INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
Siku tatu baada ya Rais John Magufuli kueleza kuwa yeye si kichaa, si
dikteta wala mnyama, Jaji Thomas Mihayo ameungana na mkuu huyo wa nchi
akisema hajauona udikteta wake.
Jaji Mihayo alikuwa akifafanua
kauli alizotoa Rais Magufuli kwenye kilele cha Siku ya Sheria, wakati
alipomuahidi Jaji Mkuu Othman Chande Sh12.3 bilioni za kuendeshea
shughuli za mahakama na kumtaka aharakishe kushughulikia kesi za ufisadi
ili Serikali iokoe Sh1 trilioni, ambazo kati ya hizo atatoa Sh250
bilioni kwa ajili ya Idara ya Mahakama.
Rais pia alitaka kesi
ambazo watuhumiwa wanakamatwa na ushahidi, zifikishwe mahakamani mara
moja na kuamuliwa, lakini akataka asichukuliwe kuwa ni dikteta kutokana
na maamuzi yake.
“Ninapochukua hatua mimi si mnyama, si dikteta,
si shetani. Ni mpole kweli, lakini inafika mahali lazima nifanye
(uamuzi). Yanayofanyika serikalini ni mambo ya ajabu sana, nataka kutoa
sadaka yangu, inawezekana hata nikifa naweza kuwa rais wa malaika,”
alisema.
Kauli hiyo imeibua mjadala miongoni mwa wanasheria
wanaodai Rais anaingilia uhuru wa mahakama kwa kutaka uamuzi wa kesi
hizo ufanywe kwa utashi wa Serikali, huku baadhi ya hatua kali
anazochukua zikielezewa kuwa zina harufu ya udikteta.
Lakini jana, mkuu
huyo wa nchi alipata mtetezi wakati Jaji Mihayo alipoongea na waandishi
kufafanua kauli hiyo ya Siku ya She ria, akisema Rais dikteta ni yule
asiyefuata misingi ya sheria.
“Wanaosema Magufuli ni dikteta
hawawajui madikteta. Hakuna kiongozi dikteta Afrika Mashariki isipokuwa
Idi Amini tu,” alisema jaji huyo mstaafu ambaye alisema ameamua kutoa
ufafanuzi huo baada ya kuona mjadala mkubwa kuhusu kauli hiyo ya Rais na
kupata baraka kutoka kwa Jaji Mkuu, Othuman Chande.
Jaji
Mihayo, ambaye ni mwenyekiti wa majaji wastaafu, alihoji inawezekanaje
kiongozi ambaye mataifa mengine wanatamani akaongoze nchi yao angalau
kwa miezi miwili, aonekane kuwa ni dikteta.
“Magufuli anafuata
sheria kwa sababu hajafanya jambo lolote ambalo linamfanya awe juu ya
sheria. Sijawahi kusikia kasema mfunge huyu au kusema sheria hii
isitumike na hii itumike” alisema.
Alisema ni kawaida kwa viongozi wanaokemea uovu kuonekana kama madikteta kwa sababu wanataka kuondoa rushwa.
Kadhalika,
Jaji Mihayo alisema anaupenda utendaji kazi wa Magufuli ili wanaokiuka
sheria wawajibishwe na walalahoi wapate haki yao.
Magufuli na
Mahakama
Kuhusu ahadi yake ya kuipa Idara ya Mahakama Sh12.3 bilioni ili
izitumie kwenye shughuli zake na agizo la kuharakisha uamuzi wa kesi
442 ili Serikali iokoe Sh1 trilioni, Jaji Mihayo alisema kitendo hicho
hakiingilii uhuru wa mahakama bali ni katika kuhakikisha kesi
zinamalizwa kwa wakati na serikali inakusanya mapato ya kutosha.
“Maneno
ya Rais ya kuwataka majaji wamalize kesi kwa haraka na kuwaahidi kiasi
kile cha fedha, si kuwahonga bali ni motisha na mbinu ya kukusanya
mapato,” alisema.
Alisema kauli ya Rais isitafisriwe kuwa ni
lazima Serikali ishinde kesi dhidi ya rufaa ya kodi, bali alitaka majaji
wafanye kazi zao kwa wepesi zaidi.
Akifafanua kesi za rufaa za
kodi, Jaji Mihayo alisema mashauri hayo yatakusanya fedha nyingi kwa
hata kama wanaodaiwa watashinda, kisheria ni lazima watoe theluthi ya
kodi wanayodaiwa.
Jaji Mihayo pia alisema maneno ya Magufuli
yasichukuliwe kuwa yatawavuruga majaji kwa sababu wanafanya kazi yao kwa
kufuata kanuni na sheria.
“Uhuru
wa mahakama upo ‘guaranteed (umehakikishwa)’ na katika kifungu namba
107 (a) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.Hata kama Rais akiamrisha
vipi, kama ni kitu ambacho ni kinyume na utaratibu, hakiwezi
kutekelezwa” alisema.
Kuhusu
Magufuli kuwachukulia hatua majaji na mahakimu 502 ambao hawajafikia
malengo ya kumaliza kati ya kesi 250 na 260 kwa mwaka, Jaji Mihayo
alisema JPM alionyesha kukerwa na ucheleweshaji wa kesi na wala si
kuingilia uhuru wa mahakama.
Alisema hata Jaji Mkuu Othman
Chande alishachukua hatua kwa kuwataka mahakimu hao watoe maelezo kabla
sheria haijachukua mkondo wake.
“Tatizo la ucheleweshaji wa kesi ni kubwa, si dogo kama unavyofikiria ndiyo maana linamkera JPM,” alisema.
Utendaji
wa mawaziri, wakuu wa mikoa
Kadhalika Jaji Mihayo pia alizungumzia pia
jinsi mawaziri wa JPM wanavyotoa kauli za kuwafukuza kazi au
kuwasimamisha watendaji wa Serikali, akisema siasa inatawala kuliko
sheria.
Alisema kisheria kiongozi wa Serikali hawezi kusimamishwa kazi au kufukuzwa bila maandishi.
“Watendaji hawatachukuliwa hatua bila kauli ya waziri kuwa katika maandishi, hilo jambo halichukuliwi kijumla tu,” alisema.
Alisema Katibu Mkuu Kiongozi akimsimamisha au kumfukuza mtu kazi, hilo linakuwa limeshafanyiwa kazi kwa kina.
“Vinginevyo,
huwezi kumfukuza mtu kazi bila mchakato na uchunguzi wa kuhakiki kama
ni kweli ana haki ya kusimamishwa au kufukuzwa,” alisema.