Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC mjini The Hague imemtia hatiani mbabe wa zamani wa kivita wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Bosco Ntaganda kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.
Ntaganda, ambaye alishikilia hana hatia wakati wa kipindi cha miaka mitatu ya kusikilizwa kwa kesi dhidi yake, anakabiliwa na kifungo cha maisha jela baada ya kukutikana na hatia leo katika mahakama ya kimataifa ya ICC.
Hakuonyesha hisia zozote wakati jaji aliyesimamia kesi hiyo, Robet Fremr, alipopitisha hukumu hiyo. Ntaganda alitiwa hatiani mara ya kwanza mnamo mwaka 2006 na kuwa ishara ya kufanya uhalifu bila hofu ya kuchukuliwa hatua kisheria katika bara la Afrika, akihudumu kama jenerali katika jeshi la Congo kabla ya kujisalimisha mwaka 2013 wakati nguvu zake ziliposambaratika.
Ntaganda mwenye umri wa miaka 45 alishtakiwa kwa kusimamia mauaji ya raia na wanajeshi wake katika eneo linalokabiliwa na machafuko na lenye utajiri wa madini la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemkorasia ya Congo mnamo mwaka 2002 na 2003.
Waendesha mashitaka walitoa taarifa za kina za kutisha za wahanga wakiwamo baadhi waliopasuliwa matumbo na koo zao, kama sehemu ya ushahidi katika kipindi cha miaka mitatu ya kusikilizwa kwa kesi yake katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC mjini The Hague.
Ntaganda, aliwaambia majaji wakati wa kesi yake kwamba alikuwa mwanajeshi na wala sio muhalifu na kwamba jina la utani la "Terminator" halimhusu.
Mzaliwa huyo wa Rwanda anakabiliwa na mashitaka 13 ya uhalifu wa kivita na mashitaka matano ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa jukumu lake wakati wa machafuko ya kinyama yaliyotokea eneo la kaskazini mashariki mwa Congo.
Mashitaka hayo yanajumuisha mauaji, ubakaji, kuwasajili watoto kama wanajeshi na kuwanyanyasa kingono, uporaji na kuwalazimisha raia kuyakimbia makazi yao.
Ntaganda ameyakanusha mashitaka yote dhidi yake katika kesi inayomkabili, ambayo ilianza kusikilizwa mnamo Septemba 2015 mjini The Hague.
0 comments:
Post a Comment