Sunday, 12 November 2023
Saturday, 11 November 2023
MBUNGE CHIKOTA ASHAURI MAMBO MATATU MAKUBWA MPANGO WA MAENDELEO 2024/25
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ameshauri serikali itoe vivutio maalum kwa wawekezaji wanaotaka kujenga vituo vya kujazia gesi asilia ili kusogeza huduma kwa wananchi wanaofunga mfumo wa gesi kwenye vyombo vyao vya usafiri.
Akichangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2024/25 bungeni, Chikota amesema kwasasa vituo hivyo vipo vinne nchini huku kampuni zaidi ya 30 zikiwa zimeomba.
“Tuwe na vivutio ili kutoka Dar es salaam kuja Dodoma kuwe na vituo vya gesi na maeneo mengine, tutoe punguzo maalum ili wawekezaji wajikite kwenye eneo hili,”amesema.
Kuhusu usambazaji wa gesi viwandani na majumbani, Chikota amesema pamoja na kazi inayofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) lakini haipewi fedha za kutosha.
“Naomba mpango ujielekeze kutoa fedha za kutosha ili usambazaji huu sasa uende kwenye mikoa yote isiwe Mtwara, Lindi na Dar es salaam,”amesema.
Aidha, amepongeza Wizara ya Nishati kwa kazi inayofanya kwenye gesi asilia huku akishauri shughuli za mradi wa gesi asilia zifanyike kwenye eneo husika.
“Likong’o ipo Manispaa ya Lindi si busara shughuli hizi zikaendelea kufanyika Dar es salaam na Arusha wakati eneo la mradi lipo naomba sasa shughuli za LNG zihamie eneo husika, kuhusu vituo vya kujazia gesi vipo vichache,”amesema.
Kadhalika, Mbunge huyo ameshauri katika sera ya elimu ya mwaka 2014 toleo la 2023, serikali ijielekeze katika ugharamiaji kwa kuwa inakwenda kubadili uendeshaji na usimamizi wa elimu.
“Kuanzia mwakani tunaanza kutekeleza mtaala mpya inamaana mtihani wa darasa la saba 2027 hautakuwepo kutakuwa na mtihani wa tathmini, takwimu zilizopo wanafunzi takribani asilimia 25 hawaendelei na kidato cha kwanza, hivyo tutakavyokuwa tunafanya tathmini wanafunzi wote wataingia kidato cha kwanza,”amesema.
Amesema kutakuwa na mahitaji mapya ikiwamo madarasa, walimu, vyoo na kwamba inakadiriwa kuhitajika madarasa ya ziada 8733, vyoo 17,467 na kusisitiza lazima mpango ujikite katika kutafuta fedha za kugharamia mfumo mpya wa elimu.
DKT. ABBAS ATEMBELEA NA KUJIONEA MAENDELEO MRADI WA UJENZI NYUMBA 5000 MSOMERA - TANGA
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas ametembelea na kujionea maendeleo ya mradi wa Ujenzi wa Nyumba 5000 mradi unaotekelezwa na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia Kampuni yake ya SumaJKT katika kijiji cha Msomera Wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Katika ziara hiyo Dkt Abbas amelisifu Jeshi la Ulinzi kwa kuendelea kukamilisha ujenzi huo licha changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani humo, na kusema amefurahishwa na shughuli zinavyoendelea kwa weledi mkubwa.
Aidha, Dkt Abbas amesema kuwa anaamini kwa jinsi alivyojionea ujenzi unavyooendelea wa nyumba hizo zinaweza kuanza kukabidhiwa hata kabla ya muda uliopangwa.
“Nalipongeza Jeshi kwa jinsi linavyojitoa katika mradi huu kwani mradi ni wa haraka na kwa muonekano wa hizi nyumba pamoja na changamoto zote za mvua na kukatika kwa umeme bado kiwango kivzuri sina shaka na kazi zenu”, amesema Dkt Abass
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Albat Msonde amesema ujio wa Katibu huyo katika kutembelea mradi huo kunazidi kutoa faraja kwa watendaji walio katika mradi huo kwani kunawaongezea hamasa Zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Msomera Bwana Martini Olenkayo amesema wananchi wa Ngorongoro wanaotarajiwa kuhamia katika kijiji hicho hawana budi kuishukuru Serikali kwa jinsi inavyoendelea kuwaandalia maeneo ya makazi ikiwemo na mahitaji yote ya kijamii na miundombinu ya umeme, maji na barabara jambo ambalo halija wahi kutokea katika nchi yetu ya Tanzania.
Akitoa Shukrani kufuatiwa kutembelewa na ugeni huo Operesheni Kamanda wa Mradi Nyumba 5000 Msomera Kanali Sadik Mihayo amesema ujio wa viongozi katika mradi huo na kujionea maendeleo ya ujenzi unavyokwenda unaleta imani kwa kazi inayofanywa na JKT.
Hii ni awamu ya pili ya Ujenzi wa nyumba katika kijiji hicho kwani awali Jeshi la Kujenga Taifa lilijenga nyumba 400 ambazo mpaka sasa wananchi kutoka Ngororo wamekwisha hamia
Friday, 10 November 2023
NEC KUFANYA UBORESHAJI WA MAJARIBIO DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa majaribio wa Daftari La Kudumu la Wapiga Kura.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa yua Uchaguzi, Ramadhan Kailima (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura na Tehama, Geofrey Mpangala (kulia) wakionesha BVR Kits zenye vifaa mbalimbali vinavyowasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura.
****************
Na Mwandishi wetu, Dodoma.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kufanya zoezi la uboreshajia wa majaribio wa daftari la kudumu la wapiga kura katika Kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.
Akitangaza uboreshaji huo leo Novemba 10,2023 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima amesema zoezi hilo litafanyika katika vituo 16 vya kuandikisha wapiga kura kati ya hivyo vituo 10 ni katika kata ya Ng'ambo na 6 vipo kata ya Ikoma.
“Uboreshaji wa majaribio utahusisha kuandikisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na atakayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 , wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo jingine, wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo daftarini,”amesema Bw. Kailima.
Kailima amesema lengo la kufanya majaribio hayo ni kupima uwezo wa vifaa na mifumo ya uandikishaji itakayotumika wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura unaotarajiwa kufanyika nchi nzima kwa tarehe na ratiba itakayopangwa na tume.
“Katika zoezi hili tume itatumia BVR Kits zenye vifaa mbalimbali vinavyowasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura, BVR Kits hizo zimeboreshwa na ni tofauti na zile zilizotumika katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2015 na 2019,”amesema Kailima.
Aidha, Kailima amesema Tume imesanifu na kuboresha mfumo wa uandikishaji wa Wapiga Kura (Voters Registration System-VRS) ili kukidhi muundo na BVR Kits za sasa ambazo zinatumia programu ya android tofauti na BVR Kits za awali ambazo zilikuwa zinatumia programu ya Microsoft Windows.
“Mfumo wa uandikishaji ulioboreshwa utawawezesha wapiga kura ambao wameshaandikishwa na wapo kwenye daftari la wapiga kura, kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zao ama kwa kubadilisha kituo cha kupigia kura iwapo amehama Mkoa au Wilaya nyingine au kurekebisha taarifa zao kwa njia ya mtandao kwa kutumia simu zao za mkononi au kompyuta,”amesema Kailima.
Amesema kuanzisha mchakato mtandaoni, mpiga kura ataingia kwenye tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi www.nec.go.tz kwa kutumia kompyuta au simu janja kisha atabonyeza kiunganishi (link) kilichoandikwa “Boresha Taarifa za Mpiga Kura” au atatumia anuani ya ovrs.nec.go.tz itakayompeleka moja kwa moja kuanzisha mchakato. Baada ya kufuata utaratibu huo, mfumo utamletea ukurasa wenye vipengele vitakavyomruhusu kuweka taarifa zake kulingana na mahitaji.
“Baada ya kukamilisha taratibu zote na kuwasilisha taarifa kwenye mfumo, mpiga kura atapokea ujumbe mfupi wenye kumbukumbu namba kupitia namba yake ya simu aliyoitumia wakati wa kuboresha taarifa zake kwenye mtandao. Kumbukumbu namba hiyo atakwenda nayo kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya kumalizia hatua zilizobaki na kupatiwa kadi,”amesema Kailima.
Katika hatua nyingine Bw.Kailima amesema kuwa uboreshaji huo utahusisha vyama vya siasa kwa kuweka wakala mmoja katika kila kituo cha kuandikisha wapiga kura lengo likiwa ni kushuhudia na kujiridhisha kuhusu taratibu zitakazotumika wakati wa uboreshaji wa majaribio wa daftari.
Amesema utaratibu huo wa uboreshaji wa taarifa kwa njia ya mtandao hautawahusisha wapiga kura wapya wanaotaka kuandikishwa kwa mara ya kwanza na waliopoteza kadi zao au kuharibika.
“Hawa wanashauriwa wafike kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura na kufuata taratibu watakazo elekezwa na maafisa wa Tume watakaokuwepo kwenye kituo,”amesema.
Pia, Kailima amesema Tume inatoa wito kwa wananchi wenye sifa zilizotajwa wa Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uboreshaji wa majaribio wa Daftari na kutoa ushirikiano kwa Tume wakati wote wa utekelezaji wa jukumu hili muhimu kwa mustakabali wa Taifa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa yua Uchaguzi, Ramadhan Kailima wakionesha BVR itakayotumika katika uboreshaji huo wa Majaribio.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa yua Uchaguzi, Ramadhan Kailima (kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura na Tehama, Geofrey Mpangala (wapili kushoto) wakionesha BVR Kits zenye vifaa mbalimbali vinavyowasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura.
Muonekano wa Mfumo wa uboreshaji wa Taarifa Mtandaoni utakao kuwa katika Tovututi na kutumika kuanzisha mchakato mtandaoni, ambapo mpiga kura ataingia kwenye tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi www.nec.go.tz kwa kutumia kompyuta au simu janja kisha atabonyeza kiunganishi (link) kilichoandikwa “Boresha Taarifa za Mpiga Kura” au atatumia anuani ya ovrs.nec.go.tz itakayompeleka moja kwa moja kuanzisha mchakato. Baada ya kufuata utaratibu huo, mfumo utamletea ukurasa wenye vipengele vitakavyomruhusu kuweka taarifa zake kulingana na mahitaji.
Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari wakifuatilia taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Bi. Giveness Aswile akizungumza jambo.
Baadhhi ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa Idara mbalimbali za Tume wakiwa katika Mkutano huo na Wanaandishi wa Habari.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa majaribio wa Daftari La Kudumu la Wapiga Kura.
Baadhhi ya Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa Idara mbalimbali za Tume wakiwa katika Mkutano huo na Wanaandishi wa Habari.
Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari wakifuatilia taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi.
WATEJA WA Y9 MICROFINANCE KUONGEZEWA DAU LA MKOPO SASA WAWEZA KUKOPA HADI LAKI TATU
Na Mwandishi wetu.
Dar es Salaam. Taasisi ya kifedha ya Y9 Microfinance imeendelea na utaratibu wake wa kukabidhi zawadi kila wiki ambapo wiki hii wamekabidhi zawadi ya pikipiki mbili kwa washindi wa Droo ya nne kwa wakazi wa Njombe na Songea.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo Mkurugenzi wa Mauzo na Usambazaji wa Taasisi ya Y9 Microfinance Bw. Fredrick Mtui amesema kuwa taasisi ya Y9 ilianzishwa mahususi kuwasadia na kuinua mitaji ya wale wenye kipato cha chini na watanzania wote nchini.
Lengo kuu la Y9 Microfinance ni kuhakikisha kila mtanzania anapata fursa hii kwa kuhakikisha anapakua app ya Y9 Microfinance na kupata huduma ya tatu ambazo ni mkopo wa fedha taslimu.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa Taasisi ya Y9 Microfinance, Sophia Mang’enya ambaye pia alieleza kuwa hii ni fursa kubwa sana kwa watanzania kwani Taasisi ya Y9 umeongeza pia kiwango cha mkopo pia siku za kulipa deni la mkopo
Mang’enya ameeleza kuwa jwasasa mteja wa Y9 anaweza kukopa kuanzia elfu mbili hadi laki tatu na muda wa kurejesha ni siku 9 ambapo awali kiwango cha juu kilikuwa laki moja na muda wa kurejesha ni siku tatu
Ameeleza kuwa nia na madhumuni ya kuongeza kiwango cha mkopo nikuridhishwa na mwenendo mzuri wa ulipaji kwa wateja wao hivyo amewasihi watanzania wachangamkie fursa hii ambayo haina mashart magumu.
amewapongeza washindi wote kwa kujiunga na huduma zao na kuweza kushinda zawadi mbalimbali ikiwemo simu, pikipiki vilevile ameongeza kwamba kwenye droo ya mwisho ambayo itanyika katikati ya mwezi Disemba kutakuwa na zawadi kubwa zaidi ya gari aina ya Toyota IST. na zawadi nyengine kemkem
Alisema kuwa washindi hao wameshinda zawadi hizo baada ya kupakuwa App yetu na kukopa kupitia app na kurejesha mikopo yao ndani ya muda uliowekwa kwa mujibu wa taratibu zetu.
Alisema kuwa zawadi bado zipo nyingi kikubwa Watanzania kuendelea kutumia humu zetu ili kujishindia zawadi.
Leo pia tumechezesha droo ambapo tumepata washindi wawili ambao ni Riziki Makame ambae amejishindia pikipiki ya matairi mawili pamoja na mkazi wa Arusha Bw. Peter ambae amejishindia simu janja.