Saturday, 2 March 2019

Picha : DIAMOND PLATNUMZ AFIKA KARIMJEE KUMUAGA RUGE MUTAHABA

Msanii Diamond Platnumz na Mama yake mzazi Bi Sandra, wamefika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kuungana na watanzania waliojitokeza katika taratibu za kuuaga mwili wa Marehemu Ruge Mutahaba. 
Share:

MSANII NANDY AMWAGA MACHOZI AKIMWIMBIA MAREHEMU RUGE



MSANII wa Bongo Fleva, Nandy ameshindwa kabisa kuendelea kuimba wimbo wa Angel Benard, Nikumbushe ambao Nandy aliufanya Cover.

Wimbo huo ulikuwa kati ya nyimbo bora sana kwa marehemu Ruge na akiwa hospitali ulipigwa mara nyingi sana kumfariji.

Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba, unaagwa leo Februari 02, katika ukumbi wa Karimjee Posta jijini Dar es Salaam.
Share:

Picha : RAIS MAGUFULI AONGOZA MAELFU YA WAKAZI WA DAR KUAGA MWILI WA RUGE MUTAHABA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitoa heshima zake za mwisho kwa Marehemu Ruge Mutahaba alipoongoza maelfu ya waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu ambaye aliyekuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Vipindi wa Clouds Entertainment kwenye hafla iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Jumamosi March 2, 2019

Share:

HARMONIZE,BABU TALE WATUA KARIMJEE KUMUAGA RUGE MUTAHABA

Babu Tale ambaye ni mmoja wa mameneja wa mwanamuziki, Diamond Platnumz amefika katika viwanja vya Karimjee inapoendelea shughuli ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba.

Mbali na Babu Tale, Msanii Harmonuze naye ameshafika kujumuika na waombolezaji kuuaga Mwili wa Ruge.

Uwepo wa Babu Tale na Harmonize katika viwanja hivyo umekuwa kivutio kutokana na uhasimu wa kibiashara uliopo baina ya Clouds Media Group na Wasafi Media.

Share:

MTOTO WA RUGE AMUOMBEA MSAMAHA BABA YAKE KWA ALIOWAKOSEA ENZI ZA UHAI WAKE

 Mwachi ambaye ni mtoto wa kwanza wa marehemu, Ruge Mutahaba amemuombea msamaha baba yake kwa watu aliowakosea enzi za uhai wake.
Mwachi aliyasema hayo leo Jumamosi Machi 2, 2019 wakati akisoma wasifu wa baba yake katika shughuli za kumuaga zinazoendelea katika viwanja ya Karimjee jijini Dar es Salaam.

“Ninamuombea msamaha baba yangu kwa wale wote aliowakosea enzi za uhai wake, nasi tunawasamehe wote waliomkosea baba,” amesema Mwachi ambaye ni mmoja kati ya watoto watano wa marehemu huku kauli hiyo ikizidisha simanzi kwa waombolezaji

Amesema baba yake alikuwa mtu aliyejitoa kwa wengine mpaka familia ilifikia wakati inaona watu wa nje wanamfaidi kuliko wao.

“Alitenga muda mwingi kusaidia kwa kuzingatia misingi ya utu, alipambana kwa hali zote kufanikisha mambo mengi katika jamii,” alisema huku akijitahidi kujizuia kutoa machozi.

Amesema jamii inachoweza kufanya ni kuchukua jukumu la kusaidia japo Watanzania wawili, watafanikisha ndoto za wengi.
Na Asna Kaniki na Tumain Msowoya, Mwananchi
Share:

KIKWETE ACHEKELEA LOWASSA KURUDI CCM "HONGERA KWA UAMUZI WA BUSARA"

Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dkt Jakaya Kikwete amempongeza Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa uamuzi wake wa kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM).

Lowassa alijiunga CHADEMA Julai 2015 baada ya jina lake kuenguliwa kwenye mchakato wa kutafuta mgombea wa urais ndani ya CCM.

"Karibu tena nyumbani, Hongera kwa uamuzi wa busara," ameandika Dkt. Kikwete kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.

Lowassa alitangaza hapo jana kurejea CCM katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba Dar es Salaam na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais John Magufuli.
Share:

Video : RAIS MAGUFULI, WAZIRI MKUU MAJALIWA, KIKWETE WALIVYOFIKA KUMUAGA RUGE, KARIMJEE

 Rais Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa, Kikwete walivyofika Kumuaga RUGE, Karimjee


Share:

AFARIKI KWENYE DIMBWI LA MAJI


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Thobias Sedeyoka, amethibitisha kutokea kwa vifo vya watu wawili kulikosababishwa na mvua kubwa za masika zilizoanza kunyesha visiwani humo.

Waliofariki dunia ni Hassan Mohamed (4) aliyezama kwenye dimbwi la maji ya mvua, na Skachi Abdallah Zahor (26) mkazi wa Kidongo Chekundu, baada ya kuanguka na pikipiki (bodaboda) aliyokuwa amepakiwa katika eneo la Mazizini mjini.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi amesema jitihada za polisi kumtafuta dereva wa bodaboda aliyehusika na ajali hiyo iliyosababisha kujeruhiwa Skachi Abdallah Zahor kwa zinaendelea na akipatikana atachukuliwa na hatua za kisheria.

Hivi karibuni mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa Zanzibar iliwataka wananchi na mamlaka husika kuchukuwa tahadhari kutokana na msimu wa mvua za masika kutarajiwa kuanza wakati wowote.
Share:

LIPUMBA : LOWASSA AMERUDI CCM BILA AIBU...MBOWE BADO YUPO GEREZANI

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema anashangazwa na uamuzi wa Edward Lowassa kurejea CCM katika kipindi ambacho mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa gerezani.

Akizungumza na Mwananchi jana Ijumaa Machi 1, 2019, Profesa Lipumba, ambaye mwaka 2015 alijivua uenyekiti kutokana na CUF kuunga mkono Lowassa kugombea urais kwa mgongo wa vyama vinne, amesema hajashangazwa na hatua ya Lowassa kurejea CCM kwa kuwa alijua ingawa hakufahamu siku.

"Lowassa amerudi CCM bila aibu. (Amerudi) wakati Mbowe bado yupo gerezani. Hakufikiria wenzake anawaachaje," alisema Profesa Lipumba.

Mbowe pamoja na mbunge wa Tarime, Esther Matiko, yupo Segerea tangu Novemba 23, 2018 baada ya dhamana yao katika kesi ya jinai inayowakabili pamoja na viongozi wengine wa Chadema, kufutwa.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Profesa Lipumba alisema kila wakati aliwaeleza Watanzania kuwa Lowassa ni mgombea wa nafasi ya urais wa CCM na si John Magufuli kama watu walivyodhani.

"Leo imedhihirika sasa hata alipokuja yule mganga wa Nigeria (kiongozi wa kanisa la Church for All Nation la Nigeria, TB Joshua) kukutana nao kwa nyakati tofauti niliwahi kusema suala hili. Leo Watanzania watakuwa mashahidi kwa Lowassa kurejea,” alisema

Alisema ni vyema wapinzani wakawa na msimamo na kwamba mapambano ya kudai haki yanahitaji muda mrefu si harakaharaka kama walivyofanya Chadema kumchukua Lowassa ili awasaidie kuchukua nchi.

"Niliwaambia Lowassa amekuja upinzani kwa ajili ya madaraka tu. Hiki cha leo ni dhambi ya usaliti waliomfanyia (katibu wa zamani wa Chadema, Willbrod) Dk Slaa inaanza kuwatafuna,” alisema

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Lowassa aligombea urais kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi vya NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.

Na Bakari Kiango, Mwananchi 
Share:

Friday, 1 March 2019

AGPAHI YAWAPIGA MSASA WASHAURI WAVIU SIMIYU


Afisa wa AGPAHI, Bw. Emmanuel Mashana, akiwezesha mada ya ufuatiliaji wa mahudhurio ya WAVIU CTC katika warsha iliyokutanisha Washauri WAVIU wa mkoa wa Simiyu ili kuwaongezea uweledi katika shughuli zao hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI.
Afisa wa AGPAHI, Bi. Harieth Novat, akiwaonyesha Washauri WAVIU rejesta za miadi ya WAVIU.
Maafisa wa AGPAHI, Harieth Novat (kushoto) na Emmanuel Mashana wakijadiliana jambo wakati wa warsha.
Washiriki wa warsha ya Washauri WAVIU Simiyu wakiendelea na zoezi la kujaza rejesta za miadi ya WAVIU.
Washauri WAVIU wakiwa kwenye kazi za vikundi katika warsha hiyo iliyoandaliwa na AGPAHI.
Washauri WAVIU wakiwa kwenye kazi  ya vikundi katika warsha hiyo iliyojumuisha  Vituo 36 vya kutolea huduma mkoani Simiyu huku wawezeshaji wakikagua ufanisi wa kazi.
Afisa wa AGPAHI, Bw. Emmanuel Mashana akiangalia kazi ya kikundi.

Asasi ya kitaifa inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI), imewapiga msasa Washauri WAVIU wa mkoa wa Simiyu ili kuwaongezea uweledi katika shughuli zao hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI.

Mratibu wa AGPAHI mkoa wa Simiyu, Bi. Dafrosa Charles, amesema ili kuwaongezea weledi washauri WAVIU hao hivyo kufanya kazi zao kwa ufanisi, AGPAHI inaendesha warsha ya siku tano mjini Bariadi ili kuwapa stadi na mbinu mbali mbali.

Kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR) chini ya Vituo vya Udhibiti wa Magonjwa na Kinga (CDC), AGPAHI imekuwa ikiisaidia serikali katika kuboresha afya za wananchi hususan wale wanaoishi na VVU. Kwa sasa AGPAHI inafanya kazi katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara na Mwanza.

Katika warsha hiyo inayojumuisha vituo 36 vya kutolea huduma kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Simiyu (Bariadi DC, Bariadi TC, Maswa DC,Meatu DC na Busega DC) , Washauri WAVIU hao 39 wanakumbushwa kuhusu wajibu na majukumu yao katika kusaidia utendaji wa shughuli kwenye vituo vya kutolea huduma hizo hasa za ufuatiliaji wa watoro katika ngazi ya jamii.

Ili kuweza kufuatilia vyema watu wanaopata huduma za VVU na UKIMWI kwenye vituo vyao, Washauri WAVIU hao wamepimwa uelewa wao kuhusiana na ujazaji wa rejesta ya miadi kwa wateja wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV).

Lengo la zoezi hilo lililoongozwa na Maafisa wa AGPAHI, Bw. Emmanuel Mashana na Herieth Novati, lilikuwa ni kubaini mapungufu katika utumiaji wa rejesta hizo ili kuyashughulikia hivyo kuboresha upatikanaji wa taarifa.

Kufuatia mapungufu yaliyojitokeza maafisa hao kwa kushirikiana na Mratibu wa UKIMWI wa wilaya ya Bariadi, Bi. Joyce Mashauri, waliwaongoza Washauri WAVIU hao katika namna sahihi ya kujaza rejesta hizo kwa ufanisi wa ufuatiliaji wateja.

Aidha Washauri WAVIU hao walipiitishwa kwenye ujazaji rejesta za miadi na ufuatiliaji wa watu wanaotumia huduma za VVU na UKIMWI. “Lengo la mazoezi haya ni kuhakikisha kuwa watakaporejea kwenye vituo vyao, kazi itafanyika kwa ufanisi kwa ufuatiliaji bora wa ufuasi wa huduma na tiba za VVU na upimaji wa wingi wa virusi katika damu,” amesema Bw. Mashana.

Kwa kufahamu kuwa ugonjwa wa kifua kikuu umekuwa ukiwashambulia watu wengi hasa wenye VVU,Washauri WAVIU hao wamefundishwa kuhamasisha matumizi ya dawa za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa usahihi kama kinga kwa wanaostahili.”

Masuala mengine ambayo Washauri WAVIU hao walifundishwa ni pamoja na kuhamasisha upimaji wa familia za wateja wa vituo vya kutolea huduma, vipaumbele katika huduma ya VVU. “Ni matumaini yetu pia kuwa mtawahamasisha wanaume nao kupima, uzoefu unaonyesha ni wanaume wachache tu wenye tabia ya kutafuta huduma za afya,” amesema Bi. Novati.

Share:

SUMAYE : UAMUZI WA LOWASSA KUREJEA CCM HAUNIPI SHIDA...KAMA KAAMUA ACHA AENDE

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye amesema uamuzi uliochukuliwa na Edward Lowassa kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM) hauwezi kumshtua.

Sumaye ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Machi 1, 2019 muda mfupi baada ya Lowassa kuchukua uamuzi huo amesema, “Mimi haunipi shida, mtu akiamua kuhama chama na kwenda kingine ni uamuzi wake.”

Akijibu swali la Mwananchi kama naye ni miongoni mwa watakaorejea, Sumaye amesema, “Kama kaamua acha aende, sisi tutaendelea kujenga chama na hicho unachokisema cha kuhama ni ndoto ambayo haipo.”

Lowassa aliyetangaza kuhama CCM Juni 28 mwaka 2015 baada ya kueleza kutoridhika na mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya chama hicho, leo Ijumaa ametangaza kurejea CCM na kupokelewa na Mwenyekiti wa chama hicho tawala nchini Tanzania, Rais John Magufuli.

Na  Ibrahim Yamola, Mwananchi
Share:

CHADEMA YAFUNGUKA LOWASSA KUREJEA CCM..."YEYE NI MTU MZIMA ANAJUA ANACHOKIFANYA"


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania kimesema kuondoka kwa mwanachama wake, Edward Lowassa na kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM) hakutakuwa na madhara yoyote.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Machi 1, 2019 na Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania, Dk Vicent Mashinji alipozungumza na Mwananchi muda mfupi baada ya Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani kutangaza uamuzi huo. 

“Tunamtakia maisha mema huko aendapo yeye ni mtu mzima anajua anachokifanya,” amesema Dk Mashinji.

Alipoulizwa iwapo uamuzi wa Lowassa unaweza kukitetelesha chama hicho kikuu cha upinzani Dk Mashinji amejibu kwa kifupi “It will never happen (haiwezi kutokea)”.

Na  Tausi Mbowe, Mwananchi



Share:

HII HAPA RATIBA YA KUAGA MWILI WA RUGE MUTAHABA KARIMJEE DAR KESHO


Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba umewasili nchini leo mchana, 2, Machi, 2019.

Mwili wake unatarajia kuagwa Jumamosi, 2 Machi, 2019 katika ukumbi wa Karimjee, Jijini Dar es salaam kabla ya kusafirishwa mkoani Kagera kwaajili ya mazishi yatakayofanyika Jumatatu, 3 Machi, kijijini kwao Kiziru wilayani Bukoba.

Hii hapa ni ratiba rasmi ya kuuaga mwili wake.

Share:

Picha 11 : MAPOKEZI YA LOWASSA BAADA YA KUHAMA CHADEMA NA KUREJEA CCM

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa leo Ijumaa Machi Mosi, 2019 ametangaza uamuzi wa kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM).

Lowassa amerejea katika chama chake cha zamani shughuli iliyofanyika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Tazama picha hapo chini

Share:

RAIS MAGUFULI ATOA ONYO KALI KWA VIONGOZI WANAOWATOZA USHURU WAJASILIAMALI



Share:

LOWASSA : NIMETAFAKARI NA KUAMUA KURUDI NYUMBANI... "CCM WACHEKELEA KILA KONA

Mwenyekiti wa CCM,Rais Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu wa zamani Mh.Edward Lowassa mara baada ya kutangaza kurejea CCM leo kwenye ofisi ndogo za chama hicho Lumumba jijin Dar es salaaam.

WAZIRI Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Edward Lowassa ametangaza rasmi kurudi Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuanzia leo Machi 1,2019.

Lowassa aliondoka CCM na kwenda upinzani katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) wakati wa mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.Aliondoka CCM na kwenda upinzani baada ya jina lake kukatwa katika kugombea urais kupitia Chama hicho.

Hivyo alipata ridhaa ya kugombea nafasi ya Urais kupitia Chadema waliokuwa wameunganisha nguvu na vyama vingine vinne vya siasa vilivyokuwa vimeunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Akiwa upinzani Lowassa aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema lakini kuna kipindi aliamua kwenda Ikulu kufanya mazungumzo na Rais Dk.Magufuli ambapo baada ya kukutana na Rais alisema amevutiwa na utendaji kazi wake na anampongeza.

Akizungumza leo katika Ofisi za ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam,Lowassa hakuwa na maneno mengi ya kueleza zaidi ya kuwaambia Watanzania kuwa ameamua kurudi nyumbani (CCM).

"Nimetafakari na sasa nimeamua kurudi nyumbani CCM ambako sehemu kubwa ya maisha yangu nimekuwa huko,"amesema Lowassa huku mamia ya wananchi wakiwamo wanachama na wapenzi wa CCM walikuwa wanamshangilia.

Wakati Lowassa anatangaza kurejea CCM alikuwa amesikindikizwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga ambaye pia aliwahi kuwa Mtunza wa fedha wa CCM Rostam Aziz.

Akizungumza baada ya Lowassa kurudi CCM, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli amesema wamempokea Lowassa na katika kuthibitisha hilo waliona ni vema uamuzi wake akautangazia Ofisi za CCM Lumumba kama sehemu ya uthibitisho.

"Kama ambavyo amezungumza kwa kifupi mwenye Mzee Lowassa kwamba amerudi nyumbani ambako ni huku CCM, tumempokea.Amekuja kutangazia hapa Lumumba kama sehemu ya kutoa shuhuda.

"Kwa upande wetu tumekaa, tumefakari na kujiridhisha Lowassa amekaa kwenye Chama kwa muda mrefu na kwa bahati mbaya zilizojotokeza aliamua kwenda upinanzani.Tumemsikiliza mawazo yake kwamba amekaaa kwenye Chama Cha Mapinduzi sehemu kubwa ya maisha yake na kwamba kutokana na sababu ambazo amezieleza aliamua kwenda upinzani na leo hii amerudi nyumbani,"amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo kabla ya Rais Magufuli kuzungumza aliamua kuwatania watu waliokuwa wamejitokeza Lumumba na kuwaambia imekuaje wako hapo au wanamaono na hivyo walijua kitakachotokea.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa CCM Dk.Bashiru Ally amesema Lowassa amefikia uamuzi wa busara kwa kurudi nyumbani kwa ajili ya kushirikiana katika kuleta maendeleo ya wananchi wote.

"Amerudi nyumbani, kwa hiyo tunaanza kazi ya kujenga Taifa letu na kujenga utu wetu, Lowassa ni kiongozi ambaye ametoa mchango mkubwa katika nchi yetu.Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama chetu tumepanga kumpokea na yupo tayari kushirikiana nasi kuwatumikia wananchi,"amesema Dk.Bashiru.

Hata hivyo uamuzi huo wa Lowassa umeonekana kuwakosha wana-CCM kwani baadhi yao wameonesha kufurahia uamuzi huo.

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
Share:

Breaking : LOWASSA AIFYEKELEA MBALI CHADEMA...ATANGAZA KURUDI CCM


Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa leo Ijumaa Machi Mosi, 2019 ametangaza uamuzi wa kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM).


Lowassa amerejea katika chama chake cha zamani shughuli iliyofanyika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Uamuzi wa Lowassa kutangaza kurejea CCM ameuchukua ikiwa imepita miaka mitatu tangu alipotangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema Julai 28, 2015 baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kuwania urais mwaka 2015.

Shughuli ya kumpokea Lowassa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vya Ukawa vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi imehudhuriwa na wanachama mbalimbali na wananchi wachache waliokuwapo.

Akizungumza kwa kifupi, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema, “Ametangaza kurudi nyumbani na tuko tayari kumpokea.”

Chanzo- Mwananchi

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger