Thursday, 15 August 2019

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu ATENGUA Agizo la Mkuu wa Wilaya Kutaka Watumishi Wachangie Fedha Kununua Mashine ya Ultra Sound Iliyoibiwa

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini ametengua agizo la Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga la kutaka Wafanyakazi wote wa Hospitali ya Wilaya hiyo,kuchangishwa fedha kulingana na kiwango cha mshahara ili kununua mashine mpya ya Ultra sound kufidia mashine iliyoibiwa.

“Kuchangisha watumishi wote sio sahihi, kuna wengine walikuwa likizo na watakuwa wanaingizwa kwenye tukio ambalo pengine hawahusiki, Serikali ina vyombo vya uchunguzi, na tukio hilo ni moja ya kazi yao, Polisi ianze uchunguzi akibainika anayehusika achukuliwe hatua"  Amesema Sagini

Katika kikao chake na watumishi wa hospitali hiyo kilichofanyika jana,  Mkuu huyo wa Wilaya  Festo Kiswaga alitoa siku saba kwa watumishi wote kuchanga kulingana na mishahara kwa kila mmoja kuhakikisha wananunua mashine hiyo.
 

Kiswaga alimtaka Mganga Mkuu wa Halmashuari hiyo na  Mkurugenzi wa Halmashuari kuhakikisha ikifika Agosti 21, wapeleke mashine hiyo Ofisini kwake.

“Kwa kuwa mashine hii iliibiwa mchana na ikaibiwa na vifaa vyake vyote, inaonyesha kuwa waliohusika ni wataalamu na kwa maana hiyo watumishi wote 137 wa hospitali hii mnahusika na wizi huu, hivyo nyie ni watuhimiwa wa kwanza wa wizi huu. 


“Kila mmoja kuanzia kwa Mganga Mkuu wa Halmashuari mtachangia kulingana na kila mtu na mshahara wake, nataka ndani ya siku saba nikabidhiwe hiyo mashine, ambaye atagoma kuchangia huyo itakuwa halali yangu,” alisema Kiswaga.


Share:

Baba Mtakatifu Francis Akubali ombi la Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kustaafu. Rasmi nafasi yake ya Askofu Mkuu Jimbo la Dar Es Salaam

Baba Mtakatifu Francis amekubali ombi la Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kustaafu rasmi nafasi yake ya Askofu Mkuu Jimbo la Dar Es Salaam.

Nafasi hiyo  itachukuliwa na Askofu Mkuu Mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwai'chi kuendelea kuongoza Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.


Share:

WAZIRI MKUU AWAOMBA WAWEKEZAJI KUTOKA NJE YA NCHI KUCHANGAMKIA FURSA TANZANIA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungazo wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaomba wawekezaji kutoka nje ya nchi kuchagamkia fursa zilizoko nchini baada ya vikwazo vilivyokuwepo hapo awali kuondolewa.

Waziri mkuu ametoa kauli hiyo jana akiwa mkoani Kagera katika uzinduzi wa wiki ya uwekezaji ambapo amesema kuwa wawekezaji toka nje ya nchi wasiogope kuja kuwekeza hapa nchini kwani tayari fulsa ni nyingi ikiwemo ya viwanda, utalii, madini,na uvuvi .

Amewaomba wawekezaji wajitokeze kwa wingi na kuanza mchakato wa kupitia mfumo wa tehama unaowezesha vitu vingi vya uwekezaji kufanyika kwa njia ya mtandao.

Mkuu wa mkoa Kagera Brigedia Generali Marco Elisha Gaguti amesema maeneo makubwa ya uwekezaji yapo katika sekta za kilimo,utalii,ufugaji,uvuvi,viwanda,misitu,madini na huduma za kijamii.

Wiki ya uwekezaji Kagera iliyoanza august 12 mwaka huu itahitimishwa august 17 mwaka huu ambapo shughuli mbalimbali ikiwemo kutambua maeneo ya uwekezaji ,namna ya kuwekeza yanajadaliwa na wadau ili kuona namna ya kuwekeza katika maeneo hayo.
Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog



Share:

UPDATES: Waliofariki Ajali ya Moto wa Lori la Mafuta Morogoro Wakifa 89

Majeruhi saba kati 32 wa ajali ya lori la mafuta ya petroli iliyoanguka na kulipuka mkoani Morogoro waliokuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam nchini Tanzania wamefariki dunia.

Hii ina maana kuwa waliofariki kutokana na ajali hiyo iliyotokea Jumamosi iliyopita ya Agosti 10, 2019 eneo la Msamvu mkoani Morogoro hadi kufikia saa 5.30 asubuhi  ya leo Alhamisi Agosti 15,2019 ni 89.

Akitoa taarifa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (MNH), Aminiel Aligaesha amesema kwa sasa wamebaki majeruhi 25 kati ya 46 waliopokelewa hospitalini hapo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Morogoro.

Amesema kati ya majeruhi hao 16 wapo katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) huku wengine tisa wakiendelea kupatiwa matibabu katika wodi maalum iliyotengwa kwa ajili ya majeruhi hao.

“Serikali imeahidi wanaozikwa Morogoro itagharamia mazishi lakini kwa wanaotaka kwenda Mikoa mingine kama Moshi, Tanga wanajigharamia wao ila serikali itatoa sanda na sanduku tu,” amesema.


Share:

WAZIRI MKUU AAGIZA WAFUGAJI KUACHA TABIA YA KUCHORA CHORA NG'OMBE



Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewaagiza wafugaji wa ng’ombe mkoani Kagera kuacha mara moja vitendo vya kuchora chora ng'ombe kwa kuwawekea alama za manundu vidonda badala yake watumie pete ya sikioni ili kuongeza ubora na thamani utakaowavutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Waziri Majaliwa ametoa agizo hilo Agosti 14,2019 katika uzinduzi wa Mwongozo wa wiki ya uwekezaji Kagera uliofanyika katika uwanja wa Gymkana uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera

Waziri mkuu amesema kuwa wafugaji walio wengi wamekuwa na utamaduni wa kuchora chora mifugo hao jambo linalosababisha kukosekana kwa soko la nje kwa wahitaji ambapo wahitaji hudai kuwa Ng’ombe hao hawana mvuto na ubora kwa kuonekana na vidonda ambavyo ni alama zisizofaa.

Kufuatia Agizo amewataka wafugaji kubadilika kwa kutumia lanchi za wilaya na kuacha kuzunguka zunguka na mifugo badala yake waiache mifugo hiyo ikue iwe katika ubora unaohitajika.

Hata hivyo ametoa kibali kwa wawekezaji kutoka nje kuwekeza mkoani Kagera kwa kujenga viwanda vya kuchakata Nyama Ngozi na kwato kwa kufuata utaratibu wa kiserikali usio na masharti magumu

Uzinduzi huo wa Mwongozo wa wiki ya uwekezaji Kagera umeudhuliwa na Magavana wa nchi ya Burundi, mabalozi kutoka Nchi za Kenya Uganda Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wajasiliamali mbali mbali toka ndani na nje ya nchi pamoja na , wakuu wa mikoa ya Tanzania, ambapo wiki hii ina lengo la kutangaza fulsa zilizopo Kagera na imeanza Agosti 12 mwaka huu itamalizika August 17 mwaka huu.
Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog
Share:

Picha : TUME YA UCHAGUZI YAKUTANA NA WADAU SHINYANGA..UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA KUFANYIKA AGOSTI 26 HADI SEPT 1,2019

Kamishina wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa nchini Tanzania,Mhe. Balozi Omari Ramadhani Mapuri amefungua mkutano wa wa Tume na Wadau wa Uchaguzi katika mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Mkutano huo umefanyika leo Alhamis Agosti 15,2019 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na kuhudhuriwa na mkurugenzi wa uchaguzi,mratibu wa uandikishaji wa mkoa,viongozi wa dini,vyama vya siasa,wawakilishi wa watu wenye ulemavu,vijana,wanawake,asasi za kiraia,watendaji wa tume na waandishi wa habari.

Balozi Mapuri alisema lengo la mkutano huo ni kupeana taarifa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ulioanza kwa awamu ya kwanza tarehe 18 Julai,2019 katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Alisema uzinduzi rasmi wa zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura ulifanyika Mjini Moshi Julai 18 ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na kwamba katika mkoa wa Shinyanga uboreshaji wa daftari la wapiga kura utafanyika Agosti 26 hadi Septemba 1,2019.

"Lengo la kukutana nanyi leo ni kuwafahamisha kuwa tume imekamilisha maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,ikiwemo uhakiki wa vituo vya kujiandikisha,uandikishaji wa majaribio,maandalizi ya vifaa vya uboreshaji wa daftari,maandalizi ya vifaa vya uboreshaji na mkakati wa elimu ya mpiga kura naamini mafanikio ya zoezi hili yanategemea nyinyi wadau",alieleza.

"Tume inatarajia kuanza uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa awamu ya nne katika mikoa ya Mwanza (halmashauri ya wilaya Kwimba),mkoa wa Shinyanga na mkoani Geita (Halmashauri ya Mji wa Geita,Nyang'wale,Bukombe na Mbogwe) kuanzia Agosti 26 hadi Septemba 1,2019",aliongeza.

Alifafanua kuwa uboreshaji wa daftari la wapiga kura unafanyika kwa kutumia teknolojia ya kielektroniki ya Biometriki (BVR) ambayo huchukua taarifa za kibaiolojia za mtu na kuzihifadhi katika Kanzidata(Database) kwa ajili ya utambuzi.

"Uboreshaji wa daftari la wapiga kura wa safari hii hautahusisha wapiga kura walioandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2015 ambao kadi zao hazihitaji marekebisho yoyote ya taarifa.Uboreshaji huu utawahusu wapiga kura wapya ambao wametimiza umri wa miaka 18 na wale ambao watatimiza umri wa miaka 18 siku ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.",alisema Balozi Mapuri.

Alisema uboreshaji huo pia utahusisha watu ambao wamehama kutoka maeneo yao ya awali na kuhamia maeneo mengine ya uchaguzi na wale ambao kadi zao zimeharibika au kupotea na wale ambao wanatakiwa kufutwa kwenye daftari baada ya kupoteza sifa wakiwemo waliofariki dunia.

Kwa upande wake, Afisa Tehama Mwandamizi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Frank Mhando aliwataka watu wenye sifa ya kujiandikisha wajitokeze kwa wingi ili waandikishwe na wanaohitaji kuboresha taarifa zao wakati ndiyo huu.

Alisema kila chama cha siasa kina wajibu wa kuweka wakala kwenye kituo cha uandikishaji daftari la wapiga kura huku akikisisitiza kuwa wakala hapaswi kuingilia majukumu ya tume ya uchaguzi na kwamba yeyote atakayeleta masuala ya siasa kwenye vituo atachukulia hatua.

Aliwataka wanasiasa kuepuka kufanya siasa kwenye vituo bali majukumu yao yawe ni kuwatambua wenye sifa ya kujiandikisha wapate sifa ya kupiga kura wakati wa uchaguzi.

"Hakuna uchaguzi bila wapiga kura,hakuna kupiga kura bila kujiandikisha,niwaombe wanasiasa mhamasishe watu wajitokeze kwenda kujiandikisha ili wawe na sifa ya kupiga kura",aliongeza.

ANGALIA PICHA
Kamishina wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa nchini Tanzania,Mhe. Balozi Omari Ramadhani Mapuri akifungua mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi katika mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura leo katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Kamishina wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa nchini Tanzania,Mhe. Balozi Omari Ramadhani Mapuri akifungua mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi katika mkoa wa Shinyanga.
Afisa Tehama Mwandamizi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Frank Mhando mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi katika mkoa wa Shinyanga.
Afisa Tehama Mwandamizi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Frank Mhando akiwataka watu wenye sifa ya kujiandikisha wajitokeze kwa wingi ili waandikishwe kwenye daftari la wapiga kura.
Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga,Charles Shigino akiiomba Tume ya uchaguzi kuruhusu mikutano ya hadhara ili wanasiasa waelimishe/wahamasishe wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Katibu wa Chama cha ACT-Wazalendo mkoa wa Shinyanga Sebastian Tafuta akichangia hoja wakati wa mkutano huo.
Wadau wa uchaguzi wakiwa ukumbini.
Wadau wa uchaguzi wakiwa ukumbini.
Wadau wa uchaguzi wakiwa ukumbini.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Share:

Katibu Mkuu CCM Dk. Bashiru Ally Awajulia Hali majeruhi waliopata ajali ya moto wa lori la mafuta Morogoro

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema ni vyema Serikali ikaona umuhimu wa kutenganisha barabara za kupita magari ya mizigo na ya kawaida ili kuepusha hatari kwa wananchi.

Dk. Bashiru aliyasema hayo jana wakati alipotembelea majeruhi waliopata ajali ya moto wa lori la mafuta lililoanguka mkoani Morogoro.

Mbali kutembelea majeruhi waliolazwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, pia alitembelea chumba cha kuhifadhia maiti, kuomba dua makaburini na eneo la Itigi-Msamvu ambako lori hilo lilipinduka kabla wananchi hawajalivamia kuiba mafuta na baadaye moto kulipuka.

Alisema kutenganishwa huko kutasaidia magari makubwa kutopita maeneo ya makazi ya watu na hata kukitokea majanga kama ya moto, wananchi hawataweza kupata madhara.

Hata hivyo, aliishauri Serikali kuweka utaratibu wa kutoa elimu ya majanga ya moto ili wananchi waweze kuwa na uelewa mara zote na kuweza kukaa mbali na matukio ya moto ikiwemo yanapoanguka magari ya mafuta.
Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally (katikati) na Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Ndg. Shaka Hamdu Shaka (wa kwanza kushoto) wakiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro leo Agosti 14, 2019 ambapo wamewajulia hali majeruhi wa ajali ya moto waliolazwa katika hospitali hiyo


Share:

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA ATANGAZA KUONDOA VIKWAZO VINAVYOWAKABILI WAFANYABIASHARA KAGERA


Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe. Innocent Bashungwa(Mb)Kagera ametangaza kuondoa vikwazo vinavyowakabili wafanya biashara wadogo na wa kati mkoani Kagera.

Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo wakati akiwa mkoani Kagera katika uzinduzi rasmi wa mwongozo wa wiki ya Kagera uliofanyika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Waziri huyo amesema ili kuweka urahisi katika biashara kwa wenye viwanda vidogo vidogo na wa kati hasa akina mama na vijana tayari serikali imeondoa kodi 54 ili waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri yatakayowawezesha kuchangia pato la Taifa.

Waziri Bashungwa amesema awali kumekuwepo na utitiri wa kodi kwa wafanya biashara jambo lililosababisha mikwamo katika sekta hiyo.

Amewataka wafanya biashara mkoani Kagera kufanya za uzakishaji kwa kuzalisha biashara zenye tija na zenye masoko nchi za nje kwani tayari nchi mbali mbali za nje zina uhitaji na bidhaa za Tanzania.

Amewahimiza wafanya biashara hao kutumia wiki hiyo ya uwekezaji kuwa chachu ya kuzalisha bidhaa mbali mbali na kutangaza fulsa zilizopo mkoani Kagera.

Hata hivyo ametoa pongezi kubwa kwa Rais Magufuli kwa kumteua kuwa Waziri wa viwanda na biashara huku akihaidi ushirikiano mkubwa kati yake na Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Marco ili kuitangaza Kagera kuwa sehemu yenye chachu katika uchumi endelevu kwa maslahi ya watanzani wote na wawekezaji toka nje ya nchi.
Na Lydia Lugakila - Malunde1 blog

Share:

Lugha Ya Kiswahili Yasubiri Baraka za Marais Ili Iwe Lugha Rasmi ya SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Tanzani imepata heshima ya pekee kwa hatua ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kukubali kukiidhinisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya jumuiya hiyo.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao cha siku mbili cha mawaziri hao, Profesa Kabudi ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa kamati ya mawaziri wa SADC kwenye mkutano wa 39 unaoendelea jijini Dar es Salaam alisema hatua hiyo ni heshima ya pekee kwa Tanzania, ambayo imefanya akzi kubwa katika ukombozi wa n chi za Kusini mwa Afrika.

“Tunawshukuru mawaziri wa Sadc kwa maamuzi mliyochukua kuikubali lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha ya ukombozi, ambayo wapigania uhuru wawe wa Frelimoi, wawe wa Swapo, wawe wa Zani-PF, wawe wa ZAPU, wawe wa ANC, PAC au MPLA waliitumia.

 “Mumekubali kuwa ndiyo lugha waliyoitumia kujifunza mbinu za kivita na mbinu za medani, kisha kukabiliana na wakoloni wa Kireno, kukabiliana na utawala ubaguzi wa rangi wa makaburu Afrika Kusini na kukabiliana na Ian Smith na leo mataifa yao yako huru,” alisema.

Alisema kwa hatua hiyo, japokuwa uamuzi huo wa mawaziri unasubiri kupitishwa kwenye kikao cha marais kitakachofanyika Agosti 17 na 18, wamempa heshima kubwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikifanya Kiswahili kuwa lugha ya ukombozi, kwa kukubali kukifanya rasmi kuwa lugha maalumu ya SADC, baada ya Kiingereza, Kifaransa na Kireno.

Profesa Kabudi alisema katika hatua nyingine, mawaziri hao kw apamoja wamekubaliana kuwa upo umuhimu wa kuhakikisha vikwazo ilivyowekewa Zimbabwe na baadhi ya mataifa vinaondolewa kwa sasa, kwa kuwa tayari hali ya nchi hiyo imeshabadilika.

“Tumekubaliana kuwa katika mwaka huu ambao Tanzania inakuwa mweyekitio wa SADC, tutasimamia kuondoa vikwazo kwa Zimbabwe ambayo inakabiliwa na vikwazo kutoka kwa baadhi ya mataifa, kwa kuwa tayari mambo yameshabadilika na uchaguzi umeshafanyika kwa hiyo haina sababu ya kuendelea kuwepo,” alisema

Alisema kuwa vikwazo hivyo vinasababisha taabu kwa wanawake na watoto hivyo tumependekeza kuwa vikwazo hivyo viondolewe, kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika  kuihimiza jumuiya ya kimataifa.


Share:

Waziri wa Kilimo: Tutaimarisha Biashara Za Mazao Katika Nchi Ya SADC

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Serikali imesema kuwa imejipanga kuimarisha biashara ya mazao ya Kilimo na mengineyo kwa nchi wanachama wa SADC ili kuwanufaisha wakulima katika nchi hizo.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo Leo tarehe 15 Agosti 2019 wakati akizungumza Mubashara (Live) kwenye kipindi cha Clouds 360 kilichorushwa na Clouds TV wakati wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi 16 wanachama wa SADC katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Center.

Amesema kuwa zaidi ya watanzania Milioni 50 nchini wanategemea chakula hivyo lazima kubadili mbinu za uzalishaji katika mazao ya kilimo kwa kuongeza tija kupitia teknolojia mpya ili kuwa na uzalishaji mkubwa na wenye tija.

Mhe Hasunga alisema kuwa Malighafi zinazohitajika zaidi ya Asilimia 66 zinatokana na mazao ya Kilimo hivyo ukamilisho wa serikali ya viwanda unaungwanishwa kwa ukaribu na sekta ya kilimo.

Waziri huyo wa Kilimo Mhe Hasunga, alisema Mkutano wa SADC ni fursa kwa wakulima wa Tanzania kwa kuwa wageni wote waliowasili na watakaoendelea kuwasili watahitaji kula vizuri hivyo mkutano huo ni sehemu ya kuimarisha na kutangaza masoko ya mazao mbalimbali hususani vyakula vya asili.

Aidha, Utoshelevu wa chakula nchini ni asilimia 119 ukilinganisha na mwaka jana ambapo ilikuwa asilimia 124 hivyo serikali imefungua mipaka ya kuuza mazao nje ya nchi lakini pia ni lazima kuwa na kumbukumbu muhimu za taarifa zote za usafirishaji wa mazao.

Mhe Hasunga alisema kuwa ni wakati wa nchi za Afrika Mashariki na nchi zote za SADC kuanza kutumia masoko ya ndani ya nchi katika mazao ya Kilimo na mengineyo kuliko kutegemea kuagiza katika nchi zingine nje ya Afrika.

Alisema kuwa kufanya hivyo kutaimarisha masoko ya mazao mbalimbali nchini hivyo kuwaimarisha wakulima katika Kilimo chao na kuwa na kipato kikubwa kinachokidhi mahitaji ya kula mkulima ikiwa ni pamoja na uimara wa ucumi wa nchi.

MWISHO.


Share:

VIDEO: Rais Ramaphosa Wa Afika Kusini akutana na Rais Magufuli- Ikulu

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amemtembelea Rais  Magufuli  katika Ikulu ya Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 15,2019.

Rais Ramaphosa ameongozana na mke wake, Dk Tshepo Motsepe ambao wamepokelewa na mwenyeji wao, Rais Magufuli na mkewe, Janeth katika viwanja vya Ikulu.

Mara baada ya kuwasili, Kiongozi huyo wa Afrika Kusini amepata heshima ya kupigiwa wimbo wa taifa na mizinga pamoja na kukagua gwaride maalum lililoandaliwa kwa ajili yake.


Share:

Watumishi waamuriwa kujichangisha kununua mashine ya ultrasound iliyoibiwa Hospitalini

Kufuatia mashine ya Ultra sound kuibiwa katika Hospitali ya Wilaya Bariadi, Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga ameagiza wafanyakazi wote wa Hospitali hiyo kuchangishwa fedha kulingana na kiwango cha mshahara ili kununua mashine mpya yenye thamani ya Tsh. Million 30 .

Kiswaga ametoa siku saba kwa watumishi wote kuchanga kulingana na mishahara kwa kila mmoja kuhakikisha wananunua mashine hiyo.

Kikao hicho ambacho kilifanyika jana katika ukumbi wa hospitali hiyo, Kiswaga alimtaka Mganga Mkuu wa Halmashuari hiyo, Mkurugenzi wa Halmashuari kuhakikisha ikifika Agosti 21, wapeleke mashine hiyo Ofisini kwake.

“Kwa kuwa mashine hii iliibiwa mchana na ikaibiwa na vifaa vyake vyote, inaonyesha kuwa waliohusika ni wataalamu na kwa maana hiyo watumishi wote 137 wa hospitali hii mnahusika na wizi huu, hivyo nyie ni watuhimiwa wa kwanza wa wizi huu.

“Kila mmoja kuanzia kwa Mganga Mkuu wa Halmashuari mtachangia kulingana na kila mtu na mshahara wake, nataka ndani ya siku saba nikabidhiwe hiyo mashine, ambaye atagoma kuchangia huyo itakuwa halali yangu,” alisema Kiswaga.

Aidha alisema tabia ya wizi katika hospitali hiyo imekuwa sugu ambapo wahusika wakuu wamekuwa watumishi wake, hali ambayo alieleza hawezi kuivumilia kama kiongozi wa Wilaya.

“Siyo mara ya kwanza kutokea wizi kwenye hospitali hii, mlihusika na wizi wa darubini (Microscope) ambapo baadaye ilipatikana ikiwa juu ya mti imeninginizwa, mkaiba tena mashine ya kufulia nguo ambayo mpaka sasa haijapatikana na leo tena Ultrasound hii haiwezekani na wala haikubaliki,” aliongeza Kiswaga.

Alisema kitendo hicho ni uhujumu uchumi hivyo watumishi wote lazima wahusike katika kuhakikisha mashine hiyo inarudishwa kwa gharama zao.


Share:

Majeruhi Wengine 3 ajali ya Moto Morogoro Wafariki Dunia

Majeruhi watatu kati ya 32 waliokuwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam  wamefariki dunia.
 
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Kebwe amesema majeruhi hao wamefariki jana jioni Jumatano Agosti 14, 2019 hivyo kufanya  idadi ya waliofariki kufikia 85.

Mkuu huyo wa mkoa amesema majeruhi 16 waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro wanaendelea vyema huku akiwaomba ndugu kujitokeza kuwajulia hali majeruhi hao pamoja na wale waliopo Muhimbili.


Share:

Rais Cyril Ramaphosa Wa Afrika Kusini Alivyowasili Nchini Kwa Ziara Rasmi Ya Siku Mbili

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na mkewe Dkt. Tshepo Motsepe wakiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius  Nyerere jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo. Rais Ramaphosa amewasili kwa ziara rasmi ya siku mbili nchini kabla ya kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama za Jumuiya ya Maendeleo  ya Kusini kwa Afrika SADC

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusine akipokewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius  Nyerere jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo. Rais Ramaphosa amewasili kwa ziara rasmi ya siku mbili nchini kabla ya kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini kwa Afrika SADC
 


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger