Saturday, 4 December 2021
MHE. GEKUL AKABIDHI BENDERA TIMU YA TAIFA YA KUOGELEA
OSHA YATOA MAFUNZO KWA WAKAGUZI WA MAENENO YA KAZI NCHINI
RC SOPHIA MJEMA AZINDUA RASMI KAMPENI YA UPANDAJI MITI YA 'PENDEZESHA TANZANIA' INAYOENDESHWA NA BENKI YA CRDB
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema amezindua rasmi Kampeni ya Upandaji miti kupitia Programu ya Pendezesha Tanzania inayoendeshwa na Benki ya CRDB inayolenga kuhamasisha upandaji miti na utunzaji wa mazingira nchini.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumamosi Desemba 4,2021 katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara na Madini wa Butulwa maarufu viwanja vya Zainab Telack uliopo kata ya Old Shinyanga katika Manispaa ya Shinyanga ambapo pia wananchi wamepatiwa miti bure kwa ajili ya kwenda kupanda kwenye maeneo yao.
Mkuu huyo wa mkoa ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kuja na Programu ya Pendezesha Tanzania kwa kuhamasisha upandaji wa miti na utunzaji mazingira nchini kupitia kanda zake 7 za Kibenki.
“Kwa upande wa Kanda ya Magharibi mkoa wetu wa Shinyanga umebahatika kuwa chaguo la Benki ya CRDB kuendesha Programu hii kupitia kwenye viwanja vyetu vya maonesho ya Biashara na Madini vya Zainab Telack. Hadi leo katika viwanja hivi Benki ya CRDB wamekwisha panda takribani miti 1,000 na leo imekusudiwa kupandwa miti 900 ili kufikisha adhima yao ya kupanda miti 2,000. Naomba tuwapongeze”,amesema Mhe. Mjema.
“Napenda kuwashukuru Benki ya CRDB kwa kuendesha Programu hii ya Kizalendo . Pia nawashukuru wadau wote mliojitokeza katika zoezi hili la upandaji miti. Napenda kuzihamasisha taasisi zote zilizopo mkoani Shinyanga kwa kuiga na kuunga mkono juhudi hizi ambazo wenzetu Benki ya CRDB wamezionesha kwa Programu yao ya PendezeshaTanzania kwa kupanda miti na kuhamasisha utunzaji mazingira”,ameongeza Mjema.
Mkuu huyo wa mkoa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za utunzaji mazingira na uwekaji wa mikakati ya kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi zilizopelekea kupata fedha za Mfuko wa Utunzaji Mazingira (GCF).
Mjema amesema Mkoa wa Shinyanga umejipanga kupanda miti Milioni 9 na sasa miti milioni 5 imepatikana tayari kwa kuanza kupandwa huku akiagiza Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri zote za wilaya Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha wanasimamia upandaji miti na miti iliyopandwa.
Amefafanua kuwa dunia kwa ujumla inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi yanayochangiwa shughuli za kibinadamu hususani ukataji miti na ukuaji wa viwanda ambao unasababisha ongezeko la gesi ukaa hali inayosababisha ukosefu wa mvua za kutosha na zisizotabilika na ongezeko la joto na kuyeyuka kwa barafu katika Mlima Kilimanjaro.
“Kwa ujumla hali siyo nzuri, sisi sote ni mashahidi siku hizi hata msimu wa mvua haueleweki hivyo kusababisha mavuno hafifu, ukosefu wa maji ya uhakika. Mwarobaini wa haya ni sisi kuamua kwa dhati kutunza mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji kwa kupanda miti na kuachana na ukataji miti ovyo kwa faida yetu pamoja na vizazi vijavyo”,ameeleza.
“Wananchi wa Shinyanga tuhakikishe katika makazi yetu tunatunza mazingira na kupanda miti hususani miti ya matunda,vivuli na mbao ili kuifanya dunia iwe sehemu salama ya kuishi”,amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko amesema tayari wilaya ya Shinyanga inaendelea na Kampeni ya Upandaji miti ya ‘Shinyanga ya Mikwaju na Miembe’ hivyo kuishukuru Benki ya CRDB kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika upandaji miti na utunzaji mazingira.
Naye Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Saidi Pamui wamesema wameanza Programu ya Pendezesha Tanzania kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kupanda miti na kutunza mazingira ili kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema lengo la Benki ya CRDB ni kupanda miti 2,000 katika viwanja vya maonesho ya Biashara na Madini vya Zainab Telack na tayari walishapanda miti 1,100 na leo wamepanda miti 900 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema.
“Sisi Benki ya CRDB ni Mabalozi wazuri wa upandaji miti na utunzaji mazingira hivyo tumeanzisha Programu ya Pendezesha Tanzania ili kuonesha mfano kwa wananchi wawe na mwamko wa kupanda miti na kutunza mazingira. Tunawashukuru wadau wote ambao leo mmeungana nasi kushiriki zoezi hili la upandaji miti”,amesema Pamui.
PAKUA APP MPYA YA MALUNDE 1 BLOG....IMEBORESHWA ZAIDI KUKUPA RAHA YA HABARI NA MATUKIO BURE KWENYE SIMU YAKO
Pakua App mpya ya Malunde 1 blog imeboreshwa zaidi ili kukidhi mahitaji ya wasomaji wetu.