Friday, 8 May 2026

WAZIRI MKUU ATAKA WATENDAJI SERIKALINI KUTUMIA USHAWISHI KUVUTIA WAWEKEZAJI

...

Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba amewataka watendaji katika taasisi na mamlaka za Serikali wawe tayari kuwawezesha wawekezaji badala ya kuwadhibiti ili wavutiwe kuwekeza zaidi na zaidi.



“Nitoe wito kwa taasisi na mamlaka za Serikali, tumieni muda mwingi kuwawezesha wawekezaji badala ya kuwadhibiti. Washawishini waongeze uwekezaji badala ya kuwafanya waonekane wanaomba. Tumieni vivutio zaidi ili washawishike zaidi na zaidi,” amesema.


Ametoa wito huo leo (Ijumaa, Mei 8, 2026) wakati akizungumza na wadau waliohudhuria uzinduzi wa hoteli ya Mikumi Wildlife katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.


Amesema hoteli hiyo ambayo zamani ilikuwa inamilikiwa na serikali lakini ikapata janga la kuungua moto, ina historia ya miaka mingi; na ana imani na uwekezaji uliofanyika kwani umesaidia kuongeza ajira na kipato kwa wananchi.


“Sina shaka uwekezaji huu utaongeza mvuto kutokana na viwango vilivyopo kwenye hoteli hii. Viwango vya hoteli hii ni vya juu sana, ninaamini vitasaidia kuongeza muda wa watalii kukaa ndani ya hifadhi na uwepo wa malazi mazuri pia utaongeza idadi ya watalii,” amesema.


Akielezea juhudi za serikali kuboresha hifadhi ya Mikumi, Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa sh. bilioni 35 za kuboresha uwanja wa ndege wa Kikoboga na ifikapo Oktoba mwaka huu, utakuwa umekamilika.


Amezitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, TANAPA washirikiane na mamlaka nyingine za Serikali na kutumia fursa ya stesheni ya Kilosa ili kufungua njia na kuboresha miundombinu itakayorahisisha watalii kuingia katika Hifadhi ya Mikumi na hivyo kuongeza idadi ya watalii.


Ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii iendelee kubuni mikakati ya kwa kuhamasisha sekta binafsi iwekeza katika maeneo ya utalii huku akizitaka taasisi zote za umma ikiwa ni pamoja na mikoa yenye maeneo yaliyo na fursa za utalii ziendelee kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi. “Suala hili litekelezwe sambamba na kutangaza vivutio vilivyopo.”


Waziri Mkuu amewataka wadau wa utalii waweke mipango ya kuendeleza mazao mapya ya utalii yatakayochochea ongezeko la watalii na kuwahamasisha kuchagua kutembelea vivutio vilivyopo katika Kanda ya Utalii Kusini.


Ametumia fursa hiyo kumwelekeza Waziri wa Maliasili na Utalii aangalie namna ya kuongeza programu za utalii kwenye Chuo cha Ufundi (VETA) kilichopo Mikumi. “Waziri wa Utalii tuongeze programu nyingi za utalii ili vijana wa hapa wanufaike na rasilimali zilizopo katika eneo lao. Kwa maono ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, alitaka hivi vyuo vinapojengwa viweke programu kulingana na shughuli za kiuchumi za eneo husika kama vile utalii, uvuvi ili viwasaidie vijana wa maeneo husika.”


Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji alisema miaka ya nyuma hifadhi ya Mikumi ilikuwa ikipokea watalii 60,000 kwa mwaka lakini mwaka jana idadi ya watalii iliongezeka sana kufikia 174,808.


“Mapato yanayotokana na utalii yalikuwa sh. milioni 2.5 lakini nayo kwa mwaka jana yaliongezeka na kufikia sh.milioni 9.81. Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2026 idadi ya watalii waliofika kwenye hifadhi ya Taifa ya Mikumi walikuwa 151,275 na mapato yaliyokusanywa yalikuwa yamefikia sh. milioni 10.12,” alisema.


Alisema tayari sh. bilioni nne za kujenga geti upande wa Kilosa zimeshatolewa na ziko hifadhini tayari kuanza kazi hiyo ambapo mtu akishuka Kilosa kwa treni ya SGR atatumia dk.20 tu kuingia hifadhini.


Naye Bw. Simon Nguka, akisoma taarifa kuhusu mradi huo, alisema ujenzi na ukarabati wa hoteli hiyo yenye vyumba 48 na ambayo inamilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100, umetumia sh. bilioni 26.8.


Alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi 24 waliyonayo. Wellworth Group inamiliki mahoteli, loji, resorts na kambi za kitalii zenye uwekezaji wa thamani ya sh. bilioni 640.




Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger