
Kila baada ya miaka mitano taifa letu hufanya uchaguzi wa kupata viongozi katika ngazi mbalimbali, ikiwemo wenyeviti wa vijiji na vitongoji, madiwani, wabunge na nafasi ya Rais wa nchi. Hivyo, kila chama cha siasa kina utaratibu wa kuwapata wawakilishi watakaopeperusha bendera ya chama husika.
CCM kama chama cha siasa kina utaratibu wa kufanya kura za maoni kwa watia nia wote. Hiki ni kipimo kimojawapo kinachowezesha na kurahisisha maamuzi ya vikao vya uteuzi wa mwisho ambao hufanywa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
MUUNDO WA CHAMA CHA MAPINDUZI
CCM mfumo wake wa kitaasisi umeanzia ngazi ya Shina hadi Taifa, na kila eneo la kiuongozi lina mamlaka sawia kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977.
SHINA ➜ TAWI ➜ KATA/WADI ➜ WILAYA ➜ MKOA ➜ TAIFA
MFUMO WA UONGOZI
Kila eneo lina mfumo wa uongozi ambao huchaguliwa kila baada ya miaka mitano na hili lina dhihirisha kuwa CCM ni chama cha siasa kinachoishi falsafa ya demokrasia ya kijamaa.
UONGOZI
➤ Mwenyekiti
➤ Katibu
➤ Katibu Mwenezi
➤ Wajumbe
Huu mfumo wa uongozi unaoanzia ngazi ya Tawi mpaka Taifa una mamlaka na majukumu yaliyoainishwa kwenye Katiba na Kanuni za CCM, ikiwemo Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM.
HAKI ZA MWANACHAMA WA CCM
✓ Haki ya kuomba kuchaguliwa.
✓ Haki ya kuhudhuria na kutoa maoni.
✓ Haki ya kujitetea au kutoa maoni mbele ya kikao.
✓ Haki ya kumuona kiongozi kwa kufuata utaratibu.
SIFA ZA MWANA CCM
➤ Mtu anayeheshimu watu.
➤ Mtu anayependa kushirikiana na watu.
➤ Mtu mwenye kuamini kuwa kazi ni kipimo cha utu.
➤ Atalipa ada ya uanachama na kutoa michango.
➤ Mtu mwenye kujielimisha na kutumia elimu hiyo kwa manufaa ya umma.
➤ Mtu mwenye kuridhika na asiye penda vyeo na kujirimbikizia mali.
MAMLAKA YA VIKAO VYA MAAMUZI VYA CCM
Mfumo wa kihierakia wa kimamlaka unaofuatwa na CCM katika kufanya maamuzi ni kama ifuatavyo:
TAWI
Mkutano Mkuu wa Tawi ndiyo kikao chenye mamlaka ya juu katika shughuli za chama katika ngazi ya Tawi. Mfano, humchagua Mwenyekiti wa Tawi. Vikao vingine ni Kamati ya Siasa ya Tawi na Halmashauri Kuu ya Tawi.
KATA/WADI
Mkutano Mkuu wa Kata ndiyo kikao chenye mamlaka ya juu katika shughuli za siasa katika ngazi ya Kata, ikiwemo kumchagua Mwenyekiti wa CCM Kata.
WILAYA
Mkutano Mkuu wa Wilaya ndiyo kikao cha juu chenye mamlaka ya mwisho ya kimaamuzi, ikiwemo kumchagua Mwenyekiti wa CCM Wilaya.
MKOA
Ngazi ya Mkoa, Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa ndiyo kikao cha juu cha maamuzi katika Mkoa chenye mamlaka ya kumchagua Mwenyekiti wa CCM Mkoa.
TAIFA
Kitaifa, CCM kimuundo ndiyo mamlaka ya mwisho ya kimaamuzi yenye wajibu wa kusimamia na kutoa maamuzi ya mwisho kuhusu kila jambo katika ngazi za chini.
VIKAO VYA CCM TAIFA
✓ Kikao cha Sekretarieti
Kikao hiki kinaundwa na:
➤ Katibu Mkuu wa CCM Taifa.
➤ Katibu wa Itikadi, Siasa na Mafunzo Taifa.
➤ Makatibu wa Jumuiya zote za CCM.
➤ Wakuu wa Idara za CCM Makao Makuu.
Jukumu kuu la Sekretarieti ni kuandaa na kuchakata agenda na shughuli za kiutendaji za CCM.
KAMATI KUU YA CCM TAIFA (CC)
Hiki ni kikao kinachoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa chenye mamlaka ya kuchambua kwa kina agenda za CCM na kuziwasilisha katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
HALMASHAURI KUU YA CCM TAIFA (NEC)
Hiki ni kikao cha maamuzi kinachoundwa na wajumbe wa NEC.
Mamlaka ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa:
✓ Kuteua wagombea wa nafasi mbalimbali za chama na za dola ikiwemo wabunge, wenyeviti wa CCM wa mikoa na wilaya pamoja na viongozi wa jumuiya za CCM Taifa.
✓ Kusimamia itikadi na mwenendo wa CCM.
✓ Kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM.
✓ Kupendekeza kwa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa majina yasiyozidi matatu ya wanachama wanaogombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo, jukumu la mwisho la uteuzi wa wagombea wa ubunge, wenyeviti wa mikoa na wilaya ndani ya CCM kwa mujibu wa Katiba linafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
MKUTANO MKUU WA CCM TAIFA
Hiki ndicho kikao kikuu cha CCM kupita vyote chenye mamlaka na madaraka ya mwisho ya kimaamuzi ya CCM.
✓ Kupanga siasa ya CCM na kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za CCM.
✓ Kupokea taarifa na kufikiria taarifa ya kazi za CCM iliyotolewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na kutoa maelekezo ya mipango na utekelezaji wa siasa ya CCM.
✓ Kuandika Katiba au kuthibitisha mabadiliko ya vifungu vya Katiba ya CCM.
HUU NDIO MCHAKATO WA KURA ZA MAONI NDANI YA CCM
➤ Zoezi la kuchukua fomu, kuzijaza na kuzirejesha.
➤ Vikao vya Kamati za Siasa za Kata na Wilaya huketi na kupitia fomu zote na kutoa mapendekezo kwa vikao vya juu.
➤ Vikao vya Kamati za Siasa za Mkoa huketi na kupitia fomu zote pamoja na mapendekezo kutoka ngazi za chini.
➤ Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa hupendekeza majina ya watia nia wa nafasi ya Udiwani watakaopigiwa kura za maoni katika Kata.
➤ Kikao cha Kamati ya Siasa Mkoa hutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuhusu watia nia wa Ubunge.
➤ Sekretarieti ya CCM Taifa huchakata mapendekezo yote na kuyawasilisha Kamati Kuu na hatimaye Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
➤ Halmashauri Kuu ya CCM Taifa huteua majina matatu au zaidi yatakayopigiwa kura za maoni.
➤ Katibu wa NEC hutangaza majina ya walioteuliwa na kutoa maelekezo ya hatua zinazofuata.
BAADA YA KURA ZA MAONI
Ifahamike kuwa CCM hufuata kanuni na taratibu zote kwa mujibu wa miongozo na maadili yake katika kupata wagombea wa nafasi za dola.
VIKAO BAADA YA KURA ZA MAONI KWA NAFASI YA UDIWANI
➤ Kikao cha Kamati ya Siasa ya CCM Kata hutoa mapendekezo kwa kuzingatia matokeo ya kura za maoni.
➤ Kikao cha Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya hujadili sifa za kila mgombea na kutoa mapendekezo kwa Mkoa.
➤ Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa hupendekeza na kuteua jina moja miongoni mwa waliopigiwa kura za maoni.
VIKAO AWAMU YA PILI KWA NAFASI YA UBUNGE
➤ Kamati ya Siasa ya Wilaya hupitia na kutoa mapendekezo kwa kila aliyepigiwa kura za maoni.
➤ Kamati ya Siasa ya Mkoa hupitia na kuwasilisha mapendekezo kwa vikao vya Taifa.
➤ Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa huteua jina moja miongoni mwa waliopigiwa kura za maoni.
Kwa msingi huu, yeyote aliyepigiwa kura za maoni ana nafasi ya kuteuliwa bila kujali idadi ya kura alizopata.
KURA ZA MAONI NA UTEUZI WA WAGOMBEA NDANI YA CCM
Kwanini kura za maoni?
✓ Kushirikisha wanachama katika maamuzi ya chama.
✓ Kuishi falsafa ya demokrasia ya kijamaa ya CCM.
✓ Kutathmini ukubalifu wa mtia nia katika jimbo, kata au wadi.
✓ Kuongeza uelewa wa watia nia kuhusu matakwa ya wanachama na wananchi.
✓ Kuongeza uimara wa chama katika ngazi za mashinani.
✓ Kurahisisha vikao vya maamuzi kwa kuwa na taarifa sahihi za watia nia.
JE, KURA ZA MAONI NDIZO KIGEZO PEKEE?
Kwa ujumla, kuna vigezo vingine vinavyozingatiwa, ikiwemo:
➤ Idadi ya kura za maoni alizopata.
➤ Maadili ya mtia nia.
➤ Uzoefu wa siasa za chama na serikali.
➤ Ukubalifu wa mtia nia kwa jamii ya eneo husika.
➤ Mchango wa hiari katika kazi za chama.
HITIMISHO
Ni dhahiri kwamba CCM kwa hapa Tanzania ndiyo chama pekee cha siasa chenye utaratibu mpana wa kupata wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuwashirikisha wanachama wake.
Pia, kila mwana CCM ni muhimu akafahamu kuwa utaratibu wa uteuzi unaofanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa hautegemei kigezo kimoja cha idadi ya kura za maoni pekee, bali huzingatia taarifa na vigezo mbalimbali.
Itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea ndiyo nguzo muhimu katika kuijenga CCM.
Kila mwanachama ajitahidi kujielimisha kuhusu mfumo wa chama na namna unavyofanya kazi ili kuepusha sintofahamu zinazoweza kujitokeza baada ya kura za maoni.
Kura za maoni siyo uteuzi, bali ni mchakato wa kuelekea uteuzini. Uteuzi hufanywa na mamlaka na vikao vya kikanuni vya CCM katika kila ngazi.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA:
JOHN FRANCIS HAULE
MKUU WA SOKO LA SAMUNGE, JIJINI ARUSHA
SIMU: 0756717987 AU 0711993907
0 comments:
Post a Comment