MASHIRIKA ya viwango vya ubora wa bidhaa kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), yamejipanga kuhakikisha masuala ya bidhaa na vipimo yanakuwa sawa, husasan upimaji na magari yanayosafirisha mafuta.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha wakati wa mkutano wa 25 wa kujadili masuala ya viwango kwa nchi wanachama wa EAC, Mkurugenzi Udhibiti Ubora Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Lazaro Msasalaga, anasema mkutano huo wa siku tatu umejumuisha wakurugenzi wa viwango kutoka nchi za EAC ni muhimu kwa ajili ya kujadili masuala yahusuyo ubora wa bidhaa.
Anasema mashirika hayo yanakutana kupitia kamati za kitaalam katika masuala ya udhibiti ubora ikiwemo kupitisha viwango 69 za bidhaa za chakula na vipodozi, ikiwemo viwango vitatu vinavyotoa maelekezo ya taarifa zinawekwa katika vifungashio vya bidhaa kama matumizi ya bidhaa husika na jinsi ya kuhifadhi.
“Hiki ni kikao muhimu na nchi ya Tanzania tutanufaika katika ubora wa viwango ikiwemo uwekaji wa maneno yanayoelezea bidhaa wanazotumia walaji zitaboresha vitu gani, ikiwemo viambata vya kilishe sanjari na ujumla wa kuweka maelezo ya aina mbalimbali katika bidhaa,” amesema.
Mkurugenzi wa Shirika la Ukaguzji wa Ubora wa Bidhaa kutoka nchini Kenya (KEBS), Bernard Njiraini, alisema mashirika hayo yanajadiliana viwango walivyokubaliana kwa pamoja, ili waweze kufanya biashara kirahisi ndani ya nchi wanachama wakati wa kupitisha bidhaa mipakani.
Meneja Upimaji Wakala wa Vipimo Tanzania, Magesa Biyani, anasisitiza masuala ya vipimo ni eneo muhimu kuhakikisha bidhaa na vipimo vinakua sahihi katika ufanyaji biashara kwa nchi za EAC hususan masuala ya upimaji katika magari yanayosafirisha mafuta, ambapo awali upimaji ulitofautina baina ya nchi na nchi, lakini pia wanatarajia kuanzisha kanuni itayoondoa vikwazo kwa wafanyabishara wanaosafirisha mafuta kwa nchi za EAC, ikiwemo usahihi wa vipimo vya bidhaa zilizofungashwa.