Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 blog, Dodoma
TAASISI ya taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) imetahadharisha kuwepo kwa ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanayopelekea ongezeko la vifo na majeruhi kwa asilimia 41 hapa nchini huku visababishi vikitajwa kuwa ni pamoja na matumizi ya pombe,sigara,na ulaji usiozingatia kanuni za afya.
Hayo yamebainishwa leo Januari 6,2022 jijini Dodoma na Mtafiti kutoka Taasisi ya NIMR Dr. Emmanuel Makundi wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti kuhusu magonjwa mbalimbali yaliyokwenda sambamba utoaji wa muhtasari ya vijarida sera vya sayansi na teknolojia vya sekta nne za Afya,kilimo,Maliasili na utalii ulioandaliwa na Tume ya taifa ya sayansi na Teknolojia[COSTECH].
Amesema ongezeko kubwa la magonjwa hayo ni mara mbili ya hali iliyokuwepo miaka 25 iliyopita na kwamba mikakati iliyopo inazingatia zaidi tiba kuliko kinga na kusababisha ongezeko la magonjwa ya moyo,shinikizo la damu ,kisukari ,saratani mbalimbali na magonjwa ya mifumo ya hewa.
"Theluthi mbili ya tatizo hili iko kwa watu walio chini ya miaka 40 ambao ni vijana na kukumbwa na vifo na ulemavu wa kudumu,ili kuondokana na tatizo hili Lazima kuwepo mabadiliko Katika mtindo wa maisha na kuepuka lishe duni,"amesema.
Pamoja na hayo makundi amesema jamii inatakiwa kuondoa dhana potofu ya kuwa magonjwa hayo ni ya watu matajiri pekee bali hutokea hata kwa watu masikini huku akitaja visababishi vya magonjwa hayo kuwa ni pamoja na matumizi ya tumbaku hasa uvutaji sigara,matumizi ya pombe,kutofanya mazoezi,ulaji wa vyakula bila mpangilio.
Aidha amesema licha ya ukubwa wa tatizo ulivyo,huduma za afya kuhusiana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza hazitoshelezi mahitaji hasa ya vijijini ambako nusu ya Hospitali zote nchini zinatoa huduma za msingi za magonjwa hayo na ulemavu.
"Upatikanaji wa huduma za msingi kwa upande wa vijijini ni hafifu mfano wagonjwa wenye tatizo la shinikizo la damu hawapati vipimo na matibabu yanayostahili Kwa muda muafaka,"amesisitiza.
Amesema kuna upungufu mkubwa wa fedha za kugharamia huduma za magonjwa hayo na kueleza kuwa nusu ya asilimia 7.8 tu kwa matumizi ya sekta ya afya ndio hutumika kwa ajili ya magonjwa hayo ikilinganishwa na ukubwa wa tatizo ambalo ni asilimia 41 ya magonjwa yote.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi ,Teknlojia na Ubunifu (COASTECH) Dkt. Wilbert Manyilizu alisema, lengo la warsha hiyo ni kuwashirikisha Wadau wakuu wa matokeo ya tafiti za kisayansi na Teknolojia ili waweze kuwasilisha na kutoa matokeo ya tafiti zao.
Amesema,Coastech imewaita watafiti katika Sekta nne za awali ambazo ni sekta ya Afya,Kilimo,maliasili na mifugo ili wawasilishe tafiti zao ambazo hufanyiwa kazi na Tume hiyo ambayo ndio yenye dhamana ya kuishauri Serikali katika masuala ya sayansi na teknolojia.
"Lengo la kuanzishwa kwa Tume hii ni kuishauri Serikali katika masuala ya sayanasi na Teknolojia na ubunifu huku akisema,jukumu kubwa la COASTECH ni kuratibu na kuhamasisha Mambo ya utafiti na ubunifu ambapo katika jukumu hilo pia kuna majukumu mengine ambàyo ni kusimamaia Menejimenti ya maarifa yanayopatikana katika ubunifu na utafiti na baadae kusambaza kwa Wadau,"amesema.