Friday, 27 June 2025

WATUMISHI WA MAGEREZA MANYARA WAPATIWA MAJIKO YA GESI



📌Mifumo ya uzalishaji wa bayogesi 126 mbioni kuanza

📌REA, Jeshi la Magereza kununua mashine 61 za mkaa mbadala

📌REA kuwajengea uwezo magereza uendelezaji miradi ya nishati safi

📌Mha. Saidy amewataka magereza kuwa mabalozi wa nishati safi

Serikali imewapatia watumishi wa Jeshi la Magereza mitungi ya gesi na majiko ya gesi ya kupikia ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi na wananchi iliyolenga kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Hayo yamebaibishwa leo Juni 26, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu wakati wa  uzinduzi wa kugawa majiko ya gesi kwa watumishi wa magereza iliyofanyika gereza la Babati mkoani Manyara.

Amesema kuwa, katika mkoa wa Manyara tayari Serikali imegawa mitungi ya gesi na majiko ya gesi yapatayo 330 kwa watumishi wa jeshi la magereza na katika gereza la Babati jumla ya majiko na mitungi 150 wamegawiwa watumishi hao wa magereza. 

Amesema kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia makubaliano na Jeshi la Magereza ya kuwawezesha magereza kuhama kutoka katika matumizi ya nishati isiyo salama kwenda katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika magereza yote nchini. 

"Kuanzia mwanzoni wa mwezi januari 2025 jeshi la magereza walishaingia kwenye matumizi ya nishati safi na salama na tayari wameachana na nishati isiyo salama na chafu kwa afya na mbaya kwa mazingira yetu, " Ameongeza. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amewataka watumishi wa jeshi la magereza  kuibeba ajenda ya Mhe. Rais Samia ya kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia hapa nchini. 

Katika hatua nyingine Mha. Saidy ameeleza kuwa, mifumo ya uzalishaji wa bayogesi ipatayo 126 tayari ipo mbioni kuanza kwa kushirikiana na jeshi la magereza ambayo itawezesha ununuzi wa mashine za kutengeneza mkaa mbadala 61, vile vile kuwajengea uwezo watumishi wa jeshi la magereza ya kuendeleza miradi hiyo ya nishati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza mkoa wa Manyara ACP Solomon Mwambingu amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia watumishi wa magereza majiko ya gesi na mitungi ya gesi na kusisitiza kuwa wataendelea kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia katika jamii yote inayowazunguka.

Share:

Thursday, 26 June 2025

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO JUNI 25,2025


Magazetini






















Share:

MAVUNDE AZUNGUMZIA TUKIO LA MAITI KWENYE PIKIPIKI LILIVYOMGEUZA KUWA MTUMISHI WA WATU




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Akiwa njiani kutekeleza majukumu yake kama Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde alikutana na jambo lililobadili kabisa mtazamo wake kuhusu uongozi  mtu mmoja aliyekuwa akibeba maiti ya mpendwa wake juu ya pikipiki, akisaka msaada wa kuisafirisha kwa heshima ya mwisho.

Tukio hilo lilimgusa kwa undani na kuacha alama ya kudumu moyoni mwake. Akieleza kwa sauti ya huzuni na huruma mbele ya hadhira iliyojitokeza kwenye hafla ya uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa kupokea kero za wananchi, Mavunde alisema:

“Moyo wangu uliniuma sana. Nikajiuliza, mimi ni mbunge, nitawezaje kulikalia kimya jambo kama hili? Nikasema hapana,badala ya kuchangia shilingi laki tatu kila siku kwenye misiba, ni bora ninunue gari la kusaidia watu wangu kusafirisha miili ya wapendwa wao.”

Uamuzi huo ulimuweka katikati ya mvutano wa mitazamo. 

Alitukanwa, alipingwa, lakini hakutikisika. Alisimama kidete kama kiongozi wa vitendo na siyo wa hotuba, na leo anasema bila hofu kuwa maumivu hayo ndiyo yaliyomfanya avae rasmi vazi la “utumishi wa watu”.

“Niliamua kuishi utumishi, siyo uongozi. Kuna tofauti kubwa kati ya kiongozi na mtumishi. Mimi ni mtumishi wa watu – niliamua kuitikia kilio cha jamii yangu,” amesisitiza.

Katika kuendeleza azma yake ya kuhudumia watu, Mavunde leo amezindua rasmi mfumo wa kidigitali wa kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi wa Dodoma Mjini mfumo wa kwanza wa aina yake nchini.

Wakati huo huo, amegawa simu janja kwa wenyeviti wa mitaa 222 wa jimbo hilo, kwa lengo la kurahisisha mawasiliano baina ya viongozi na wananchi.

“Kupitia mfumo huu, hata kama kiongozi mmoja hapokei simu, taarifa ya mwananchi itafika kwa wengine wote kwa wakati mmoja. Hii ndiyo teknolojia tunayopaswa kutumia kwa maendeleo ya watu wetu,” alieleza kwa msisitizo.

Mavunde amesema mfumo huo utaendelea kutumika hata baada ya yeye kuondoka madarakani, na tayari maandalizi yamefanyika kuhakikisha mbunge ajaye anaelekezwa na kuendeleza huduma hiyo muhimu kwa wananchi wa kata zote 41 za Dodoma Mjini.

“Naondoka bila deni. Huu ni mwisho wa safari yangu kama Mbunge wa Dodoma Mjini, lakini mwanzo wa zama mpya za utumishi kwa teknolojia. Nawashukuru kwa kuniamini kwa miaka kumi,” amesema kwa hisia.

Aidha, Mavunde ametangaza kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuanzisha SACCOs ya wenyeviti wa mitaa  hatua itakayowawezesha kiuchumi na kuwaongezea uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Amesisitiza kuwa simu walizopewa si za anasa, bali ni nyenzo muhimu za kutatua matatizo ya wananchi. Simu hizo zimetengenezwa nchini kwenye kiwanda cha Mkuranga, ikiwa ni hatua ya kuunga mkono ajira na uzalishaji wa ndani.

“Tutatenganishwa na mipaka ya kijiografia tu, lakini roho yangu itaendelea kuwa nanyi. Nawashukuru kwa safari hii ya kipekee, nitaendelea kuwa mtumishi wa watu hata nje ya ubunge,” alihitimisha huku akipigiwa makofi ya heshima.





Share:

SABABU ZA KWANINI UWE NA APP YA MALUNDE 1 BLOG KWENYE SIMU YAKO

Share:

Wednesday, 25 June 2025

SERIKALI KUENDELEA KUWASHIRIKISHA WADAU WA ELIMU KUTATUA CHANGAMOTO ZA SEKTA YA ELIMU NCHINI- DKT. SHINDIKA


Na OR – TAMISEMI, Arusha

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Elimu nchini ili kuhakikisha changamoto zinazoikabili Sekta ya elimu zinatatuliwa kwa kufanya maboresho mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 24 Juni, 2025 Jijini Arusha katika ukumbi wa Kibo Palace Hotel na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu na Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt Emmanuel Shindika kwa niaba ya Bw. Atupele Mwambene, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo alisema ili kuhakikisha Sekta hiyo inakwenda vizuri, Serikali itawashirikisha Wadau wote wa Elimu waliopo ndani na nje ya nchi, wa kitaifa na kimataifa kuendelea kuzikabili changamoto za Sekta hiyo hapa nchini kama vile ajira za walimu na ujenzi wa miundombinu.

Aidha, Dkt. Shindika alisema Serikali inafuatilia kwa karibu na kufanya utafiti kwa kutumia taarifa za kimfumo za kujua maeneo yaliyo na uhaba wa walimu na pindi wanapoajiriwa walimu wapya basi hupelekwa kwenye maeneo yenye upungufu wa walimu hususani maeneo ya pembezoni yenye uhaba mkubwa wa walimu.
“Ofisi ya Rais TAMISEMI imejipanga vema katika kupanga walimu kulingana na mahitaji ya eneo husika na hivyo, hakutaweza kutokea mlundikano wa walimu wengi sehemu moja kwani kabla ya kuwapanga, tayari Wizara inajua wapi kuna mahitaji kutokana na utafiti ambao utakuwa umefanywa” alisisitiza Dkt. Shindika.

Naye Bi. Stella Mayenje Msimamizi wa Miradi ya Ufadhili wa Serikali ya Sweden kwa Serikali ya Tanzania alisema wamekutana kama Wadau wa Elimu Tanzania kufanya tathmini ya pamoja kama ambavyo walikubaliana na Serikali na Wadau wote mwaka 2022 (Midterm Review Partnership Compact, 2025) lakini pia kama wadau, wamejikita katika kusaidia ufadhili hususani Sekta ya elimu kwa kuangalia wapi wanafanya vizuri na wapi kunahitaji maboresho kwa mfano kuimarisha mipango ya kuwa na walimu wa kutosha, mazingira ya kufundishia na kujifunzia na masuala ya jinsia.
Bi. Mayenje aliongeza kuwa katika Mradi wa GPE LANES II ulifanikiwa kwa asilimia 95.4 na katika Mradi wa sasa wa Kuboresha Kada ya Ualimu (GPE TSP), umekuja na vigezo vya kuangalia takwimu za walimu wanaoajiriwa kama ipo sawa na wanafunzi waliopo shuleni na hapa alisema kama sehemu ya motisha kwa Serikali upande wa ufadhili unatoa Dola za Kimarekani 10,000 kwa kila walimu 3,000 walioajiriwa na Serikali ambapo fedha hizo za Msaada hupelekwa kufanya maboresho kwenye masuala ya elimu yaliyoainishwa.

Kwa upande wake Dkt. Jordan Busingu Mshauri wa Elimu kutoka Ubalozi wa Uingereza, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Wadau wa Maendeleo, alisema kikao kazi hicho cha mapitio kina lengo kubwa kwao kama kama Wadau wanaoshirikiana na Serikali katika kuhakikisha elimu inamfikia kila mtoto na hakuna anayeachwa nyuma kama vile kuweka usawa (equity) katika utoaji wa elimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kufanya tathmini yao na Serikali kuhusu maendeleo ya Sekta ya elimu nchini.

Kikao Kazi cha siku mbili kwa mwaka 2025 kinaangazia kufanya mapitio ya Kati ya Mpango wa Ushirikiano wa Wadau mbalimbali wa elimu kutoka ndani na nje pamoja na Wadau wa Maendeleo ili kutathmini maendeleo ya Sekta ya Elimu nchini kwa kuibua hoja za nini kifanyike katika kuendeleza na kukabiliana na changamoto za elimu.

Share:

Tuesday, 24 June 2025

WAFANYABIASHARA MKOANI KILIMANJARO WASISITIZWA KUENDELEA KULIPA KODI KWA MAENDELEO YA TAIFA

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu ametoa hamasa kwa Wafanyabiashara Mkoani hapo kuendelea kulipa kodi stahiki ili maendeleo ya nchi yazidi kupatikana.

Kauli hiyo ameitoa tarehe 23 Juni, 2025 wakati wa kuanza kwa Kampeni ya utoaji elimu ya kodi ya mlango kwa mlango mkoani hapo yenye lengo la kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanaelimishwa kuhusu kodi, wanatatuliwa kero zao za kikodi na kujengewa mazingira mazuri ya kulipa kodi.

Amesema kuwa, ulipaji kodi unaleta manufaa kwa Taifa kwa kuleta maendeleo mbalimbali nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara, afya, elimu bure, maji safi na salama na hivyo waache visingizio vya kushindwa kulipa kodi zao stahiki kwani kutolipa kodi hizo ni dhuluma kwa Serikali.

“Kuna wengine wakorofi hawataki tu kulipa kodi na wanatoa visingizio kuwa hawajui kutumia mifumo ya TRA, lakini bora mmefika kuwaelimisha ili waache visingizio hivyo na hatimaye walipe kodi zao stahiki”, alisema Babu.

Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. James Jilala amewashukuru Walipakodi mkoani hapo wanaoendelea kulipa kodi zao stahiki na kutoa wito kwa wale ambao bado wamekua wagumu katika kulipa kodi zao stahiki wawe wazalendo na walipe kodi.

Ameongeza kuwa, Wafanyabiashara wanapaswa kufanya matumizi sahihi ya mashine za EFD kwa kutoa risiti halali na kuwaonya wafanyabiashara wenye tabia kupitisha bidhaa za magendo kupitia njia zisizo halali kuacha mara moja na kuhakikisha kwamba wanapitisha bidhaa hizo katika njia sahihi. 

“Ili uweze kulipa kodi iliyo sahihi ni lazima utumie vizuri mashine ya EFD, lakini vile vile nchi yetu hii inapakana na nchi jirani ya Kenya, niwaombe wafanyabiashara wenye tabia ya kupitisha bidhaa za magendo kuacha mara moja kupitisha njia zisizo halali na badala yake watumie njia zilizo sahihi”, alisema Jilala.

Baadhi ya wafanyabiashara mkoani hapo wamepongeza kampeni hiyo na kuomba iwe endelevu na wengine wakishauri kuwa Maafisa wa TRA wanapopita inasaidia kuona uhalisia wa biashara wanazofanya na itasaidia katika suala la makadirio ya kodi.

Kempeni ya elimu kwa Mlipakodi ya mlango kwa mlango ni zoezi endelevu ambalo TRA imekua ikiliendesha nchi nzima kwa kuhakikisha kwamba, Wafanyabiashara wanapewa elimu ya kodi na kukumubushwa haki na wajibu wao katika masuala ya kodi ambapo kwa sasa zoezi hilo lipo mkoani Kilimanjaro na Dar es Salaam.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger