Na Frank Mvungi- MAELEZO, Morogoro
Waandishi wa Habari nchini wameaswa kuzingatia uzalendo na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao wakati wote wa kuripoti habari zinazohusu fursa zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na mkutano wa wakuu wa nchi wanachama utakaofanyika Jijini Dar es Salaam Agosti 17 na 18, 2019.
Waandishi wa Habari nchini wameaswa kuzingatia uzalendo na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao wakati wote wa kuripoti habari zinazohusu fursa zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na mkutano wa wakuu wa nchi wanachama utakaofanyika Jijini Dar es Salaam Agosti 17 na 18, 2019.
Akizungumza leo mjini Morogoro wakati akifungua awamu ya kwanza ya mafunzo yakuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kuandika na kuripoti habari za Jumiya hiyo, Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza amesema kuwa mkutano wa Wakuu wa nchi wanachama unakuja na fursa nyingi zitakazowanufaisha wananchi wote.
“ Tunawaomba Waandishi wa Habari kutekeleza jukumu la kutangaza habari zinazohusu SADC kwa uzalendo, weledi na kwa ufanisi ili watanzania waweze kushiriki kikamilifu kutokana na umuhimu wa Jumuiya hii na kutumia fursa za kiuchumi na biashara zinazopatikana kupitia wananchi takribani milioni 450 wa nchi zote za SADC”Alisisitiza Mhe Shonza
Akifafanua Mhe Shonza amesema kuwa kila mwandishi wa habari analo jukumu la kuhakikisha kuwa kila mwananchi anafahamu fursa zilizopo katika Jumuiya hiyo na mamna zinavyoweza kuwanufaisha wananchi wote katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
Aliongeza kuwa waandishi wa habari wa Tanzania kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na uelewa wa pamoja wakati wa mkutano huo kwa kutambua kuwa wao ni daraja kati ya wananchi na Serikali pamoja na Jumuiya zote ambazo Tanzania ni mwanachama ikiwemo SADC.
“Ni matumanini yangu kuwa baada ya mafunzo haya mtawaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa SADC kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi wanachama, fursa za kiuchumi, Namna nchi yetu inavyotekeleza mikakati mbalimbali ya SADC, Fursa za masoko ndani ya SADC kutokana na bidhaa na mazao ya kilimo yanayozalishwa katika nchi wanachama” Alisisitiza Mhe Shonza
Katika kusisistiza umuhimu wa amani na utulivu Mhe. Shonza aliwaasa wanahabari kuwaelimisha wananchi umuhimu wa amani kipindi choche cha mkutano huo wa wakuu wa nchi wanachama na hata baada ili kuendelea kujenga taswira nzuri ya Tanzania.
Baadhi ya fursa zinazotokana na mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo utakaofanyika mwezi ujao hapa nchini ni pamoja na usafiri na usafirishaji, malazi na utalii kwa wageni hao zaidi ya 1000 wanaotarajiwa kuja hapa nchini kutokana na mkutano huo.
Aidha, Mheshimiwa Shonza aliwataka waandishi wote wa habari hapa nchini kutumia nafasi zao kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani iliyopo hapa nchini ambayo ni moja ya kivutio kikubwa kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali kuja na kuwekeza hapa nchini.
“ Sitarajii mwandishi wa habari wa Tanzania kutumia kalamu yake kuchafua taswira ya nchi yetu katika kipindi hiki cha mkutano huu mkubwa na hata baada ya mkutano, matarajio ya Serikali ni kuendelea kuona mnatangaza mafanikio ya Jumuiya na fursa zilizopo ili ziweze kuwanufaisha wananchi” Alisisitiza Mhe. Shonza
Katika kutekeleza jukumu hilo amewaasa waandishi hao kuzingatia kuwa jukumu la kutangaza fursa zilizopo katika Jumuiya hiyo ni la kila mwanahabari ili kuwajengea uelewa wananchi juu ya namna watakavyoweza kunufaika na idadi kubwa ya wananchi waliopo katika jumiya hiyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) linalodhamini mafunzo hayo kwa kushirikiana na Sekretarieti ya SADC, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw. Dagmore Tawonezvi amesema kuwa mafunzo hayo yanatokana na maombi ya Serikali ya Tanzania na yatasaidia kujenga uelewa kuhusu fursa zilizopo na namna ya kuzitumia ili kuchochea maendeleo hapa nchini na katika nchi wanachama wa SADC.
Aliongeza kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na nchi wanachama kujenga uwezo kwa waandishi wa habari ili waweze kutangaza na kuwaelimisha wananchi kuhusu jumuiya hiyo na manufaa yake katika kukuza uchumi.
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi Agnes Kayola amesema kuwa mafunzo hayo yanafanyika kwa awamu mbili zitakazoshirikisha waandishi wa habari 30 kwa kila awamu.
Mkutano huo utatanguliwa na maonesho ya wiki ya viwanda yatakayotumika kutangaza bidhaa zinazozalishwa hapa nchinina nchi za SADC kwa madhumuni ya kuhamasisha ukuaji wa viwanda katika nchi za SADC .
Mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo unafanyika Tanzania mwezi Ujao ambapo Tanzania inatarajiwa kupokea wageni zaidi ya 1000 kutoka nchi wanachama wa SADC, katika mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatarajia kuwa mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2019 hadi Agosti 2020.
Mkutano huo wa wakuu wa nchi wanachama utakuwa na kauli mbiu ”Mazingira wezeshi ya Kibiashara kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda” utatanguliwa na vikao vya awali vya ngazi ya Makatibu Wakuu na Mawaziri wa SADC, Unatarajiwa kuhudhuriwa na wakuu wa nchi 16 wanachama wa SADC .