Saturday, 5 August 2023

TUME YATANGAZA UCHAGUZI MDOGO WA MBARALI NA KATA SITA


Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima akizungumza leo Agosti 5,2023 wakati akitoa taarifa uwepo wa Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Mbarali Mkoani Mbeya na Kata sita za Tanzania bara. Taarifa hiyo ameitoa jijini Dodoma baada ya kikao cha Tume kilichokutana leo .
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mh. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele (katikati) akiongoza kikao cha Tume kilichokutana leo Agosti 5,2023 jijini Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufaa (Mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk na Kulia Katibu wa Tume hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima.

Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakiendelea na kikao chao hii leo Agosti 5,2023 jijini Dodoma.

Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakiendelea na kikao chao hii leo Agosti 5,2023 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mh. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele (wanne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi baada ya kumalizika kwa kikao chao kilichokutana leo jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine walipitisha tarehe ya uchaguzi mdogo katika jimbo la mbarali na Kata sita za Tanzania bara.
**********
Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 Septemba, 2023.


Akisoma taarifa kwa umma jijini Dodoma leo tarehe 05 Agosti, 2023, baada ya kikao cha Tume, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima amesema wagombea watachukua fomu kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023, siku ya uteuzi itakuwa tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20 Agosti, 2023 hadi tarehe 18 Septemba, 2023.

Amezitaja kata zitakazofanya uchaguzi mdogo kuwa ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.


“Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huu mdogo,” amesema Bw. Kailima.


Aliongeza kuwa, Tume imetoa taarifa hiyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiitaarifu Tume kuhusu uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Mbarali, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya. Nafasi hiyo wazi inatokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Francis Mtega. Spika ametoa taarifa hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.


“Tume imepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye Dhamana ya Serikali za Mitaa, akiitarifu juu ya uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika kata sita za Tanzania Bara. Waziri ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292,” alisema Bw. Kailima.


Aliongeza, “Tume kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 37(1)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 inatoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Mbarali na Madiwani katika kata sita za Tanzania Bara”.
Share:

KARIBU VANILLA VILLAGE DODOMA - 0629300200

Share:

Friday, 4 August 2023

RC MWASSA ARIDHISHWA UJENZI JENGO LA DHARURA HOSPITALI YA WILAYA KARAGWE

Na Mariam Kagenda - Kagera
Ikiwa ni mwendelezo wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo Wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa amepongeza ukamilishaji majengo ya kutolea huduma katika hospitali ya Wilaya ya Karagwe na utendaji kazi.

Akizungumza baada ya kukagua jengo hilo la huduma ya dharula Mhe. Mwassa ametoa wito kwa watumishi wa sekta ya afya kufanya kazi kwa kukidhi matakwa ya wananchi ikiwemo kuwapa huduma bora na kuwaelewesha juu ya umuhimu wa kupata huduma za matibabu kwa wakati.


Amesema kuwa anawapongeza kwa usimamizi mzuri pamoja na usafi wa Mazingira ya Hospital nzima ikiwemo utunzaji wa miundombinu ambapo hospitali nyingi ukitembelea unakuta Mazingira hayaridhishi.


Serikali kupitia TAMISEMI imetoa fedha shilingi bilioni 3.5 kuhakikisha wanakuwa na hospitali ya kisasa ambayo haiwatofautishi na hospitali nyingine zilizoko Mwanza, Dar es salaam na Dodoma kinachotakiwa ni kufanya kazi kwa kukidhi matakwa ya wananchi.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ambayo imewaondolea kero wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wamesema wanaridhishwa na huduma zinazotolewa katika Hospitali hiyo na hakuna wasiwasi, ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo walilazimika kufuata huduma nyingi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo Mwanza.

Wamesema kuwa kipindi cha nyuma changamoto kubwa ilikuwa ni kupata huduma nzuri za afya ambapo kwasasa Serikali imerahisisha huduma zote za upasuaji, masuala ya upumuaji hakuna tofauti tena kati ya Bugando na Karagwe, kwa ujumla wananchi naridhishwa na huduma zote zinazotolewa, changamoto ndogondogo za uwepo wa watumishi wanaamini Serikali itazitatua.

Katibu wa Hospitali, Samson Hingi ameeleza kuwa ujenzi wa Hospitali hiyo ulianza mwaka 2019 na kwasasa huduma nyingi zinapatikana hospitalini hapo hivyo gharama za wananchi kupewa Rufaa na kufuata huduma za afya mbali zimepungua. Mpaka sasa asilimia 60 ya vifaa tiba vya kisasa vimefungwa na wagonjwa wanapata huduma nzuri.
Share:

RC FATMA MWASSA ATEMBELEA NA KUKAGUA SHULE MPYA NYAKAHITA

Na Mariam Kagenda - Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amefanya ukaguzi ujenzi wa vyumba 16, jengo la utawala na matundu 18 ya vyoo shule mpya ya awali na Msingi Nyakahita iliyopo Kata ya Kanoni wilaya ya Karagwe Mkoa wa Kagera.


Akiongea na wananchi wa kata hiyo mara baada ya kukagua ujenzi wa shule amewataka wananchi waendelee kumtumia Mbunge ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa katika kuwaletea maendeleo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye dira yake ni kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata elimu bure

Mhe. Mwassa amesema kuwa anaona leo wanaweza kuwa na madarasa mazuri mwanafunzi wa chekechea kutembea umbali wa kilometa 8 kwenda na kurudi sawa na kilometa 16 sio suala la kawaida kwa mtoto wanachoka sana , sasa Serikali imewasikia kinachobaki ni kuhakikisha watoto wote katika kijiji hicho wanapata haki yao ya kusoma na kuzifikia ndoto zao.


Mkuu wa wilaya ya Karagwe, Mhe. Julius Laizer ameeleza kuwa kutokana na wananchi wa Kijiji hicho kuwa na uhitaji wa shule mara baada ya kupokea fedha kutoka Serikalini walijitoa kushiriki katika ujenzi wa shule hiyo kwa kuchimba msingi, kusafisha eneo na kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.


Naye mmoja wa wananchi wa kijiji cha Nyakahita Novath Ndibalema amesema kuwa kabla ya ujenzi huo wananchi waliamua kujenga vyumba vya udongo ili kuwanusuru watoto wadogo ambao walitembea umbali mrefu kwenda shule kwani wanafunzi hao walilazimika kuamka saa 10:30 alfajiri ili kuwahi masomo hivyo ukamilishaji wa shule hiyo na usajili wa wanafunzi utarahisisha mwendo kwa watoto wao na kupunguza wasiwasi ambapo watakaosajiliwa katika shule hiyo wanaotoka mbali hawatazidi kilometa moja.


Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Nyakahita Mtungi Tirutangwa ameeleza kuwa shule mama ina wafunzi 1765 kuanzia darasa la nne hadi la saba na shule shikizi ina wanafunzi 218 kuanzia chekechea hadi darasa la tatu huku ufaulu wa shule hiyo ni asilimia 60, hivyo anaamini uwepo wa shule mpya utaongeza ufaulu.

Share:

TIKTOK YASITISHWA KWA MUDA USIOJULIKANA SENEGAL



Mamlaka ya Senegal ilisimamisha ombi la TikTok Jumatano hadi “taarifa zaidi” kutokana na kueneza jumbe za “chuki na uasi” kufuatia maandamano ya kupinga kufungwa jela kwa kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko siku ya Jumatatu.

Tayari walikuwa wamekatiza ufikiaji wa mtandao kwenye simu za mkononi Jumatatu

“Imebainika kuwa TikTok ni mtandao wa kijamii unaopendelewa na watu wenye nia mbaya kusambaza jumbe za chuki na uharibifu zinazotishia utulivu wa nchi,” alisema Moussa Bocar Thiam, Waziri wa Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali, katika taarifa.

Kuzuiliwa kwa Bw Sonko mnamo Jumatatu kwa mashtaka mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuitisha uasi, kulizua maandamano. Watu watatu waliuawa kusini mwa nchi na katika vitongoji vya Dakar.

Watu wengine wawili waliuawa siku ya Jumanne huko Dakar katika shambulio la kifaa cha kichomaji kwenye basi walilokuwa wakisafiria, bila uhusiano wowote wa wazi kuanzishwa kati ya shambulio la basi na maandamano ya kupinga kufungwa kwa Bw. Sonko.

Siku ya Jumatatu, Amnesty International ilishutumu vikwazo kwenye mtandao kama “mashambulizi dhidi ya uhuru wa habari” na kutoa wito kwa mamlaka “kurejesha mtandao”.

Kwa utaratibu huu wa tatu, ambao unakuja juu ya hukumu zingine mbili, Bw. Sonko, aliyetangazwa mgombea katika uchaguzi wa urais wa 2024, hatari, kulingana na wataalam wa sheria, kifungo cha miaka mitano hadi 20 jela.

Mwanasiasa huyo, ambaye aliibuka wa tatu katika uchaguzi wa urais wa 2019, alihukumiwa Juni 1 katika kesi nyingine kifungo cha miaka miwili jela. Kuhukumiwa kwake kulizua machafuko makubwa zaidi katika miaka ya Senegal, ambayo yalisababisha vifo vya watu kumi na sita kulingana na mamlaka, na karibu thelathini kulingana na upinzani.

Share:

BSL COLLEGE KAHAMA YATANGAZA NAFASI ZA USAJILI WA KOZI YA UALIMU MALEZI AWALI

Share:

e-GA YASHAURI TAASISI KUTUMIA MFUMO WA TEHAMA

 



Picha za Matukio mbalimbali ya wananchi wakipatiwa Elimu na  huduma mbalimbali katika Banda la Mamlaka ya Serikali Mtandao lililopo katika viwanja vya John Mwakangale-Nanenane jijini  Mbeya.

Na Mwandishi maalum, Mbeya 

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) inashiriki Maonesho ya kimataifa ya Nanenane mwaka 2023 kwa lengo la kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu kazi na Majukumu ya mamlaka.

Kupitia maonyesho hayo imezitaka  Taasisi za umma kutumia TEHAMA katika utoaji wa huduma zao ili kumrahisishia mwananchi kupata huduma hizo kwa urahisi na gharama nafuu

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA AUGOSTI 4,2023





























Share:

Thursday, 3 August 2023

WATANZANIA WAKO TAYARI UWEKEZAJI WENYE TIJA NA MABADILIKO BANDARINI - CHONGOLO

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo akiwahutubia Maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara Uwanja wa CCM Kirumba,jijini Mwanza mwishoni mwa wiki.

*********************

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo amesema Watanzania kwa ujumla wao wameonesha utayari na uhitaji mkubwa wa kuona uwekezaji na uendeshaji utakaoleta maboresho, ufanisi na kuongeza mapato katika Bandari ya Dar Es Salaam, hivyo ameielekeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kuharakisha utekelezaji wa hatua mbalimbali zilizobakia za uwekezaji bandarini hapo, ili wananchi waanze kuona matokeo.

Ndugu Chongolo amesema kuwa CCM inatambua kuwa wapo Watanzania wenye nia njema na mapenzi mema kwa nchi yao, ambao wametoa maoni ya aina mbalimbali yanayolenga kuboresha mkataba wa uwekezaji katika Bandari ya Dar Es Salaam, ambapo amesema maelekezo ya Chama kwa Serikali ni kuhakikisha mawazo ya wananchi hao yanachukuliwa na kufanyiwa kazi ili yasaidie kupatikana kwa tija na matokeo makubwa zaidi yanayotarajiwa kwa ajili ya maendeleo ya watu na ustawi wa Tanzania.

Ndugu Chongolo ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano mkubwa uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Jumapili Julai 30, 2023, wakati akihitimisha ziara yake iliyotumika kuwapatia elimu wananchi kuhusu makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, yanayolenga kuweka msingi wa uwekezaji katika Bandari ya Dar Es Salaam ili kuboresha utendaji na ufanisi wa kazi bandarini hapo.

“Msimamo wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu uwekezaji wa bandari ni kuitaka serikali kuhakikisha kasi ya utekelezaji wake iende kwa haraka iongezwe ili tuanze kupata manufaa na matokeo kwa haraka. Tunasema hivyo kwa sababu msingi wake ni Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020/25 tuliyoinadi na kupitishwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na kwetu kwenye suala la utekelezaji wa ilani mtu yeyote akitaka kutukwamisha ni lazima tusimame kuwa kitu kimoja tushikamane tuhakikishe haturuhusu fitina, hila, maneno ya uchokozi ili tusifanikishe hilo na kwenye hili wana CCM wameonesha kwa dhati kabisa kulikubali na kuwa kitu kimoja, niwashukuru sana.

“Wananchi na wanaCCM wameonesha utayari mkubwa sana, wameonesha uhitaji mkubwa wa kuona mabadiliko na tija tunayoizungumzia kwenye uwekezaji wa bandari ikitokea kwa haraka, niwapongeze sana kwenye maeneo yote tuliyopita. Chama Cha Mapinduzi tunasema hili ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020/25 kwa sababu kwenye ibara ya 22 na 59 tumeahidi na tulieleza kwa kina mpango wa suala hilo. Msimamo wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu uwekezaji wa bandari ni kuitaka Serikali kuhakikisha kasi ya utekelezaji wake iende kwa haraka iongezwe ili tuanze kupata manufaa na matokeo kwa haraka,” amesema Ndugu Chongolo na kuongeza;

"Chama Cha Mapinduzi kinaisisitizia serikali kuweka msukumo katika hatua zinazoendelea ili kama kuna jambo au maoni ya kuongeza tija kwenye kuboresha mkataba yachukuliwe yawekwe ili kutupeleka kwa spidi kule tunapotaka. Sasa kuna watu wametoa maoni ya aina mbalimbali kuna watu wamesema uwekezaji huu ni muhimu sana lakini kwenye ule mkataba kuwe na mambo kidogo yanayoendana na kile wanachokipendekeza, hayo ndiyo mawazo ya msingj yenye tija.

“Na sisi CCM tunaiagiza serikali pia kuhakikisha inatekeleza hilo na kufanya mapitio kuangalia mazingira na kuona umuhimu wa kuyaruhusu mawazo yenye tija kuingia na kuchangia uboreshaji wa mkataba huu ili utufikishe kule ambapo tutapata tija na matokeo makubwa zaidi. Tunasema hivyo kwa sababu mkataba sio Msahafu wala Biblia, hatuwezi kushikilia tukasema aah hauna dosari…hapana, umeandikwa na wanadamu, macho na elimu vinatofautiana na elimu inatofautisha watu kuona mambo kwa namna tofauti,” amesema Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Chongolo.

Katika ziara hiyo ya kuwaelimisha Watanzania kuhusu uwekezaji unaolenga kuboresha utendaji na ufanisi wa Bandari ya Dar Es Salaam, aliyoihitimisha Mwanza, baada ya kufanya mikutano mikubwa iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi kwa kuanzia Mbeya, Mtwara, Tanga, Arusha, Singida, Kigoma, Dar es Salaam na hatimae Mwanza, Ndugu Chongolo aliambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa – Oganaizesheni, Ndugu Haji Issa Usi Gavu, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ndugu Stephen Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Mhe. Jerry Silaa (Mbunge wa Ukonga) na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Wakili Albert Msando.

Mbali ya kuielekeza Serikali kuzingatia na kufanyia kazi maoni chanya na yenye tija yanayotolewa kuboresha uwekezaji, Katibu Mkuu Ndugu Chongolo pia ligusia uwepo kwa kundi dogo la wanasiasa na wanaharakati wanaopita na kutumia majukwaa mbalimbali kufanya upotoshaji na kufanya uchonganishi, wakilenga kupinga suala hilo muhimu lenye maslahi makubwa kwa taifa lisifanyike na baada ya hoja zao zote kujibiwa, sasa kundi hilo limeanza kutumia lugha za matusi dhidi ya viongozi wakuu wa nchi, waliopo madarakani, waliostaafu na wale waliotangulia mbele ya haki.

"Kuna kundi la pili ambalo lenyewe linapinga tuu…mwanzo lilianza kwa kukosoa mkataba. Baada ya kuona kwenye mkataba wanakosa eneo la msingi la kusimamia sasa wamebadilika wanaenda wanasema hakuna uwekezaji huu kufanyika, eti hauna tija. Maana yake ni nini…maana yake CCM tusitekeleze ilani yetu kwa kiwango cha juu chenye tija ili wakija wawe na kazi rahisi ya kuichonganisha CCM na wananchi wasitupatie ridhaa kwa mara nyingine. Sasa nani yupo tayari kuchonganishwa? Hatupo tayari. Tuliahidi na tutatekeleza kwa hiyo serikali lazima itekeleze kwa kishindo.

"Sasa hawa jamaa wamegundua msimamo wetu umenyooka na hatuyumbi wameamua sasa kuanza matusi na wanatukana kweli, hadi mara nyingine unajiuliza huko duniani kuna chuo kinachotoa shahada ya matusi? Kwa sababu ukiangalia namna wanavyopanga na kuyasema vizuri hayo matusi unajiuliza hawa wenzetu hii professional (taaluma ya kutukana) wameisomea wapi,” amesema Ndugu Chongolo, na kurudia tena wito wake alioutoa mara kadhaa, hasa katika mikutano ya Tanga, Arusha, Singida na Dar Es Salaam, kuwataka wanaCCM kuonesha ukomavu wa Chama chao, kwa kutojibu matusi, bali wasimame imara kutekeleza dhamana ya kuongoza nchi;

"Ndugu zangu niwaombe sana CCM ni kubwa mno na ina historia kubwa na heshima kubwa barani Afrika na dunia nzima kwa ujumla tusihangaike kuingia kujibizana nao sisi tuna kazi kubwa ya kujenga nchi yetu, kuratibu maendeleo ya Watanzania na kutatua changamoto za wanachi, tukianza kuhangaika na matusi wanayotoa tutaondoka kwenye reli na baadae mambo yetu hayatakaa vizuri ni lazima tusimame imara, tunyooshe mguu tuhakikishe tunafikia tija ile tuliyoaihidi kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/25. Matusi kwetu tuachane nayo, tuyadharau na ndugu zangu kila mmoja huchagua kile ambacho anakiweza, sisi tumeamua kufanya kazi kwa bidii, wao wameamua kututukana tuwaache, walichagua huko kwa sababu ndio kazi wanayoiweza na sisi watuache tuendelee kujenga nchi sababu ndio kazi tunayoiweza, CCM OYEE.

“Hawa jamaa wa upinzani wametukana sana watu juzi wakiwa huko Bukoba na walianza kutukana viongozi wetu wastaafu marais wetu, wamemtukana sana Hayati Benjamini Mkapa, wamemtukana sana mzee wetu Jakaya Kikwete, wakamtukana sana Hayati John Magufuli na wakamtukana sana Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wote nyinyi ni mashahidi na mmewasikia matusi makubwa, matusi ya ajabu yasiyo na staha na sisi pia tuliwasikia"

"Majibu yetu kwao kama Chama Cha Mapinduzi ni…tunawashukuru sana kwa matusi yao hatuna muda wa kuwajibu hiyo ndiyo heshima waliyojijengea na hiyo ndio hadhi yao kukosa heshima na kuishiwa sera. Sisi kazi yetu ni maendeleo na matusi yetu ni kuisimamia serikali kuhakikisha inatekeleza ipasavyo ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2020/25,” amesema Katibu Mkuu Chongolo.

Aidha, Ndugu Chongolo aliwaambia maelfu ya wananchi hao kuwa kuwepo kwa kundi la watu wanaopinga kila jambo kubwa, lenye malengo mazuri ya kuimarisha misingi ya kujenga mazingira ya fursa za maendeleo ya watu na ustawi wa Tanzania, haijaanza kwa mradi wa uwekezaji wa Bandari ya Dar Es Salaam, akitolea mifano ya jinsi baadhi ya wanaharakati na wanasiasa wa vyama vya upinzani kwa kushirikiana na watu kutoka nje ya Tanzania walivyowahi kupinga miradi mingine ya uwekezaji mkubwa wenye manufaa ya nchi, ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR) na Bomba la Mafuta la Uganda – Tanzania.

“Labda mnadhani kwamba upingaji wa maendeleo umeanzia hapa kwenye suala la uwekezaji wa bandari leo…niwapitishe kidogo miaka ya nyuma serikali iliwahi kufanya maamuzi ya kujenga mradi wa kuzalisha umeme katika mto Malagalasi. Baada ya uamuzi huo wakaja jamaa wanaitwa Jumuiya ya Kimataifa na wataalamu wa huko duniani wakisema wao ni wataalamu wa viumbe hai na viumbe adimu wakatuambia tukitekeleza mradi pale mto malagalasi kuna samaki wadogo kwa dagaa yaani wale dagaa mnaowajua sasa samaki hao ni wadogo kuliko hata dagaa.

“Lakini samaki hao hawafai hata kwa mboga wala chochote lakini wakasema tukiweka huo mradi samaki hao watapotea, tukawasikiliza tukasema labda jambo la ukweli lakini mpaka leo hii mniambie hapa mmewahi kusikia kuna pesa imekuja kusaidia nchi yetu ili tuwalinde wale samaki? Yaani samaki wasiofaa kwa mboga wale chochote walikuwa bora kuliko Watanzania kupata umeme. Kuanzia hapo tuliweka nukta kwamba wakija na jambo lolote watusikilize sisi na sio kusikiliza ya kwao zaidi.

“Changamoto ya umeme ilikuwa kubwa tukaenda kujenga Bwawa la Kihansi kule Morogoro. Tulipoanza wakaja wakasema mpango wenu utapoteza vyura adimu duniani. Yaani vyura wenyewe lazima uwaangalie kwa darubini ndiyo unaweza kuwaona halafu eti tuache kujenga bwawa lituzalishie umeme tutunze vyura. Tukawaambia akili za kuambiwa tunachanganya na zetu hivyo hilo tumeligundua na tukasimamia msimamo wetu na kujenga Bwawa la Kihansi. Leo hii umeme tunaoutumia sehemu yake unachangiwa na Bwawa la Kihansi. Tuliwaambia toeni vyura wahifadhiwe pembeni gharama ya kuhifadhi vyura haiwezi kuwa kubwa kuliko Watanzania kukosa umeme wa uhakika"

"Tulipokuja kwenye bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Mkoani Tanga wakaibuka na kubeba mabango wanasema mradi utahatarisha mazingira. Tulisimama na leo mradi unaendelea na wana Kanda ya Ziwa hii ni sehemu ya wanufaika wa mradi huo…CCM OYEE.

“Tulienda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere kule Mto Rufiji…nyinyi ni mashahidi uamuzi wa kujenga bwawa ulifanywa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere miaka ya 70, muda mwingi tumekuwa tukitafuta namna ya kutekeleza ule mradi, mwaka 2016/17 uamuzi ukafanyika mpango wa ujenzi ukaanza na tukaweka mazingira yote sawa lakini jamaa hawakukaa kimya wakaja kusema Hifadhi ya Selous ni maalum, tukijenga bwawa itaharibika na mazingira yataharibika na tutaiondosha kwenye vivutio vya dunia, Serikali ya CCM tukalikataa hilo na kufanya uamuzi wa kujenga na tukabadilisha jina la hifadhi kuita Mwalimu Nyerere ili vivutio vitokane na jina jipya na kujengwa na yaliyopo katika jina jipya. Leo hii tunasubiria zaidi ya megawati 2000 za umeme hayo ndio mambo ya watu wanaofikiria kwa ajili ya wananchi, walitaka tukose umeme tuendelee kuwa kwenye mgao.

"Hata wakati tumeanza ujenzi wa reli ya umeme (SGR) bado walikuwa na lengo la kutukwamisha kuanzia mchakato ulivyokuwa umeanza. Zabuni ilipotangazwa, walijitokeza wengi sana, lakini wakajitoa wote ili tu kutukwamisha. Lakini leo hii SGR imekuwa hadithi inayoenda kutimia kwa vitendo nchini. Utaweza kusafiri kutoka Dar Es Salaam hadi Kigoma kwa masaa kadhaa na hii ndio kazi kubwa inayotokana na misimamo ya CCM kwa Serikali kutekeleza Ilani ya CCM ya uchaguzi, wenye hila tusihangaike kupoteza muda nao.”

Katibu Mkuu Chongolo amesema lengo la watu wanaopinga hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tanzania katika kuimarisha misingi ya maendeleo ya watu wake na ustawi wa taifa, hasa ni kutotaka CCM itekeleze ilani yake kikamilifu, hali ambayo itawakosesha wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wachache agenda wakati wa uchaguzi, pia ni kutaka kuikwamisha nchi ili iendelee kuwa tegemezi kwenye mifumo ya kinyonyaji na ukandamizaji ya kidunia, jambo ambalo alihitimisha kwa kusema “Kwenye hilo wana bahati mbaya tulishavuka, tupo mbali sana.”
Maelfu ya Wananchi kutoka kila kona ya jiji la Mwanza na baadhi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa wakiwa wamekusanyika katika uwanja wa CCM Kirumba kwenye mkutano wa Hadhara wa Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo uliofanyika mwishoni mwa wiki

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Chato Mhe.Dkt Medard Kalemani wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.


Katika mkutano huo Komredi Chongolo na ujumbe wake walieleza na kufafanua hatua kwa hatua kuhusu uamuzi wa Serikali kuingia makubaliano ya uwekezaji wa kuboresha uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, lengo likiwa kuhakikisha bandari hiyo inatoa huduma kwa ufanisi mkubwa tofauti na ilivyo sasa, ambayo ni Sehemu ya Utekelezaji wa Vitendo wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025.

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo akitafakari jambo kabla ya kupanda jukwaani kuwahutubia wananchi waliokuwa wamefurika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa wiki
Mwasisi wa Kampuni ya TICTS Nazir Karamagi akizungumza mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Komredi Daniel Chongolo katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Julai 30,2023, jinsi anavyounga mkono uwekezaji mpya wa Bandari ya Dar es Salaam baada ya Kampuni yake kumaliza mkataba wa uendeshaji wa Bandari hiyo.Pichani kushoto ni Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo akipeana mkono na Muasisi wa Kampuni ya TICTS Nazir Karamagi mara baada ya kuzungumza mbele ya Katibu Mkuu huyo wa CCM na Maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mwishoni mwa wiki Julai , jinsi anavyounga mkono uwekezaji mpya wa Bandari ya Dar es Salaam baada ya Kampuni yake kumaliza mkataba wa uendeshaji wa Bandari hiyo.



Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo akiwahutubia Maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara Uwanja wa CCM Kirumba,jijini Mwanza mwishoni mwa wiki
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo akifurahia jambo na Muasisi wa Kampuni ya TICTS Nazir Karamagi mara baada ya kuhutubia Maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara Uwanja wa CCM Kirumba,jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. PICHA ZOTE NA MICHUZI JR @michuzijr.



Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger