
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera akizungumza na waandishi wa Habari
Na Mbuke Shilagi Kagera.
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kurejesha zaidi ya shilingi milioni 624, kupitia kesi za rushwa ilizoshinda mahakamani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji na matumizi bora ya fedha za umma.
Akizungumza leo Mei 21, 2026, na vyombo vya Habari Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Bw. Leonard Swai, amesema kuanzia Julai 2025 hadi sasa taasisi hiyo imefungua jumla ya kesi 61 mahakamani, ambapo mashauri 52 tayari yamehitimishwa.
Amesema kati ya hayo, Jamhuri imeshinda kesi 50 sawa na asilimia 97, huku kesi mbili zikishindwa na nyingine tisa zikiendelea kusikilizwa mahakamani.
Amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026, TAKUKURU Kagera pia imepokea taarifa 132, ambapo 83 zilihusu rushwa na 49 hazikuhusu rushwa na kwamba taarifa zisizo za rushwa zilielekezwa kwa ushauri, huku zile za rushwa zikiendelea kuchunguzwa.
Aidha, majalada 12 yamefikishwa mahakamani kutokana na uchunguzi uliofanyika, huku mengine yakiendelea kushughulikiwa.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Wilaya ya Kyerwa imefanikiwa kurejesha shilingi milioni 30 zilizotolewa kama mkopo wa kikundi cha wanawake cha ufugaji nyuki cha Kata ya Katera kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Uchunguzi ulibaini kuwa kikundi hicho kilitumika kama kivuli cha upatikanaji wa mkopo, ambapo fedha zilihamishwa kutoka akaunti ya kikundi na kuingizwa kwenye akaunti binafsi ya Bw. Benjamin Barthazary, kisha kutumika kwa matumizi binafsi.
Kufuatia makosa hayo, TAKUKURU ilielekeza fedha hizo kurejeshwa katika Halmashauri ili ziwanufaishe walengwa halali, huku hatua za kisheria dhidi ya mtuhumiwa zikiendelea.
Wakati huo huo, TAKUKURU Wilaya ya Ngara imebaini dosari katika ujenzi wa msingi wa zahanati ya Kijiji cha Runzenze Kata ya Ntobeye, inayojengwa kwa nguvu za wananchi ambapo mchanganyiko hafifu wa zege ulisababisha msingi kuanza kuharibika kabla ya kukamilika.
TAKUKURU pia imesema imefuatilia matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 2.25 katika miradi 29 ya maendeleo, ambapo ilitoa ushauri wa marekebisho ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.
Bw. Swai amesisitiza kuwa TAKUKURU itaendelea kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma na kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.


0 comments:
Post a Comment