Saturday, 22 January 2022
Friday, 21 January 2022
SERIKALI KUWABAINI WATU 200,000 WANAOISHI NA VVU BILA KUJUA
MCHAKATO wa kuwapata watu 200,000 waishio na virusi vya Ukimwi bila kujua ni mbinu mojawapo ambayo Wizara ya Afya imesema itaitumia ili kupunguza maambukizi mapya na kufikia malengo ya milenia mwaka 2030.
Pamoja na hayo Wizara imesema inakusudia kupunguza idadi ya watoto wachanga wanaozaliwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka 6000 wanaozaliwa kila mwaka kwa kuhakikisha inamfikia kila mwanamke mwenye ujauzito.
Hayo yamesemwa jana Alhamisi Januari 20, 2022 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati alipokuwa akizindua mpango mkakati wa miaka mitano ya tafiti na mafunzo katika masuala ya afya ya jamii na lishe.
“Nchini Tanzania inakadiriwa watu milioni 1.7 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi lakini wanaotambua hali zao za afya ni milioni 1.5 pekee, hii ni changamoto kwetu lazima tuwatafute hawa 200,000 kwani ndiyo wanaochangia maambukizi mapya bila kujua.
“Tutawapata hawa kwa kuwashauri na kuhamasisha ili wapime kupitia mtaa kwa mtaa, kata kwa kata, halmashauri kwa halmashauri lazima tuhakikishe tunamaliza ugonjwa huu Tanzania ifikapo mwaka 2030. Mpaka sasa wanaotambua hali zao ni asilimia 88, wanaotumia dawa ni asilimia 98 na waliofanikiwa kufubaza makali ya virusi ni asilimia 92,” amesema Waziri Ummy.
Amesema suala la mtoto kuzaliwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi halikubaliki. “Matamanio ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona watoto wote wanazaliwa na afya njema pasipo virusi vya ukimwi, kaswende wala homa ya ini, hii ni changamoto kwetu lazima tuwatafute wote tuwapime na tukiwabaini tuwaingize kwenye dawa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” amesema.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk Donald Wright amesema kati ya vipaumbele ambavyo ubalozi wa Marekani umewekeza ni kusaidia tafiti za masuala ya ukimwi kupitia Usaid na mafunzo pamoja na tafiti za masuala ya afya na lishe.
Chanzo - Global Publishers
HOSPITALI YABURUZWA MAHAKAMANI KWA KUMPA MGONJWA MAJIBU YA UONGO...MWENYEWE ADAI FIDIA MILIONI 40
Kituo kimoja cha kutolea huduma za matibabu kilichopo Mombasa Kenya kimetakiwa na Mahakama kulipa fidia ya Ksh. milioni 2 (Tsh. milioni 40) kwa Mgonjwa aitwaye Roberto Macri baada ya kumpa majibu ya uongo ya vipimo kuwa ana cancer wakati hana cancer.
Jaji wa Mahakama ya Malindi, Julie Oseku amesema Mgonjwa huyo alifika Kituoni hapo ‘Jamu Imaging Centre’ akiwa na changamoto ya kupata shida ya kumeza chakula na akaambiwa ana ‘Cancer Stage Four’ hali iliyomlazimu kusafiri hadi Italia ambako aliambiwa hana Cancer.
“Mgonjwa kama asingeambiwa ana Cancer asingelazimika kutumia gharama kwenda Italia baada ya kuwa na hofu, pia majibu yalimsababishia stress na maumivu zaidi ndio maana aliporudi tu kutoka Italia akafungua kesi,” amesema Jaji Oseku.
WAZALISHAJI WA BIDHAA ZA VIWANDANI WATUMA OMBI KWA SERIKALI NA TRA , KUSHUSHA GHARAMA ZA STEMPU ZA KODI ZA KIELEKTRONIKI (ETS)
Wazalishaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru kwa kutumia Stempu za Kodo za Kielektroniki (Electronic Tax Stamps - ETS) wameiomba Wizara ya Fedha na Mipangopamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupunguza zaidi viwango vilivyotangazwa Jumatatu wiki hii kwa vile viwango vya sasa vya ushuru huo ni vikubwa sana.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya wazalishaji wanaotozwa ushuru huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Bwana Leodegar Tenga amesema kwamba sekta binafsi inaunga mkono uanzishwaji na matumizi ya stempu za kodi za kielektroniki na kusisitiza kuwa kiwango cha gharama hizo kiwezeshe ukuaji wa viwanda nchini.
"Wenye viwanda wanaunga mkono mpango wa serikali kutekeleza matumizi ya ETS kwakuwa yanaleta usawa na ushindani sawia na kuboresha mazingira ya biashara kwa ajili yakuchochea ukuaji wa uchumi, Wanachama wa Shirikisho pia wanaunga mkono matumizi ya ETS kwa kuwa ETS inasaidia kuleta uwazi katika uendeshaji wa biashara na kupunguza undanganyifu kwenye biashara na kuondoa ongezeko la biashara haramu kwenye soko, lakini pia ushuru wa ETS unaotozwa sasa siyo tu kwamba unaongeza gharama za uzalishaji, vilevile unaathari kwenye maendeleo ya sekta ya viwanda na uchumi kwa ujumla, wenye viwanda wamewahi kuwa na majadiliano na TRA, na kuwasilisha kwa serikali mfumo mbadala kama jawabu la kupunguza kiasi kikubwa cha viwango vya gharama vinavyotozwa kwenye ETS. Hata hivyo, maombi yetu ya kuomba viwango vya gharama za ETS upunguzwe hayakuchukuliwa kabisa kufuatia kutangazwa wiki hii kwa viwango vipya vyenye mabadaliko madogo sana” ,alisema Mkurugenzi Mtendaji wa CTI
Na kuongezea kuwa CTI kwa niaba ya wenye viwanda ilishawahi kupeleka mapendekezo ya wenye viwanda serikalini ambayo yalitarajiwa yazingatiwe katika kutoa maamuzi ya kuweka viwango vipya vya gharama za ETS kutokana na Vigezo ivyo tunaomba kupitia upya na kupunguza gharama za ETS ili kupunguza athari za viwanda ambavyo vinaendelea kulipa kodi mbalimbali, wazalishaji wakiwakilishwa na shirikisho kama wadau, washirikishwe katika mchakato wa kurekebisha mfumo mzima wa ETS , Mchakato wa kutafuta mzabuni uwe wa wazi na shindani, kuwepo mpango mahususi wa kutoa huduma ya ETS kwa kutumia mfumo unaoendeshwa na sisi wenyewe, Malipo ya Stempu za ETS yafanyike kwa shilingi za Kitanzania badala ya dola za kimarekani, na mwisho Tunaomba mchakato wa kutafuta mbadala wa ETS ufanyike kukidhi vigezo vya serikali na kupunguza mzigo wa gharama za viwanda",alisema Tenga.
Aidha wameipongeza Serikali kwa kuruhusu ulipaji wa gharama za ETS kwa fedha za Kitanzania na kukiri kuwa ukweli ni kwamba punguzo la gharama za ETS Haliwatii moyo wazalishaji hao wa Bidhaa za Viwandani.
SHILINGI BILIONI MBILI KUKARABATI MITAMBO YA UJENZI WA SKIMU ZA KILIMO CHA UMWAGILIAJI
Picha Ikimuonesha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Daudi Kaali alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari hawapo katika picha, kuhusu matengenezo ya Mitambo, katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Umwagilijai Jijini Dodoma jana.
Picha ikionesha moja ya mtambo uliokarabatiwa unaotumika katika ujenzi wa skimu za kilimo cha umwagiliaji.
Mhandisi Hassan Dyali akizungumza na waandishi wa habari kuhuasiana na sehemu ya majukumu ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ya Ukarabati wa Mitambo inayotumika katika Ujenzi wa Skimu za Kilimo cha Umwagiliaji nchini.
**
Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Kiasi cha fedha shilingi Bilioni Mbili za Kitanzania, zitatumika katika ukarabati na matengenezo ya mitambo inayotumika katika ujenzi wa miundombinu katika skimu za kilimo cha Umwagiliaji nchini.
Hayo yamesemwa jana jioni jijini Dodoma, na kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Daudi Kaali alipokuwa akizungumza waandishi wa habari katika viunga vya ofisi za Tume hiyo wakati zoezi la ukabati wa mitambo hiyo ukiendelea.
Bw. Kaali alisema nchi nzima ina mitambo zaidi ya 53 na inayoweza kutengenezwa ni mitambo 44 na malengo yaliyowekwa na Tume hiyo ni kutengeneza mitambo 43 hadi kufikia mwakani 2023. “Tutaokoa fedha nyingi kwani kukodi mtambo mmoja siyo chini ya Sh. Milioni moja kwa siku moja na unaweka kukuta, skimu moja inaweza ikahitaji siku hata ishirini au theathini kwa ajili ya matengenezo , hivyo kwa mahesabu ya haraka utaona ni fedha nyingi sana zinahitaji kukodisha mtambo mmoja kwa siku”. Alisisitiza Kaali.
Aidha alifafanua kuwa, Tume hiyo imetenga wastani wa hekta laki mbili na hamsini kwa mwaka zinazoweza kuendelezwa, hivyo matengenezo ya mitambo hiyo yataweza kuongeza kasi ya kuweza kuendeleza eneo hilo. “Tukienda hivi baada ya miaka mitano tunaweza kuwa tumeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kufikia hekta milioni moja na laki mbili. Alisema.
Mhandisi Hassan Ndyali, ni Msimamizi wa kitengo cha mitambo hiyo anafafanua kuwa, pamoja na kuwa kazi ya kukarabati mitambo hiyo ni sehemu ya majukumu ya ofisi, alisema kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe “Ambaye alitamani sana kuona tunafanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa na kukamilisha kwa wakati ili mitambo hiyo iweze kuleta tija kwa Taifa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji”,alisisitiza Mhandisi Ndyali.
Mmoja wa fundi wa mitambo hiyo Bw. Raphael Kanuha, amewahakikishia wakulima kuwa mashine hizo zitakamilika ndani ya muda mfupi na zitaingia kazini na kufanya kazi kwa ufanisi.
Thursday, 20 January 2022
MABALOZI WA KODI WATEMBELEA MIKOA YA KASIKAZINI KUHAMASISHA ULIPAJI KODI
Afisa Afya kutoka Wizara ya Afya Bw. Mohamed Mtosa akitoa maelezo kwa Mabalozi wa Kodi walipotembelea Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Forodha Namanga mkoani Arusha. Kutoka kushoto ni Balozi Zulfa Omary, ambae ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar, Balozi Bw. Edo Kumwembe na Balozi Subira Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani. Afisa Forodha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. James Mwasambili akitoa maelezo kwa Mabalozi wa Kodi waliotembelea Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Forodha Namanga mkoani Arusha. Kutoka kulia ni Meneja Msaidizi wa Forodha Kituo cha Namanga Bw. Paul Kamukulu, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Bw. Richard Kayombo, Balozi Zulfa Omary, ambae ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar na Balozi Subira Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani.Mshauri wa Kodi Bw. Nikolaus Duhia (wa kwanza kulia) akitoa maoni yake wakati wa kikao kazi cha Mabalozi wa Kodi, baadhi ya Wafanyabiashara na Wadau wa Kodi wa Mkoa wa Arusha uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo. Lengo la kikao kazi hicho ni kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na wakati.
Mkurugenzi wa kiwanda cha A to Z cha mkoani Arusha akiwaonesha Mabalozi wa Kodi bidhaa mbalimbali wakati Mabalozi hao walipofanya ziara kiwandani hapo. Lengo la ziara hiyo ni kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na wakati.
Baadhi ya Mabalozi wakiangalia bidhaa zilizotengenezwa na kiwanda cha A to Z cha mkoani Arusha wakati Mabalozi hao walipofanya ziara kiwandani hapo. Lengo la ziara hiyo ni kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na wakati.
(Picha na TRA)
*************************
Na Mwandishi wetu,Namanga
Mabalozi wa Kodi walioteuliwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wako katika mikoa ya Kaskazini ambayo ni Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa ajili ya kuhamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari ili kuongeza mapato ya Serikali.
Mabalozi hao wamepata fursa ya kutembelea Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha mpakani Namanga mkoani Arusha na kukutana na baadhi ya wadau na walipakodi ambapo wamewahimiza kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati.
Wakizungumza wakati wa ziara hiyo Mabalozi hao wa kodi, wameipongeza Serikali kwa kuwa na Vituo vya Huduma kwa Pamoja mipakani kwani vimeondoa kero zilizokuwepo kipindi cha nyuma na kusifu ushirikiano uliopo katika ya TRA na wafanyabiashara ambao umesaidia Mkoa wa Arusha kuvuka malengo ukusanyaji mapato.
“Katika kituo hiki cha Namanga, nimejifunza mambo mengi, moja wapo ni namna nchi hizi mbili za Tanzania na Kenya zilivyoondoa urasimu uliokuwepo kipindi cha nyuma.
Nikiwa kama Balozi, nitatumia elimu hii niliyoipata kutoka TRA kuwahamasisha wananchi kujenga tabia ya kulipa kodi kwa wakati kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Bw. Edo Kumwembe mmoja wa mabalozi hao.
Kwa upande wake Balozi Zulfa Omari, ambae ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar akizungumza wakati wa kikao kati ya wafanyabiashara wa Arusha na mabalozi hao, alisema kuwa ni nadra sana kukuta wafanyabiashara wakiizungumzia vizuri TRA lakini amefarijika kuona walipakodi wa Arusha wakiipongeza TRA kwa kuboresha huduma zao.
“Kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi kulikuwa na mambo mengi niliyokuwa nikiyasikia kuhusu TRA na yalikuwa yakiniumiza sana lakini hapa Arusha nimesikia kitu cha faraja kwamba TRA inazungumzwa vizuri mbele yetu kitu ambacho si kitu cha kawaida maana wafanyabiashara mara nyingi huwa hawaizungumzii vizuri TRA,” alisema Balozi Zulfa.
Balozi mwingine ni Subira Khamis Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani ambae alisema kuwa kupitia ziara hii amejifunza taratibu mbalimbali zinazotumika wakati wa uingizaji wa mizigo kutoka ndani na nje ya nchi kupitia Kituo cha Namanga.
“Kama Balozi nimefahamu kwa kina jinsi mifumo inavyofanya kazi katika kituo hiki cha Namanga ambayo huisaidia Serikali kukusanya mapato stahiki kutoka vyanzo mbalimbali.
Kwa upande wa walipakodi na wadau ambao tumekutana nao Arusha Mjini, naweza kusema kuwa, usemi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan umedhihilika wazi kuwa, kodi inaweza kukusanywa bila kutumia mabavu kwa sababu Mkoa huu wa Arusha umevuka malengo bila kuwasumbua walipakodi wake.”
Balozi Mgalu amewasisitiza walipakodi hao kuongeza ushirikiano kwa TRA ili kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuwaahidi kwamba, changamoto zote walizozitoa wamezipokea na watazifanyia kazi.
Kazi wanazozifanya Mabalozi hao wa Kodi katika ziara yao ya kikazi kwenye mikoa hiyo ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga ni pamoja na kutembelea viwanda, kutembelea vituo vya huduma kwa pamoja mipakani na kukutana na wafanyabiashara kwa ajili kuwahamasisha kulipa kodi kwa hiari na wakati.
5G YAHARIBU SAFARI ZA NDEGE MAREKANI
Mashirika makubwa ya ndege Emirates, Air India, Air Nippon na Japan Airlines yamesitisha safari zake za kwenda Marekani kutokana na huduma ya mtandao wa 5G.
Jana asubuhi huduma ya mtandao wa 5G ilianza kutumika nchini Marekani kwa kuwashwa minara 4500 ya 5G.
Mashirika hayo ya ndege yamesitisha huduma zake nchini Marekani kwa madai kwamba mtandao wa 5G unaingilia mawasiliano ya ndege. Ndege za Boeing 777 mawasiliano yake huathiriwa na huduma ya 5G na kufanya kampuni hizo zitumie ndege nyingine.
WANAFUNZI WALIONUSURIKA AJALI YA LUCKY VINCENT WAFANYA MAAJABU KIDATO CHA IV
WANAFUNZI watatu walionusurika kwenye ajali ya Shule ya Lucky Vincent, wamefanya maajabu katika mtihani wa kidato cha nne na kufaulu vizuri kwenye masomo ya sayansi.
Wanafunzi hao ni Doreen Elibariki ambaye amepata daraja la pili, Wilson Godfrey (daraja la kwanza) na Sadia Awadh (daraja la pili).
Akizungumza kwa furaha kwa njia ya simu ya kiganjani, mzazi wa Sadia, Zaituni Abdul, alisema katika matokeo hayo anamshukuru Mungu kuwapigania watoto wao.
“Hakika namshukuru sana Mungu maana kwa matatizo waliyopitia hawa watoto sikutegemea kama watapata matokeo haya, hakika furaha yangu kubwa sana,” alisema.
Alisema mwanawe ndoto yake kubwa ni kuwa daktari wa binadamu au rubani.
Mama mzazi wa Doreen, Neema Mshana, alisema alipopata matokeo hayo alimuona Mungu akimshika mkono mwanawe na wenzake.
“Hakika Mungu mwema anajua waja wake na hajawaacha, naamini ataendelea kutembea na watoto hawa mpaka watakapofikia ndoto zao,” alisema.
Mwalimu wa darasa wa wanafunzi hao, Pascal Safari, aliwapongeza watoto hao kupata ufaulu mzuri licha ya matatizo waliyopitia.
Alisema katika darasa lao walikuwa jumla ya wanafunzi 65 ambao kati yao 26 wamepata daraja la kwanza akiwamo Wilson, 30 walipata daraja la pili akiwamo Doreen na mwenzake Sadia. Pascal alisema wanafunzi wengine nane walipata daraja la tatu na mmoja daraja la nne.
Alisema watoto hao ambao manusura ya ajali wote walikuwa mkondo wa sayansi na wamefaulu vizuri. “Naamini watoto hawa wanaweza kurudi hapa shuleni kuendelea na masomo yao ya kidato cha tano na sita kwani mazingira yaliyoko mazuri yanawafaa kuendelea na masomo,” alisema.
Wanafunzi hao walipata ajali ya gari Mei 6, mwaka 2017, wakati wakielekea kwenye Shule ya Tumaini Junior iliyoko wilayani Karatu kwa ajili ya kufanya mtihani wa kujipima.
Katika ajali hiyo wanafunzi 32, walimu wawili na dereva walifariki papo hapo eneo la Rhotia wilayani Karatu, huku wanafunzi hao watatu wakinusurika.
Baada ya ajali hiyo Shirika lisilo la kiserikali la STEMM chini ya mratibu wa safari hiyo, Lazaro Nyalandu, liliwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo nchini Marekani, Steve Meyer, ambaye kwa ushirikiano na serikali waliwezesha kupatikana kwa hati ya kusafiria haraka kwenda nchini Marekani kwa matibabu zaidi baada ya kugundulika kuvunjika mara 36 mwilini mwao kila mmoja.
Doreen alilazimika kupelekwa kituo maarufu duniani cha Madona nchini Marekani, kutokana na tatizo la uti wa mgongo.
Agosti 18, mwaka 2017 walirejea nchini kwa msaada wa Shirika la Ndege la Mfuko wa Msamaria la Marekani linaloendeshwa na Frankline Graham, mtoto wa mwimbaji maarufu duniani, Bill Graham, wakiwa wameambatana na wazazi wao watatu na daktari bingwa wa mifupa wa Hospitali ya Mount Meru, Elias Mashalla na Dk. Siniphorosa Silalye.
KAMATA HADI BONUS YA SH. 300,000 KWENYE AKAUNTI YAKO IJUMAA HII
Pata bonus ya asilimia 100% ukiweka pesa kwenye account yako ya 22bet Ijumaa hii, hadi 300,000 kumbuka bonus hiyo itakuwa mara mbili ya pesa uliyoweka kwenye account yako. Ofa hii ni kwa kila mteja atakayeweka pesa kwenye account weeekend hii. Pia kwa wateja wapya watapata bonus ya kuweka fedha kwenye account yake ya 22bet kwa mara ya kwanza.
COASTER YAGONGA TRENI DAR, WATU WAWILI WAFARIKI, 11 WAJERUHIWA
UONGOZI wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) umethibitisha kutokea kwa tukio la ajali lililotokea Januari 19, 2022 maeneo ya Banana jijini Dar es Salaam katika kivuko cha reli na barabara, ambapo gari la abiria aina ya ‘Coaster’ lenye namba za usajili T701 CKD linalofanya safari kati ya Tandika na Mbezi limegonga treni.
"Ajali imetokea majira ya saa 11:10 jioni na imehusisha treni ya mjini inayotoa huduma ya usafiri wa abiria kati ya Kamata na Pugu jijini Dar es Salaam, katika ajali hii majeruhi ni abiria 6 waliokuwa wakisafiri na basi ambapo wanawake ni watatu na wanaume watatu na kuna vifo vya wanawake wawili, majeruhi wote wamepelekwa Hospitali ya Amana kupatiwa matibabu.
"Dereva wa basi alitahadharishwa kwa kupigiwa honi na dereva wa treni, hakuzingatia na hata aliposimamishwa na mshika bendera dereva wa basi aliamua kukatiza reli na kupelekea ajali.
"Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania unaendelea kusisitiza Umma kuwa makini na kufuata Sheria na taratibu zinazoonesha alama zilizopo katika vivuko vya reli na barabara na dereva anapokaribia makutano anapaswa kupunguza mwendo na kusimama umbali wa mita 100 kuhakikisha endapo njia ni salama ili kuendelea na safari;
Wednesday, 19 January 2022
COMORO YAICHAPA 3-2 GHANA NA KUITUPA NJE AFCON
TIMU ya taifa ya Comoro imeitupa Ghana nje ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuichapa mabao 3-2 katika mchezo wa mwisho wa Kundi C usiku wa Jumanne Uwanja wa Roumdé Adjia Jijini Garoua, Cameroon.
Mabao ya Comoro yalifungwa na El Fardou Mohamed Ben Nabouhane dakika ya nne na Ahmed Mogni mawili, dakika ya 61 na 85, wakati ya Ghana iliyomaliza pungufu baada ya Nahodha wake, Andre Ayew kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 25, yalifungwa na Richmond Boakye dakika ya 64 na Alexander Djiku dakika ya 77.
CHELSEA YAZIDI KUPUNGUZWA KASI MBIO ZA UBINGWA EPL YATOKA SARE YA 1-1 NA BRIGHTON
TIMU ya Chelsea imetoa sare ya 1-1 na wenyeji, Brighton & Hove Albion katika mchezo wa Ligi Kuu ya England usiku wa Jumanne Uwanja wa The AMEX, Falmer, East Sussex.
Hakim Ziyech alianza kuwafungia wageni dakika ya 28, kabla ya Adam Webster kuwasawazishia wenyeji dakika ya 60 na sare hiyo ya nane ya msimu inazidi kuiondolea Chelsea matumaini ya ubingwa sasa kikosi cha kocha Mjerumani, Thomas Tuchel kikiachwa pointi 12 na mabingwa watetezi, Manchester City.
Chelsea inafikisha pointi 44 katika mchezo wa 23 nafasi ya tatu, nyuma ya Liverpool pointi 45 za mechi 21 na Man City pointi 56 za mechi 22, wakati Brighton imefikisha pointi 29 katika mechi ya 21 nafasi ya tisa.