Friday, 1 May 2026

RAIS SAMIA: MSIDANGANYIKE, HAKUNA USTAWI BILA AMANI NA UTULIVU WA TAIFA

...

  

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyakazi nchini kote kudumisha amani na utulivu akisisitiza kuwa hakuna ustawi wa mfanyakazi unaoweza kupatikana bila kuwepo kwa utulivu wa taifa. 

Aidha amewataka wafanyakazi nchini kuendelea kuchapa kazi na kwamba serikali itaboresha maslahi yao kadri uchumi unavyoendelea kuimarika.

Akizungumza mkoani Njombe kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), Rais alibainisha kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha tofauti zilizopo hazigeuki kuwa sababu ya kuhatarisha misingi ya umoja na mshikamano iliyoachwa na waasisi wa taifa.

“Sasa ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba tofauti zetu hazigeuki kuwa sababu ya kuhatarisha misingi ya amani, umoja na mshikamano tulioachiwa na waasisi wetu, tushikamaneni tufanye kazi, tujenge taifa letu na tujenge heshima ya nchi yetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo kuelekea Dira ya Taifa 2050 na kuwataka Watanzania kushikamana katika kuijenga heshima ya nchi.

Katika hatua nyingine, Rais Samia alieleza namna Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) wakiongozwa na Rais wa Shirikisho  hilo, Tumaini Nyamhokya walivyompa pole kwenye kikao chao cha pamoja na kumtaka Rais achape kazi, wafanyakazi mwaka huu watafunga mkanda kutokana na mambo iliyopitia nchi baada ya uchaguzi.  lilivyompa pole kwa mambo mazito ambayo nchi imepitia.

“Katika kikao kile walikuja kunipa pole (Tucta)… hawakuwa na madai mapya waliniambia ‘mama wewe chapa kazi tutakuja kukudai mwakani,’ na mimi nikawaambia mwakani ikiwa tutachapa kazi na uchumi utakuwa kwa kiwango kinachoridhisha tutakuja kuangaliana”.

“Nataka niwahakikishie kwamba pamoja na changamoto zilizopo kadri uchumi unavyoendelea kuimarika tutaboresha maslahi ya wafanyakazi wetu, nawaomba tuendelee kuchapa kazi kwa bidii, weledi na uzalendo wa hali ya juu, kwa kufanya hivyo tutaendelea kukuza uchumi wa nchi yetu na kugawana vizuri ile keki ya taifa kama matunda na juhudi ya jasho letu,” alisema.

Alisema serikali ilitumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye uchaguzi mkuu kwa vile uligharamiwa na serikali na kwa uharibifu uliotokea baada uchaguzi, kila fedha inayopatikana inatumika kwenye kurekebisha mali zilizoharibiwa na miundombinu iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha na kulipa madeni ya wafanyakazi na wakandarasi ili utakapoanza utekelezwaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uanze kukiwa na mwelekeo mzuri unaoleweka. 

“Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi kwa kadri uchumi utakavyoruhusu, tutaendelea kuchukua hatua zaidi za kuimarisha ustawi wa wafanyakzi na kwa hivyo ndugu zangu chapeni kazi serikali ipo inawasikiliza na inawathamani,” alisema.Licha ya kuyumba kwa uchumi duniani, Rais Samia amewahakikishia wafanyakazi kuwa serikali inathamini mchango wao na itaendelea kuboresha maslahi yao kadri hali ya kifedha itakavyotengamaa. 

Aidha Rais alieleza kwa ufupi mambo makubwa yaliyofanywa katika kipindi cha pili cha serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya kazi ni kutoa ajira 12,000 za ndani katika sekta ya umma ajira 12,000...“hii ni kwa ujumla mbali na ambazo zimetangazwa na watu wanaendelea kuomba,” alisema. 

“Lingine serikali imeendelea kuratibu upatikanaji wa ajira nje ya nchi na vijana wa kitanzania 7,593 tumewapatia ajira nje ya nchi, mipango ya kutafuta fursa zaidi za ajira nje ya nchi inaendelea ili kupunguza changamoto za ajira kwa vijana wetu… na katika hili nakubaliana na Tucta kwamba tunahitaji kuwa na utaratibu wa wazi na usimamizi madhubuti wa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ili kuhakikisha haki na maslahi yao yanalindwa ipasavyo,” alisema.

Aliishukuru Tucta kuanzisha kitengo maalumu cha kushughulikia masuala hayo na kuilekeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano kuratibu na kusimamia kikamilifu suala hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na balozi.

“...kuratibu na kuharakisha…  najua kuna maombi mengi kutoa nje wanataka wafanyakazi kwa hiyo mratibu na muharakishe vijana wetu wapate kazi nje lakini msimamie maslahi yao,” alisema. 

Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kukuza ujuzi,hususan kwa vijana, ili kuwaandaa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaohitaji maarifa, teknolojia na ubunifu.

“Dhamira ya Serikali ni kuona kila mfanyakazi anafanya kazi katika mazingira salama, yenye heshima, haki na yanayomwezesha kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa,”amesema Rais Dkt. Samia.

Kwa upande wa Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwepo kwenye sherehe hizo, aliwataka wafanyakazi kutokana tamaa na badala yake wawe wavumilivu wanapokuwa maeneo ya kazi.  

Akiwasilisha Risala kwa niaba ya Wafanyakazi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Ndugu Herry Mkunda, amepongeza jitihada za Serikali katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi, ikiwemo nyongeza ya mishahara, kuboresha mazingira ya kazi na majadiliano ya wadau wa utatu, huku akiiomba Serikali kuendelea kuimarisha hifadhi ya jamii, usalama kazini na fursa za ajira.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu, amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali imeimarisha huduma za jamii na mazingira ya uzalishaji, ikiwemo uwekezaji katika afya, elimu, miundombinu na sekta zakiuchumi zinazogusa moja kwa moja maisha ya wafanyakazi na wananchi.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dkt. Oscar Mgaya, amepongeza hatua za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na ajira, ikiwemo kuundwa kwaTume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, akisema hatua hiyo itaongeza uwekezaji wa sekta binafsi na kutengeneza fursa zaidi za ajira zenye staha.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Caroline Mugala, ameipongeza Tanzania kwa kuimarisha ajenda ya kazi zenye staha, haki za kijamii na majadiliano ya wadau wa utatu katika sekta ya kazi.

Ameongeza kuwa, ILO itaendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kazi zenye Staha, kuimarisha sheria na viwango vya kazi, kukuza ujuzi kwa vijana na wanawake, pamoja na kuimarisha mifumo salama ya ajira kwa Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi.









Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger