Na Jackline Minja, Mtwara
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Maryprisca Mahundi, amezindua rasmi Mfuko wa Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika Jimbo la Mtwara Mjini (UWEZO Program) na kusema Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za uwezeshaji wa wanawake.
Akizungumza katika hafla hiyo Juni 30, 2026, Naibu Waziri Mahundi amesema Serikali inaamini kuwa maendeleo ya Taifa hayawezi kupatikana bila kuyawezeaha makundi maalum wakiwemo wanawake na vijana.
Amesema ushiriki wa makundi maalum katika shughuli za kiuchumi ni hatua ya kujivunia na kuongeza kuwa mafanikio yatapatikana kwa makundi hayo kupatiwa mafunzo stahiki.
"Serikali inaamini kuwa maendeleo ya Taifa hayawezi kupatikana bila wananchi wake kuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na hii ndiyo sababu kuwndelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake na vijana kupata fursa za kiuchumi kupitia sera na programu mbalimbali," alisema Naibu Waziri Mahundi.
Aidha, ameeleza kuvutiwa kwake na Programu ya UWEZO kwa kuanza kutoa mikopo na kuwajengea wanawake uwezo kupitia mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu za biashara na uundaji wa vikundi, akieleza kuwa msingi huo utasaidia kuhakikisha mikopo inazalisha matokeo chanya na kuongeza maendeleo ya wanawake pamoja na familia zao.
Awali akitoa maelezo kuhusu Programu ya UWEZO, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesema wazo la kuanzisha mfuko huo limetokana na ahadi aliyoitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Amesema kupitia mfuko huo wenye mtaji wa shilingi milioni 150, wanawake zaidi ya 5,000 walitambuliwa kutoka kata zote 18 za jimbo hilo, wanawake 300 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na wanawake 81 wamekabidhiwa mikopo katika awamu ya kwanza.
"Mikopo hiii haina riba kutokana na ushirikiano kati ya Joel Nanauka Foundation na Benki ya Ushirika (Coop Bank), sababu lengo la programu hii si kutoa fedha pekee bali kujenga wanawake wajasiriamali wenye uwezo wa kujitegemea, kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mtwara Mjini na Taifa kwa ujumla". alisema
Nao baadhi ya wanufaika wa Mkopo huo wameipongeza Serikali na kumpongeza Waziri Nanauka kwa maono na kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni zake ambapo kwa sasa wataweza kujiendesha kiuchumi na kupunguza makali ya ugumu wa maisha na kuingizia taifa mapato.




0 comments:
Post a Comment