Sunday, 17 August 2025

UJENZI BARABARA YA KAHAMA - BULYANHULU KWA UWEZESHAJI WA MIGODI YA BARRICK NI MFANO WA UWEKEZAJI BORA SEKTA YA MADINI NCHINI

Mnamo mwezi Machi mwaka jana wakati Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) iliposaini mkataba wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kahama-Bulyanhulu JCT- Kakola yenye kilomita 73 na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa ufadhili wa Barrick wa gharama ya shilingi bilioni 101.2 , ilikuwa ni faraja kubwa kwa watumiaji wengi wa barabara hiyo ambayo ilikuwa ni moja ya kero kubwa ya muda mrefu kutokana na kuwa katika hali mbaya wakati wote iwe kipindi cha mvua ama kipindi cha kiangazi.

Wananchi waliona kuwa sasa wakati wao wa kujikwamua kiuchumi umewadia, kwa kuwa ujenzi huo ukikamilika utazidi kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo madini, Kilimo, Misitu na Utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma.

Kilichofurahisha zaidi ni kuona ujenzi huo unafadhiliwa na migodi ya Barrick nchini ambayo inaendeshwa kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation. Migodi hiyo ni Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi ambao uko katika mchakato wa kufungwa.
Kutekelezwa kwa mradi huu mkubwa unaofadhiliwa na mwekezaji mkubwa nchini katika sekta ya madini, ni moja ya kielelezo kinachodhihirisha kuwa Serikali ikishirikiana na sekta binafsi inaweza kufanya mambo makubwa mojawapo ikiwa ni ujenzi wa miundombinu bora ya barabara,reli na mingineyo ambayo ni moja ya kichocheo cha ukuaji uchumi katika taifa na kufanya maisha ya wananchi kuwa mazuri.

Pia mradi huu unadhihirisha kuwa usimamizi wa rasilimali ya madini na nyinginezo nchini ukipata wawekezaji wazuri na kusimamiwa ipasavyo unaweza kuleta maendeleo makubwa nchini kwa haraka.

Kama kampuni moja imeweza kutoa kiasi cha shilingi bilioni 101.2 kujenga kipande kikubwa kama hiki cha barabara kwa kiwango cha lami tafsiri yake ni kwamba ukiwa na wawekezaji wakubwa wapatao hata 100 kwa idadi wakawekewa mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kuwekewa sheria na sera rafiki zisizobadilika kila wakati na kusimamiwa ipasavyo wanaweza kutoa mchango mkubwa wa fedha za kufanikisha miradi mikubwa ya maendeleo .
Mpaka sasa kasi ya mradi huu unaojengwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa kusimamiwa na kitengo maalumu cha ushauri wa Kihandisi ndani ya Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS (Tanroads Engineering Consulting Unit-TECU) unaendelea vizuri na madaraja katika baadhi ya maeneo korofi yanaendelea kujengwa.

Waziri wa Ujenzi wa wakati huo,Innocent Bashungwa aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa kusaini mkataba wa kuanza ujenzi wa barabara hii uliofanyika wilayani Kahama mkoani Shinyanga, alisema barabara hiyo imekuwa moja ya kero kubwa kwa wananchi kwa muda mrefu na sasa Rais Samia Suluhu Hassan ameipatia suluhisho kwa ushirikiano mzuri na wawekezaji wa ndani ya nchi ikiwemo kampuni ya Barrick na kutoa kibali barabara hiyo iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Kwa niaba ya Serikali,Waziri Bashungwa aliishukuru kampuni ya Barrick kwa kufadhili mradi huu mkubwa wa kilometa 73 na kuahidi kuwa kwa mujibu wa mkataba ujenzi wa barabara hii utatekelezwa ndani ya miezi 27 kwa maana ya kwamba utakamilika mwaka wa 2027.
Hivi karibuni Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Shinyanga Mhandisi Joel Samwel Mwambungu,alikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kukaririwa na vyombo vya habari ekieleza kuwa ujenzi unaendelea vizuri na kuielezea barabara hiyo kuwa ni fursa ya kufungua milango ya kiuchumi nchini na inafungua milango kwa wawekezaji na wafanyabiashara wazawa pia ni moja ya mikakati ya serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

Mradi huu pia umeleta faraja kwa wananchi mbalimbali ambao wameajiriwa kufanya kazi mbalimbali katika mchakato huu wa ujenzi na wanaendelea kujipatia kipato sambamba na wafanyabiashara katika eneo inapopita barabara wameanza kunufaika kwa biashara zao kuchangamka kutokana na kuongezeka kwa watu.

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo na watumiaji wa mara kwa mara wa barabara hii inayoendelea kujengwa walipohojiwa wiki hii, walisema barabara ilikuwa katika hali mbaya na kuwasababishia usumbufu mkubwa na hasara na walitoa shukrani kwa Serikali na kampuni ya Barrick kwa kuijenga tena kwa kiwango cha lami.
Akiongea kwa niaba ya Wananchi wenzake, Mwandu John, mkazi wa kijiji cha Ntobo kilichopo Halmashauri ya Msalala, alisema barabara hiyo ilikuwa na mashimo makubwa ambayo yamekuwa yakisababisha kuharibika kwa vyombo vya usafiri na kuongeza gharama za maisha kutokana na kupoteza muda mwingi kutoka Kahama mpaka Bulyanhulu wakati kupande hicho kama barabara ni nzuri ni kifupi.

“Tunayo furaha kubwa kuona barabara hii inatengenezwa kwa kuwa mbali na kurahisisha maisha itaaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo haya yaliyokuwa yanafifishwa na ubovu wa miundombinu.Tunashukuru Barrick kwa kuendelea kudhihiriha kuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika mkoa huu” alisema Mwandu John kwa furaha akiungwa mkono na wenzake.

Naye Samwel Petro akiongea kwa niaba ya madereva wa vyombo vya moto wanaotumia barabara hiyo alisema kwa muda mrefu ubovu wa barabara unawasababishia hasara kubwa ya kuharibika kwa vyombo vyao,anaamini sasa ujenzi ukikamilika tatizo hilo litaisha na fursa za biashara zinaongezeka sambamba na wananchi wengi kuweza kujiajiri na kuboresha maisha yao.
Akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa mrejesho wa mkakati wake endelevu wa miaka sita wa kampuni ya Barrick Mining Corporation akiwa nchini Canada hivi karibuni, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu, Mark Bristow, alisema kampuni inaendelea kuendeleza miradi ya ukuaji wa msingi iliyoundwa kuleta thamani ya muda mrefu kwa wadau wote kupitia ushirikiano wa kweli.

Alisema vipaumbele vya uendelevu vya Barrick ni pamoja na utekelezaji Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), kudumisha dhamira yake isiyoyumba ya usalama mahali pa kazi, na kuchukua tahadhari za matukio ya mbele na udhibiti wa uchafuzi wa hali ya hewa kutokana na shughuli zake.

"Mkakati wetu wa uendelevu sio tu mfumo - ni jinsi tunavyounda athari za kudumu, zinazowajibika,"alisema Rais wa Barrick na Afisa Mtendaji Mkuu Mark Bristow na kuongeza "Uchimbaji madini ukifanyika kwa umahiri ni nguvu kubwa ya kuleta maendeleo. Jamii zinazoishi kwenye maeneo ya shughuli zetu zikipata mafanikio ni mafanikio kwetu pia .”
Share:

WAOMBA KUONDOLEWA VIKWAZO BIASHARA YA MAZAO YA KILIMO IKOLOJOA MIPAKANI



Mussa Juma,Arusha

Serikali katika nchi za Afrika ya Mashariki, zimeombwa kuondoa vikwazo ambavyo vinaathiri biashara za mipakani za mazao ya kilimo Ikololojia, hasa kwa wajasiriamali wadogo ili kuwezesha kukuza biashara hiyo.

Utafiti uliofanywa kuhusiana na biashara za kilimo Ikolojia (Kilimo Hai) mipakani zimebaini kuna changamoto kadhaa ikiwepo viwango vya ubora wa bidhaa,mifumo ya ulipaji kodi,vikwazo vya barabarani,udhibiti wa bidhaa zisizo na ubora na uelewa mdogo wa wajasiriamali katika masuala ya biashara ya mipakani.

Akisoma mapendekezo ya kisera kutokana na  warsha ya wadau kuhusu biashara  ya mipakani kwa mazao ya bidhaa za kilimo Ikolojia,Afisa wa Utetezi na Ushawishi wa Shirikisho la  wakulima Tanzania(SHIWAKUTA),Thomas Laizer alisema   wamekubaliana ni  muhimu, kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kuondoa au kupunguza  vikwazo visivyo vya kikodi (NTBs) ikiwemo mazuio yasiyo rasmi ya barabarani ambayo kwa kiasi kikubwa inaathiri biashara za mipakani (cross-border trade).  

Laizer alisema  vikwazo hivyo  sio tu  vinavuruga mfumo wa kibiashara, bali unamuumiza mkulima kwani wafanyabiasha huishia kununua mazao kwa bei ya chini kufidia hasara wanayoitarajia kukumbana nayo wasafirishapo mazao. 

"Hali hii huchochea wafanyabiashara na wazalishaji kutumia njia zisizo rasmi (njia za panya) kusafirisha mazao na bidhaa na hivyo kukosesha serikali mapato ambayo huyatumia kuwaletea wananchi maendeleo"alisema

Alisema pia wanapendekeza Serikali na wadau, kuchukua hatua ya kuwekeza katika kuwaelimisha wakulima kuhusu mahitaji ya kisera na kisheria yanayohusu uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo ikolojia ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika biashara za mipakani (cross-border trade) na kukuza uchumi wa kilimo endelevu.

Laizer alisema, pia wanahimiza Serikali  kuchukua jukumu la msingi katika kuweka miundombinu wezeshi, sera rafiki na mikakati shirikishi ili kuwawezesha Watanzania kufikia masoko ya kimataifa kwa bidhaa ghafi na zilizosindikwa, hivyo kuongeza thamani ya mazao na kukuza pato la taifa.

"Tunatambua na kukubali kuwa uwepo wa wanunuzi na wafanyabiashara toka nje ni fursa kwa wazalishaji wadogo nchini na  Tunatoa wito kwa serikali yetu kuweka mazingira wezeshi na ya uwazi yatakayolinda maslahi ya wazalishaji wa ndani kwa kuhakikisha biashara inayoendeshwa inanufaisha wazalishaji hao, inazingatia haki na usawa, na serikali inapata mapato stahiki ili kuweza kuwaletea wananchi wake maendeleo"alisema

Laizer alisema  , wamekubaliana Serikali ya Tanzania inapaswa kuzijengea uwezo wa kirasilimali, ikiwa ni pamoja na rasilimali watu na vifaa, mamlaka zinazodhibiti ubora wa mazao ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha walaji wanalindwa dhidi ya mazao yaliyozalishwa kwa kutumia pembejeo zenye viambata hatarishi kwa afya na mazingira.

Alisema wanapendekeza  Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutumia nafasi yake kuzihimiza nchi wanachama kuweka sera na mikakati ya pamoja itakayoielekeza Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa ukanda wa uzalishaji na biashara ya mazao na bidhaa zilizozalishwa kiikolojia, kwa lengo la kulinda afya ya walaji, kuhifadhi mazingira, na kuongeza ushindani wa bidhaa za ukanda huu katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Awali wakizungumzia Utafiti huo, uliofanywa na Washauri wa biashara za kilimo Ikolojia mpakani, kwa udhamini wa  Shirika la Muungano wa Uhuru wa chakula Afrika(AFSA),Afisa Miradi wa SHIWAKUTA na MVIWAARUSHA,Damian Sulumo  alisema kama vikwazo vya biashara ya mazao ya kilimo Ikolojia vikiondolewa uzalishaji utaongezeka.

Sulumo alisema hata hivyo, bado kunahitajika mafunzo kwa wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo Ikolojia  ili kuboresha bidhaa zao na badala kuendelea kuuza nje bidhaa kama  malighafi wanatakiwa kuuza bidhaa zilizosindikwa katika masoko ya kimataifa.

Mshauri wa biashara za mazao ya Kilimo Ikolojia wa AFSA , Africa Kiiza  ambaye aliongoza utafiti huo, alisema anaamini mapendekezo ambayo wametoa baada ya utafiti huo, yatakwenda kufanyiwa kazi.

Alisema AFSA ,kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kuwajengea uwezo wadau mbalimbali, ikiwepo wabunge wa EAC,Wanahabari  na wafanyabiashara wamazao ya kilimo Ikolojia.

Mratibu wa SHIWAKUTA  Richard Masandika , alisema utafiti huo uliofanyika katika mipaka ya  Tanzania na Kenya, Kenya na Rwanda na nchi mipaka mingine katika nchi za Afrika ya Mashariki, umekuwa na manufaa makubwa.

Alisema wanaimani kuna taratibu za kikanda na kiserikali za EAC, zinaweza kufanywa ili kuondoa vikwazo kwa wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo Ikolojia.

Wadau wa kilimo Ikolojia katika nchi za Afrika ya Mashariki, wakiwepo wakulima, vyama vya wakulima, watafiti na wanahabari za kilimo Ikolojia walishiriki warsha ya siku mbili jijini Arusha, kuhusiana na utafiti uliofanywa wa AFSA  kuhusiana na biashara za kilimo Ikolojia (Kilimo Hai) mipakani.

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAPILI AGOSTI 17,2025

magazeti    

Magazeti

Share:

Saturday, 16 August 2025

MATUKIO KATIKA PICHA: MAFUNZO YA WAANDISHI WA HABARI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025













Na Mwandishi wetu, Arusha

Leo, tarehe 16 Agosti 2025, jijini Arusha, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC, kumezinduliwa rasmi mafunzo maalum kwa waandishi wa habari na watangazaji yanayolenga maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Mafunzo hayo yamefunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Kali Salum, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenani Kihongosi.

Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwaongezea uelewa wanahabari kuhusu weledi, maadili na wajibu wao katika kipindi cha uchaguzi, ili kuhakikisha taarifa sahihi na zenye kuzingatia misingi ya kitaaluma zinawafikia wananchi kwa wakati.







Share:

“SERIKALI IMEENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA KUJIFUNZIA NA KUFUNDISHIA” MWAMBENE


Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. Atupele Mwambene amesema serikali kupitia miradi mbalimbali imeboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kuyafanya yawe salama, yanavutia na rafiki kwa walimu na wanafunzi kufundisha na kujifunza ili kuendelea kuboresha Sekta ya elimu kote Nchini.

Bw. Mwambene ameyesema hayo wakati wa akifunga mafunzo ya Walimu wa ushauri, unasihi na ulinzi wa Watoto wa shule za Msingi Nchini, kupitia mpango wa shule salama unaotekelezwa kupitia mradi BOOST, yaliofanyika katika Chuo Cha Ualimu mkoani Tabora.


Amesema, Serikali imewezesha kujengwa kwa shule mpya 2,441 zikiwemo za msingi 1,399 na za sekondari 1,042 katika maeneo ya vijijini ambayo hayakuwa na shule na yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi, na jumla shule kongwe 906 zilikarabatiwa na miundombinu mingine kama vile; vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, mabweni, mabwalo, maabara na maktaba imejengwa na kukarabatiwa.

“Ofisi ya Rais – TAMISEMI katika kipindi cha mwaka 2022/23 hadi 2024/25 ilipeleka jumla ya shilingi bilioni 539.6 shuleni na kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 656 za awali na msingi, lengo la msingi la uwekezaji huu ni kuhakikisha sisi kama Taifa, Wazazi na Walezi tunatoa fursa sawa ya Watoto kupata elimu” Mwambene.


Aidha, amewataka kwenda kuimarisha mifumo na taratibu za kushughulikia malalamiko ya wanafunzi kwa kuweka masanduku ya maoni, mabaraza ya watoto pamoja na madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto shuleni kwa kufuata miongozo na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zitakazowasilishwa na wanafunzi.

Vile vile, Bw. Mwambene amewaelekeza walimu kote Nchini kuhakikisha wananazingatia nidhamu, maadili na miiko ya ualimu ili kuhakikisha wanafunzi wanatendewa haki na kuondoa kabisa vitendo vya ukatili ambavyo vinaweza kufanywa na walimu dhidi ya Wanafunzi kwa sababu ya kutozingatia maadili ya ualimu.

Akitoa neno la utangulizi, Mratibu wa Mradi wa BOOST kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwal. Ally Swalehe amesema mradi huo ulianzisha ukiwa na malengo ya kupambana na changamoto ya uhaba na uchakavu wa miundombinu, baadhi ya wanafunzi wa darasa la pili kushindwa kumudu stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika na baadhi ya wanafunzi kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger