Wednesday, 5 July 2023

SEKTA YA MADINI IMECHANGIA ASILIMIA 56 MAUZO YA BIDHAA NJE YA NCHI

    
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, amesema kuwa mchango wa Sekta ya Madini katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni umekuwa ukiimarika ambapo kwa mwaka 2022 Sekta ya Madini imechangia asilimia 56 ya mauzo yote ya bidhaa zilizouzwa nje ya nchi.



Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Mbibo leo Julai 5, 2023 alipotembelea wadau mbalimbali wa madini katika banda la Wizara ya Madini katika Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.


Aidha, amewataka wadau kuzitumia taasisi zilizo chini ya wizara Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ili Sekta ya Madini iweze kuchangia zaidi katika Pato la Taifa.


Katika hatua nyingine, Mbibo amezungumza na wadau wa Sekta ya Madini waliopo katika banda hilo ambao wamemweleza huduma wadau wanazotoa, fursa zilizopo katika maeneo ya shughuli zao.


Naibu Katibu Mkuu Mbibo aliongozana na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba na wadau wengine wa Sekta ya Madini.
Share:

BARRICK NORTH MARA RUNNERS CLUB KUSHIRIKI CAPE TOWN MARATHON 2023

Baadhi ya wakimbiaji wa klabu ya Barrick North Mara Runners Club wakifurahi baada ya kumaliza kushiriki kukimbia katika mbio za Lake Victoria Marathon zilizofanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
Baadhi ya wakimbiaji wa klabu ya Barrick North Mara Runners Club wakifurahi baada ya kumaliza kushiriki kukimbia katika mbio za Lake Victoria Marathon zilizofanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
Baadhi ya wakimbiaji wa klabu ya Barrick North Mara Runners Club wakifurahi baada ya kumaliza kushiriki kukimbia katika mbio za Lake Victoria Marathon zilizofanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
Baadhi ya wakimbiaji wa klabu ya Barrick North Mara Runners Club wakifurahi baada ya kumaliza kushiriki kukimbia katika mbio za Capital City Marathon zilizofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.
Kapteni wa timu ya Barrick North Mara Runners Club,Sarah Cyprian (mwenye Tshirt ya bluu) akitimka mbio wakati wa mashindano ya Lake Victoria Marathon zilizofanyika jijini Mwanza karibuni ambao aliibuka mshindi wa 4 katika mbio za kilometa 21 kwa upande wa Wanawake.

****
Wakati mchezo wa mashindano ya riadha yanazidi kuwa na mwamko mkubwa nchini, yakijumuisha watu wenye umri wa rika mbalimbali, klabu mbalimbali za marathon zimezidi kuanzishwa na baadhi yake zinazidi kuwa tishio katika mashindano mbalimbali kutokana na kuwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa.

Barrick North Mara Runners Club, inayoundwa na wafanyakazi wa mgodi wa Barrick wa North Mara, ni moja ya timu ambayo inazidi kuja juu kwa kasi ambapo kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya kwenda kushiriki, Capetown Marathon ya umbali wa kilometa 42. Mashindano ya mbio hizi yanatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini Afrika kusini.

Katika mahojiano na kapteni wa timu hiyo Sarah Cyprian karibuni, alisema timu hiyo ilianzishwa mwaka 2016 na inajumuisha wakimbiaji 66,miongoni mwao Wanaume wapo 53 na Wanawake 13.

Alisema baadhi ya mashindano ambayo klabu hiyo imeshiriki ameyataja kuwa ni Kilimanjaro International Marathon -Moshi, Capital City Marathon -Dodoma(ilitoa mshindi wa tisa wa umbali wa kilometa 21 ) , Serengeti Migration marathon 21km-Mugumu, Serengeti Safari Marathon 21km-Lamadi na Lake Victoria Marathon -Mwanza (ilitoa mshindi wa 4 kwa wanawake umbali wa kilometa 21).

Mashindano makubwa ambayo timu hiyo imeshiriki na kung’ara ameyataja kuwa ni Kilimanjaro International Marathon ambapo ilishiriki mbio za kilometa 21 na kilometa 42.Kwa mbio hizo za masafa marefu ya kilometa 42 klabu iliwakilishwa na yeye mwenyewe. (Sarah Cyprian).

Akielezea siri ya mafanikio ya klabu Sarah alisema “Kampuni ya Barrick inayo sera mathubuti katika kusaidia wafanyakazi kwenye upande wa michezo. Kwanza kwa kuwa na miundo mbinu ya mazoezi kama gym, swimming pool, uwanja wa mpira wa miguu , uwanja wa mpira wa kikapu pamoja na uwanja wa mpira wa pete. Pia inatoa vifaa na nyenzo mbalimbali za kufanyia mazoezi,vilevile kugharamia huduma zote tunapoenda kwenye mashindano nje”.

Aliongeza kusema kuwa Kampuni pia kupitia kitengo cha Afya na Usalama huwa inaandaa mashindano ya ndani kwa kushindanisha idara mbali mbali hii ni kama njia moja wapo yakuweza kuweka vizuri afya za mwili na akili za wafanyakazi wawapo kazini.

Kuhusu ni jinsi gani wanaweza kutenga muda wa kazi na muda wa kufanya mazoezi Sarah alisema “ Kila mtu ana masaaa 24 katika siku.Klabu ya North Mara Runners huwa tunatenga muda wa saa moja katika siku kufanya mazoezi.Mazoezi hayo huwa tunafanya jioni mara baada ya kutoka kazini,na mara chache ratiba zinapokuwa zinabana jioni huwa tunafanya mazoezi saa kumi alfajiri kabla ya kwenda kazini”.

Kuhusiana na changamoto wanazokutana nazo katika mazoezi na kushiriki mashindano alisema kulingana na majukumu ya kazi huwa kuna wakati ni vigumu wote kwenda kushiriki mashindano, lakini huwa wanajitahidi kutoa wawakilishi kwa ajili ya kushiriki mashindano, na kampuni huwa inawaunga mkono wakati wote.

Akitoa maoni kuhusu maendeleo ya tasnia ya mchezo wa mbio za marathon nchini alisema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mwitiko mkubwa katika mchezo wa mbio na kushauri kuwa ni vizuri kuanza maandalizi mapema kwa vijana wadogo ili kuweza kuwa na washiriki wengi katika mbio za kimataifa.Aliongeza kusema kuwa kuna wakimbiaji wengi wenye vipaji nchini kwa sasa ambao wanashiriki mashindano ya marathon mbalimbali yanayoandaliwa nchini.

Sarah alitoa wito kwa jamii kujitahidi kutenga muda hata nusu saa kwa siku kufanya mazoezi. “Mazoezi yanasaidia kuimarisha afya ya akili na mwili. Pia mazoezi yanasaidia kuweza kujikinga na magonjwa yasioambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na unene wa kupindukia”alisema.

Kuhusu malengo ya baadaye ya klabu hiyo alisema “Kauli mbiu ya club yetu ni ‘We run for fun and healthy’ hivyo basi bado tunajukumu la kuhimiza wafanyakazi wengi zaidi kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zetu, kwani mazoezi pia yamekuwa yakituweka vizuri kiakili hata kuweza kutimiza majukumu yetu kazini kwa ufanisi zaidi.Lakini pia kuweza kushiriki zaidi katika marathoni za kimataifa.”

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATANO JULAI 52023













Share:

Tuesday, 4 July 2023

VANILLA INTERNATIONAL LTD YAZINDUA SHAMBA KUBWA LA KISASA KILIMO CHA VANILLA KANDA YA ZIWA

Mkurugenzi Mwanzilishi wa Makampuni ya Vanilla International Limited, Simon Mnkondya akionesha zao la Vanilla katika Shamba kubwa la Kilimo cha Vanilla kwa njia za kisasa katika Kijiji cha Nyamikoma kata ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Na Mwandishi wetu – Malunde 1 blog

Kampuni ya Vanilla International Limited imezindua Shamba kubwa la Kilimo cha Vanilla kwa njia za kisasa Kanda ya Ziwa katika Kijiji cha Nyamikoma kata ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Jumanne Julai 4,2023 Mkurugenzi Mwanzilishi wa Makampuni ya Vanilla International Limited, Simon Mnkondya amesema katika shamba hilo la Vanilla lenye ukubwa wa hekari tatu wanategemea kupata Kilo 6000 za Vanilla kila mwaka zenye thamani ya zaidi ya Dola Milioni 2.5 kwa soko la kimataifa sawa na takribani Shilingi Bilioni 6 za Kitanzania.


“Mazao ya Vanilla katika shamba hili yamestawi kwa ustawi kwa ubora kwa sababu ya upatikanaji wa unyevu hewa wa asilimia 85% ( Humidity 85%) ambayo ni (hali ya hewa wezeshi) mazingira wezeshi ya kilimo cha Vanilla ambayo tumeitengeneza kwa kutumia umwagiliaji wa njia ya bunduki”,ameeleza Mnkondya ambaye pia Mwanzilishi wa mashamba makubwa ya kilimo cha Vanilla (Vanilla Village) yaliyopo Zanzibar, Arusha, Dodoma na Mwanza.


“Katika huu mradi ambalo ndiyo shamba kubwa Kanda ya Ziwa ambalo limelimwa kwa njia ya Mashamba kitalu/mashamba ya mahema (Green Houses). Shamba hili limetoa vanilla ambayo ni ndefu kuliko vanilla zote duniani na kuvunja rekodi ya kuwa na mita 10 kwa urefu”,ameongeza Mnkondya.


Amesema Vanilla zilizolimwa kwenye shamba hilo ni vanilla ambazo zimewahi kuzaa kuliko vanilla zote za Kanda ya Ziwa kwani zimezaa ndani ya miezi saba.

Akifafanua Zaidi amesema shamba hilo la Vanilla lilikuwa ni nusu jangwa ambapo kwa kutumia mifumo ya maji ya kisasa za Umwagiliaji wa matone na Umwagiliaji wa bunduki (Rain gun)’ umefanya hilo eneo la jangwa kutoka kuwa kavu mpaka eneo la kijani.

“Hii imetokana na kwamba tumefunika shamba kwa kutumia vifaa vinavyokata mionzi ya jua kwa asilimia 55% na hivyo kutengeneza kivuli cha 55% hali iliyosababisha mimea isiathiriwe na jua.
Katika eneo hili kulikuwa na upepo mkali ambapo tumekata upepo huo kwa kutumia vyandarua kivuli (shade net)”,amesema Mnkondya.
Mkurugenzi Mwanzilishi wa Makampuni ya Vanilla International Limited, Simon Mnkondya akiwa kwenye Shamba la Vanilla.

“Eneo hili lilikuwa na vumbi jingi linalotoka kwenye machimbo ya dhahabu, hilo vumbi limekatishwa kwa kutumia vyandarua vivuli. Vumbi hili lingeathiri mimea kwa kuziba matundu hewa (stomatas) ambayo inatumika kwa ajili ya kutoa hewa ukaa na Oksijeni”,ameeleza.


Amebainisha kuwa kutokana na ukubwa wa bei ya Vanilla ambalo ni zao la pili kwa bei duniani inayofikia dola 430 kwa kilo moja sawa na shilingi Milioni ya Tanzania, wananchi wengi wa Kanda ya Ziwa na nchi kwa ujumla wamefika hilo kutembelea shamba hilo na kuhamasika kulima zao la Vanilla.


“Kampuni yetu ya Vanilla International imeweza kujitwalia wawekezaji (wakulima) wa zao la Vanilla kufikia 1350 nchi nzima ambapo kabla ya uhamasishaji huo wawekezaji wa zao la Vanilla walikuwa hawafiki 50.Mwanza hapakuwa na hata mkulima mmoja sasa hivi wanazidi 12 ambao wote wamejifunza kwenye shamba letu la Kwimba”,amesema.


Ameongeza kuwa zao la Vanilla ni zao lenye bei kubwa kuliko Silver (fedha) na linachuana na dhahabu na hivyo kufanya wachimbaji wa dhahabu Kanda ya Ziwa kuanza kujikita kwenye zao la Vanilla kama ilivyo kwa Dkt. Daniel Mrema wa Nyamikoma Mwanza ambaye ameanza kilimo hicho.

Kampuni hiyo pia imezindua Namba za Simu  0624300200 na 0769300200 kwa ajili ya kufundishia wananchi bure Kanda ya Ziwa kuhusu Kilimo cha Vanilla. Kupitia namba hizo mwananchi anaweza kutumia lugha yoyote ikiwemo Kisukuma, Kihaya. nk kupata huduma juu ya kilimo cha Vanilla.

“Kampuni yetu ya Vanilla International Limited inakukaribisha kuwekeza katika kilimo cha vanilla chenye uwezo mkubwa wa kukuinua kiuchumi. Zao la vanilla linaanza kuvunwa baada ya miezi 7(vikonyo) na mwaka 1 (matunda) lakini unavuna kwa miaka 60. Ukilima vanilla nasi utanufaika wewe,watoto na wajukuu. kwa sasa bei ya kilo moja ni 1,000,000/= na baada ya miaka 6 itakuwa 3,000,000/= kwa kilo ya vanilla. Soko la vanilla liko Dubai na dunia nzima”,ameeleza.
Mkurugenzi Mwanzilishi wa Makampuni ya Vanilla International Limited, Simon Mnkondya akionesha zao la Vanilla wakati akizindua Shamba kubwa la Kilimo cha Vanilla kwa njia za kisasa katika Kijiji cha Nyamikoma kata ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Muonekano wa sehemu ya Shamba kubwa la Kilimo cha Vanilla kwa njia za kisasa katika Kijiji cha Nyamikoma kata ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Muonekano wa sehemu ya Shamba kubwa la Kilimo cha Vanilla kwa njia za kisasa katika Kijiji cha Nyamikoma kata ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Muonekano wa sehemu ya Shamba kubwa la Kilimo cha Vanilla kwa njia za kisasa katika Kijiji cha Nyamikoma kata ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Mkurugenzi Mwanzilishi wa Makampuni ya Vanilla International Limited, Simon Mnkondya akionesha zao la Vanilla wakati akizindua Shamba kubwa la Kilimo cha Vanilla kwa njia za kisasa katika Kijiji cha Nyamikoma kata ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Mkurugenzi Mwanzilishi wa Makampuni ya Vanilla International Limited, Simon Mnkondya akiwa kwenye Shamba kubwa la Kilimo cha Vanilla kwa njia za kisasa katika Kijiji cha Nyamikoma kata ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.


Share:

TSB YAWAFUNDA WAWATA KUHUSU KILIMO FURSA NA MASOKO YA MKONGE

 




Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), imetoa elimu ya kilimo cha zao la Mkonge, masoko na fursa zitokanazo na zao hilo kwa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), katika Semina ya kuhitimisha kongamano la Wawata Kanda ya Mashariki jijini Tanga.

Akizungumza kwenye semina hiyo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Zao la Mkonge na Masoko wa TSB, Olivo Mtung’e, amesema Bodi hiyo ambayo pia ni mdhamini wa kongamano hilo, imeona ni vema kuwashirikisha wanawake Wakatoliki kwenye katika suala zima la kuinua kipato chao na kujiimarisha kwenye familia kwa sababu wao ndiyo wasimamizi wa familia.

“Kama tunavyofahamu zao la Mkonge ni zao ambalo linavumilia sana ukame hasa ukizingatia sasa hivi tunapambana na hili tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa Kanisa Katoliki wao walishaanza tangu mwaka 2015 kuzungumzia jambo hili ambapo Papa Francis alitoa waraka unaozunguzmia namna ya kukabiliana na changamoto hii ya mabadiliko ya tabia nchi.

“Kwa leo tumezungumza mambo machache tu kwamba miaka mitatu iliyopita tumekuwa na shida ya mvua na mazao mengi ambayo yanategemea sana mvua yalikuwa ya shida hata bei za vyakula zilipanda. Kwa hiyo Wawata wao tumewashauri kwenye mashamba yao ya kawaida wapande kama uzio baadaye watavuna na kupata pesa za kulisha familia zao. Lakini wanaweza kupanda katika mazao yao wakapanda kama uzio au mpaka lakini yakawa chanzo cha pesa ambacho kinaweza kusaidia familia,” amesema.

Mtung’e amesema lengo la kuwakaribisha Wawata kwenye kilimo kwa maana hiyo ya faida hizo zilizotajwa kwamba unaweza ukawa ni uzio au mpaka, lakini pia Mkonge wenyewe unarutubisha ardhi ambapo Wachina wameanza kulima milimani kwa ajili ya kukabiliana mabadiliko ya tabia nchi kwamba yenyewe inahifadhi mazingira lakini zao la Mkonge lenyewe halina msimu.

Kutokana na hali hiyo, amesema pia wanaweza wakaingia katika hatua ya pili ya ujasiriamali tunafahamu wanawake sasa hivi  wana vitu vingi vikiwamo vikundi vya ujasiriamali ambapo wanaweza wakafuma mazuria, vitambaa vya mezani (table mats) kwa ajili ya kuuza.

“Rais wetu Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan amefungua nchi yeye amefungua nchi kwa mataifa mbalimbali kupitia filamu yake ya Royal Tour sasa watalii wanakuja. Ukiangalia Mkonge na bidhaa zake ni za asili kwa hiyo wenzetu wanaokuja kutoka mataifa mbalimbali wanategemea waje Afrika ambako watapata vitu vya asili.

“Kwa hiyo mwanamke anao uwezo wa kuzipata hizo bidhaa akazitengeneza akapata pesa hata za kigeni kupitia hao watalii watakaokuja nchini. Lakini pia wale wanaoweza kuingia moja kwa moja kwenye biashara kwa maana tuna wakulima wengi ambao wameingia kwenye kilimo hilki ambapo wanazalisha, wanasindika sasa na wenyewe wanaweza kuingia kwenye ule mnyororo wa thamani kwa maana ya kununua na kuuza na wakawa wanendelea kuimarisha familia zao,” amesema.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Wawata Kanda ya Mashariki, Theodora Mtegeta amesema Bodi ya Mkonge Tanzania ni mkombozi wa mwanamke ikiwa kama kikundi au mmoja mmoja na kuongeza kuwa hata yeye ni shahidi ambapo ana shamba amelima Mkonge hivyo anajua hela ya Mkonge ilivyo tamu.

“Kwa hiyo kinamama wengine wamehamasishwa leo tunamshukuru Mkurugenzo Olivo kwa kutupitisha kwenye kilimo, akatupitisha kwenye masoko, fursa zilizopo kwenye Mkonge, mashamba yapo na hata kama una shamba lako au la familia unaweza kulima mkonge. Kwa hiyo tumepata somo zuri sana kinamama,” amesema.

Share:

VYUO VYA UALIMU VETA NA FDC KIINI CHA UTOAJI ELIMU UJUZI



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula amesema Vyuo vya Ualimu, VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vina mchango mkubwa katika mageuzi ya elimu yanayofanyika nchini na kumtaka kila mtumishi kutimiza wajibu wake.

Dkt. Rwezimula amesema hayo Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma alipofanya ziara Chuo cha Ualimu Kasulu kwa lengo la kujitambulisha na kufahamu mazingira ya utendaji ya watumishi katika Chuo hicho.

Amesema kwa sasa Wizara inakaamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala hivyo ili kufanikisha utekelezaji wa Mageuzi hayo taasisi hizo za elimu zinatakiwa kuwa tayari.

“Vyuo vya ualimu ndipo kunazalishwa walimu watakaokwenda kufundisha katika shule zetu hapa nchini na lengo ni kutoa elimu ujuzi hivyo walimu wataandaliwa kwa mlengo huo vilevile kwa VETA na FDC tunategemea kupata wahitimu wenye ujuzi wa kutenda hivyo tunapaswa kuwa tayari,”amesema Dkt. Rwezimula.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na masilahi ya watumishi hivyo Wizara itaendelea kuhakikisha mazingira ya utumishi katika taasisi hizi yanaendelea kuboreshwa ili kuleta ufanisi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kasulu Hellen Cheyo ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kuendelea kuboresha mazingira ya Chuo hicho. Amesema katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2020/21- 2023 Chuo hicho kimepatiwa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia. Ametaja miradi iliyotekelezwa Chuo hapo kuwa ni ujenzi wa ukumbi wa mihadahara kupitia fedha za UVIKO 19, ujenzi wa maktaba, maabara za TEHAMA, Biolojia, Kemia pamoja na ukarabati wa maabara ya biolojia.

Share:

DIASPORA WAOMBWA KUCHANGAMKIA FURSA MBALIMBALI ZA UWEKEZAJI ZA NSSF ZIKIWEMO ZA NYUMBA NA VIWANJA

 

 

Na MWANDISHI WETU

Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana, amewaomba Watanzania wanaoishi nje ya nchi  (Diaspora) kuona fursa ya kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika miradi ya uwekezaji inayotekelezwa na Mfuko kwenye maeneo mbalimbali nchini.


"Naomba Diaspora wote kuchangamkia miradi mbalimbali ya NSSF ikiwemo ya nyumba zilizopo Toangoma, Kijichi na Dungu jijini Dar es Salaam, pamoja na viwanja vilivyopo kwenye maeneo mbalimbali ambavyo vinauzwa kwa gharama nafuu," amesema Balozi Bwana.

Amesema hayo tarehe 2 Julai, 2023 wakati alipotembelea banda la NSSF, ambapo ameweza kujionea namna wafanyakazi wa NSSF wanavyowahudumia kwa weledi wanachama na wananchi wanaotembelea banda hilo.

Balozi Bwana ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Diaspora wote kuitikia wito huo kwa kunufaika na fursa za uwekezaji kwa kununua nyumba na viwanja vya NSSF ambavyo ni vya uhakika.

Balozi Bwana amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni mdau muhimu wa NSSF, na kwamba wanashirikiana katika masuala mbalimbali ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na NSSF zinawafikia Watanzania wote wakiwemo wanaoishi nje ya nchi 'Diaspora'.

"Natumia fursa hii kuwapongeza NSSF wamekuwa na jukumu hili kwa muda mrefu wamekuwa na mifumo mbalimbali ya kutoa huduma za Hifadhi ya Jamii kwa Diaspora, lakini hivi sasa wanakamilisha mifumo mipya ambayo itaongeza ushiriki zaidi kwa Watanzania waliopo nje ya nchi," amesema Balozi Bwana.

Amesema pia Mfuko umekuwa ukiendesha miradi mbalimbali ya uwekezaji, na kwamba tayari wana ushirikiano wa karibu na NSSF ambapo hivi karibuni wana miradi mikubwa ya uwekezaji na uendelezaji inayofanyika nchini Kenya ili kuendeleza vitega uchumi vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini nje ya nchi.

Balozi Bwana amesema uwekezaji wa NSSF hauishii tu katika uwekezaji wa ndani ya nchi, lakini sasa wanavuka mipaka na kwenda katika maeneo mengine nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kwenda kukusanya na kuleta faida zaidi kwa ajili kuwanufaisha wanachama wa NSSF.

"Nitumie fursa hii kumpongeza kwa dhati Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bwana Masha Mshomba, kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya ya kuhakikisha Mfuko unaendelea kusimama," amesema Balozi Bwana.

Aidha, ameipongeza Menejimenti na Bodi ya NSSF kwa kazi nzuri na miongozo ambayo wamekuwa wakiitoa katika kuhakikisha malengo makuu ya kuanzishwa kwa Mfuko yanaendelea kusimamiwa na kutekelezwa. Malengo hayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na NSSF, wakati alipotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. Kulia kwa balozi ni Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele.

Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa NSSF, wakati alipotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger