Thursday, 23 June 2016

TANGAZO LA KAZI SUMAJKT Guard Ltd





                                                                     SHIRIKA LA UZALISHAJI MALI JESHI LA KUJENGA TAIFA
                                                                                            TANGAZO

Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) kupitia Kampuni Tanzu ya SUMAJKT Guard Ltd, linatangaza nafasi za kazi za ulinzi kwa vijana wa Kitanzania wenye sifa, nidhamu na uadilifu waliohitimu mafunzo ya JKT na Mgambo, kuomba nafasi tajwa katika kampuni hiyo.
Vijana hao wawe wenye sifa zifuatazo:-
  1. Awe raia wa Tanzania
  2. Awe anajua kusoma na kuandika
  3. Awe na elimu ya msingi na kuendelea
  4. Awe na umri kuanzia miaka 18 hadi 30
  5. Awe na afya njema.
Vijana wote watakaofanikiwa kupata nafasi watapatiwa mafunzo maalumu, kabla ya kuanza kazi.

Barua za maombi zinaweza kuwasilishwa kwa mkono, SUMAJKT Guard Ltd Mwenge au kwa
Afisa mtendaji Mkuu,
SUMAJKT
Sanduku la Posta 1694
DAR ES SALAAM.

Mwisho wa kupokea maombi ni Tarehe 25 June 2016
Share:

Kauli ya Magufuli kuhusu kusitishwa kwa ajira


Rais Dr. John Magufuli amesema uamuzi wa serikali wa kusitisha ajira mpya na kupandisha vyeo kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kwa miezi miwili umelenga kukamilisha zoezi la uhakiki wa wafanyakazi hewa ambao bado wanaligharimu taifa kwa wao kuendelea kupokea mishahara pasipo kufanya kazi.
Rais Dr.Magufuli amesema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka hamsini ya benki kuu ya Tanzania na kusema kuwa hawezi kuendelea kuvumilia kuona wafanyakazi hewa wakiwepo na kwamba kasi ya kuwabaini inaenda sambamba na kutakiwa kurejeshwa kwa mishahara ambayo wamelipwa ama wanaendelea kulipwa.
 
Kuhusu miaka hamsini ya benki kuu, Rais Magufuli amesema benki hiyo inapaswa kujiimarisha katika kuyasimamia maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo baadhi yake hutumika kusafirisha fedha nje ya nchi kinyume na taratibu na kutakatisha fedha haramu zikiwemo zile zinatokana na mauzo ya dawa za kulevya sambamba na benki hiyo na hazina kuboresha ukusanyaji kodi katika madini.
 
Naye Gavana wa benki kuu Prof Benno Ndulu pamoja na mwenyekiti wa jumuiya za mabenki nchini Dr.Charles Kimei ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa benki ya CRDB wamesema miaka hamsini ya uwepo wa benki hiyo kuu umekuwa mfano wa kuigwa duniani kutokana na kuisimamia vyema sekta ya fedha na kufanya huduma zitolewazo nchini kuigwa na. Mataifa mengine.
Share:

WATUMISHI WA SEKRETARIETI YA AJIRA WATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU


Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amewataka watumishi wa Taasisi hiyo kuendelea kuwa wabunifu na wachapa kazi zaidi katika utoaji wa huduma kwa wananchi hususan waombaji kazi ambao wamekuwa wakikutana nao katika uendeshaji wa mchakato wa Ajira.

Amesema hayo leo wakati wa kikao cha pamoja na Watumishi wote wa Taasisi hiyo ikiwa ni utekelezaji ratiba yake katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu, ambapo siku ya tarehe 21 Juni, 2016 ofisi hiyo iliitenga kama siku maalum ya kukutana na wananchi kwa ajili ya kupokea hoja na maswali mbalimbali na kuyapatia ufumbuzi.

 
''Pamoja na yote tuliyozungumza lakini ningefurahi zaidi endapo kila mmoja wetu anapokuja kazini kila siku anafanya kazi kwa ubunifu na kujituma akitambua huduma tunayotoa inagusa maisha ya watu na pia inahitaji mtu mwenye maadili, anayejali muda, mbunifu na mchapakazi ili kuweza kuleta tija kwa Taasisi na wale tunaowadumia'' alisema Daudi.

Aidha, aliwapongeza watumishi hao kwa kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hali iliyopelekea Sekretarieti ya Ajira kushika nafasi ya kwanza katika uzingatiaji wa maadili, kati ya Taasisi za Umma ishirini (20) zilizokaguliwa na Idara ya Ukuzaji wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

''Ni jukumu letu kama taasisi kutathimini ushindi huu na kuufanya kama chachu ya kuendelea kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika kutekeleza majukumu yetu ili tuweze kuongoza tena mwakani'' alisisitiza Daudi.

Katibu huyo alihitimisha kikao hicho kwa kuishukuru Menejimenti na Watumishi wote kwa ushirikiano, kwa hoja na michango waliyotoa, akiamini yale yote waliojadiliana yanalenga kuboresha utendaji kazi wa mtu mmoja mmoja na Taasisi kwa ujumla ili kuweza kuisaidia Serikali kutimiza malengo iliyojiwekea.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
 
source: ajira.go.tz
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger