Wednesday, 27 August 2025
Monday, 25 August 2025
TARIME CCM HAIJATUTENGA, IMETUUNGANISHA-KEMBAKI
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Aliyekuwa Mbunge wa Tarime Mjini na Mtia Nia wa nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2025 Michael Kembaki, ameonyesha ukomavu wa kisiasa na uzalendo kwa chama chake kwa kukubali maamuzi ya vikao vya CCM vilivyopitisha jina la Ester Matiko kuwa mgombea wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kembaki ambaye aliibuka mshindi wa kwanza kwenye kura za maoni kwa kupata kura 1,572, amethibitisha kuwa si kila ushindi unaolengwa ni wa sanduku la kura, bali kuna ushindi mkubwa wa kusimamia misingi ya chama na kuvunja makundi kwa ajili ya mshikamano.
Mbunge huyo wa Tarime anayemaliza muda wake ameeleza hayo leo Agosti 25,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo ameeleza, “Nawashukuru sana wananchi wa Tarime kwa kuniamini na kunipa kura zenu,lakini kama mnavyojua, utaratibu wa chama chetu hauishii kwenye kura za maoni pekee bali Mgombea hupatikana kupitia mchakato wa kina wa vikao halali vya chama,” amesema
Kembaki pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa imani na nafasi aliyopewa kulitumikia Taifa kama Mbunge kwa miaka mitano na kueleza kuwa ametambua kuwa uongozi si kiti cha kudumu, bali ni fursa ya kupokezana kwa wakati sahihi.
“Mwaka 2020 nilikuwa wa pili kwenye kura za maoni lakini nikaaminiwa kupeperusha bendera ya chama,leo, pamoja na kuongoza kura za maoni, sikuteuliwa lakini nimepokea maamuzi ya chama kwa mikono miwili,” amesema kwa utulivu.
Kembaki ametumia nafasi hiyo kuwatoa hofu wafuasi wake akisisitiza kuwa CCM haina upendeleo kama inavyoaminika na baadhi ya watu, bali ina utaratibu wake madhubuti wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia vigezo vyenye mashiko.
“Mwaka 2020 nilipata kura 64 tu, mpinzani wangu alipata zaidi ya 200 – lakini chama kilinichagua. Leo nimeongoza kura, lakini chama kimempitisha mwingine hii ni ishara kuwa CCM haijengwi kwa hisia, bali kwa vigezo na utaratibu,” ameeleza.
Katika ujumbe wake kwa wanachama na mashabiki, Kembaki amesisitiza kwamba huu si wakati wa lawama wala migawanyiko badala yake, amewataka kuvunja makundi yote, kusimama pamoja na kuhakikisha ushindi wa chama kwa kuhamasisha wananchi kumchagua mgombea aliyeteuliwa.
“Sitabomoa nyumba niliyoijenga. Nitaendelea kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo. Huu si wakati wa hisia binafsi – huu ni wakati wa CCM. Mgombea tayari amepatikana; sasa kazi yetu ni moja tu – kumnadi na kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo,” alisema kwa msisitizo.
Akiangazia hali ya maendeleo wilayani Tarime, Kembaki amesema kuwa ahadi nyingi zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita tayari zimetekelezwa kwa kiwango cha asilimia 85, huku akibainisha kuwa fedha nyingi zimepelekwa mkoani humo kwa ridhaa ya Rais Samia.
“Hii ni sababu ya msingi ya kuhakikisha serikali inaendelea kuaminiwa. Wanachama na wananchi wa Tarime tuendelee kuiunga mkono serikali na chama – kwa sababu miradi tuliyoahidi tumetekeleza, na mengine bado yanaendelea,” alisema.
Kembaki ametuma ujumbe mzito kwa wale wote wanaohisi kuumizwa na mchakato wa ndani ya chama.
Ametoa mfano wake kama ushahidi kuwa demokrasia ndani ya CCM ipo, na kwamba nafasi ya uongozi ni fursa ya muda, si haki ya kudumu.
“Uhai wa CCM ndio unaosababisha watu kulalamika lakini hiyo ndiyo dalili kuwa chama hiki kipo hai na kinafuata taratibu zake,Mimi nitaendelea kuwa mwanachama mtiifu na mwenye kuisapoti CCM kwa moyo wote,” amesema Kembaki.
Tanzia : ASKOFU SHAO AFARIKI DUNIA

Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Martin Shao, amefariki dunia leo baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Mhandisi Zebadia Moshi, kupitia taarifa yake aliyoitoa leo (Agosti 25,2025), imeeleza kuwa Askofu Dk. Shao, amefariki dunia akiwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya KCMC, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Dk. Martin Shao, alikuwa Askofu wa awamu ya tatu wa Dayosisi hiyo ya Kaskazini, tangu mwaka 2004 alipochaguliwa kumrithi mtangulizi wake, Askofu Dk. Erasto Kweka (sasa marehemu).
Alitunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa (PhD), na Chuo Kikuu cha Midland Lutheran College of Nebraska, USA kutokana na uongozi wake uliotukuka na utumishi wa muda mrefu katika huduma za dini.
Chanzo - Nipashe
TTCL KUJENGA MINARA ZAIDI YA 1,400 KUIMARISHA MAWASILIANO NCHINI
Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), CPA (T) Moremi Marwa, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali kupitia shirika hilo imepanga kujenga zaidi ya minara 1,400 ya mawasiliano nchini, ikianza na minara 600 mwaka huu, na mingine 850 kufuata mwaka 2026/2027.CPA Marwa ameyasema hayo Agosti 24, 2025, katika banda la TTCL kwenye Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum 2025) kinachoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC jijini Arusha, kilichofunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango.
Amesema TTCL ndiyo taasisi pekee nchini inayomiliki Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huku Serikali ikiendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa ili kufanikisha ajenda ya uchumi wa kidijitali.
“Hatua hii inalenga kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na yenye changamoto ambazo kwa kawaida watoa huduma binafsi hawawezi kufika kutokana na kutolipa kibiashara,” alisema CPA Marwa.
Aidha, amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mpango huu miezi sita iliyopita, zaidi ya minara 100 imekwishajengwa, na matarajio ni kwamba ifikapo Juni 2026, minara yote 620 iliyopangwa kwa mwaka huu itakuwa imekamilika.
Ameongeza kuwa TTCL imejipanga kuhakikisha minara hiyo inaunganishwa moja kwa moja na Mkongo wa Taifa, ili wananchi wapate huduma za intaneti yenye kasi na uhakika.
Vilevile, CPA Marwa amekumbusha kuwa mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mkakati wa kidijitali unaolenga kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kidijitali, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeweka msisitizo mkubwa katika eneo hilo.
Mbali na Mkongo wa Taifa, TTCL pia ina kituo cha Data Center kinachowezesha mifumo ya kidijitali nchini kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Uwekezaji huu unaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya teknolojia, huku wananchi wakinufaika na huduma bora za mawasiliano, ikiwemo intaneti ya kasi kubwa inayosaidia kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
KISHINDO CHA AHMED ALLY SALUM AKICHUKUA FOMU YA UBUNGE WA SOLWA
Sauti za hamasa, nyimbo za mshikamo na umati wa watu waliofurika leo katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ziliashiria tukio kubwa la kisiasa: Ahmed Ally Salum amechukua rasmi fomu ya kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Solwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kiongozi huyu, aliyeidhinishwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, alipokelewa kwa kishindo kikubwa na mamia ya wanachama, viongozi na wapenzi wa chama waliomsindikiza kwa shangwe na nderemo, wakionesha mshikamano wa dhati na matumaini mapya kwa Solwa.
Baada ya kuchukua fomu, Ahmed Ally Salum amewashukuru wananchi na wanachama kwa mshikamo wao, huku akiahidi kuendeleza kasi ya maendeleo katika nyanja za afya, elimu, maji, kilimo, biashara na miundombinu.
“Nina imani kubwa kuwa mshikamano wetu ndiyo ngao ya ushindi. Tukiungana, Solwa itaendelea kusonga mbele kwa maendeleo endelevu,” amesema kwa kujiamini.
Wananchi waliokuwa sehemu ya tukio hilo wamesema uteuzi wake ni uthibitisho kwamba CCM imeweka mbele kiongozi sahihi, mwenye dira na rekodi ya utendaji uliowagusa wengi kwa matokeo chanya.
Kwa pamoja wameahidi kusimama naye bega kwa bega kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.













































