Sunday, 14 February 2016

MAGUFULI AGOMA KUINGILIA MGOGORO WA ZANZBAR

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Rais John Magufuli jana alitumia dakika 55 kuzungumza na wazee wa Dar es Salaam, akigusa kila sekta wakati akizungumzia mambo aliyoyafanya katika siku 100 na anayotarajia kufanya.

Katika hotuba hiyo ambayo aliendelea kuzungumzia jinsi nchi inavyotafunwa, kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano aliweka msimamo wake kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, akisema hataingilia.

Pia alidokeza kuhusu uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya, akimhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuendelea au kupandishwa cheo.

Mambo mengine aliyozungumzia ni mafanikio na changamoto ya elimu bure, ujenzi wa barabara na madaraja, utendaji wa mawaziri, miradi ya umeme, huduma kwenye Hospitali ya Muhimbili, vyombo vya habari, na kuwataka wananchi wajitathmini wamefanya nini katika siku 100 za kwanza za utawala wake.

Dk Magufuli aliyekuwa ameambatana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Spika Dk Tulia Ackson, alikuwa akizungumza na baraza la wazee wa Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, ikiwa ni siku yake ya 102 tangu alipoapishwa Novemba 5, 2015 kuwa Rais.

Mkutano huo ulihudhuriwa na watu zaidi 3,000, wakiwamo mawaziri, viongozi wa CCM na viongozi wa dini, walioongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Rais Magufuli aliyeingia katika ukumbi huo saa 8:30 mchana, alianza kuzungumza saa 9:36 alasiri na kumaliza saa 10:32 jioni, akisisitiza wananchi wamuombee aweze kutekeleza majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kutumbua majipu.

 Uchaguzi  Zanzibar
Rais ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar, hatimaye jana aliweka bayana msimamo wake akisema hataingilia kwa kuwa anaheshimu utawala wa sheria.

“Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ni huru kwa mujibu wa Kat iba ya Zanzibar kifungu kati ya 112 au 115. Lakini kama ilivyo kawaida Tume huru ya uchaguzi duniani haiwezi kuingiliwa na rais yoyote. Ni kama ilivyo ZEC na (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) NEC ndivyo ilivyo,” alisema Rais.

Alisema uamuzi wa ZEC kufuta uchaguzi Zanzibar na kisha kutangaza tarehe ya marudio, hauwezi kuingiliwa na mtu yeyote, akisisitiza kuwa wanaotaka tafsiri ya kisheria juu ya uamuzi wa ZEC, waende mahakamani.

“Mahakama ipo hutaki kwenda halafu unasema Magufuli ingilia! Nenda mahakamani ukapewe tafsiri ya haki. Siingilii na nitaendelea kukaa kimya. Jukumu langu ni kuhakikisha usalama wa Zanzibar, Pemba na Tanzania unaimarika,” alisema.

“Ukifanya “fyokofyoko” katika eneo lolote nchini, utashughulikiwa na vyombo vya ulinzi na usalama.”

Mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliibuka baada ya ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani kwa maelezo kuwa sheria na kanuni zilikiukwa na baadaye kutangaza Machi 20 kuwa siku ya kupiga kura upya.

Wakati mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha akitangaza kufuta matokeo siku ambayo alitakiwa amtangaze mshindi wa kiti cha urais, tayari matokeo ya majimbo 31 yalikuwa yameshatangazwa huku majimbo tisa yakiwa yameshahakikiwa. Pia washindi wa viti vya uwakilishi na udiwani walishatangazwa na kupewe hati za ushindi.

Chama kikuu cha upinzani Zanzibar, kimepinga ZEC kufuta matokeo kikisema ni kukiuka katiba kwa kuwa ushindi unapingwa mahakamani tu na kimejitoa kwenye uchaguzi wa marudio huku kikimtaka Rais Magufuli aingilie katika kutatua mgogoro huo mezani.

“Sitaingia suala la Zanzibar,” alisema Magufuli.

Akizungumzia mabadiliko ambayo Serikali yake inayafanya, Rais alisema yana changamoto zake ambazo zinaweza kuwagusa baadhi ya watu, lakini akasema watakaoguswa ni wachache kwa faida ya wengi.

“Tanzania haitakiwi kuwa na wanafunzi wanaokaa chini, watu kukosa maji, Muhimbili watu kulala watano kitandani. Tanzania hii ina neema ila lazima tutambue wapo watu wachache waliotufikisha hapa,” alisema.

Alisema mabilioni ya fedha za Watanzania yanatumika hovyo.

“Ifike mahali Watanzania tujiulize tumemkosea nini Mungu? kwa nini asitusamehe kwa makosa tuliyoyafanya. Serikali imejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania,” alisema.

“Ndani ya Serikali tumejipanga, anayetaka kutukwamisha tutambomoa kwa faida ya Watanzania, hasa wanyonge. Haiwezekani kila mahali unapokwenda ukute wananchi wanalia wakati nchi ina rasilimali za kila aina.”

Ufisadi 
Katika hotuba yake ambayo mara kwa mara alikuwa ikikatishwa na shangwe za wananchi, Dk Magufuli alianza kuzungumzia ufisadi, akisema katika siku 100 ambazo amekaa madarakani, wamejifunza mengi na kukumbana na changamoto lukuki.

“Wapo watu katika nchi hii kwao fedha sio tatizo, fedha hizo hawajazipata kwa uhalali wamezipata kutoka kwa masikini wanaohangaika . Kila tulipokuwa tunagusa kuna maajabu,” alisema 
Alisema alimtuma Majaliwa kwenda bandarini na Katibu Mkuu wa Tamisemi kwenda wilayani Bariadi na wakakumbana na madudu.

“Akiwa Bariadi alikuta barabara ya kilomita moja imejengwa kwa Sh2 bilioni tena ni barabara ya halmashauri ya wilaya. Mimi nimekaa Serikalini sijawahi kujenga barabara kuu ya kilomita moja kwa Sh2 bilioni, ila hii ya halmashauri imejengwa kwa kiasi hicho?” alihoji.

“Barabara ya kilomita nne na nusu ya Halmashauri ya Bariadi imejengwa kwa Sh9.2 bilioni, wakati mkuu wa mkoa, wilaya, mkurugenzi na mhandisi yupo.
 “Ninapozungumza kutumbua majibu, Watanzania mtuunge mkono tuyatumbue kwelikweli.”

Alisema kiwango hicho cha fedha kingeweza kutengeneza kilomita 22 hadi 23 za lami.

Wizi bandarini 
Akizungumzia wizi wa mafuta bandarini alieleza kushangazwa na kitendo cha mita za mafuta kutofanya kazi kwa miaka mitano.

“Waziri Mkuu alikwenda bandarini na kukuta flow meter ya kupimia mafuta yanayoingia nchini haifanyi kazi kwa miaka mitano,” alisema.

“Mafuta yanaingia nchini yanagawiwa kwa watu na ndiyo maana mnaona kutoka Dar es Salaam kwenda Kibaha kila mahali kuna sheli (vituo vya mafuta).”

Kutokana na wizi huo wa mafuta, juzi Majaliwa alimsimamisha kazi mtendaji mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) na meneja wake wa kitengo cha bandari kupisha uchunguzi.

Alisema fedha ambazo zingepatikana kama mafuta hayo yangepimwa na kulipiwa kodi zingeweza kutumika kununua dawa hospitali, kusomesha wanafunzi bure na kujenga barabara.

“ Hiyo ndiyo Tanzania tuliyoikuta sisi. Mifano ni mingi ya kila aina,”alisema. 
Madudu muhimbili 
Alisema alitembelea Muhimbili na kusimamishwa na akinamama waliomtaka aende wodi ya wanawake, lakini wasaidizi wake wakamzuia.

“Walinizuia ila nilikataa. Niliwambia naenda hukohuko na niliyoyakuta ni maajabu,” alisema.

Alisema katika wodi namba 36, alikuta maji kutoka chooni yanavuja huku akina mama wakiwa wamelala chini, watano kwenye godoro moja.

“Ukiwa unaenda Muhimbili jirani kuna jengo la ghorofa tatu, linatumika kama ofisi ya uzazi na watoto. kuna wafanyakazi 70. Ukisogea mbele zaidi kuna jengo lilianza kujengwa tangu utawala wa Serikali ya Awamu ya Pili mpaka leo halijaisha,” alisema.

“(Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan) Mwinyi hakulimaliza, akaja (wa Awamu ya Tatu, Benjamin) Mkapa hakulimaliza, akaja (wa Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete hakulimaliza na sasa nipo mimi bado halijaisha.”

Alisema inashangaza kuona viongozi wa hospitali hiyo wakishindwa kumfukuza mkandarasi anayejenga jengo hilo ambaye ni Masasi Construction Engineering .

Alisema alipokuwa Waziri wa Ujenzi alifukuza makandarasi 3,000, lakini akashangazwa kuona jengo la ghorofa nne likijengwa zaidi ya miaka 20.

“Nadhani jengo hili limeweka rekodi duniani,” alisema.

Alisema jengo hilo likimalizika linaweza kuchukua watu 342, lakini hivi sasa lina watu 100, waliopo eneo la chini la ghorofa hilo, halina umeme wala maji.

Alisema Muhimbili kuna jengo la Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (Moi), kuna jengo la ghorofa sita lililoanza kujengwa miaka minne iliyopita, lakini mpaka leo halijamalizika kutokana na mvutano kati ya Moi na mkandarasi anayetaka kulipwa Sh9 bilioni.

“Wamechukua wagonjwa wachache na kuwaweka ghorofa ya kwanza hadi ya tatu. Lina jenereta ila haijafungwa. Hiyo ndiyo Tanzania,” alisema.

Alisema ameshatoa maagizo kwamba ndani ya siku mbili wafanyakazi hao 70 waondolewe kwenye jengo hilo linalotumika kama ofisi na badala yake viwekwe vitanda vya wagonjwa. 
“Sasa Waziri wa Afya na Katibu Mkuu watajua watawatafutia wapi pa kuwapeleka. Wanaweza kuwapeleka pale wizara ya Afya wakakae nao huko. Ndani ya siku mbili hizohizo ofisi hiyo ijae vitanda na akina mama waliokuwa wanalala chini wahamishiwe kwenye jengo hilo,” alisema.

Alisema ili Tanzania isiwe ombaomba lazima viongozi wajifunze kutokukubali kulea makosa.

“Kama ni majipu tutayatumbua kwelikweli. Likienda kichwani tutalitumbua, likienda kifuani tutalitumbua, likienda mgongoni tutalitumbua ili mradi majipu yaishe na Tanzania iende mbele,” alisema.

Tanzania bila mapato haiwezekani
 Alisema Tanzania haiwezi kuendelea bila kuwa na mapato yake.

“Wafanyabiashara wamekuwa wakikwepa kulipa kodi. Mara ya kwanza tulipoanza kuchukua hatua tulipata zaidi ya Sh1 trilioni, mwezi uliofuata tulipata Sh1.592 trilioni na Januari tulikusanya Sh1.063 trilioni,” alisema.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuona fedha hizo zikiwahudumia wananchi masikini.

“Zipo kejeli nyingi, wanasema ni nguvu ya soda. Hata kama ni soda ukiweka gongo utalewa. Hii ni soda ‘special’ ambayo tumedhamiria kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania. Haiwezekani nchi tajiri kama Tanzania tuwe ombaomba, inatakiwa iwe inaombwa misaada,” alisema.

Aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa kodi na kudai risiti kwa kila manunuzi wanayoyafanya.

Kukwama kwa mradi wa umeme 
Kuhusu mradi wa umeme wa gesi wa Kinyerezi 2 uliokwama tangu mwaka 2012, alisema wafadhili kutoka Japan walitoa dola 292 za Marekani na Serikali ya Tanzania ilitakiwa kuchangia asilimia 15 ya fedha hizo.

Alisema mradi huo utaingiza zaidi ya megawati 240 za umeme.

“Fedha hizo tumezitoa na kampuni kutoka Japan imeshaanza kazi na mwezi ujao tunakwenda kuweka jiwe la msingi. Mradi wa ujenzi wa barabara ya juu Dar es Salaam mkandarasi ameshaanza kazi na fedha za awali ameshalipwa,” alisema.

Alisema upembuzi yakinifu wa mradi wa barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze, umeshamalizika na kuna kandarasi zaidi ya 12 wameshaomba zabuni.

“Katika kipindi hikihiki cha awamu ya tano itajengwa ili tuwe na barabara ya njia sita kupunguza msongamano wa magari,” alisema.

Rais pia alidokeza kuhusu mradi wa ujenzi wa daraja la urefu wa kilomita saba litakalopita baharini kutoka ufukwe wa Coco hadi Hospitali ya Aga Khan, akisema Serikali imeshapata zaidi ya Sh260 bilioni.

“Kuhusu barabara ya Mbagala rangi tatu kuja mjini (Posta), nilikuwa nazungumza na ubalozi wa Japan wapo katika utaratibu wa kutangaza tenda,” alisema.

Pia alizungumzia ujenzi wa barabara za juu zitakayojengwa kwenye makutano ya Ubungo.

Alisema makutano hayo yatakuwa na ghorofa tatu ambazo zitakuwa na barabara zinazokutana eneo hilo ili kuondoa tatizo la foleni.

“Benki ya Dunia imekubali kutoka Sh67 bilioni kujenga interchange (mzunguko wa juu wa barabara) ya ghorofa tatu pale Ubungo, nina uhakika watani zangu wazaramu watakwenda pale kufunga ndoa,” alisema.

Kuifufua ATCL 
 Alisema Serikali ina mpango wa kufufua Shirika la Ndege (ATCL), ambalo hivi sasa lina ndege moja lakini limeajiri wafanyakazi 200.

Alisema kwa sasa wanakusanya fedha za kutosha ili kuweza kununua ndege aina ya Airbus yenye uwezo wa kuchukua kuanzia abiria 120 na kuendelea, akisema bei yake ni takriban Sh140 bilioni.

“Mkijipanga mnaweza kuwa mnanunua ndege moja kila mwezi,”alisema. 
Elimu bure 
Akizungumzia changamoto ya elimu bure alisema wanafunzi walioanza darasa la kwanza nchini mwaka huu ni 1,337,000, jambo ambalo alisema linaonyesha kuwa wananchi walikuwa wakishindwa kuwapeleka watoto wao shule kwa sababu ya kukithiri kwa michango.

Alisema changamoto zilizojitokeza baada ya Serikali kuanza kutoa elimu bure watazimaliza, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kuzipeleka katika shule.

Aliwashukuru wananchi ambao wameanza kujitokeza kuchangia ujenzi wa madarasa na kumsifu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa kuendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa shule.

Awashukia wakuu wa mikoa na wilaya
 Dk Magufuli pia alizungumzia utendaji wa wakuu wa wilaya na mikoa na wakurugenzi wao, akiwataka kutathmini hali ilivyo kwenye shule na ofisi zao.

“Kama unajua kujipima vizuri, ujitambue kuwa hutoshi kuwa kiongozi. Sijateua wakuu wa mikoa, wakuu wilaya na wakurugenzi ili niendelee kuwachambua vizuri (waliopo) ni nani anatosha na nani hatoshi,” alisema..

“Kutosha kwao ni lazima wajipange watatatua vipi kero za wananchi. Lazima ifike mahali viongozi tujue jukumu letu. Unapopewa jukumu la uongozi wewe ni mwakilishi wa wanyonge.”

Huku akiwataka Watanzania wa kada zote nao kujipima walichoifanyia nchi ndani ya siku 100, alisema haingii akilini kiongozi kusimama na kusema chakula hakuna wakati mvua inanyesha kila mkoa nchini.

“Kiongozi umeshindwa hata kuhamasisha watu walime. Natoa wito kwa viongozi wenzangu. Katika mkoa, wilaya au tarafa itakayokuwa haina chakula kwa mwaka huu ambao mvua inanyesha, ajitambue hafai kuongoza katika nchi,” alisema.

Alisema aliahidi kuwalipa wazee waliolitumikia taifa lakini jambo hilo haliwezekani kama kutakuwa na vijana wanaoshinda mitaani bila kufanya kazi.

“Najua mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, wakuu wa mikoa wenzako watakuuliza nitateua lini wakuu wa mikoa na wilaya. Kwanza tarehe ya kuteua hawataijua na ninaendelea kuwachambua,” alisema Magufuli.

“Lakini angalau Makonda umeshajihakikishia walau utakuwepo ila na wewe usiende kulala, endelea kufanya juhudi. “Ukipanda cheo watu wasikuonee wivu.”

Alisema Makonda amejijengea heshima kubwa kwa kuhamasisha watu wa kada mbalimbali kumaliza changamoto za kuongezeka wa wanafunzi, uhaba wa madarasa na madawati.

Kuhusu changamoto za elimu bure, Rais alisema asilimia 80 ya viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano wanaishi Dar es Salaam, akiwamo yeye, waziri mkuu, mawaziri, makatibu wakuu na naibu spika.

“Wao wakitoa milioni moja moja zinafika milioni 82 na zitabaki milioni 18, lakini kuna Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na mimi. Tuigawane hii na kila mmoja achangie Sh6 milioni itimie Sh100 milioni na tutaileta kwenye uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam,” alisema.

Alisema kwa mamlaka aliyonayo ataongeza Sh2 bilioni na kumtaka mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kutozitumia vibaya, akitaka zigawanywe kwa kila wilaya ili zijengwe shule za kutosha kufidia wanafunzi wanaokaa chini. 
Afagilia vyombo vya habari 
Kiongozi huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano pia alizungumzia vyombo vya habari ambavyo alisema vimefanya kazi kubwa na kuisaidia Serikali.

“Hata sisi huwa tunafuatilia. Mfano katika gazeti la Jamhuri waliweka michoro fulani mpaka sisi (Serikali), tukajiuliza wamejuaje tunachotaka kukifanya?” alisema.
Share:

Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally Aruhusiwa kutoka hospitali....Aitaka Serikali iboreshe hospitali za ndani

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir, ameitaka Serikali iweke mikakati thabiti ya kuzipa uwezo hospitali za ndani ili kupunguza gharama kwa Watanzania wengi kwenda kutafuta matibabu nje ya nchi.

Mufti aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kuruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki moja akipatiwa matibabu.

Alisema kuna haja ya hospitali kubwa kama Muhimbili kuangaliwa kwa jicho la tatu ili iweze kutoa huduma za kimataifa, hilo litawezekana endapo kutakuwa na vitendea kazi vya kutosha na madaktari kufanya kazi katika mazingira mazuri.

Mufti alisema kwa kufanya hivyo Watanzania watarudisha imani kwa hospitali za nyumbani na madaktari wake, tofauti na hali ilivyokuwa miaka ya karibuni ambapo wengi walikuwa wakikimbilia nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta matibabu.

“Binafsi nilikuwa siamini kama naweza kutibiwa hapa nchini, tayari nilishakata tiketi kwa ajili ya kwenda nje ya nchi lakini nashukuru Mungu siku moja kabla ya safari nilihakikishiwa kwamba naweza kupata matibabu hapa.

“Niwasihi Watanzania wenzangu kuamini kwamba Tanzania nayo tuna madaktari bingwa wengi ambao wanafanya kazi nzuri, muhimu kwa Serikali ni kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi,”alisema Sheikh Zubeir 
Kwa upande wake Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu alisema ni matarajio ya Serikali kuona viongozi wote wanatibiwa hospitali za nyumbani, jambo litakalowashawishi Watanzania wengine kuamini huduma zinazotolewa.

Alisema kwa viongozi wakubwa kama Mufti kutibiwa nchini kumewasukuma kuongeza vifaa na huduma bora zaidi, ili kuifanya Muhimbili kuwa miongoni mwa taasisi zinazoheshimika.

“Kama Mufti ametibiwa hapa nyumbani kuna sababu gani ya kupeleka watu nje, kwa sasa tumepata hamasa ya kuongeza vitendea kazi na huduma, ili Muhimbili iendelee kuheshimika na ivuke mipaka itoe huduma ndani na nje ya nchi,” alisema Mwalimu 
Akitoa salamu za Bakwata Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Suleiman Said Lolila alimshukuru Rais John Magufuli kwa kufanikisha matibabu ya Mufti.

“Madaktari wamefanya kazi kubwa tuna kila sababu ya kushukuru kwa hilo na Watanzania wote kwa ujumla kwa dua zao hatimaye leo Mufti ameruhusiwa kurudi nyumbani,” alisema Lolila 

 Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akimualika Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally kuongea na wanahabari katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya madaktari kumruhusu kurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.
Share:

Naibu Waziri wa Afya, Dk Khamis Kigwangalla Aupa Siku 60 Uongozi Wa Hospitali ya Rufaa Mbeya Kununua Mashine ya CT Scan

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Khamis Kigwangalla amewapa siku 60 viongozi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya (MRH) wawe kununua mashine ya CT-scan.

Dk Kigwangalla alitoa agizo hilo juzi jioni, baada ya kuwasili jijini Mbeya ghafla na kwenda moja kwa moja kwenye hospitali hiyo na kupokea taarifa iliyoeleza pia kwamba ni ya kanda, lakini haijawahi kupata mashine za CT scan.

Kukosekana kwa CT-scan kumesababisha wagonjwa kwenda Dar es Salaam au watumie mashine ya mtu binafsi iliyofungwa jijini hapa miaka miwili iliyopita.

“Haingii akilini mtu binafsi hapahapa Mbeya anamiliki CT-scan, lakini hospitali kubwa kama hii imekosa,”alisema.

Dk Kigwangalla alishangazwa zaidi aliposikia kuwa mapato ya hospitali hiyo ni zaidi ya Sh500 milioni kwa mwezi.

“Sasa nawapa siku 60 nataka kuona mashine hiyo imefungwa, vinginevyo mtakuwa mmeshindwa kazi, nitakula sahani moja na nyie viongozi,” alisema.

Aliwataka watumishi wa hospitali hiyo kuwa na mawazo chanya kwa maendeleo na kutoa mfano wa CT-scan nzuri na ya kisasa kama ile iliyonunuliwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN) inauzwa Sh3 bilioni jambo ambalo wanaweza kulitekeleza badala ya kusubiri Serikali iwapelekee.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Maabara cha hospitali hiyo, Abednago Mwakila alisema mbali ya kukosa mashine hiyo kwa miaka yote, nyingine zilizopelekwa hapo hazifanyi kazi baada ya kuharibika na hawajui mafundi wanapatikana wapi.

Alitoa mfano wa mashine ya kuangalia mgando wa damu aliyodai ni kifaa muhimu, lakini haifanyi kazi kwa zaidi ya miaka minne kutokana na kukosekana kwa fundi.

Baada ya kuelezwa hivyo, Dk Kigwangala aliuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuorodhesha mashine ambazo hazifanyi kazi na kumpelekea ofisini aweze kufanya utafiti na kubaini watu walioingia mkataba na Serikali wapeleke mashine hizo.

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Idsory Thomas alisema agizo lililotolewa na Dk Kigwangalla litatelekezwa kwa wakati.
Share:

TCU YAFUTIA CHUO KIKUU KINGINE USAJILI ,KIJUE HAPA

Share:

magazeti ya leo jumapili february 14 2016

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Share:

Saturday, 13 February 2016

New AUDIO | Domo Kaya Feat Chibwa - Ananiacha Hoi | Download

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
http://old.hulkshare.com/dl/myvgvk3jpts0/Domo_Kaya_Feat_Chibwa_Ananiacha_Hoi.mp3?d=1
Share:

Download video | Shollo Mwamba Ft. Mesen Selekta - Sembe Tembele

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
https://www.youtube.com/watch?v=vWiLjVIAL8c
Share:

Friday, 12 February 2016

HAYA HAPA MAJINA YA WANAFUNZI SUA WALIOPATA MKOPO AWAMU YA 14 2015/2016

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Share:

Waziri Nchemba Afanya Ziara Ya Kushtukiza Saa Saba Usiku Machinjio Ya Ukonga Mazizi Na Kufukuza Viongozi Wote Wa Machinjio

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Waziri wa Kilimo na Mifugo Mwigulu Nchemba amefanya ziara ya Kushtukiza saa saba usiku wa kuamikia leo katika Machinjio ya Ukonga Mazizi.

Katika ziara hiyo, Waziri Nchemba  amekamata
ng'ombe 200 wakiwa wanaingizwa kwenye machinjio bila kibali halali, na kati yao ni ng'ombe 20 tu ndo walikuwa na kibali cha kuchinjwa, hivyo ushuru  wa ng'ombe 180  ulikuwa  unatafunwa  na  watumishi  waovu.
 
Baada  ya  kubaini  hali  hiyo,Waziri Nchemba ameufukuza  uongozi wote  wa  machinjio  hayo  na  kuagiza  vyombo  vya  dola  viwakamate  viongozi  wote waliohusika  na  kuwafikisha  mahakamani.

Share:

Maalim Seif Aiandikia Barua Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec)

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameithibitishia rasmi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kujiondoa kuwania wadhifa huo katika Uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20, mwaka huu.

Mbali na Maalim Seif, wagombea wote wa chama hicho wa nafasi ya Uwakilishi na Udiwani wamejiondoa kwa kuwasilisha barua rasmi kuwa hawatoshiriki uchaguzi huo wa marudio wa Zanzibar.

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, amesema Maalim Seif amewasilisha waraka wa barua wa kujiondoa kwa Zec, Febuari 8, mwaka huu.

Amesema hatua aliyochukuwa mgombea huyo ni utekelezaji wa wa azimio la Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kutoshiriki uchaguzi mkuu wa marudio visiwani hapa.

Shehe alisema kuwa Zec imetakiwa kutotumia jina wala picha za Maalim Seif  na taarifa zozote katika karatasi za wapigakura kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Alisema kuwa katika Barua yake Maalim seif amesisitiza kuwa uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana ulikuwa uchaguzi huru na wa haki na Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jecha salim Jecha hakuwa na mamlaka ya Kikatiba na sheria kufuta matokeo ya Uchaguzi huo.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Salum Kassim alisema jana kuwa ni mapema kueleza vyama vingapi vimekamilisha kuthibitisha wagombea wake kama wapo hai na watashiriki uchaguzi kabla ya kufanyika Machi 20, mwaka huu.
Share:

Siku 100 Za Rais Magufuli Ikulu

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY


Ni kweli siku hazigandi kwamba Rais John Magufuli aliyeingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, ametimiza siku 100 leo. 

Tangu alipotoa hotuba yake siku ya kuapishwa na ile ya uzinduzi wa Bunge la 11, Rais Magufuli  amejitahidi kuishi katika maneno yake kwa kutenda kile anachokisema.

Miongoni mwa mambo aliyoahidi ni kupambana na rushwa pamoja janga la dawa za kulevya, akisema dawa za kulevya zimeathiri vijana wengi, hivyo akaahidi kushughulikia mtandao huo na wakubwa wanaohusika.

 Kwa upande wa rushwa, Rais Magufuli aliahidi kupambana na ufisadi na rushwa na katika kutekeleza hilo, alisema ataunda mahakama maalumu ya kushughulikia wezi wakubwa yaani mafisadi.

 Pia aliahidi kuwashughulikia wafanyakazi wazembe ili Serikali yake isiendelee kulea watu wanaolipwa mishahara tu wakati hawafanyi kazi yoyote.

Katika kubana matumizi ya serikali, aliahidi kudhibiti warsha ambazo hazina umuhimu katika Serikali wala kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi.

Aliahidi pia kudhibiti safari za nje, ambazo zimekuwa zikigharimu Serikali fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Rais Magufuli pia alisema Serikali yake itaongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato, ukizingatia kuwa kodi ni kitu muhimu na ni lazima zikusanywe.

Aliahidi kufufua viwanda viliyobinafsishwa, ambavyo baadhi alidai vimegeuzwa mazizi ya mbuzi wakati waliopewa kwa madhumuni ya kuviendeleza.

Aliahidi pia kushughulika na kero zinazolalamikiwa kutendwa na polisi, hospitali, mizani, Mahakama, maliasili na vilio vya wachimbaji.

Tayari Rais Magufuli ametenda yale ambayo aliyaahidi kwa Watanzania. Amebana matumizi ya serikali kwa kudhibiti safari zisizo na tija, matumizi yasiyo ya lazima, ameshughulikia watumishi wazembe, ameshughulikia mafisadi ndani ya serikali na kutoa elimu ya bure.
 Alivyoanza kazi
Mara tu baada ya kuingia ofisini, alimuapisha Mwanasheria Mkuu, George Masaju aliyemteua muda mfupi tu baada ya kuapishwa.

Katika siku zake hizo za mwanzo, alitumia mtindo wa kufanya ziara za kushtukiza katika taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na kukemea viongozi wazembe na wanaoendekeza ufisadi na rushwa serikalini.

Mtindo wake huo, ukatumiwa pia na watendaji wengine wa Serikali wakiwamo mawaziri na wakuu wa mikoa na wengine.

Katika siku zake hizo za mwanzo, Rais Magufuli pia alifanya mabadiliko makubwa Ikulu kwa kufuta baadhi ya vitengo, kikiwamo cha lishe na benchi la wageni na kuagiza wananchi wote wenye matatizo waanzie ngazi za chini.
 
Atoa Msimamo wake
Novemba 7, mwaka jana akiwa Ikulu, Dar es Salaam, alikutana na watumishi wa Serikali ikiwa ni pamoja na manaibu katibu wakuu, manaibu wakuu na watendaji wakuu wa Serikali.

Katika kikao hicho, aliwataka kujiandaa kufanya kazi kwa ufanisi katika Serikali ya awamu ya tano chini yake. huku akiwasisitiza juu ya dhamira yake ya kuendeleza kaulimbiu yake ya “Hapa kazi tu”.

Kikao hicho pia kiliudhuriwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade ambapo alitoa mwelekeo wa Serikali anayoitaka.

Afuta Safari za Nje
Rais Magufuli alitumia kikao hicho kutangaza kufuta safari zote za nje ya nchi hadi hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine, na kueleza shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi.

Alisema mtumishi atasafiri nje iwapo kutatokea jambo la dharura, na lazima kibali kitolewe na yeye, Katibu Mkuu Kiongozi au Makamu wa Rais.

Badala yake aliwataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi.

Hadi sasa, Rais Magufuli bado hajakwenda safari yoyote ya nje ya nchi zaidi ya kuwatuma Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenda kumwakilisha kwenye shughuli mbili tofauti.

Safari zake  ndani ya nchi
Novemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alisafiri kwa mara ya kwanza nje ya Dar es Salaam alipokwenda mkoani Dodoma ambako alifungua Bunge la 11.

Katika mkutano wake, Rais Magufuli alijikuta akisusiwa hotuba yake na wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga uteuzi wake na kutomtambua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kama rais halali, baada ya kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Januari 12, mwaka huu, Rais Magufuli alisafiri kwa ndege ya kukodi kwenda Zanzibar ambako alihudhuria maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Januari 21, mwaka huu alifanya ziara ya kwanza mkoani Arusha, ambako alikwenda pia katika Chuo cha Maofisa wa Kijeshi (TMA) Monduli kutunuku vyeo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuhitimu mafunzo, huku naye akiwa amevalia sare za jeshi hilo.

Februari 5, mwaka huu pia Rais Magufuli alisafiri kwa gari kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Singida kuhudhuria maadhimisho ya miaka 39 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akataa sherehe ya kifahari Bungeni
Rais alionekana tofauti na viongozi wengine waliomtangulia baada ya kuifanya sherehe ya kuzindua Bunge kutokuwa ya kifahari na hivyo akaokoa Sh milioni 251, ambazo aliagiza zikanunue vitanda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Jumla ya vitanda 300, magodoro 300, viti maalumu vya wagonjwa 30, vitanda vya kubeba wagonjwa 30 na mashuka 1,695.

Afuta gwaride la Uhuru
Novemba 9, mwaka jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alitangaza kuwa Rais Magufuli aliamua kufuta shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru na kwamba fedha zitakazookolewa atazipeleka sehemu nyingine.

Fedha Sh bilioni nne zilizopaswa kutumika kugharimia shamrashamra za Siku ya Uhuru, ambazo zingefanyika tarehe 9 Desemba 2015, Rais aliamuru zitumike kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3.
Baraza la Mawaziri
Desemba 10, mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri ambalo alianza kwa kuteua mawaziri 19, ingawa wizara ni 18. Mawaziri sita kati ya hao ni wanawake.

Katika uteuzi wake, aliacha wazi nafasi nne za uwaziri kwa madai alikuwa akitafuta watu watakaofaa kuteuliwa kuongoza wizara husika.

Wizara ambazo hakuteua mawaziri katika baraza lake la awali alilolitangaza ni Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Desemba 23, mwaka jana ikiwa ni siku 13 tangu alipotangaza Baraza la Mawaziri, Rais Magufuli alikamilisha baraza lake kwa kuwataja mawaziri wanne waliokuwa wamebakia.

Uteuzi wa Rais Magufuli umekuwa wa tofauti ambapo viongozi wengi aliowateua kushika nafasi mbalimbali ni wasomi wa ngazi ya uprofesa na udaktari.

Mabalozi Wapigishwa  Kiapo cha Utii
Katika mwendelezo wa kuhakikisha kuwa wale anaowateua wanakubaliana na kasi yake, Rais Magufuli aliwapa kiapo cha utii makatibu wakuu wa wizara na manaibu wao.

Akiwaapisha kiapo hicho aliwaeleza wazi kwamba yule atakayeshindwa kufanya kazi ni bora ajiondoe mwenyewe na kupisha wengine watumikie wananchi. 

Majipu 152  Yatumbuliwa
Ndani ya siku hizi 100  za  uongozi  wa  Rais  Magufuli, watumishi wa umma 152  wamefukuzwa  kazi  kutokana na kasoro mbalimbali za kiutendaji.

Hao ni watumishi waliotimuliwa kwa majina au vyeo vyao, lakini ukijumlisha na wengine waliosimamishwa au kufukuzwa kwa matamko bila kutajwa majina, idadi ni kubwa zaidi.

Watumishi hao wamesimamishwa na baadhi wamefukuzwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali za kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma, Rais kutoridhishwa na utendaji wao, wizi kwenye taasisi zao, ukwepaji kodi, tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma na utovu wa nidhamu.

1.Muhimbili
Hatua za kusimamisha na kutimua zilianza siku nne tu baada ya Rais kuapishwa, ambapo Novemba 9, 2015 Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hussein Kidanto, alihamishwa na bodi iliyokuwa na wajumbe 11 ilivunjwa.

2.TRA
Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Rished Bade Novemba 27.

3.Bodi ya TPA
Desemba 7, mwaka jana, Magufuli alivunja bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pamoja na kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka, Mwenyekiti wa Bodi ya Bandari, Profesa Joseph Msambichaka na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadh Massawe.

Pia, aliwasimamisha kazi wasimamizi wanane wa Bandari Kavu (ICD). Jumla ya waliotimuliwa TPA na TRA ni watu 47.

4.Takukuru
Akiendelea na kasi yake, Desemba 16, 2015 Rais alitengua uteuzi wa nafasi nyeti ya Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah. Rais alisema alichukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji wa Takukuru chini ya mkurugenzi huyo.

Maofisa wengine wa taasisi hiyo walisimamishwa kazi kwa kukiuka maagizo yaliyohusu safari za nje.

Waliosimamishwa kazi ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas, wakiwa watumishi waandamizi wa taasisi hiyo.

5.Rahco
Rais JPM alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco), Benhadard Tito, Desemba 23, 2015 kwa kile kilichoelezwa ni “ukiukwaji mkubwa wa taratibu za ununuzi” katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.

Pia alivunja bodi ya Rahco yenye wajumbe wanane na bodi ya TRL yenye wajumbe wanane pia.
6. Katibu Tawala Mwanza 
Akiendelea na kasi hiyo, Januari 15, alitengua uteuzi na kumfukuza kazi Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Faisal Issa kutokana na “utovu mkubwa wa nidhamu” aliounyesha katika kikao cha cha kamati ya ulinzi kilichofanyika mjini Mwanza. 
7.Idara ya Uhamiaji 
Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia utawala na fedha, Piniel Mgonja Januari 21 ili kupisha uchunguzi baada ya kubaini dosari kadhaa kwenye ofisi hiyo.

8.NIDA
Januari 25, Dk Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu kutokana na matumizi yasiyoridhisha ya Sh179 bilioni.

Wengine waliosimamishwa Nida ni Joseph Makani ambaye ni mkurugenzi wa Tehama, Rahel Mapande (ofisa ugavi mkuu), Sabrina Nyoni (mkurugenzi wa sheria) na George Ntalima, ofisa usafirishaji.

Pia, aliwarudisha nyumbani mabalozi wawili, Dk Batilda Buriani aliyekuwa Japan, Dk James Msekela (Roma, Italia). Pia, Peter Kallaghe (Uingereza) na kurejeshwa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano, Kikanda na Kimataifa.
                          Dunia nzima Yamkubali
Kutokana na kasi yake ya mabadiliko ya kweli ya uongozi wake, hasa kudhibiti matumizi na kuelekeza fedha katika huduma za kijamii, Rais Magufuli amekuwa gumzo kwenye anga za kimataifa.

Uongozi wake umeelezwa kuwa wa mfano, kwani miongoni mwa mambo anayoyafanya, yanagusa ulimwengu na anatekeleza yote bila kufanya safari yoyote ya nje ya nchi kama wanavyofanya viongozi wengine.

Tangu aingie madakarani, amedhibiti mabilioni ya fedha na kuzielekeza katika kuboresha huduma za afya, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s), ruzuku ya shule na miundombinu ya barabara.

                        Changamoto: Sakata  la  Zanzibar
Pamoja na yote, suala la kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar limekuwa likiitesa Serikali ya Rais Magufuli.

Wakati Chama Cha Mapinduzi kikitaka uchaguzi huo urudiwe, Chama cha Wananchi (CUF) kimeendelea kushikilia msimamo wake kuwa hakitakubali marudio ya uchaguzi huo na hakitashiriki.

CUF wanaamini Rais Magufuli pekee ndiye anayeweza kumaliza mzozo huo ulioibuka visiwani humo, lakini kiongozi huyo hajazungumza lolote hadi hivi sasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alipotangaza kufutwa na kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Kuendelea kuwako kwa mgogoro huo, ni wazi kwamba kunaitia doa Serikali ya Dk. Magufuli nje ya nchi.
         
Share:

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa taarifa ya siku 100 za kwanza za Serikali ya awamu ya tano Ikulu jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 12, 2016

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa taarifa ya siku 100 za kwanza za Serikali ya awamu ya tano Ikulu jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 12, 2016

Mpekuzi blog

Tazama video hii ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa taarifa ya siku 100 za kwanza za Serikali ya awamu ya tano Ikulu jijini Dar es salaam leo Ijumaa Februari 12, 2016
Share:

JIPU JINGINE LATUMBULIWA,WIMBO WA NAY WA MITEGO WAFUNGIWA RASMI NA BASATA,BARUA HII HAPA

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Siku ya jana BASATA uongozi wa BASATA ulisema bado haujaufungia wimbo wa Ney wa Mitego mpaka pale watakapofuata taratibu zote za kisheria.Leo BASATA wametoa tamko rasmi kupitia barua waliyoituma kwenye vyombo vya habari inayothibitisha kuwa wameufungia wimbo wa Shika adabu yako wa msanii wa bongo fleva,Ney wa Mitego kutokana na wimbo huo kuwa na lugha ya maudhi,udhalilishaji,uchochezi n.k na kutaka msanii huyo kutouongelea wimbo huo popote kwenye vyombo vya habari.
Barua ya Basata hii hapa isome….
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 4 (1) (j) cha sheria ya BASATA
namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepwa mamlaka ya kuratibu na kufuatilia
mienendo ya mtu yeyote anayehusika na kazi za Sanaa na kuhakikisha
linalinda maadili ya kitaifa miongoni mwa Wasanii wanapokuwa jukwaani au
wanapobuni kazi yoyote ya Sanaa.
Aidha, kifungu cha 4 (2) cha sheria hii kinalipa Baraza nguvu ya
kisheria kufanya jambo lolote lile kuliwezesha kufanya majukumu yake kwa
faida na ustawi wataifa.
Baraza la Sanaa la Taifa limekuwa likipokea simu za maswali na
malalamiko kadhaa kutoka kwa waandishi wa habari na wadau wa Sanaa ambao
kwa njia moja ama nyingine wameguswa na kuchukizwa na kazi hiyo ambayo
si tu inadhalilisha tasnia ya Sanaa bali inawafanya watu makini kuanza
kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya Sanaa kwa ujumla.
BASATA mara kadhaa limekuwa likikemea na kuchukua hatua kadhaa dhidi ya
tabia hii chafu ambayo ilianza kujitokeza kwenye kampeni za uchaguzi
mkuu wa mwaka jana wa 2015. Kukemea huku ni kwa msingi mmoja kwamba
asili ya tasnia hii ya Sanaa ni kuelimisha jamii, kukosoa pale
kunapokuwa na tatizo, kuburudisha na kujenga jamii yenye staha, umoja wa
kitaifa, mshikamano na amani.
Ni wazi wasanii wengi wanafanya kazi zao vizuri, kwa kubuni kazi zenye
ubora, zenye kujenga jamii na zaidi zinazoburudisha rika zote kiasi cha
kuzifanya zililetee heshima taifa. Kati ya hawa wengi, kuna wachache
ambao wanaipaka matope tasnia ya Sanaa na kwa kiasi kikubwa wanaonesha
wazi kutokuwa na nia njema.
Kwa mantiki hii BASATA halitavumilia hawa ‘wasanii’ wachache ambao
wanataka kuigeuza tasnia ya Sanaa na wasanii genge la wahuni, wasio na
staha, wa kudharaulika na waliojipanga kuibomoa jamii na kuharibu amani
na utulivu uliopo nchini.
BASATA linapenda kueleza yafuatayo:
1. Vyombo vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya
Sanaa kabla ya kuingia kwenye mtego wa kuwa mawakala wa uharibifu wa
jamii kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa. BASATA lilishaziandikia radio
zote kuzishauri kuwa na kamati za maudhui ya kazi za Sanaa lakini
inashangaza baadhi ya vyombo vya habari vinakuwa vya kwanza kushabikia
nyimbo hizo chafu na kuwapa muda mrefu wa mahojiano wasanii hao na
baadaye kurudi BASATA kuhoji uhalali wa nyimbo husika. Hii si sawa hata
kidogo.
2. Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli
imejipanga kuwajengea mazingira bora ya utendaji Wasanii wote nchini
kupitia kuboresha miundombinu ya Sera, Sheria na Kanuni. Hata hivyo,
uwepo wa Wasanii kama hawa unafanya jamii kuhoji hadhi ya wasanii,
nafasi yao katika jamii na kwa maana hiyo kukatisha tamaa juhudi za
kuipa msukumo sekta hii maana wadau wakuu ambao ni wasanii wanaanza
kuoneasha kuwa mawakala wa uharibifu wa jamii.
3. BASATA linawataka wasanii kujiuliza mara mbili kabla ya kubuni kazi
zao za Sanaa. Wafikirie wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao
watazipokeaje? Wavae nafasi ya wale wanaowatukana na kuwadhalilisha,
Waelewe kwamba Sanaa si uwanja wa kutusi na kudhalilisha watu hata
kidogo. Ikitokea wale wanaotukanwa na kudhalilishwa kughafilika Sanaa
itakuwa uwanja wa vita. Hili halikubaliki.
4. Tunafahamu kuna wasanii wamekuwa wakifanya hivyo makusudi kutafuta
‘umaarufu uchwara’ ambao wanadhani utakuja kutokana na kuzungumziwa
sana. Tunapenda kusema wazi kwamba umaarufu hauji kwa upuuzi wa namna
hiyo unakuja kwa msanii mwenyewe kujiheshimu, kujituma, kubuni kazi bora
na zenye kulifahamu vema soko la ndani na la kimataifa.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
Source: Times Fm
Share:

Thursday, 11 February 2016

Bandarini Hapakaliki.......TRA Yatangaza Kuwafilisi Wateja 24 Kwa Kutorosha Makontena

INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Mamlaka  ya Mapato Tanzania (TRA) imeikabidhi Kampuni ya Udalali ya Yono kuwafilisi wateja 24 wanaodaiwa kodi ya Sh bilioni 18.95 baada ya kutorosha makontena ya mizigo yao kwenye Bandari Kavu (ICD) ya Azam mwishoni mwa mwaka jana.

Majina ya wadaiwa hayo yametolewa jana kwenye vyombo mbalimbali vya habari, na Kampuni hiyo ya Udalali ya Yono baada ya TRA kuwakabidhi kazi ya kuwafilisi kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wao baada ya kupewa muda wa kulipa kodi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Yono Kevela jana alisema wamepewa amri na TRA ya kisheria ya kukamata mali za wadaiwa na kuwafilisi ili kulipia kodi wanazodaiwa.

Kevela alisema baada ya kupata kazi hiyo, wao wameona busara kuwatangaza kwenye vyombo vya habari na kuwapa siku 14 kulipa kodi wanazodaiwa na kwamba baada ya muda huo kumalizika, hatua za kukamata mali za wadaiwa hao zitaanza na kuwafilisi.

“Tumekabidhiwa wadaiwa 24 na TRA, hawa wamekwepa kodi kwa kutorosha kontena katika Bandari Kavu ya Azam mwishoni mwa mwaka jana, sasa walipewa muda wa kulipa ila wamekaidi, sasa kazi tumepewa sisi na tutawafilisi mali zao zote ili kulipa deni hilo,” alifafanua Kevela.

==>Majina ya wadaiwa hai na kiasi cha fedha wanachodaiwa kwenye mabano ni 
  1. Zulea Abas Ali  (16,760577.24) 
  2. Omary Hussein Badawy  (21,346,615.40)
  3. Libas Fashion  (26,593,245.78)
  4. Said Ahmed Said  (28,249,352.50)
  5. Strauss International  (45,393,769.95) 
  6. Farid Abdallah Salum (52,185, 614.97)
  7. Ally Awes Hamdani  (55,485,904.07)
  8.  Nasir Saleh Mazrui  (60,105,873.77)
  9.  Simbo Yona Kimaro  (64,221,009.10)
  10.  Zuleha Abbas Alli  (75,508,551.88)
  11.  Issa Ali Salim  (94,543,161.96)
  12. Ally Masoud Dama  (102,586,719.22)
  13. Juma Kassem Abdul  (130,182,395.12)
  14.  Salum Link Tyres  (233,447,913.31)
  15. Tybat Trading Co. Ltd  (448,690,271.90)
  16. IPS Roofing Co. Ltd  (966,723,692.10)
  17. Tifo Global Trading Co Ltd (1,573,300,644.58)
  18.  Lotai Steel Tanzania Ltd (5,476,475,738.19)
  19. Tuff Tyres General Co Ltd (7,435,254,537.03)
  20.  Swalehe Mohamed Swalehe (34,687,165.00)
  21.  Rushwheel Tyre General Co Ltd, (1,802,988,679.20)
  22.  Said Ahmad Hamdan  (68,362,558.31)
  23. Ahmed Saleh Tawred  (59,237,578.40)
  24.  Farida Abdullah Salem (75,334,871. 85).
Kevela alisema wadaiwa hao wanapaswa kulipa madeni yao ndani ya siku 14 walizopewa na kwamba iwapo watashindwa kutekeleza amri hiyo, kampuni hiyo itaanza kazi ya kukamata mali zao na kuwafilisi.

Alisema ili kurahisisha kazi hiyo, Kampuni ya Said Salum Bakhresa (SSB) ambayo ndiyo mmiliki wa Bandari Kavu ya Azam pamoja na Kampuni ya Regional Cargo Services wanapaswa kutoa ushirikiano kuhakikisha wadaiwa hao wanalipa kodi walizokwepa.

“Kampuni hizo zinahusishwa na kutoroshwa kwa kontena 329 zilizokuwa Azam ICD, sasa ni vyema watoe ushirikiano ili wadaiwa walipe fedha za serikali,” alifafanua Kevela. 
Alisema baada ya muda waliotoa kumalizika, wahusika watapaswa kulipa na gharama za ziada ambazo ni pamoja na faini na usumbufu wa kuwatafuta.

Desemba 12, mwaka jana, aliyekuwa Kaimu Kamishna wa TRA, Dk Philip Mpango aliwaambia waandishi wa habari kuwa kampuni 15 kati ya 43 zilizokwepa kodi baada ya kutorosha kontena 329 katika ICD ya Azam, zimelipa.

Dk Mpango alisema Desemba 12, mwaka jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho aliyotoa Rais John Magufuli ya siku saba kwa wakwepa kodi hao 43 kulipa wenyewe kwa hiari, vinginevyo sheria zitachukua mkondo wake.
Kutokana na kauli hiyo ya Rais Magufuli, wadaiwa 15 walijitokeza na kulipa na waliobaki hawakujitokeza kulipa.
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger