Kampuni ya Mawasiliano ya MIC Tanzania Public Limited Company (Tigo), leo imetangaza rasmi kuungana na kampuni ya Zanzibar Telecom Public Limited Company (Zantel) baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria na kiumiliki ambapo lengo kuu ni kukuza na kuboresha huduma za mawasiliano nchini.
Pamoja na kupata vibali kutoka mamlaka zinazohusika, mchakato wa kuhamisha hisa na umiliki kamili kutoka Zantel kwenda Tigo sasa umekwisha kamilika. Kufuatia kukamilika kwa zoezi hili sasa makampuni haya yataunganisha shughuli zake za kiutendaji Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.
Akizungumza kuhusu muungano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Simon Karikari alisema hatua hiyo ina manufaa makubwa kwa Taifa; “Ninaamini kuwa kuunganishwa kwa kampuni hizi - Tigo na Zantel kutajenga huduma jumuishi kwa watanzania wote siku za usoni. Wateja wote wa Tigo na Zantel wataweza kufurahia huduma bora kutoka kwenye soko imara litakalosaidia kuchochea ubunifu kwenye sekta ya mawasiliano,” alisema Karikari.
Muunganiko wa makampuni haya mawili utasaidia katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja wa Tigo na Zantel waliopo kote Tanzania Bara na Visiwani. Aidha, muungano huu utawezesha kupanua wigo wa huduma zetu pamoja na kuongeza ubora wa upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ya mijini na vijijini. Vile vile muungano huu utasaidia katika usambazaji wa huduma za mawasiliano kwa makampuni na taasisi mbalimbali nchini na pia kupanua huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi.
Tunategemea mafanikio chanya kutokana na muunganiko wa makampuni haya mawili wenye lengo la kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa.
Zoezi la kuunganisha taratibu za kiutendaji wa makampuni haya mawili zinatazamiwa kuanza hivi punde. Aidha, wateja wa Tigo na Zantel wataendelea kupata huduma bila usumbufu wowote kutoka mtandao husika kwani namba na laini za wateja hazitabadilika.
Mwisho