Tuesday, 21 April 2020

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kuongoza maombi ya Kitaifa kesho tarehe 22/04/2020 katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Dodoma,  Jumanne 21 Aprili, 2020 
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Viongozi wa madhehebu ya Dini nchini, imeandaa maombi maalum Kitaifa kuiombea Nchi dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayotokana na Virusi vya Corona.

 Maombi hayo  yatakayoongozwa na Viongozi Wakuu wa  madhehebu ya Dini nchini, yatafanyika Jumatano tarehe 22 Aprili, 2020 katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar Es Salaam, kuanzia Saa 3.00 Asubuhi ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Hatua hii ni utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa viongozi wa Dini na Serikali uliofanyika tarehe 9 Aprili, 2020 Jijini Dar Es Salaam kuwa yafanyike maombi ya kitaifa yanayojumuisha madhehebu yote nchini kuomba dhidi maambukizi ya Corona.

 Aidha, maombi haya ni mwendelezo wa maombi ya siku tatu mfululizo yaliyotangazwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuanzia tarehe 17-19 Aprili, 2020.

 Viongozi wachache watahudhuria maombi haya kuwakilisha wananchi ikiwa ni katika hali ya kuchukua tahadhari ya maambukizi hivyo, wananchi mnasisitizwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona na kufuatilia maombi haya mkiwa katika maeneo yenu kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

JIKINGE, WAKINGE WENGINE CORONA INAZUILIKA.
 
IMETOLEWA NA
   
Prudence Constantine,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
(Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii).


Share:

Abiria Wanaotoka Mikoa Iliyoathirika na Corona Kukaa Karantini Rukwa Huku Wananchi Wakitakiwa Kuvaa Barakoa

Katika harakati za kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID – 19) Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa maelekezo kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanavaa barakoa wanapokuwa katika mikusanyiko pamoja na maeneo yao ya kibiashara hasa kwa wale wanaohusika na kutoa huduma kwa jamii huku akivitaka vyombo husika kuhakikisha abiria wote wanaotoka katika maeneo yaliyoathirika ndani ya nchi kuingia mkoa wa Rukwa washauriwe kujitenga kwa hiari kwa muda wa siku 14.

Mh. Wangabo amesema kuwa abiria hao wanaoingia ndani ya mkoa wanatakiwa kupimwa afya zao kwa kipima joto (Thermal Scanner) kwenye vituo vitatu vya mabasi mkoani humo ikiwemo Laela kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kituo cha mabasi Namanyere kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pamoja na kituo kikuu cha mabasi Sumbawanga na kuongeza kuwa abiria hao wanatakiwa kuvaa Barakoa.

“Abiria wanaoingia Mkoa wa Rukwa kutoka kwenye maeneo yaliyoathirika wanashauriwa kujitenga wao wenyewe kwa hiari yao kwa muda wa siku kumi na nne (14). Endapo watahisi au kugundua kuwa wanaona dalili zozote za matatizoya kiafya watatakiwa kuripoti kwenye kituo chochote cha Afya cha karibu,” Alisema.

Aidha, Mh. Wangabo amewashauri wafanyabiashara wote ndani ya mkoa wenye tabia za kusafiri kwa nia ya kufuata mizigo ya kibiashara kuacha kufanya hivyo na badala yake wajenge tabia ya kuagiza bidhaa hizo kwa njia ya sim una kulipa kwa njia za mitandao ya simu ama benki inapobidi na pia kuwashauri wafanyabiashara wadogo kujiunga na kuagiza mzigo kwa pamoja ili kuwa na urahisi wa kupata usafiri wa pamoja.

“Watu wote wanaofanya kazi za kutoa huduma kwenye maduka, Maeneo yote ya kuuza vyakula, Saluni, Super Market, Wahudumu wa nyumba za kulala Wageni wanatakiwa kuvaa barakoa. Familia zinapotaka kufanya manunuzi ya jumla, inashauriwa aende mtu mmoja tu kutoka kila familia kufanya manunuzi hayo. Hata kwenda hospitali kuona wagonjwa aende mtu mmoja tu na mtu huyo asisahau kuvaa barakoa,” Alisisitiza.

Halikadhalika, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa minada yote na Magulio inadhibitiwa na kuendeshwa kulingana na maelekezo ya wataalamu wa afya na serikali kwa ujumla, na kubainisha kuwa serikali ya mkoa haitasita kusitisha mnada ama gulio endapo taratibu na maelekezo ya wataalamu ama ya serikali yatakiukwa.

Mh. Wangabo ameyasema hayo katika taarifa yake aliyoitoa  tarehe 20.4.2020 kwa vyombo vya habari.




Share:

Waziri Wa Viwanda Na Biashara Atoa Wito Kwa Wawekezaji Kuwekeza Kwenye Viwanda Vya Kutengeza Barakoa Na Vitasamkono

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa amesema kwamba Serikali imejipanga kuzalisha zaidi ya Barakoa Milioni tatu na nusu kwa mwezi ili kukidhi mahitaji ya Watanzania wote.

Hayo ameyasema Aprili 20, 2020 jijini Dar es Salaam alipokua katika ziara ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa (face mask) na Vitakasa mikono (Hand sanitizer) ambapo kwa siku ya leo ziara hiyo imefanyika katika Kiwanda cha Uzalishaji cha Prestine, Kiwanda cha Uchapishaji cha Five stars na Kiwanda cha Uzalishaji Mafuta na Vilainishi cha Total.

Waziri Bashungwa ameeleza kwamba Uzalishaji wa Barakoa za kutosha kwa sasa ni muhimu sana na Serikali inahakikisha kwamba Viwanda hivi vinapata malighafi ya kutosha ili viendelee kuzalisha vizuri.

“Kiwanda cha Prestine sasa hivi kinatengeneza Barakoa elfu thelathini kwa siku (30,000) lakini baada ya vifaa kuingia kitazalisha elfu hamsini kwa siku (50,000) na Kiwanda cha Five Star kitazalisha barakoa laki moja kwa siku (100,000) hivyo kwa ujumla Viwanda hivi vitazalisha barakoa zisizopungua milioni tatu na nusu kwa mwezi mmoja (3,500,000) hii ni hatua muhimu sana.”alisema Waziri Bashungwa.

Akizungumza kuhusiana na ziara yake katika Kiwanda cha Total Waziri Bashungwa ameeleza kwamba Uongozi umekubali kushirikiana na Serikali katika kuzalisha vitakasa mikono na tayari maandalizi ya awali yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuangalia sehemu ambayo itatumika kwa ajili ya uzalishaji.

“Baada ya kuangalia Kiwanda na eneo maalumu ambalo wamelitenga kwa ajili ya uzalishaji wa vitakasa mikono, na kwa uwezo wa kiwanda hiki kwa siku kitakua na uwezo wa kutengeneza lita elfu sita (6000) ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kudhibiti ugonjwa huu.” Aliongeza Waziri Bashungwa.

Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuzingatia melekezo na kanuni za kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona (COVID -19).


Share:

Maendeleo Ya Ubunifu Wa Mji Wa Serikali Yajadiliwa

Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea na zoezi la kuratibu awamu ya pili ya uendelezaji wa mji wa serikali eneo la Mtumba, makao makuu ya nchi jijini Dodoma. Awamu hii ya pili inahusisha Ubunifu na ujenzi wa majengo makubwa ya Ofisi zitakazotumiwa na Wizara za serikali.

Akiongea, tarehe 20 Aprili, 2020,  katika kikao cha Kamati ya Makatibu wakuu na Wataalamu wa michoro ya Ubunifu na usanifu , Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu, (Waziri Mkuu na Bunge), Tixon Nzunda, amefafanua kuwa awamu hii ya pili ya mpango huo inajikita katika kuboresha ubunifu na usanifu wa mji wa serikali, ulioko Mtumba, Jijini Dodoma.

Aidha, kufanikiwa kwa  mpango huo ni kutachangiza jiji la  Dodoma kuwa jiji bora na la kisasa linaloendana na mahitaji na mifumo ya majiji bora duniani. Ili kufikia azma hiyo, tayari Timu ya Wataalam  imepitia michoro ya ubunifu na usanifu. Pia Wakala wa majengo Tanzania (TBA), inaendelea kufanya kazi kwa karibu na  Taasisi nyingine zinazohusika na miundo mbinu katika mji wa Serikali kama vile TARURA, DOWASA, TANESCO, ZIMAMOTO, TPDC, TTCL na eGA.

Hivi karibuni , Mwezi Februari mwaka huu, 2020, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alizindua Mpango Kabambe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambapo aliwataka wadau mbalimbali kutoa ushirikiano kwa kiwango cha juu katika utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kulifanya kuwa jiji bora na la kisasa nchini.

Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kutekeleza zoezi la kuhamishia shughuli za Serikali Kuu Dodoma. Tangu utekelezaji wa zoezi hilo uanze mwezi Septemba 2016.

Uamuzi wa kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma ulifanyika mwaka 1973 ikiwa ni maelekezo ya Chama cha TANU kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

MWISHO.


Share:

NIDA Yawataka Wananchi Kuepuka Vishoka wakati wa mchakato wa kuomba Vitambulisho vya Taifa

Na: Hadija Maloya-NIDA.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewaasa wananchi kuacha kutumia njia na watu wasio rasmi kisheria maarufu kama vishoka wakati wa mchakato wa kuomba Vitambulisho vya Taifa badala yake wafuate utaratibu rasmi uliowekwa na Serikali katika kuomba Vitambulisho hivyo.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Bw. Geofrey Tengeneza kufuatia tukio la mwananchi mmoja (Jina limehifadhiwa) mkazi wa Kigogo fresh jijini Dar es salaam kufika ofisi ya NIDA Wilaya ya Ilala iliyoko Ukonga Mombasa kupiga picha ya Kibaometriki kwa ajili ya Kitambulisho cha Taifa, kuwadokeza Maafisa usajili wa NIDA kuwa mara baada ya kukamilisha zoezi hilo la kupiga picha ameelekezwa na mtu mmoja kupeleka fomu yake ya maombi kwake ili amkamilishie vipengele vilivyobaki pamoja na kumpatia cheti cha kuzaliwa.

Mwananchi huyo alisema kuwa hata fomu yake ya maombi ya Kitambulisho cha Taifa imesainiwa na kugongwa muhuri na mtu huyo na kumpata barua baada ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa anakoishi wa Kigogo Fresh kukataa kutoa barua na kusaini fomu zake kutokana na kutokuwepo kwa cheti cha kuzaliwa kama utaratibu unavyotaka.

Mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni na kisha kufanyiwa upekeuzi kwenye ofisi yake katika duka moja la steshenari lililoko Ukonga Mombasa ambako walikuta nyaraka mbalimbali za Serikali kama vile nakala za Fomu za Maombi ya Vitambulisho vya Taifa (F1A) ambazo tayari zimegongwa muhuri, nakala za Hati za Kiapo cha Kuzaliwa (Affidavit form) na nakala za barua za Utambulisho wa Makazi zenye muhuri wa ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu.

Mtuhumiwa huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, tayari amefunguliwa mashtaka kwa kosa la kukutwa na Nyaraka za Serikali kinyume cha sheria na kosa la kujifanya Afisa wa NIDA.

Akizungumzia tukio hilo Bw. Tengeneza amesema mtu huyo atakuwa ni kishoka ambaye bila shaka hata muhuri wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa aliogonga na barua ya Serikali ya Mtaa aliyoitoa kwa mwananchi huyo ili awasilishe katika ofisi ya NIDA wilaya ya Ilala kwa ajili ya kupatiwa Kitambulisho cha Taifa, vitakuwa vyote ni feki. 

Ameonya watu wanaojihusisha na kuwarubuni wananchi waache tabia hiyo mara moja kwani Mamlaka haitasita kuwachukulia hatua kali za sheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha Mahakamani.


Share:

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye Azindua Safari Za Ndege Za Mizigo Uwanja Wa KIA

Na Prisca Ulomi, WUUM, KIA
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amezindua safari za ndege za mizigo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara, wakulima wa mazao, matunda na mboga mboga wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Manyara na mikoa ya jirani kutumia usafiri huo kusafirisha mizigo yao kwenda nje ya nchi ya Tanzania.

Nditiye amesema kuwa uzinduzi wa safari za ndege za mizigo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe wakati akizindua bodi ya Maendeleo ya Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (KADCO) mwaka jana mwezi Desemba.

“Niwapongeze sana KADCO kupitia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wenu, Christopher Mukomu na kwa kushirikiana na Umoja wa Wakulima wa Mboga Mboga na Maua Tanzania (TAHA), mmeweza na kuhakikisha ujio wa ndege hii muhimu kwa ajili ya kusomba mizigo yetu hapa Tanzania, hilo kwangu mimi ni kitu kikubwa sana kwa sababu kwa miaka mingi hatukuwa na huduma ya mizigo kwa ndege kubwa kama hii, naipongeza sana Ethiopian Airline kwa utayari wao wa kushirikiana na Serikali na kuamua kuleta ndege yao ya mizigo kuja kubeba mizigo,” amesema Nditiye.

Pia, amekagua chumba cha barafu cha kuhifadhi mizigo inayosafirishwa na ndege kwenda nje ya nchi ya Tanzania na kujiridhisha kuwa chumba hicho cha kisasa kimejengwa, kinafanya kazi vizuri na kina uwezo wa kubeba tani 110 na kina hali nzuri na amewaomba wadau mbali mbali kutumia huduma hii kusafirisha mizigo yao badala ya kupitisha nchi za jirani.
 
Ameilekeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kukaa na wadau wa usafirishaji wa mizigo hiyo ili kuweza kutoa kibali cha muda mrefu cha wiki mbili au hata mwezi ili kuwawezesha wasafirishaji kutumia vizuri fursa hii na amewataka wazingatie sheria, taratibu na kanuni husika na siyo kutoa kibali tu, bali kutoa kibali cha kuhakikisha kuwa biashara hii inakuwa endelevu na kuzingatia usalama.

Nditiye ametoa maelekezo hayo baada ya Afisa Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacquline Mkindi kuiomba Serikali kuweka mazingira wezeshi ya usafirishaji wa mizigo kwenda masoko ya Ulaya ikiwa ni pamoja na ndege hizo kuja nchini kwa gharama nafuu kwa kupunguza tozo mbali mbali kwa ndege kila inapotua, kuongeza muda wa kibali cha ndege na kuwa na tozo tofauti baina ya ndege za mizigo na za abiria ili kuendelea kuzivutia ndege hizo na ndege nyingine za mizigo kuja KIA na kutumia fursa hiyo kuiwezesha sekta binafsi na wakulima wa mboga mboga na maua kufanya biashara kwenye soko lolote duniani.

Uzinduzi wa safari za ndege za mizigo umehudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ambapo ameshuhudia wakulima wa mboga mboga na maua wa TAHA wakipakia mizigo ya bidhaa zao kwenda nje ya nchi ambapo Nditiye na Hasunga wameshiriki kupakia mizigo hiyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi na wakulima na lazima sekta binafsi ikuzwe a ilelewe kwa kupewa mashaerti nafuu ya kufanya biashara zao na itaendelea kuunganisha mnyororo wa thamani kwa kutumia viwanja vyake vya ndege na kununua ndege za mizigo kama ambavyo Serikali imefanya kwa kununua ndege za abiria.

Nditiye amefafanua kuwa kwa muda mrefu ndege ya KLM imekuwa ikitumia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo Dar es Salaam kusafirisha mizigo kwenda nchi mbali mbali, Serikali imeanza kujenga chumba cha barafu cha kuhifadhi mizigo kwenye uwanja wa ndege wa Mbeya na katik mwaka wa fedha wa 2020/2021, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imetenga fedha ya kununua ndege ya kusafirisha mizigo


Share:

Wizara Ya Ardhi Yatoa Ufafanuzi Juu Ya Utoaji Huduma Kukabiliana Na Maambukizi Ya Virusi Vya Corona




Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne April 21






















Share:

Monday, 20 April 2020

SERIKALI YAJIPANGA KUZALISHA BARAKOA ZA KUTOSHA


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (kulia) akipata ufafanuzi kuhusu mtambo wa kutengeneza Barakoa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Uchapishaji cha Five stars, Bw. Ashik Abbas Karim (kushoto), leo Aprili 20, 2020 alipokua katika ziara ya Jijini Dar es Salaam ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa na Vitakasa Mikono. 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (katikati) akisikiliza kwa makini maelezo ya eneo la uzalishaji kutoka kwa Msimamizi wa Mradi wa Uzalishaji Vitakasa mikono kutoka Kampuni ya Total, Bw. Umesh Ankoleker (kulia) leo Aprili 20, 2020 alipokua katika ziara ya Jijini Dar es Salaam ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa na Vitakasa Mikono.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (katikati) akipata ufafanuzi kuhusu matumizi ya mashine ya Cherehani katika utengenezaji wa Barakoa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Uchapishaji cha Five stars, Bw. Ashik Abbas Karim (kushoto), leo Aprili 20, 2020 alipokua katika ziara Jijini Dar es Salaam ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa na Vitakasa mikono.

========  =======  =========

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa amebainisha kwamba Serikali imejipanga kuzalisha zaidi ya Barakoa Milioni tatu na nusu kwa mwezi ili kukidhi mahitaji ya Watanzania wote.

Hayo ameyasema leo Aprili 20, 2020 alipokua katika ziara ya Jijini Dar es Salaam ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa (face mask) na Vitakasa mikono (Hand sanitizer) ambapo kwa siku ya leo ziara hiyo imefanyika katika Kiwanda cha Uzalishaji cha Prestine, Kiwanda cha Uchapishaji cha Five stars na Kiwanda cha Uzalishaji Mafuta na Vilainishi cha Total.

Waziri Bashungwa ameeleza kwamba Uzalishaji wa Barakoa za kutosha kwa sasa ni muhimu sana na Serikali inahakikisha kwamba Viwanda hivi vinapata malighafi ya kutosha ili viendelee kuzalisha vizuri.

“Kiwanda cha Prestine sasa hivi kinatengeneza Barakoa elfu thelathini kwa siku (30,000) lakini baada ya vifaa kuingia kitazalisha elfu hamsini kwa siku (50,000) na Kiwanda cha Five Star kitazalisha barakoa laki moja kwa siku (100,000) hivyo kwa ujumla Viwanda hivi vitazalisha barakoa zisizopungua milioni tatu na nusu kwa mwezi mmoja (3,500,000) hii ni hatua muhimu sana.”alisema Waziri Bashungwa.

Akizungumza kuhusiana na ziara yake katika Kiwanda cha Total Waziri Bashungwa ameeleza kwamba Uongozi umekubali kushirikiana na Serikali katika kuzalisha vitakasa mikono na tayari maandalizi ya awali yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuangalia sehemu ambayo itatumika kwa ajili ya uzalishaji.

“Baada ya kuangalia Kiwanda na eneo maalumu ambalo wamelitenga kwa ajili ya uzalishaji wa vitakasa mikono, na kwa uwezo wa kiwanda hiki kwa siku kitakua na uwezo wa kutengeneza lita elfu sita (6000) ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kudhibiti ugonjwa huu.” Aliongeza Waziri Bashungwa.

Katika hatua ya mwisho Waziri Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuzingatia melekezo na kanuni za kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona (COVID -19).
Share:

WAGONJWA WAPYA 84 WA CORONA WAONGEZEKA TANZANIA,WANATOKA MIKOA MBALIMBALI IDADI YAFIKA 254


Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imethibitisha kuwepo kwa Wagonjwa wapya 84 wenye maambukizi ya Virusi vya Corona (COVID -19) nchini Tanzania. Kati ya hao wagonjwa 16 ni waliotolewa taarifa na Waziri wa Afya wa Zanzibar leo Aprili 20,2020. 




Share:

MBUNGE MMOJA WA BUNGE LA TANZANIA AKUTWA NA VIRUSI VYA CORONA


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Tulia Ackson, amesema kuwa mmoja wa Wabunge wa Bunge hilo amethibitika kuwa ana maambukizi ya Virusi vya Corona.

Taarifa hiyo ameitoa mchana wa leo wa Aprili 20, 2020, wakati akiahirisha Mkutano wa Tisa kikao cha 12 cha Bunge hilo Jijini Dodoma, na kuwataka Wabunge kuzingatia kanuni zote za afya zilizotolewa ikiwemo kila Mbunge kukaa kwenye kiti chake na siyo sehemu ya mtu mwingine.

"Tumepata taarifa kuwa mmoja wetu tayari amepata maambukizi ya COVID-19, mgonjwa huyo anaendelea vizuri na Serikali inaendelea kumuangalia na kumpatia matibabu stahiki, na maelezo ya Mbunge huyo alisafiri kwenda Dar es Salaam siku za hivi karibuni" ameeleza Naibu Spika.

Kwa mujibu wa Dkt Tulia ameeleza kuwa Mbunge huyo alianza kujisikia vibaya kuanzia Jumatano ya wiki iliyopita kwa kuona dalili zote za ugonjwa huo na hatimaye alipofanyiwa vipimo alibainika kuwa na ugonjwa huo.

"Kwa maelezo ya Mbunge huyo ni kwamba alisafiri kwenda Dar es Salaam na aliporejea kuanzia Jumatano alianza kuhisi dalili kama zilivyotangazwa na baada ya kupimwa ilithibitishwa kuwa amepata maambukizi ya virusi vya Corona" Naibu Spika-Tulia Ackson


Share:

MAASKOFU WAKAMATWA NA WAUMINI WAO KATAZO LA KUKUSANYIKA BALAA LA CORONA


Baadhi ya waumini waliokamatwa

Watu hamsini na tano (55) wamekamatwa na polisi Jumapili, Aprili 19 katika Kaunti ya Trans Nzoia nchini Kenya kwa kukiuka marufuku ya mikusanyiko ya Wizara ya Afya iliyotangazwa ili kujikinga na kuenea kwa COVID-19.

Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Nation nchini Kenya, waumini 41 kati yao ni washirika wa Kanisa la Kimataifa la Alpha Omega Healing Foundation na washiriki 14 ni wa Kanisa la Rapha Foundation, ambapo walikamatwa katika maeneo mawili tofauti.

Kamanda wa Polisi wa Trans Nzoia, Ayub Ali amesema kuwa Askofu wa Kanisa la Alphon Healing Foundation, Mchungaji Joram Solo alikamatwa katika eneo la Premium katika eneo la Tuwani akiwa na waumini 40 .

Kwenye Kanisa la Rapha Foundation, Askofu Harlington Olwenyi na Mchungaji Anjeline Olwenyi walikamatwa ndani ya mji wa Kitale pamoja na waumini wao 12.

"Tumeweka wote ndani ya kituo chetu wakati tunasubiri hatua inayofuata," amesema Kamanda Ali.

Nchi ya Kenya imetangaza kuwa na visa 281 vya watu walioambukizwa virusi vya Corona mpaka sasa, idadi ya waliopona imefikia 69 baada ya leo Aprili 20 kuongezeka watu wawili huku idadi ya vifa ikisalia 14.
Share:

WATEJA WA TIGO PESA SASA WANAWEZA KUTUMA NA KUPOKEA PESA KUTOKA M-PESA YA KENYA, MTN NCHINI UGANDA, AIRTEL NA MTN NCHINI RWANDA

Share:

WAGONJWA WA CORONA KENYA WAFIKA 281....NI BAADA YA WENGINE 11 KUONGEZEKA


Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe ametangaza visa vipya 11 vya COVID-19 nchini humo na idadi ya waathirika wa ugonjwa huo imefikia 281.

Wagonjwa wapya wote hawajasafiri siku za hivi karibuni, na watatu waliotokea Mombasa walikuwa karibu na Mgonjwa wa Corona aliyepoteza maisha wiki moja iliyopita

Mbali ya ongezeko la waathirika nchini humo, imetangazwa kuwa wagonjwa wawili wa COVID-19 wamepona na jumla ya waliopona nchini humo hadi sasa ni 69

Watu wapatao 13,872 wamepimwa tangu Virusi vya Corona viripotiwe kwa mara ya kwanza nchini humo

Idadi ya waliofariki dunia imebakia 14 na hakuna vifo vipya vilivyoripotiwa


Share:

VYAMA VYA SIASA VYATAKIWA KUWA NA OFISI NDOGO ZA MAKAO MAKUU JIJINI DODOMA

Na  Mwandishi Wetu - ORPP

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ametoa wito kwa vyama vya siasa kufungua ofisi za makao makuu Jijini Dodoma kwa kuwa ndiyo makao makuu ya serikali.

Wito huo umetolea na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alipotembelea ofisi ndogo za makao makuu ya Chama cha Wakulima (AAFP) jijini Dodoma hivi karibuni.

Nyahoza alisema kuwa Vyama vyote vya Siasa vinatakiwa kuwa na ofisi za makao makuu jijini Dodoma kwa kuwa ndiko shughuli zote za serikali zinapofanyka kutokana na serikali kuhamishia makao makuu yake jijini humo.

“Natoa wito kwa vyama vingine vya siasa ambavyo havina ofisi ndogo za makao makuu jijini Dodoma kufungua ofisi zao ukizingatia kuna vyama vya siasa ambavyo vinapata ruzuku ya Serikali ninategemea viwe na ofisi bora na nzuri hapa Dodoma kwa sababu uwezo huo wanao”, alisema Nyahoza.

Aliongeza kuwa awali vyama vya siasa vilifungua ofisi zao jijini Dar es Salaam kwa kuwa shughuli za kiserikali zilikuwa huko kabla ya kuhamishiwa Dodoma ambapo ndio makao makuu.

“Kama ambavyo mlienda kufungua ofisi za vyama vya siasa jijini Dar es Salaam kutokana na kuwa karibu na ofisi za serikali, natoa wito sasa kwa vyama hivyo kuja Dodoma na kufungua ofisi zao kwakuwa huku ndiko makao makuu ya nchi na Serikali”, alisisitiza Nyahoza.

Katika hatua nyingine Msajili huyo Msaidizi wa Vyama vya Siasa Sisty Nyahoza, amevitaka vyama vya siasa nchini kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa COVID -19 unaosambazwa na virusi vya Corona.

 “Kuna vyama vingine sasa hivi vinajiandaa kufanya mikutano mikuu ya kitaifa ya uchaguzi tunaomba hili jambo walizingatie kabisa kama ikiwezeka waahirishe mikutano kuepuka kuleta mikusanyiko kinyume na maelekezo ya Serikali badala yake wasogeze mbele mikutano hiyo.” Aliongeza Nyahoza.

Ziara hiyo ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutembelea ofisi ndogo za makao makuu ya vyama vya siasa zilizoko makao makuu ya nchi jijini Dodoma ni muendelezo wa zoezi wa uhakiki wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililoanza tarehe 17 Machi 2020. Katika ziara hiyo vyama viliyotembelewa jijini Dodoma ni pamoja na CCM, AAFP, NRA, CHADEMA, Demokrasia Makini na UMD.

Mwisho


Share:

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA YAKABIDHI TAARIFA KUHUSU MAPITIO YA SHERIA ZINAZOSIMAMIA UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imekabidhi Taarifa ya Mapitio ya Sheria Zinazosimammia Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi nchini kwa Waziri wa Katiba ba Sheria Dkt  Balozi Augustine Mahiga.

Taarifa hiyo imekabidhiwa kufuatia Tume ya Kurekebisha Sheria kufanya utafiti baada ya kupokea maelekezo ya Wizara ya Katiba na Sheria yakitaka kupitia Mfumo wa Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Tanzania.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 20 Aprili 2020 katika ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria zilizopo Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Mstaafu Januari Msofe alimkabidhi Waziri wa Katiba na Sheria Dkt  Balozi Augustine Mahiga.

Akielezea Utafiti wa Mapitio ya Sheria hiyo wakati wa makabidhaino ya Taarifa hiyo, Jaji Mstaafu Msofe alisema, katika kukamilisha mapitio ya sheria hiyo Tume ilikusanya maoni ya wadau mbalimbali kwenye mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Iringa , Mbeya , Songwe na Dar es Salaaam.

‘’Baada ya Tume kukusanya maoni ya wadau wakiwemo Majaji, Mawakili, Wasajili wa Mabaraza ya Ardhi, Wenyeviti wa Mabaraza  na  Wajumbe wa Kata na Wazee wa Mabaraza  Tume imebaini changamoto mbalimbali  zilizosababisha kutofikiwa malengo yaliyokusudiwa  ambayo ni mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi  wa haraka , haki  na unaofikika kwa urahisi’’ alisema Jaji Mstaafu Msofe.

Alizitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na Mamlaka za Kipekee za Mahakama za Ardhi ambazo utafiti wake ulionesha lengo kutofikiwa kutokana na kukosekana rasilimali fedha, watu na vitendea kazi sambamba na idadi ndogo ya mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya.

Aidha, Mwenyekiti wa Tume, ameeleza Uhuru wa Mahakama za Ardhi kuwa ni changamoto yenye kasoro kutokana na baadhi ya mahakama hizo kuwa chini ya mhimili wa serikali  na kutolea mfano wa Mabaraza ya  Ardhi ya Vijiji, Kata na Wilaya.

Hata hivyo, Jaji Mstaafu Msofe amezitaja changamoto nyingine kuwa ni kufikika kwa mabaraza ya kata na ya wilaya, Ada zitolewazo na mahakama za ardhi, lugha inayotumika kwenye mahakama za ardhi, vigezo vya wajumbe wa baraza la ardhi  la kijiji na kata, Uharaka katika kusikiliza na kuamua mashauri, Wazee wa Baraza katika mabaraza ya nyumba ya wilaya, miongozo katika utatuzi migogoro, utozaji ushuru wa hati za madai ya gharama na muongozo wa mwenendo wa maadili ya wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kijiji na mabaraza ya kata.

Kwa upande wake waziri wa Katiba na Sheria Dkt Balozi Augustine Mahiga aliipongeza Tume ya Kurekebisha sheria kwa kutekeleza kazi ya utafiti kuhusiana na sheria ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kubainisha kuwa kazi hiyo ni moja ya masuala mengi ambayo Tume inatakiwa kuyafanyia kazi huku Tume hiyo ikiwa na mzigo mkubwa wa kazi mbalimbali za mapitio ya sheria.

‘’Kama kuna sehemu ambayo Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inahitaji msaada basi ni katika eneo la Mapitio mbalimbali ya sheria ambazo nyingi zimepitwa na wakati na zinahitaji kupitiwa upya’’ alisema Dkt. Balozi Mahiga.

Naye Katibu Mkuu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Casmir Kyuki alisema kati ya ripoti ambazo tume imezifanyia kazi , Ripoti ya Utafiti Kuhusiana na Mapitio ya Sheria Zinazosimamia Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi imefanyika kwa haraka na kasi kubwa kufuatia mhimu wa sheria yenyewe sambamba na kutekeleza matakwa ya sheria kama inavyoelekeza.

Utafiti uliofanywa na Tume ni utekelezaji wa majukumu yake kama yalivyoanishwa katika kifungu cha 4 (1), (2) na (4) cha Tume ya Kurekebisha Sheria kinachotamka kuwa jukumu kubwa la Tume ni kufanya Mapitio, Utafiti na Kutathmini maeneo yote ya sheria zote za Tanzania Bara na kutoa mapendekezo serikalini ya namna ya kuboresha sheria hizo ili ziakisi mabadiliko yanayotokea.


Share:

Mwandishi Wa Habari Asimamishwa Kazi Zanzibar Baada Ya Kutoa Taarifa Za Mgonjwa Wa Corona Bila Ridhaa Ya Mhusika




Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger