Sunday, 3 May 2020

Korea Kaskazini Na Korea Kusini Zashambuliana Kwa Risasi

Serikali ya Korea Kusini imesema leo wanajeshi wake wamefyatuliana risasi na wanajeshi wa Korea Kaskazini katika eneo lisilo na shughuli za kijeshi linalozitenganisha Korea mbili. 

Taarifa ya mkuu wa majeshi wa Korea Kusini imesema kituo kimoja cha walinzi kilishambuliwa kwa risasi kadhaa kutoka upande wa kaskazini, lakini hakuna aliyejeruhiwa.

 Afisa huyo wa jeshi amesema jeshi la Korea Kusini lilifyatua risasi kujibu shambulizi hilo na kutoa onyo kwa wanajeshi wa upande wa kaskazini. 

Makabiliano hayo ya nadra yametokea siku moja tangu vyombo vya habari vya Korea Kaskazini kuripoti kuwa kiongozi wake Kim Jong Un ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu wiki tatu. 

Kutoonekana kwa Kim kulizusha uvumi kuhusu hali yake ya afya na wasiwasi juu ya hatma ya taifa hilo


Share:

Naibu Waziri wa Kilimo: Tumekusudia NFRA Lazima Ijiendeshe Kibiashara

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imeweka bayana mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) unajiendesha  kibiashara pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba (Mb) amebainisha mkakati huo jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha Bodi ya Ushauri ya NFRA hivi karibuni.

Mhe Mgumba amesema kuwa serikali imetathmini mwenendo wa NFRA katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo na kujiridhisha kuwa umeanza kutekeleza majukumu yake ipasavyo hivyo kuongezewa jukumu muhimu la kununua nafaka kwa ajili ya kuhifadhi kadhalika kujiendesha kibiashara.

Ameutaka wakala huo kufanya manunuzi ya mazao kwa ajili ya kuhifadhi kama akiba kwenye maghala ya serikali lakini pia kwa ajili ya biashara kwa kutafuta masoko ndani na nje ya Nchi.

Naibu Waziri Mgumba amesema wakala huo una jukumu la kuhifadhi mazao ya kila aina na siyo kuchagua mazao ya kuhifadhi akitolea mfano Mahindi kuwa ndiyo yamekua yakipewa kipaumbele ukilinganisha na mazao mengine.

Amesema kuwa serikali imetekeleza maelekezo ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa hivyo NFRA inapaswa kuhakikisha kuwa inanunua nafaka ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi kadhalika kufanya biashara.

Amesema kuwa NFRA inapaswa kununua mahindi, mpunga na mtama kwani Mazao hayo ni fursa kutokana na uhitaji mkubwa wa Chakula nchini na nje ya nchi.

"Unaweza kuwa na fedha nyingi lakini Kama huna mipango mizuri ya ununuzi  huwezi kupata Mazao hivyo NFRA ni lazima mjipange vizuri ikiwemo kuongeza vituo vya ununuzi" Alisema na kuongeza kuwa

"Msije mkanunua mahindi kisiasa, ni lazima mtenganishe siasa na biashara, mkifanya hivyo mtajichimbia shimo wenyewe, hivyo lazima mkafanye biashara kwa ajili ya kupata faida"

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Yustas Kongolle ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwaamini yeye na wajumbe wa bodi hiyo kiasi cha kuwateua kuhudumu kwa miaka mitatu huku akisema watafanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa zaidi.

"Kuaminiwa na Wizara maana yake Nchi imetuamini, tunaahidi kufanya kazi kwa bidii na kutimiza maagizo yote ambayo tumeelekezwa kufanya ikiwa ni pamoja na kuifanya NFRA ijiendeshe kibiashara," Amesema Mhandisi Kongolle

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Delphina Mamiro ambaye ni Mjumbe wa Bodi hiyo ya NFRA amesema kuwa Bodi hiyo imejipanga kufanya kazi kubwa na nzuri zaidi ili kutekeleza imani hiyo.

Amesema kuwa mradi wa ujenzi wa maghala na Vihenge vya kisasa utakamilika hivi karibuni hivyo kuna jukumu kubwa na muhimu la kuhakikisha kuwa utekelezaji wa ununuzi unakamilika kwa wakati.


Share:

Rais Magufuli Ahoji Papai, Mbuzi Kukutwa na Virusi Vya Corona....Awashangaa Wanaotaka Dar es Salaam Ifungwe, Biashara Zifungwe

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameeleza kushangazwa kufuatia sampuli za Papai, Mbuzi kukutwa na Virusi vya Corona baada ya kupimwa kwenye Maabara kuu ya Taifa.

Rais Magufuli ameyasema hayo hii leo katika hafla fupi ya kumwapisha Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Augustine Mahiga aliyefariki dunia.

“Tulipeleka Sample ya Ndege Kware ilikuwa Positive, Mbuzi akawa Positive, Kondoo akawa Negative, ukishaona sampo ukamwambia huyu ni binadamu halafu ana Corona maana yake Mapapai yote yangewekwa Isolation.

"Tulipopeleka sampo ya Papai tukaipa jina la Elizabeth (26) Papai lile lilikuwa Positive kwamba lina Corona, maana yake maji ya Papai ni Positive.


”Tulichukua sampo za Mbuzi, Kondoo, Papai, Oil ya gari tukavipeleka maabara na tukazipa majina, mfano Oil tuliipa jina la Jabir Hamza (30), ili leta Negative, sampo ya Fenesi tuliipa jina la Sarah Samweli (45), matokeo inconclusive.

“Kama tunapeleka sampuli za wanyama zinakutwa Positive inawezekana wafanyakazi wa Maabara wanatumika na Mabeberu, kama mapapai, mbuzi yana corona WHO wanapaswa kufanya kazi kubwa ya ziada, kwa hili lililotokea lazima kuna Watu wameambiwa wana corona wakati hawana

“Mbuzi awe na corona, fenesi liwe na corona, ndege kware awe na corona, lazima tujiulize inawezekana kuna kitu fulani hakijaeleweka Tanzani na hata Duniani hakijaeleweka, natoa wito Wanasayansi Nchi nyingine wachukue sampuli za wanyama, ukuta na yoyote wataamini nachosema

“Tusitishane, kama sampuli maabara inasema papai na fenensi yana corona, inawezekana papai lingekuwa na masikio lingeoza kwa uoga, Waziri Nchemba kachunguze, inawezekana hivi vifaa vimetengenezwa kwamba vikipima Watu 30 anayefuata ana corona, tuwe makini hata na hivi vifaa" amesema Rais Magufuli

Aidha Rais Magufuli ameendelea kuwasisitiza watu wasitishane kisa Corona na badala yake waendelee kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya ujenzi wa Taifa. 

“Watanzania corona isitutishe, inawezekana kuna Watu wengine wamekufa kwasababu ya hofu tu, Viongozi wa Dini msitupotoshe, nampongeza Mufti amesema sisi tutaendelea kufunga, Watanzania tusimame imara tumeshashinda hii vita.

“Wengine wako Dar es Salaam  wanasema Watu wasiende Bungeni, na nimeagiza wasilipwe posho maana utalipwa kwa kazi uliyofanya, kuna mambo ya ajabu yanafanyika, sina imani na Mkuu wa Mabaara ya Taifa maana haiwezekani tupeleke sampuli za papai zioneshe zina corona.

“Wengine wanazungumza eti tufunge biashara au shughuli za kiuchumi wakati wengine wanaendesha magari yameandikwa STK na inawekwa mafuta na Serikali amesahau alichokalia ndicho kinatoa mafuta, mishahara tutalipaje tukifunga

“Mambo ya kucopy na kupaste Nchi hii hatuwezi kuyafanya, wapo wenzetu waliofunga mipaka na shughuli za kiuchumi mnaona wanavyoteseka, sisi mpaka sasa tuna vifo vya corona 16, huu ni wakati wa kuwapima Watu imani hata Viongozi wa Dini, unawazuiaje Watu kwenda kuabudu

“Mkuu wa Mkoa wa Mtwara nikamuona siku moja anazungumza kwamba Mkuu huyu wa Wilaya amefariki hatuwezi kusafirisha atazikwa hapahapa, ilinisikitisha sana, walishindwaje Viongozi wa Mtwara kumsafirisha DC akaenda kuzikwa kwa heshima kule kwao Moshi!?

“Jaji Mkuu Augustino Ramadhan hapa Mzee wangu alikuwa na tatizo la Kansa tumehangaika nae lakini amefariki Vijana wanapost eti corona...siku hizi hata Mtu akijiua wanasema corona, ikitokea ajali Polisi wamefika kuchukua miili napo corona

“Kwahiyo natoa wito kwa Watanzania tusiogope, tuchape kazi, Wanasiasa waache kutumia corona kuleta manenomaneno, wanasema nifunge Dar es Salaam , sifungi nishasema, nafikiria kuruhusu hata Ligi ya mpira iendelee,tuache kutishana"- Amesema


Share:

RAIS MAGUFULI ASHANGAA PAPAI, FENESI NA MBUZI KUKUTWA NA CORONA...ASHTUKIA MCHEZO WA AJABU


CORONA
Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameeleza kushangazwa kufuatia sampuli za Papai, Mbuzi kukutwa na Virusi vya Corona baada ya kupimwa kwenye Maabara kuu ya Taifa.

Rais Magufuli amesema hayo wakati akimuapisha Waziri wa Katiba na Sheria Mwigulu Nchemba Chato mkoani Geita ambapo amemtaka kwenda kufanya uchunguzi kwenye suala la maabara ya Taifa.

"Waziri nimekuapisha leo itabidi wewe kwa kushirikiana na Wizara ya Afya mkafanye uchunguzi kwenye masuala flani katika maabara ya taifa ya Tanzania iliyokuwa inahusika kupima Corona kuna Controlversal nyingi za ajabu,tuliona walikuwa wanatoa matokeo chanya..positive positive tu mara nyingi.

Nilizungumza na vyombo vya ulinzi na usalama na nikatoa maelekezo,hebu nendeni mkacheki hivi vipimo vikoje,hivyo vifaa vikoje na mara nyingi nimekuwa nikisisitiza kwamba si kila kitu unachopewa lazima kiwe kizuri..wanaweza kutumika watu,vinaweza kutumika hivyo vifaa lakini pia hii inaweza kuwa sabotage tu kwa sababu hii ni vita"- Amesema Rais Magufuli.

Ninamshukuru sana Katibu Mkuu Mpya Prof. Mchembe ,wameenda na kufanya mambo yafuatayo kwa kutumia na vyombo vyetu pia:

"Tulichukua Sample za Mbuzi,tukachukua sample za kondoo,tukachukua sampo za papai,tukachukua sampo za Oil ya gari na sample za vitu vingine mbalimbali tukavipeleka pale kwenye Maabara bila wao kujua na tukazipa majina..Sample ya Oil iliyotoka kwa gari tuliipa jina la Jabir Hamza mwenye miaka 30,ile ilileta Negative,tulipoleka sample ya Fenesi ambalo tulilipa jina la Sarah Samwel (45) matokeo yake yalikuwa Unconclusive,tulipopeleka sampo ya papai tukalipa jina la Elizabeth Anne (26) papai lile lilikuwa positive maana yake lilikuwa na Corona.

"Tulipeleka sample ya ndege Kware majibu yakawa positive,tumepeleka Sungura ikawa Undetermined,tumechukua mbuzi akawa Positive,tukachukua kondoo akawa Negative nk.
Sasa umepeleka sample ukamwambia huyu ni binadamu halafu ikaleta positive kwamba ina Corona maana yake yale mapapi yote yale yangewekewa Isolation,ukipeleka mbuzi wa sample nao wakawa positive maana yake mbuzi wote tulionao au huyo aliyepelekwa naye apelekwe Isolation,ukipeleka Fenesi likawa positive maana yake makamasi kamasi yake yale ambayo tuliyapa jina la Elizabeth nayo mafenesi yalitakiwa yawekwe Isolation", ameeleza Rais Magufuli.

"Kwa hiyo ukishagundua hivi lazima ujue kuna mchezo wa ajabu unafanyika kwenye vipimo hivi...kwamba kuna mambo ya ajabu yanafanywa katika nchi hii..Either Wahusika wa Maabara 'Laboratory' ile wamenunuliwa na Mabeberu,Either hawana utaalamu which is not True kwa sababu maabara hii imetumika sana kwenye magonjwa mengine!, Either zile sample zinazoletwa kwa sababu mpaka Reagent zinatoka nje,mpaka zile Swap..vile vipamba vinatoka nje..lazima kuna kitu flani kinafanywa

Na kama mapapai yanaonekana Positive yana Corona basi WHO inatakiwa ifanye kazi kubwa katika haya,na kama mbuzi nao wana Corona,na kama hawajajua kuwa hii Corona ina affect binadamu,mbuzi hata miti basi wanasayansi hatujafanya cha kutosha katika hili...Kwa hiyo kutokana na taarifa hizi zilizonazo lazima  kuna watu wameambiwa Positive wakati siyo wagonjwa wa Corona na inawezekana wengine wakafa kwa hofu..Papai lile lipo halijafa, lipo tu linaiva, mbuzi yule yupo tu wala hajafa, fenesi lile lipo labda lije lioze tu kwa muda wake lakini yale ni Positive na vitu vingine",ameongeza Rais Magufuli.

Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli amesema licha ya kwamba Corona ipo amewataka Watanzania kutokuwa na hofu kutokana na Corona
Share:

Watu Waanza Kuruhusiwa Kutoka Nje Hispania Baada ya Amri ya Kubaki Ndani Kutokana na Virusi Vya Corona

Wananchi nchini Hispania, wameruhusiwa kutembea nje  baada ya kukaa ndani kwa Siku 48 kufuatia Mlipuko wa virusi ya Corona ulioikumba dunia, ambapo lengo la kukaa ndani lilikuwa ni kupambana na kupunguza kuenea kwa VirusI hivyo

Karibu watu milioni 47 wa Uhispania tangu Machi 14 waliishi chini ya kizuizi cha kutoka nje huku walioruhusiwa kutoka nyumbani ni watu wazima tu ambao walitoka nje kwa ajili ya kwenda kufanya manunuzi ya chakula, dawa au kutembeza Mbwa.

Ubakiaji wa Nyumbani ulisogezwa tena mbele mwishoni mwa Mwezi uliopita hadi Mei 9 lakini Waziri Mkuu Pedro Sanchez Jumanne alifungua mpango wa kuanza hatua kwa hatua kupunguza vizuizi katika awamu nne ambazo zinapaswa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni.

Aidha watoto chini ya miaka 14 waliruhusiwa wiki iliyopita kutoka nje kwa matembezi hivyo hali ya kuendelea kupunguza vizuizi bado inaendelea mpaka leo.

Visa 216,582 na vifo 25,100 vimeripotiwa nchini Hispania ikiwa ni nchi mojawapo ambayo imeathirika zaidi na maradhi ya Corona Ulimwenguni.


Share:

Taarifa rasmi ya Wizara ya Afya kuhusu Mazishi ya wanaofariki katika kipindi hiki.




Share:

Taarifa ya Serikali kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona (Covid-19).




Share:

RAIS MAGUFULI : TUTATUMA NDEGE MADAGASCAR KUFUATA DAWA INAYOTIBU CORONA


Dawa ya mitishamba inayodaiwa kutibu Covid-19 
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema atatuma ndege kwenda nchini Magascar kuchukua dawa inayodaiwa kutibu ugonjwa wa Corona.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumapili Mei 3,2020 wakati akimuapisha Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

"Nimewasiliana na Madascar na wameshaandika barua wanasema kuna dawa zimepatikana kule,tutatuma ndege kule na dawa zitaletwa pia ili Watanzania nao waweze kufaidika nayo kwa hiyo sisi serikali tupo tunafanya kazi usiku na mchana",amesema Rais Magufuli.

"Wengine wanasema nipo Chato kwani waliambiwa huku Chato sitakiwi kuwepo..huku si ndiko nitazikwa..nikienda Moshi kesho napo watasema nipo Moshi nimekimbia wapi,makao makuu yapo Dodoma lakini hizi ni siasa za kutumia kila kitu ni siasa..hapa ndipo wakati ambao tunatakiwa kusimama pamoja katika kupambana na ugonjwa wa Corona",ameongeza.

Wakati wanasayansi duniani wakihangaika kupata chanjo na tiba ya virusi vya corona, hivi karibuni rais wa Madagascar Andry Rajoelina amezindua dawa ya mitishamba inayotibu' Covid-19 .

Ikizinduliwa kwa jina Covid-Organics, dawa hiyo imetengenezwa kutoka kwa mmea artemisia (pakanga)-ambao ni mojawapo ya miti ambayo huchanganywa pamoja na mimea mingine ya Madagascar kama tiba ya ugonjwa wa Malaria.

Dawa hiyo ambayo imepakiwa kwenye chupa na kutangazwa kama chai ya miti shamba baada ya kujaribiwa kwa watu kadhaa kwa kipindi cha wiki tatu.

Rais Rajoelina aliwataka watafiti kuja na tiba ambayo waliipata kwa muda muafaka

"Vipimo vimefanyika-watu wawili wamekwishapona kutokana na tiba hii," Bwana Rajoelina alisema katika uzinduzi wa Covid-Organics uliofanyika katika taasisi ya utafiti ya Madagascar- Malagasy Institute of Applied Research (Imra), ambayo ndiyo iliyotengeneza dawa hiyo ya mitishamba.

"Kinywaji cha dawa hii ya mitishamba huonesha matokeo katika kipindi siku saba," alisema rais huyo mwenye umri wa miaka 45, ambaye aliwataka watu kuitumia kama hatua ya kujikinga na ugonjwa wa corona.

"Watoto wa shule wanapaswa kupewa kinywaji ... kidogo kidogo kwa siku nzima," aliwaambia mabalozi na watu wengine waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya uzinduzi wa kinywaji hicho.

Share:

RAIS MAGUFULI : BAADHI YA VIONGOZI WA DINI WAMEANZA KUYUMBA..WAMEMSAHAU MUNGU KWENYE CORONA



Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema baadhi ya viongozi wa dini wameanza kuyumba na kumsahau Mungu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona.


 Rais Mafuguli ameyasema leo Jumapili Mei 3,2020 akiwa Chato Mkoani Geita wakati wa hafla fupi ya kumuapisha Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Malunde 1 blog imefuatilia hotuba ya Rais Magufuli iliyokuwa inarushwa Live katika vyombo vya na imefanikiwa kupata nukuu zifuatazo

⇒⇒⇒"Wapo hadi baadhi ya viongozi wa dini wamemsahau Mungu ambaye kila siku wamekuwa wakituhubiria, wanashika vitabu wanafahamu yupo Mungu" - Rais Magufuli.

⇒⇒⇒Leo kuna baadhi ya viongozi wa dini wameanza kuyumba na kumsahau Mungu ambaye waliapa ndiyo kiapo chao Biblia au Quraan,wameanza kuisahau na kuiweka pembeni na kuuweka ubinadamu mbele.. Acheni kuomba tunajiokoa,acheni sijui nini nini..

⇒⇒⇒Ni mambo ya ajabu lakini ndiyo hivyo katika kipindi hiki cha mpito tutayasikia mengi na huu ndiyo wakati wa kuwapima imani viongozi tulionao.. Hata viongozi wa dini ..ukizuia waumini wako wasiende kanisani,ukazuia waumini wako wasiende msikitini na unaweza ukakuta hata huo msikiti wala hukuujenga wewe,umejengwa na hao waumini..hilo nalo ni suala la ajabu la kujiuliza, si uwafungulie hao waumini wenye nia waende mle wakamuombe Mungu hata kama wewe hutaenda kuhubiri pale?

⇒⇒⇒Ndiyo hapa tutayaona, na hizi ni changamoto..Tuendelee kumuomba Mungu na Mungu atatusaidia katika kutupitisha kwenye changamoto hizi wala hali siyo mbaya kama inavyotishwa sisi tupo vizuri na biashara zinaendelea na ndiyo maana tuna uwezo wa kulipa hata mishahara" - JPM

⇒⇒⇒Tufunge kila kitu utawalipa mishahara? hata wanaozungumza hao funga huku wanaendesha magari yameandika STK,mafuta yanawekwa mule na serikali lakini anasema fungeni,amesahau alichokalia ndiyo kinachomlisha..

⇒⇒⇒Watanzania simameni Imara,huu ugonjwa utaisha,utapita tunapata changamoto lakini tunazitatua.


Share:

RAIS MAGUFULI AWAONYA VIJANA WANAOPOST UJINGA KUHUSU CORONA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania kubadilika na kuacha tabia ya kuichafua nchi na kuogopesha wananchi kuhusu ugonjwa wa Corona kwamba kila mtu anayekufa basi ameugua Corona.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumapili Mei 3,2020 wakati akiwa Chato mkoani Geita akimuapisha Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

"Corona kweli ipo lakini isituyumbishe katika msimamo wetu na direction yetu , Tusitishwe',amesema Rais Magufuli.

 "Naendelea kutoa wito kwa hasa vijana ambao wamekuwa kila siku wanapost, wakimuona mtu, amekufa na Corona..Marehemu Jaji Mkuu tumehangaika naye zaidi ya mwaka mzima, siyo vizuri kutaja matatizo yake..Jaji Mkuu amekufa kwa Kansa lakini watu wamebadilisha maneno ya ajabu",amesema Rais Magufuli.

"Kwa hiyo Watanzania tujifunze hata kumuogopa Mungu,Tujifunze hata kumuogopa mtu, si vyema kila mtu anayekufa ni Corona..It is not Possible..Mbona Maleria yameua watu wengi tu,mbona ajali zimeua watu wengi tu.

"Siku hizi hata mtu akikutwa na ajali polisi wanakwenda,wanavaa gloves zao wanasema huyu ana Corona,mtu hata akijiua chumbani kwake wanapokwenda kuchukua mwili wake wanasema ni Corona..Ninawaomba Watanzania tubadilike, Tunaichafua nchi yetu,tunaiharibu nchi yetu,tunajiogopesha sisi wenyewe wakati hili suala Mungu atali - Handle na tutapita salama",amesema JPM

Share:

LIVE: Rais Magufuli Akizungumza Baada ya Kumuapisha Mwigulu Nchemba

LIVE:  Rais Magufuli  Akizungumza Muda Huu


Share:

Rais Magufuli Kumuapisha Mwigulu Nchemba Leo Saa Nne Asubuhi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Mei, 2020 atamuapisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. 

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawsiliano ya Rais, Gerson Msigwa  imesema tukio hilo litarushwa moja kwa moja na vyombo vya habari kutoka Chato Mkoani Geita, kuanzia saa 4:15 asubuhi.


Share:

Naibu Waziri Stella Manyanya Aelekeza Viwanda Vya Plastiki Kuzalisha Ndoo Kwa Wingi, Atangaza Msako Mkali Kwa Wafanyabishara Wanaouza Bei Kubwa Ndoo Za Kunawia

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Stella Manyanya ameelekeza Viwanda ya plastiki nchini kuzalisha ndoo kwa wingi na ametoa onyo kali kwa wafanyabishara wanaouza bei za juu vifaa vya kunawia mikono.

Mhe. Stella Manyanya ametoa maagizo haya jana 02 mei 2020, Jijini Dar es salaam alipotembelea viwanda vinavyozalisha plasitiki ambavyo ni kiwanda cha Silafrica Tanzania Ltd {Sumalia} na Kiwanda cha Cello Industries Ltd.

Amevipongeza Viwanda vyote kwa  kwa kuendele kuzalisha ndoo na Vifaa vingine  kwa wingi vinavyotumika kunawia mikono ambavyo vinahitajika sana katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugojwa wa Corona

“Nawapongeza na nimefurahishwa sana na uzalishaji mzuri na hakuna wasiwasi kwamba tutakuwa na upungufu wa ndoo za kunawia mikono katika maeneo yetu maana nimejionea uzalishaji mkubwa unaoendelea na ambao utaweza kukidhi maahitaji ya watanzania ya upatikanaji wa ndoo za kunawia mikono”

Aidha, ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaendelea kuuza bei Kubwa ndoo na vifaa vingine vya kunawia mokono kwa kufanya mapambano ya ugojwa huu kuwa fursa kwao ya kujinufaisha maradufu na kujipatia kipato kikubwa tofauti na ilivyokuwa awali.

“Natoa onyo kwa wafanyabiashara wote hasa wa reja reja kuna baadhi yao ambao wanatumia muda huu wa mapambano ya Corona kama fursa ya kujinufaisha maradufu, Ni marufuku kwa mtu yeyote kuongeza bei kupita kiasi maana kuna wafanyabishara wanaongeza mara mbili ya bei walizonunulia kiwandani”

Sambamba na hayo Mhe. Stella Manyanya ameendelea kusisitiza kuwa serikali itaendelea kufuatilia na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote wanaenda kinyume na maelekezo yanayotolewa na serikali kwa kuongeza bei bidhaa mbalimbali katika kipindi hiki cha Mfungo wa ramadhani pia cha mapambano ya Corona

“Niendelee kuwakumbusha kuwa Serikali inaendelea kufanya msako mkali nchi nzima kwa wafanyabiashara wote wanaoenda kinyume na maelekezo ya serikali, kama tulivyofanya msako kwa wafanyabiashara wa sukari sasa tunaendelea kwa wafanyabiashara wanaouza vifaa vianavyotumiaka kunawia mikono na bidhaa nyingine ili kila Mtanzania aweze kuhimili bei za bidhaa ili kwa pamoja tuweze kutokomeza huu ugojwa wa Corona”

Ameongeza kuwa “Wizara inaendelea kufanya mahesabu kamili ya bei za ndoo za kunawia mikono ambayo yatazingatia kuazia bei inayouzwa kiwanda pia usafirishaji,  baada hapo tutatangaza bei elekezi kwa kila Mkoa maana kuna watu wameshindwa kuwa wazalendo na vita hii ni ya sisi sote kushirikiana kwa pamoja na kuhakikisha tunaishinda kwa pamoja”.

Na Eliud Rwechungura - Wizara ya viwanda na biashara


Share:

Serikali Yaanza Mkakati Wa Malisho Bora Ya Kisayansi Kwa Ajili Ya Mifugo

Na. Edward Kondela
Serikali imesema itahakikisha changamoto ya malisho ya mifugo nchini inatatuliwa kwa wafugaji kuelimishwa namna ya kulima malisho bora yenye tija kwa mifugo yao.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amebainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akikagua shamba darasa la malisho ya mifugo katika Kijiji cha Mahambe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida na kubainisha kuwa, serikali itaendelea kuwatia moyo wafugaji ili wawe na mashamba ya malisho bora ya mifugo yao pamoja na kuhakikisha uwepo wa maji ya kutosha ya kunyweshea mifugo mambo ambayo yatasaidia kudhibiti migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumaji wengine wa ardhi.

“Makatibu tawala wa mikoa mingine waige mfano wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa mashamba ya malisho ya mifugo, lazima iendelezwe kwenye mikoa mingine. Wafugaji wengine nchini wakiweza kutenga maeneo yao na kupewa mafunzo na kulima malisho yao itakuwa njia sahihi pia ya kuwasaidia wafugaji kuondokana na hali ya kuhamahama ya mifugo yao kutafuta malisho.” Amesema Prof. Gabriel 

Aidha Prof. Gabriel ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa kuhakikisha anashirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kutunza mashamba hayo dhidi ya uvamizi wowote wa watu kukata malisho hayo au kuingiza mifugo yao kulisha bila utaratibu unaokubalika.

Pia amewataka wafugaji kote nchini kufahamu nchi yeyote duniani inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni hivyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi haitamtetea mfugaji yeyote atakayeenda kinyume na sheria kwa kulisha mifugo yake katika eneo au shamba la mmiliki mwingine bila kufuata utaratibu.

Katibu mkuu huyo ameongeza kuwa lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha uwepo wa mifugo bora nchini ambayo inatokana na kula malisho bora ya kisayansi, ambapo badala ya kula wingi wa majani wale majani yaliyo bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bw. Justice Kijazi ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, kusambaza wataalam wake wa malisho katika maeneo mengine hapa nchini ili kuwashauri wakulima kuwa na mashamba mengi ya malisho bora ya mifugo ambayo yatakuwa na tija kwa wafugaji kwa kuwa na mifugo bora.

Bw. Kijazi amefafanua pia Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ina majosho 10 ya kuoshea mifugo huku akiishukuru wizara kwa kuwapatia fedha ya kukarabati majosho matatu na kuiomba wizara iwasaidie pia fedha nyingine kwa ajili ya kukarabari majosho saba yaliyobaki ili wafugaji wengi zaidi katika halmashauri hiyo waweze kuogesha mifugo yao.

Kuhusu idadi ya mifugo iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bw. Kijazi amesema kuna jumla ya mifugo takriban 600,000 ambapo ng’ombe wapo 350,000 mbuzi na kondoo zaidi ya 200,000 licha ya halmashauri kuwa na changamoto ya kutokuwa na machinjio nzuri, ameiomba wizara kutoa msaada wowote ili kuiwezesha halmashauri hiyo kuwa na machinjio nzuri na kisasa kulingana na idadi ya mifugo iliyopo na hatimaye kuweza kuuza nyama ndani na nje ya nchi.

Akibainisha umuhimu wa uwepo wa mashamba bora ya malisho yanayotokana na kupandwa kwa aina mbalimbali za nyasi zilizofanyiwa utafiti wa kisanyansi na kuthibitishwa kuwa ni bora kwa malisho ya mifugo, Afisa Mifugo Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bibi Bezia Rwongezibwa amesema wafugaji wanafundishwa kulima, kupalilia, kuweka mbolea, kuvuna na hatimaye kuhifadhi malisho hayo ambayo yatatumika wakati wa uhaba wa malisho.

Nao baadhi ya wananchi wakiwemo wa vikundi vya wajasiriamali ambao wamejitolea kulima mashamba darasa kwa ajili ya mifugo kutoka katika Kijiji cha Mahambe Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida, wamesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewatia moyo namna ya kulima malisho na kuyahifadhi ambapo baadhi yao wameanza kupanda malisho hayo ili wapate mifugo bora wakiwemo ng’ombe.

Wamesema uwepo wa mashamba darasa katika eneo lao ni darasa tosha kwao kwa kuwa wataweza kujifunza zaidi kuhusu malisho bora ya mifugo na hatimaye kulima katika mashamba yao.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, wakati akikagua shamba darasa la malisho ya mifugo katika Kijiji cha Mahambe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida, amezungumzia pia kuhusu uwepo wa virusi vya corona nchini vinavyosababisha ugonjwa wa Covid 19 ambapo amebainisha kuwa kwenye sekta ya mifugo wizara imeweka mkazo mkubwa kwa jamii ya wafugaji kote nchini kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kukabiliana na janga hilo kwa kuchukua tahadhari, kufanya maombi pamoja na kufanya kazi kwa bidii.

Mwisho.


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili May 3















Share:

Saturday, 2 May 2020

Breaking News : RAIS MAGUFULI AMTEUA MWIGULU NCHEMBA KUWA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  amemteua Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria ambapo Uteuzi huo umeanza leo Jumamosi Mei 2,2020

Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani anachukua nafasi ya Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga aliyefariki dunia jana Mei 1,2020.


Share:

Picha : MSAMBAZAJI WA GESI 'KIBIRA GAS' ATOA MSAADA WA VIFAA VYA KISASA KUKABILIANA NA CORONA KWA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA SHINYANGA

Msambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC),Kadama Malunde vifaa vya kisasa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga.


Na Estomine Henry - Mratibu SPC
Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ ametoa msaada wa vifaa vya kisasa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC).

Msambazaji huyo wa Gesi Maarufu ‘Kibira Gas’ amekabidhi vifaa hivyo kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Kadama Malunde leo Jumamosi Mei 2,2020 katika ofisi ya SPC iliyopo Mjini Shinyanga.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo zikiwemo sabuni 5 za maji,tishu 6,ndoo mbili,barakoa,beseni moja na kifaa cha kisasa cha kunawia mikono kwa kukanyaga, Kibira amesema vifaa hivyo vitawasaidia waandishi wa habari kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Corona wanapotekeleza majukumu yao ya kuhabarisha jamii.

“Nimewiwa kufika hapa kuwachangia vifaa hivi kwani Waandishi wa habari ni miongoni mwa makundi ambayo yapo hatarini kupata maambukizi ya Virusi vya Corona kutokana na shughuli zao ambazo zinafanya wakutane na watu mbalimbali kila siku”,amesema Kibira.

Naye Mwenyekiti wa SPC, Kadama Malunde amemshukuru Kibira kwa msaada huo akibainisha kuwa amekuwa mdau wa kwanza mkoani Shinyanga kuliangazia kundi la waandishi wa habari ambao kutokana na kazi yao wanahitaji vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona.

“Tunamshukuru sana mdau wetu Kibira Gas kwa msaada huu ambao tunaamini utaongeza nguvu katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona”,amesema Malunde.

Katika hatua nyingine Malunde amewakumbusha waandishi wa habari kuzingatia maelekezo yanayotolewa na serikali kuhusu ugonjwa wa Corona na kuhakikisha wanachukua tahadhari kwa kuepuka mikusanyiko,kuvaa barakoa,kunawa maji tiririka na sabuni pamoja na matumizi ya Sanitizer.
Kushoto ni Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC),Kadama Malunde vifaa vya kisasa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga leo Jumamosi Mei 2,2020 -Picha zote na Marco Maduhu na Frank Mshana.
Kushoto ni Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga ,Kadama Malunde vifaa vya kisasa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga.
Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ akionesha namna ya kunawa mikono kwa kutumia kifaa cha kisasa wakati akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga ,Kadama Malunde (kulia)vifaa vya kisasa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga ,Kadama Malunde akinawa mikono kwa kutumia kifaa cha kisasa kilichotolewa na Kibira Gas kwa ajili ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona.
Kushoto ni Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vya kisasa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga.
Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vya kisasa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) ,Kadama Malunde akimshukuru Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ kwa msaada wa vifaa vya kisasa vya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga leo Jumamosi Mei 2,2020. Kibira pia ametoa msaada wa Barakoa maalumu zenye nembo ya Malunde 1 blog kwa waandishi wa habari wa mtandao wa Malunde 1 blog
Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ (kushoto) akipiga picha ya kumbukumbu na Mwenyekiti wa SPC, Kadama Malunde ambaye pia ni Mkurugenzi wa Malunde 1 blog baada ya kumkabidhi barakoa maalumu zenye Nembo ya Malunde 1 blog kwa ajili ya waandishi wa habari wa Mtandao wa Malunde 1 blog
Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’ (katikati) akipiga picha ya kumbukumbu na Mwenyekiti wa SPC, Kadama Malunde ambaye pia ni Mkurugenzi wa Malunde 1 blog na Mwandishi wa Malunde 1 blog , Marco Maduhu (kushoto) baada ya kumkabidhi barakoa maalumu zenye Nembo ya Malunde 1 blog kwa ajili ya waandishi wa habari wa Mtandao wa Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Malunde 1 blog  Kadama Malunde (kulia) na Mwandishi wa Malunde 1 blog , Marco Maduhu (kushoto) wakiwa wamevaa barakoa maalumu zenye Nembo ya Malunde 1 blog zilizotolewa na Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’.
Barakoa maalumu zenye Nembo ya Malunde 1 blog zilizotolewa na Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’.
Barakoa maalumu zenye Nembo ya Malunde 1 blog zilizotolewa na Mfanyabiashara maarufu anayejihusisha na Usambazaji wa Gesi katika Manispaa ya Shinyanga Sadiki Idrisa Kibira ‘Kibira Gas’.
Picha zote na Marco Maduhu na Frank Mshana.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger