Sunday, 14 September 2025
JAMBO GROUP YAIMARISHA SOKA LA KANDA YA ZIWA! SASA MDHAMINI MKUU PAMBA JIJI FC
Viongozi wa Jambo Group na viiongozi wa Pamba Jiji FC katika picha ya pamoja.
Pamba jiji FC wakitembelea kiwanda cha Jambo Food product.
Na Eunice Kanumba-Shinyanga
Kampuni ya Jambo Group ya mjini Shinyanga sasa ni mdhamini mkuu wa timu ya Pamba FC ya jijini Mwanza katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza rasmi Septemba 16, 2025. Makubaliano ya udhamini huo yamesainiwa leo katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Kata ya Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza hayo leo Septemba 13 ,kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jambo Group, Meneja wa Jambo Media na msimamizi wa chapa, Nickson George, alisema hatua hiyo siyo tu udhamini, bali ni ushirikiano wa kibiashara na kijamii utakaosaidia kukuza chapa za pande zote mbili kupitia michezo.
“Leo ni historia ya azimio la pamoja kati ya taasisi yetu na uongozi wa Pamba FC. Mkataba huu una lengo kuu la kukuza chapa zote mbili, hususan bidhaa za Jambo Group,” alisema George.
Viongozi wa Jambo Group na Pamba jiji Fc wakisaini mkataba wa ushirikiano wa chapa za pande mbili.Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Pamba FC, Peter Lehlet, alisema udhamini huo ni mwanzo wa ukurasa mpya wa mafanikio kwa klabu hiyo. Alifafanua kuwa Pamba na Jambo Group walishirikiana awali, wakasitisha kwa muda, lakini sasa wamerejea tena kuendeleza gurudumu la michezo.

Naye Mwenyekiti wa Pamba FC, Bikhu Cotecha, aliishukuru Jambo Group kupitia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salum Khamis, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, kwa mchango wao kuhakikisha klabu hiyo inaendelea kushiriki Ligi Kuu. Alisisitiza kuwa historia ya ushirikiano kati ya Pamba na Jambo Group ni ya muda mrefu na yenye matunda.
Kwa upande wa wachezaji, Nahodha wa timu hiyo, James Mwashinga, aliahidi kupambana na kufanya vizuri katika msimu huu ili kuipa heshima chapa ya Jambo Group na mashabiki wa Pamba FC.
Pamba FC inatarajiwa kushuka dimbani Septemba 18, 2025 dhidi ya Namungo FC katika Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi, ikiwa ni mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.
Kampuni ya Jambo Group imekuwa mdau mkubwa wa soka nchini kwa nyakati tofauti, ikiwahi kudhamini timu mbalimbali za ukanda wa ziwa, ikiwemo Stand United ya Shinyanga.

Wachezaji na viongozi wa pamba fc wakitembelea kiwanda cha Jambo Food product.
Saturday, 13 September 2025
VISION VIKOBA WAADHIMISHA MIAKA 10 YA MAFANIKIO
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KIKUNDI cha Vision Vikoba ambacho ni kikundi mama cha vikundi 13) kimeadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ambapo mshikamano na mshikamanifu wa kijamii umetajwa kuwa siri ya mafanikio yaliyowezesha kuendelea kwao hadi leo.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho hayo jijini Dar es Salaam, Mwanzilishi wa Vision Vikoba, Bi. Sharifa Mohamed, alisema walipoanza walikuwa na ndoto ya kuunda eneo la mshikamano na kusaidiana, lakini sasa ndoto hiyo imezaa matunda makubwa.
“Kikundi chetu mama kilikuwa kama mbegu, na vikundi 13 vilivyochipuka leo hii ni kama miti yenye matunda mema. Hii ndiyo maana ya mshikamano na mshikamanifu wa kijamii,” alisema.
Kwa mujibu wake, kikundi kina jumla ya wanachama 314, ambapo asilimia 80 ni wanawake na asilimia 20 ni wanaume, huku dira ikiwa ni kukua zaidi na kugeuka kuwa vyama vya ushirika, taasisi za kifedha na hata kushiriki katika miradi ya kijamii.
Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji kwa wajasiriamali wadogo, akisema vikoba vimekuwa darasa la kujitegemea kiuchumi na kusaidia familia nyingi.
Akihutubia katika maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Warda Abdallah, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika ofisi za wakuu wa wilaya ili kuchangamkia mikopo nafuu ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali.
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa wananchi ili kuwawezesha kujikomboa kutoka katika umaskini.
“Mkiwa mnajuana kitabia ni rahisi kuepusha migogoro. Changamkieni fursa hizi ili muondokane na umaskini,” alisema Bi. Warda.
Mwenyekiti wa Smart Vikoba Endelevu, Bi. Dainess Kalinga, amesema kupitia vikoba ameweza kununua ardhi, pikipiki na kuendesha biashara zake huku akisisitiza upendo na heshima kama nguzo ya kikundi.
Mdau kutoka Bakhresa Food Products, Bi. Rehema Salim, amesisitiza nidhamu ya fedha na mshikamano kama silaha ya vikoba endelevu.
Kwa upande wake, mwanachama Shedrack Sheria alitoa rai kwa umma kuachana na dhana kwamba vikoba ni kwa ajili ya wanawake pekee, akisema ni kwa watu wote wenye maono ya kuinuana kiuchumi.
MGOMBEA UBUNGE AZZA HILLAL HAMAD ANAZINDUA KAMPENI JIMBO LA ITWANGI

Mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Jimbo jipya la Itwangi, Azza Hillal Hamad, leo Septemba 13, 2025 anazindua rasmi kampeni zake katika Mkutano mkubwa wa hadhara unaofanyika Didia, wilayani Shinyanga.
Uzinduzi huo unahudhuriwa na maelfu ya wananchi, wanachama wa CCM pamoja na wagombea udiwani.
CCM inaendelea kuwaomba wananchi wa Jimbo la Itwangi kumpa kura za ushindi ili awe mwakilishi wao bungeni.
Vilevile, inasisitiza umuhimu wa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, mgombea urais kupitia CCM pamoja na Madiwani wa CCM.
Mkutano huu wa leo ni sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambapo wananchi watapiga kura kuwachagua viongozi wa ngazi mbalimbali.

INEC YAMTEUA MPINA KUGOMBEA URAIS

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele akimkakabidhi nakala ya fomu za uteuzi kwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT - WAZALENDO), Mhe. Luhaga Joelson Mpina aliyeambatana na Mgombea Mwenza, Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej (kushoto) leo Septemba 13, 2025 Jijini Dar es Salaam, baada ya wagombea hao kuteuliwa na Tume kuwania nafasi hizo katika uchaguzi Mkuu wa utakao fanyika Oktoba 29, 2025. (Picha na INEC).
























