Kumeshuhudiwa kizazaa kwenye mtaa mmoja nchini India baada ya jamaa aliyedhaniwa kufariki 'kufufuka' wakati wa shughuli ya mazishi yake.
Mohammad Furqan, kutoka mtaa wa Uttar Pradesh, alikuwa amelazwa katika hospitali moja mnamo Juni 21, 2019 na akatangazwa kufariki.
Kulingana na gazeti la Hindustan Times, Furqan alikuwa amehusika katika ajali ya barabara iliyomwacha katika hali mbaya.
Huku akiwa amelazwa kwenye hospitali hiyo, familia yake iliambia usimamizi wa kituo hicho cha afya kuwa hawakuwa na fedha za kugharamia malipo.
Ni hapo ambapo famili ilijulishwa kuwa jamaa wao alikuwa 'amefariki'.
Furqan alipelekwa nyumbani na shughuli za mazishi zikaanza. Huku shughuli hizo zikiendelea, 'maiti' alionekana akiamka na kuzua kizazaa huku waombolezaji wakiwa mguu niponye kila mmoja.
"Tulikuwa tunaendelea na shughuli za mazishi wakati ambapo tuliona maiti akiamka. Alikimbizwa katika hospitali ya Ram Manohar Lohia na madaktari wakasema hakuwa amefariki" nduguye Furqan aliambia gazeti hilo.
Furqan inaarifiwa yuko katika hali mahututi lakini madaktari wanasema yungali hai.
Daktari mkuu wa Lucknow Narendra Agarwal alithibitisha tukio hilo na kusema litachunguzwa zaidi.
0 comments:
Post a Comment