Saturday, 8 July 2023

WANANCHI KARAGWE WAMSHUKURU RAIS SAMIA KWA MIRADI YA KIMKAKATI...BASHUNGWA ATIA NENO

Na Mariam Kagenda _ Karagwe

Wananchi wa wilaya Karagwe wametoa Salamu za shukrani na Pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi mikubwa ya kimkakati kila sekta iliyojengwa na inayoendelea kutekelezwa ndani ya wilaya Karagwe mkoa Kagera.


Salamu hizo zimetolewa na Wananchi katika nyakati tofauti wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ya kukagua miradi ya maendeleo na kuongea na wananchi katika kata za Bugene, Nyakakika, Igurwa na Kanoni.


Wananchi wamemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuridhia na kutoa shilingi bilioni 70 kwa ajili utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Lwakajunju ambao tayari umeishaanza kutekelezwa.


Aidha, Wamemshukuru Rais samia kwa kutoa shilingi bilioni 4 kujenga shule maalum ya Sayansi wa Wasichana katika eneo la Rwambaizi kata ya Kanoni ambayo ipo katika hatua za Ukamilishaji ili kuanza kupokea wanafunzi kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.

Katika Sekta ya Miundombinu, Wamemshukuru kwa Ujenzi wa barabara za lami zitakazofungua uchumi wa wilaya ambazo ni barabara ya Karagwe - Nyaishozi mpaka Benako inayoendelea kujengwa, ujenzi kiwango cha lami barabara za Omugakorongo-Igurwa-Murongo ambayo ipo katika maandalizi ya kuanza utekelezaji.


Kadhalika, Barabara ya Omurushaka-Kaisho-Murongo ambayo ipo katika hatua za mwisho za kusaini mikataba na Kipande korofi cha barabara ya Nyakahanga-Bushangaro eneo la "Kujura Nkeito" kimewekwa lami na eneo korofi la "Bigoro" mkandarasi ataanza kazi ya ujenzi wa kilometa 2 za lami. 

Vile vile, Wameshukuru kwa Ujenzi na ukamilishaji wa Hospitali ya Wilaya Karagwe ambayo inaendelea kutoa huduma pamoja na ujenzi wa kituo cha afya cha Kibona kwa ajili ya tarafa ya Kituntu, ujenzi wa kituo cha afya katika tarafa ya Nyabiyonza utakaoanza katika bajeti ya mwaka huu wa 2023/24. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa amewahakikishia Wananchi wa Jimbo la Karagwe kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwatumikia kwa jitihada kubwa na unyenyekevu mkubwa.


Share:

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA INDIA ATEMBELEA DIT


Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imepongezwa kwa kuwa miongoni mwa Taasisi za Elimu Tanzania yenye ushirikiano mwema na nchi ya India kwenye masuala ya Teknolojia ya habari na mawasiliano.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya nje wa India Dkt.Sabrahmanyam Jaishankar katika ziara yake DIT alipotembelea kituo cha Umahiri cha Tehama (ITCoEICT) kwa ajili ya kuona maendeleo ya Tehama yaliyofikiwa.


Katika ziara yake Mh Waziri amefurahishwa kusikia mafanikio yaliyofanyika kwenye kituo ikiwemo kutoa elimu pamoja na huduma za Tehama kwenye sekta binafsi, Elimu,kilimo na afya pamoja na mamlaka za hali ya hewa.


"Nimefahamishwa kusikia supercomputer ambayo ni Teknolojia ya haraka kuwa zinatumika na zimeweza kusaidia baadhi ya watafiti toka Chuo kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Taasisi nyingine nyingi za elimu haya ni mafanikio makubwa kwa DIT na kwetu hivyo ninafurahi na kupongeza juhudi hizi nina uhakika juhudi hizi zinazofanyika zitasaidia kufika mbali hasa kwenye Teknolojia.amesema Dkt.Jaishankar


Dkt.Jaishankar amesema amelisikia ombi la DIT kuhusu kuboresha na kuinua zaidi supercomputer na kuahidi kulifanyia kazi kwa kuwa maendeleo ya kituo yanaridhisha na hana shaka


"Nimepewa taarifa kuhusiana na ombi lenu la kuboresha supercomputer niseme kuwa nimelipokea kwa furaha na niahidi kuwa ombi hili litafanyiwa kazi"amesema Dkt. Jaishankar


Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda amesema kuwa, Wanafunzi wanaohitimu elimu ya Sekondari na kufanya vizuri katika masomo ya Sayansi mwaka huu watapata ufadhili kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha India (IIT) kinachotarajia kuanzishwa tawi lake Zanzibar, kupitia Mfuko wa ufadhili wa Elimu wa Samia.


Waziri amesisitiza kuwa, atahaikikisha kwamba wanatoa mikopo na ufadhili wa masomo kupitia Mfuko wa Samia ili wanafunzi wakasome Zanzibar katika fani hiyo ambayo ni muhimu kwa Taifa.


"Kuanzia Oktoba au Novemba mwaka huu tunaanza kuchukua wanafunzi 50 wa shahada ya kwanza na 25 wa Shahada ya Uzamili wale wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu na kufanya vizuri sana wanaweza kuomba kusoma shahada katika chuo hiki."amesema Prof.Mkenda


Nae Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Mhandisi Dk Richard Masika amefurahishwa na ujio wa Waziri wa Mambo ya nje wa India Subrahmanyam Jaishankar alipowasili katika taasisi hiyo na kukagua kituo cha Umahiri cha Tehama (ITCoEICT) kilichoanzishwa mwaka 2009.


Amesema kituo hiki kimekuwa ni lango la teknolojia kwa kutoa huduma za tehama inayokuwa kwa kasi zaidi nchini.


Amesema ushirikiano na India ni kwa ajili ya kuboresha teknolojia ziweze kuendana na maendeleo ya tehama nchini ikiwepo katika huduma za kilimo, jeshi na utabibu kwa njia ya mtandao kwa kutumia tehama.


Dk Masika amesema hiyo itakwenda kusaidia vijana wenye mawazo mbalimbali madogo kuwawezesha kuwapa elimu ya msingi katika kuwalengesha kwenye maeneo waliojikita.


"Kwa sasa hivi kuna teknolojia mpya zimeingia ikiwepo mapinduzi ya viwanda kutoka taaluma hadi zana za kazi hivyo ujio wa taasisi ya teknolojia ya India itasaidia kupandisha ubora wa Teknolojia kwa vijana wa kitanzania wanaopita DIT kupata kwa ajili ya mafunzo".


Share:

RAIS WA KAMPUNI YA MAFUTA YA SHELL TANZANIA ATEMBELEA BANDA LA TPDC SABASABA

Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Shell Tanzania Bw. Jared Kuehl akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Julai 6,2023 katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Sabsaba Jijini Dar es Salaam.

************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

RAIS wa Kampuni ya Mafuta ya Shell Tanzania Bw. Jared Kuehl ametembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Sabsaba Jijini Dar es Salaam.

TPDC wamekuwa wakishiriki Maonesho hayo mara kwa mara ambapo wanatoa elimu kwa wananchi ambao wanatambelea banda lao ikiwemo kuwaoneha na kuwaelezea miradi mbalimbali inayoendelea kwenye Shirika hilo ikiwemo mradi wa LNG.

TPDC inawakaribisha wadau mbalimbali kuweza kuona na kujifunza Visikuku ambavyo vinasaidia kujua umri wa mwamba na mazingira ambapo mwamba ulitengenezwa baharini au nchi kavu katika uzalishaji wa mafuta na gesi.
Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Shell Tanzania Bw. Jared Kuehl akitumia hadubini kutazama visikuku vidogo vidogo vinavyopatikana kwenye miamba wakati alipotembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Julai 6,2023 katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Sabsaba Jijini Dar es Salaam.



Share:

Friday, 7 July 2023

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI JULAI 08 2023





















Share:

RC MNDEME ASHIRIKA TAMASHA LA SANJO YA BUSIYA WILAYANI KISHAPU

 






RC MNDEME ASHIRIKI TAMASHA LA SANJO YA BUSIYA WILAYANI KISHAPU

Na. Shinyanga RS.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Solomon Mndeme leo tarehe 7 Julai, 2023 ameshiriki katika Tamasha la Sanjo ya Busiya ambalo limefanyika katika Kijiji cha Negezi Kata ya Ukenyenge Wilaya ya Kishapu hapa Mkoani Shinyanga na kuwapongeza sana waandaaji kwakuwa tamasha hili limeanza rasmi tarehe 1 Julai, 2023 na linatajwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 10,000 kutoka pande mbalimbali na kwamba huu ni mwaka wa 13 tangu kuanzishwa kwa tamasha.


Pamoja na pongezi nyinhi kwa ma Chifu na uongozi wote kwa kufanikisha sherehe hizi lakini pia amewasihi kukemea kwa nguvu zote mmomonyoko wowote wa maadili ambao unaweza kuharibu jamii yetu na vizazi vyetu kwa ujumla huku akiwakumbusha watambue kazi njema anayoifanya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu, miundombinu, ustawi wa jamii huku akiwataka kumuunga mkono kwa kazi zote za kuwaletea maendeleo wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme.

"Ndugu zangu wanaTamasha la Busiya nawapongeza sana kwa kufanikisha vema sana tamasha hili muhimu ambalo limehudhuriwa na watu zaidi ya elfu kumi kutoka ndani nan nje ya Mkoa wa Shinyanga, lakini pia niwakumbushe ndugu zangu kuendelea kusimamia maadili yetu ya Kitanzania na tuendelee kumuunga mkono Rais wetu kwa kazi kubwa na njema ambazo anazifanya katika kutuletea maendeleo sisi wananchi," amesema Mhe. Mndeme.

Serikali imepokea changamoto zote zilizowasilishwa na Chifu Edward na kwamba zitashulikiwa kulingana na zilivyo kwakuwa zipo za kisera na kibajeti.
Kwa upande wake Mtemi wa Busiya Ndugu Edward Makwaiya aliipongeza sana Serikalikwa kazi inazozifanya kwa wananchi huku akiomba Serikali kuanzisha Chombo Maalumu kiwe na Mamlaka kama zilivyo Mamlaka nyingine ili waweze kuwa na maamuzi katika kuisaidia Serikali kupambana na mila potofu zenye kuharibu jamii.
Mtemi wa Busiya Ndugu Edward Makwaiya.

Aidha Mtemi Mwakwaiya alisema kuwa lengo la tamasha hili ni pamoja na kumshukuru Mungu kwa mwaka uliopita, na kukaribisha mwaka mwingine ikiwa ni pamoja na kudumisha tamaduni zetu na kuwaelimisha wananchi wote kuacha kuiga utamaduni wa nje na kuhamasisha utalii wa ndani kwa mashindano ya ngoma za jadi.
Share:

NAIBU WAZIRI KATAMBI ASISITIZA WAAJIRI WOTE KUWASILISHA MICHANGO NA TOZO MBALIMBALI KWENYE MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII WCF PSSSF NA NSSF

  NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi amewataka waajiri kote nchini kuhakikisha wanalipa Michango na tozo mbalimbali kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya WCF, PSSSF na NSSF.

Mhe. Katambi ameyasema hayo Julai 6, 2023 baada ya kutembelea mabanda ya Mifuko hiyo mitatu ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Agizo hilo la Mhe. Katambi linakuja ikiwa ni wiki chache tangu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ambaye wakati akitoa hotuba ya kuahirisha kikao cha Bunge la Bajeti alielekeza ifikapo Septemba 30 mwaka huu, Waajiri kote nchini kutoka sekta ya umma na binafsi wahakikishe wanalipa michango na tozo mbalimbali kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

“Agizo kwa waajiri wote nchini, iwe ni mamlaka za serikali, iwe ni watu binafsi hakikisheni mnapeleka michango, iwe ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), PSSSF au NSSF, mlipe kwa wakati vinginevyo tutachukua hatua kali za kisheria.” Alionya Mhe. Katambi.

Alisema kila mwezi Mamlaka za serikali zinatengewa bajeti ya kutekeleza wajibu huo wa kisheria kuwasilisha michango, hivyo wanao wajibu wa kuhakikisha wanalipa michango hiyo kwa wakati.

“Kwa sekta binafsi mtu ambaye hawasilishi michango kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ukimfuatilia vizuri ni mkwepa kodi pia, kwa hivyo inabidi tuwajue vizuri na ikibidi tutawatangaza kwenye (list of shame)”, Alionya Mhe. Katambi.

Aliwapongeza watendaji wakuu wa Mifuko hiyo, Dkt. John Mduma (WCF), CPA. Hosea Kashimba (PSSSF) na Masha Mshomba (NSSF) kwa kuleta mapinduzi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

“Kwakweli Mhe. Rasi anaona mbali sana hawa wakurugezni wa Mifuko hii, ni watu wa aina yake wameleta mapinduzi makubwa sana kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii, niliwahi kuwakaribisha wageni kutoka Kenya waliokuja kujifunza masuala ya hifadhi ya Jamii kwakweli wameshangaa sana ubora wa huduma zinazotolewa na Mifuko hii.” Alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Wakurugenzi Wakuu wa Mifuko hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema, Mifuko yote iko vizuri na itaendelea kutoa huduma kwa weledi katika kukusanya Michango na kutoa Mafao, majukumu ambayo wamekabidhiwa na serikali kuyasimamia.

“ Nataka niwahakikishie kuwa tutaendelea kuimarisha eneo la TEHAMA, ulimwengu huu sasa unatoa huduma kwa njia ya TEHAMA, Mifuko yote mitatu inawekeza kwa kasi ili kuhakikisha kwamba sehemu kubwa ya kazi zetu zinatolewa kwa njia ya mtandao ili kupunguza gharama kwa wateja wetu wawe ni waajiri au wafanyakazi wanaofuatilia Mafao yao.” Alitoa hakikisho Dkt. Mduma

Aidha Mhe. Katambi ambaye alifuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Zanzibar (ZEA) Bw.  Juma Buruhani Mohammed ambaye alisema amefarijika sana kupata fursa ya kujionea shughuli za Mifuko hiyo.

Aliwashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Sukuhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mpainduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussen Ali  Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri yanayowezesha ushirikiano mkubwa wa pande zote mbili za Muungano.

Aidha mmoja wa waajiri Bw. Isani Longo kutoka kampuni ya Elfatel Enterprises Company Limited iliyoko Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma ambaye alifika kwenye banda la WCF kupata elimu ya fidia kwa wafanyakazi alisema yeye ni mmoja wa waajiri ambao Mfanyakazi wake aliumia akiwa kazini na amepata huduma za utengamao kutoka WCF lakini pai amelipwa fidia.

“Mwanzo nilijisajili kwa kutekeleza sheria (compliance) lakini leo nimefika hapa na baada ya kujua kwa undani WCF wanafanya nini, kwakweli nimebaini kuwa kiwango tunacholipa ni kidogo sana cha asilimia 0.5 ya mshahara wa mfanyakazi, ukilinganisha na faida anayopata mfanyakazi endapo atapatwa na madhila akiwa kazini.” Alisema.

Bw. Longo aliwaasa waajiri kutekeza wajibu wa kisheria wa kujisajili kwani kiwango ambacho mwajiri anatakiwa kuchangia ni kidogo sana.

“Kama kila mwajiri akijua kazi ya WCF na dhamira iliyoko mbele, ataona umuhimu wa kutokuwa msumbufu na kutekeleza wajibu wake ili kuhakikisha anajisajili na Mfuko. Alisema.

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi (wapili kushoto) akimpongeza Mwajiri ambaye ni Mwanachama wa WCF, Bw. Isani Longo kutoka kampuni ya Elfatel Enterprises Company Limited iliyoko Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma ambaye alifika kwenye banda la WCF kupata elimu ya fidia kwa wafanyakazi. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma ( wapili kulia) na  Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Zanzibar (ZEA) Bw.  Juma Buruhani Mohammed 
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi  akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Mhe. Katambi akishuhudia jinsi wanachama wa WCF wanavyohudumiwa.


Share:

WAZIRI GWAJIMA ATOA WITO KWA UMOJA WA WANAWAKE VIONGOZI AFRIKA KUFIKIA JAMII



Na.Mwandishi Wetu_ARUSHA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka nchi za kiafrika kuongeza ushiriki wa wanawake katika majukwaa ya maamuzi ikiwa ni moja ya njia za kuelekea kwenye usawa wa kijinsia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa AWLO jijini Arusha Julai 06, 2023 Dkt. Gwajima amesema kuwa moja ya vikwazo vikuu kufikia usawa wa kijinsia ni sekta ya elimu kwani wanawake hawapati nafasi sawa ya kujiendelea kielimu.

Ameshauri kuongeza fursa sawa za kupata elimu kwa wanawake na wanaume ili kufikia malengo ya kuwa na usawa wa kijinsia katika nchi za Afrika.

Dkt. Gwajima amezungumzia fursa za kiuchumi kuwa na nafasi kubwa katika kufikia malengo ya usawa wa kijinsia kwani jamii yenye uchumi imara inaweza kutoa fursa sawa kwa jinsia zote katika elimu, biashara na fursa nyingine zinazopatikana kwenye jamii husika.

Pamoja na mambo mengine Dkt. Gwajima amebainisha kuwa kufikia usawa wa kijinsia siyo suala la kuchagua bali ni swala la lazima na kwamba kila nchi iangalie namna ya kuondoa vikwazo vyote vinavyosababisha kuchelewesha kufikia usawa wa kijinsia na kuviondoa.

Awali akiwakaribisha washiriki wa mkutano huo, mwanzilishi na rais wa AWLO (African Women in Leadership Organization) Dkt. Elisha Attai amesema kuwa kwa sasa bado wanawake wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazosababisha washindwe kufikia mafanikio katika majukumu wanayotekeleza kila siku kwenye kazi zao kwa sababu tu ni wanawake.

Mkutano wa Wanawake katika Uongozi unafanyika Jijini Arusha kwa siku tatu kuanzia tarehe 6 hadi 8 Julai 2023 ambapo washiriki watajadili hatua zilizofikiwa kuelekea usawa wa kijinsia, changamoto zilizopo na namna bora ya kuzitatua.
Share:

NAIBU WAZIRI AWABANA WAWEKEZAJI WANAOKIUKA SHERIA ZA KAZI

Naibu Waziri – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na wawekezaji wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa mbalimbali za chuma cha Steel Master Limited kilichopo Chang’ombe Dar es salaam alipofanya ziara akiambatana na viongozi mbalimbali wa taasisi zilizochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo OSHA kwa lengo la kukagua utekelezaji wa sheria mbalimbali za kazi.

****************

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, amefanya ziara katika viwanda vya Mkoa wa Dar es Salaam ambapo ameeleza kutoridhishwa na hali ya utekelezaji wa Sheria za Kazi, Usalama na afya pamoja na hifadhi kwa jamii katika baadhi ya viwanda.

Akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya na uzingatiaji wa sheria za kazi katika kiwanda cha Colourful Industry Limited kilichopo Buza-Temeke jijini Dar es Salaam kinachozalisha bidhaa za plastiki ikiwemo mifagio na vifungashio, Naibu Waziri Katambi, ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kushughulikia changamoto mbali mbali za wafanyakazi ndani ya siku 14.

“Nimetembelea sehemu mbali mbali za uzalishaji katika kiwanda hiki na kubaini ukiukwaji mkubwa wa taratibu za usalama na afya mahali pa ikiwemo wafanyakazi kutopatiwa vifaa vya kujikinga na vihatarishi vya magonjwa na ajali. Hali ya mazingira ya kazi sio nzuri kuna mzunguko finyu wa hewa na hata mwanga hautoshelezi,” amesema Katambi na kuongeza:

“Aidha kuna ukiukwaji wa haki nyingine za wafanyakazi ikiwemo ujira mdogo, wafanyakazi kulazimishwa kufanya kazi kwa zaidi ya masaa yanayoruhusiwa kisheria bila kupatiwa malipo ya ziada pamoja na kutowasilisha michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi kwa jamii.”

Aidha, Katambi alitembelea kiwanda cha Steel Masters Limited kilichopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam kinachozalishaji bidhaa za chuma na kufanya ukaguzi wa maeneo ya uzalishaji pamoja na masuala mengine yanayohusu utekelezaji wa sheria za kazi, usalama na afya na hifadhi kwa jamii.

Akiwa katika kiwanda hicho halikadhalika alibaini mapungufu katika utekelezaji wa sheria tajwa ikiwemo wafanyakazi kutokingwa na kilele zinazalishwa na mitambo pamoja na taarifa zisizojitosheleza kuhusiana na uwasilishwaji wa michango katika mifuko ya hifadhi kwa jamii.

Naibu Waziri huyo mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi aliwaagiza maafisa kutoka Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kurudi tena katika kiwanda hicho kwa ukaguzi zaidi na kushauri namna bora zaidi itakayowezesha kiwanda hicho kutekeleza sheria za kazi, usalama na afya pamoja na hifadhi kwa jamii.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya Steel Masters Limited, Gajendra Narendra, amemshukuru Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika kiwanda chao na kutoa ushauri na maelekezo mbali mbali.

“Tupo tayari kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, tunamuahidi kwamba tutayafanyia kazi kwa mwongozo wa wataalam wake na tupo tayari kumwalika tena baada ya kukamilisha maboresho hayo,” ameeleza Bw. Narendra.

Taasisi zilizoambatana na Naibu Waziri Katambi katika ziara hiyo ni pamoja na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), NSSF, WCF pamoja na Idara ya Kazi.



Naibu Waziri – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi Pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi zilizochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakizungumza na mfanyakazi wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa mbalimbali za plastiki cha Colourful Industries Limited walipofanya ziara katika kiwanda hicho kwa lengo la kukagua utekelezaji wa sheria mbalimbali za kazi Pamoja na mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi.



Baadhi ya Wafanyakazi wa Kiwanda cha kuzalisha bidhaa mbalimbali za plastiki cha Colourful Industries Limited wakimsikiliza Naibu Waziri – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi mara baada ya wafanyakazi hao kutoa kero mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wakitekeleza shughuli zao kiwandani hapo.



Meneja wa Kanda ya Pwani wa OSHA,Mhandisi George Chali (wakwanza kushoto- waliosimama) akitoa ripoti fupi ya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi aliofanya wakati wa ziara ya Naibu Waziri – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi zilizochini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya kutembelea kiwanda hicho.



Naibu Waziri – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi akitoa maelekezo kwa wawekezaji wa kiwanda cha chuma cha Steel Master Limited kuhusu uboreshaji wa mifumo ya usalama na afya katika baadhi ya maeneo ya kiwanda hicho yaliyobainika kuwa na mapungufu.



Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger