WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia na kuwezesha miradi zaidi ya madini nchini.Mavunde ameyasema hayo baada ya kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Marvel Gold ya Australia, Timothy Strong, ambaye alifika kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa uchimbaji wa dhahabu unaotarajiwa kuanzishwa katika Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara.
Amesema Serikali imefurahishwa na kasi ya utekelezaji wa hatua za awali za mradi huo, ambao kwa sasa upo katika hatua ya uchorongaji baada ya kukamilisha utafiti wa awali kwa kutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani (drones).
“Tunapongeza wawekezaji kwa kasi wanayoionesha katika kuendeleza mradi huu muhimu. Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha sekta ya madini inachangia kikamilifu katika uchumi wa taifa,” amesema Mavunde.
Kwa upande wake, Strong amesema kampuni hiyo imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa mazingira rafiki ya uwekezaji, akibainisha kuwa hatua ya awali ya uchorongaji inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Julai 2026.
Amesema lengo la kampuni ni kuanza uzalishaji wa madini mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kiufundi na kisheria.
Mradi huo unatarajiwa kutoa ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Hanang na Mkoa wa Manyara kwa ujumla.



0 comments:
Post a Comment