia 74.3 tangu uanze kutekelezwa mwaka 2022, hatua iliyotajwa kuwa mafanikio makubwa.
Hayo yameelezwa leo Septemba 15,2025 , katika ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mratibu wa Mradi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Kenneth Hosea, wakati akimkaribisha Mgeni rasmi kufungua kikao cha siku tano cha tathmini ya Mradi, kikihusisha wadau wote muhimu wanaotekeleza Mradi huo.
Dkt. Hosea amesema, juhudi hizi kubwa ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba Wizara inaendelea kutoa hamasa kwa Taasisi za Elimu ambazo zinatekeleza mradi huu kuendelea kuongeza kasi ili kuhakikisha malengo yanafikiwa katika kipindi kilichopangwa.
Akifungua kikao kazi hicho, mgeni rasmi, Prof. Nelson Boniface, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo amesema inatia moyo kuona mafanikio makubwa ya Mradi kitaifa na kuwataka washiriki katika kupokea mawasilisho kuwa makini kujifunza na kutumia fursa hiyo kujifunza kutoka kwa wale waliofanikiwa ili kwa pamoja kufikia malengo makubwa kama Taifa.
“Hii ni fursa kwa Taasisi ambazo bado ziko nyuma kwenye utekelezaji, tuitumie kwa kujifunza wenzetu walikopita wakafanikiwa ili tuongeze juhudi za tufikia malengo yaliyokusudiwa” Alisisitiza.
Katika Mkutano huo, Mratibu msaidizi wa Mradi Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Happiness Nnko, amewasilisha taarifa ya maendeleo ya Mradi kwa kueleza baadhi ya Miradi imekamilika kwa asiliamia 100, wakati miradi ya ujenzi ikiendelea kutekelezwa ukiwemo ujenzi wa Maabara ya Sayansi katika Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati, ambapo ujenzi wake umefika asiliamia 55.3, Ujenzi wa vyumba vya Madarasa Ndaki ya Sayansi za Ardhi ya Uhandisi umefikia asilimia 61, wakati ujenzi wa Kampasi Mpya, Njombe ulioanza mwezi Juni 2025, umefikia asilimia 10.3.
Amesema,kuwa Menejimenti ya Chuo inaendelea kufuatilia kwa karibu ujenzi unaoendelea ikiwemo vikao vya mara kwa mara na wakandarasi, ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kabla Mradi kwisha, Juni 2026. Kwa upande wa mitaala mipya ya elimu, Dkt. Nnko amesema Chuo kimefanikiwa kubuni na kufanya mapitio ya programu 39, na mchakato wa kuzianzisha uko kwenye hatua mbalimbali za mapitio na kupata ithibati.
“Mbali na mapitio ya programu, pia Chuo kimepeleka Wakufunzi 18 masomoni kwa ngazi mbalimbali za elimu (Masters na PhD), kati yao wanaume wakiwa 13 na wanawake watano(5). Baadhi wanasoma hapa Tanzania na wengine wako nje ya nchi, Ghana, Uganda, Africa Kusini, Uingereza, Japan na Zambia.
Aidha, Chuo kinaendelea na ununuzi wa vifaa na samani vya majengo, ambapo hadi kufika Septemba 15, 2025 tayari manunuzi 23 yameanzishwa, kati ya hayo 11 wazabuni wameshapatikana, huku taratibu za manununi kwa maeneo mengine zikiendelea.
Mkutano huu umekutanisha Waratibu wa Mradi kutoka kwenye Taasisi zote za Elimu ya Juu nchini zinazotekeleza Mradi wa HEET, waratibu Wasaidizi, Wataalamu wa Maeneo mbalimbali ya Mradi ikiwemo Ufuatiliaji na Udhibiti, Mazingira, Tehama, Mahusiano na Viwanda na Mawasiliano.

,Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Nelson Boniface,akifungua Kikao Kazi cha Waratibu na Wasimamizi wa Mradi wa HEET kilichoanza leo Dar es Salaam.

Mratibu wa Mradi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Kenneth Hosea, akizungumza wakati wa kumkaribisha Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa kikao cha Mradi wa HEET

Mratibu Msadizi wa Mradi wa HEET toka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Happiness Nnko, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Mradi kwa UDOM wakati wa Kikao cha Wadau.

Mratibu wa Mradi wa HEET toka Chuo Kikuu cha Dodoma akisikiliza kwa makini wasilisho wakati wa kikao cha wadau kinachoendekea katika ukumbi wa Maktaba, UDSM
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi wakifuatilia kwa makini kikao kuhusu maendeleo ya Mradi wa HEETMonday, 15 September 2025
TBA KUANZA OPARESHENI YA KUWATOA WADAIWA SUGU OKTOBA MOSI
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umetangaza kuanza oparesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba za Serikali kuanzia Oktoba 1, mwaka huu endapo watashindwa kulipa kodi zao za pango hadi Septemba 30.
Wito huo umetolewa leo Septemba 10, 2025 Jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua hiyo.
Arch. Daud Kandoro amesema wadaiwa wote wanapaswa kulipa kodi zao kulingana na mikataba yao kabla ya mwisho wa mwezi huu ili kuepuka kuondolewa kwa nguvu na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Hakutakuwa na muda wa ziada wa kulipa madeni. Wapangaji wote wanapaswa kulipa ndani ya muda uliopangwa,” amesema.
Aidha, amefafanua kuwa TBA ina utaratibu wa kisheria wa kuwapangisha watumishi wa umma na watu binafsi wenye sifa, na sasa inawataka wapangaji wasio na sifa kuzikabidhi nyumba hizo na kulipa malimbikizo ya kodi.
Amesema miongoni mwa wasiokuwa na sifa ni pamoja na watumishi waliopangiwa nyumba kisha kuhamia vituo vingine nje ya mkoa husika, waliostaafu kwa mujibu wa sheria, waliokufa na wale walioondoka kwenye utumishi wa umma.
Arch. Daud Kondoro ameongeza kuwa oparesheni hiyo itafanyika nchi nzima na hakuna atakayeachwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Miliki TBA, Said Mndeme, amesema taasisi hiyo inadai zaidi ya shilingi bilioni 4 kutoka kwa wapangaji ambao hawajalipa kodi ndani ya kipindi cha miezi mitatu na kuendelea.
MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA YASHIRIKI MAONESHO YA BIASHARA MBEYA, YAWASHAURI WANANCHI KUTUMIA DAWA KWA SAHIHI
Meneja wa TMDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Anitha Mshighati
akitoa maelezo kwa mkuu wa mkoa wa mbeya Beno Malisa alipotembelea Katika banda lao lililopo Katika maonyesho ya biashara Ya kimataifa ya kanda ya nyanda za juu kusini
Na Woinde Shizza ,Mbeya
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imeshiriki maonesho ya pili ya biashara ya kimataifa yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ikitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanatumia dawa za binadamu na mifugo zilizosajiliwa na zilizo salama.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa TMDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Anitha Mshighati alisema kuwa lengo la ushiriki wao ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhakikisha watumia sawa kwa usahihi ilikuondokana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa pamoja na kuhakikisha wananunua dawa katika maeneo rasmi.
“Tumeona ni nafasi nzuri ya kutoa elimu kwa wakazi wa Mbeya na wageni wanaoshiriki maonesho haya kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba tunasisitiza wananchi kununua dawa katika maduka ya dawa yaliyoidhinishwa na kuacha kutumia dawa kiholela bila ushauri wa kitaalamu,” alisema.
Maonesho hayo yamekusanya wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi, yakilenga kukuza biashara na uwekezaji katika Mkoa wa Mbeya na ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
TMDA imesisitiza itaendelea kushirikiana na wananchi, wafanyabiashara na wadau wa afya ili kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinavyotumika nchini ni salama, bora na fanisi.
CCM YAZINDUA KAMPENI KATIKA JIMBO LA KAHAMA MJINI, WAGOMBEA WASISITIZA SIASA SAFI NA MAENDELEO

Na Neema Nkumbi, Kahama
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ushetu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Cherehani, amemnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, kwa wananchi wa jimbo hilo.
Cherehani amemnadi Ngayiwa katika uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika Jumapili Septemba 14,2025 eneo la Phantom, Kata ya Nyasubi, Manispaa ya Kahama.
Tukio hilo la kumnadi Ngayiwa limepewa baraka na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, ambaye amempa ridhaa Cherehani kufanya utambulisho huo na kumnadi kwa kuwa yeye ni mbunge mwenyeji wa wilaya hiyo katika nafasi ya ubunge.
Akizungumza mbele ya wananchi waliojitokeza kwa wingi, Cherehani amewasihi wakazi wa Kahama kumpa kura Ngayiwa katika uchaguzi mkuu ujao huku akisisitiza kuwa Ngayiwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kuwasemea wananchi bungeni na kushughulikia changamoto za msingi ikiwemo maji, ujenzi wa miundombinu, na huduma za kijamii.
“Mahitaji ya wana Kahama ninayafahamu, na naamini Ngayiwa ataweza kuyasimamia vizuri bungeni ili maendeleo yaende kwa kasi hivyo mchagueni Ngayiwa,” amesema Cherehani.
Kwa upande wake, Ngayiwa amenadi ilani ya Chama Cha Mapinduzi huku akiwaomba wananchi kumchagua Rais samia madiwani na yeye pia ili kuleta maendeleo zaidi kwa wananchi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amewataka wananchi kuhakikisha wanawachagua wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge hadi Udiwani, ili kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo.


























