Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imeagiza hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya maafisa rasilimali watu wanaochelewesha watumishi wa umma kupanda madaraja licha ya kukidhi vigezo vinavyotakiwa, huku ikisisitiza uwajibikaji na haki katika usimamizi wa rasilimali watu serikalini.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Profesa Riziki Shemdoe, alisema baadhi ya watumishi wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa kufuatilia stahiki zao licha ya kutimiza masharti yote ya kupandishwa madaraja.
Amesema ni muhimu kwa maafisa rasilimali watu kutekeleza majukumu yao kwa wakati ili kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima na kuongeza motisha kwa watumishi wa umma.
"Jaribuni kuvaa viatu vya watumishi hawa,Wapo wanaotoka maeneo ya mbali na kutumia muda na fedha nyingi kufuatilia stahiki zao hapa Dodoma ilhali wamekidhi masharti yote yanayotakiwa," amesema Prof. Shemdoe.
Kutokana na hali hiyo,ameagiza kufanyika tathmini maalumu ya maafisa rasilimali watu waliosababisha ucheleweshaji wa madaraja katika mwaka wa fedha 2025/2026 ili hatua stahiki zichukuliwe.
Katika hatua nyingine,ameeleza kufurahishwa na mafanikio ya vijana wenye ulemavu wanaopata mafunzo ya ufundi stadi na kuibua vipaji vinavyoweza kuchangia maendeleo ya taifa.
Miongoni mwa waliovutia ni kijana Joseph ambaye ameonesha uwezo mkubwa katika usanifu wa majengo kwa kutumia mifumo ya kompyuta, jambo lililopelekea kuagizwa kutafutiwa ufadhili wa masomo pamoja na kuanza mchakato wa kupatiwa ajira ya kudumu serikalini.
Aidha, Serikali imeagiza kufanyika sensa ya mifumo yote ya TEHAMA inayotumika katika taasisi za umma ili kubaini kiwango cha matumizi yake na kuhakikisha mifumo hiyo inaunganishwa kwa lengo la kuongeza ufanisi, kupunguza urudufu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha utawala bora, matumizi ya teknolojia na utoaji wa huduma bora kwa wananchi kupitia taasisi za umma.



0 comments:
Post a Comment