Fundi Kiongozi anayekarabati kiwanda cha kuchambua pamba Sola kilichopo Wilayani Maswa Athuman Shabani (mwenye kofia) akiwaonyesha Viongozi wa chama kikuu cha ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU) wakiongozwa na Mwenyekiti wao ( Mwenye tisherti ya bluu) baadhi ya shughuli zinazofanyika kwenye ukarabati wa kiwanda hicho baada ya kutembelea.
Na Derick Milton, Simiyu.
CHAMA kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU), kimeanza kukarabati kiwanda cha kuchambua Pamba Sola kilichopo katika Wilaya ya Maswa, ambacho kimekaa zaidi ya miaka saba bila ya kufanya kazi.
Kiwanda hicho ambacho kilikuwa kinamilikiwa na Chama kikuu cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU) kabla ya kufanyika kwa mgawanyiko wa mali baada ya kuundwa kwa SIMCU, hakikufanya kazi kwa muda huo baada ya umiliki wa awali kushindwa kukiendesha.
Kiwanda cha Sola ni kati ya viwanda vitatu ambavyo SIMCU imevipata kama mgao baada ya kuundwa kwake kutoka vyama vikuu vya SHIRECU na NYANZA, ambapo viwanda hivyo ni pamoja na NASSA GINNERY pamoja na RUGURU GINNERY.
Wakiwa na waandishi wa habari viongozi wa SIMCU wametembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kujionea shughuli za ukarabati zinavyoendelea, ambapo wameridhishwa na kazi ya mhandisi aliyepewa kazi ya kukarabati.
Akitoa maelezo mbale ya viongozi hao, fundi kiongozi Athuman Shabani amesema kuwa tangu wameaza zoezi la ukarabati wamefikia asilimia 20 ambapo ndani ya siku 20 zijazo zoezi zima litakuwa limekamilika.
Amesema kuwa zoezi ambalo wameanza nalo ni kufungua mashine za kuchatakata pamba na sehemu za kupitisha umeme, ambapo asilimia kubwa ya vipuli vya mashine hizo bado imara.
“ Kuna vifaa vichache sana ambavyo tumekuta vimeharibika, lakini kwa kiwango kikubwa mashine bado nzima na zinafanya kazi, kwa kasi ambayo tumeanza nayo ndani ya siku 20 kiwanda kitaanza kufanya kazi,” amesema Shabani.
Mwenyekiti Kamati ya Uchumi SIMCU Simioni Magoma, amesema kuwa katika mikakati ya Chama chao, wamepanga kuhakikisha kiwanda hicho kinaanza kufanya kazi haraka iwezekanavyo hasa kuanza kuchakata pamba katika msimu wa mwaka huu.
Amesema kuwa zoezi la ukarabati linahusisha mashine za kuchambua pamba ikiwemo ukarabati wa maghala matatu ya kuanzia kwa ajili ya kutunza pamba, huku mkakati mkubwa ikiwa ni kukarabati kiwanda kizima.
“ Tunashukuru sana serikali ambayo imeendelea kutuunga mkono katika zoezi hili la kuanza kufufua viwanda vyetu, tumeanza na hii sola lakini tunao mpango wa kuanza kufufua viwanda vingine ambavyo SIMCU tunamiliki,” amesema Magoma.
Kwa upande wake Meneja wa SIMCU Shigela Magembe amesema kuwa Mhandisi Malando Zamu ndiye amepewa kazi ya ukarabati wa kiwanda hicho, kazi ambayo itatumia muda wa mwezi mmoja hadi kukamilika kwake.
Magembe ameeeleza kuwa SIMCU ilipata mkopo kutoka benki ya Kilimo (TADB) kiasi cha shilingi Bilioni 1.5 ambazo zinatumika kwa ajili ya ukarabati huo pamoja na kuanza ununuzi wa pamba katika msimu huu.
“ Katika mkopo ambao tumepewa na TADB fedha zake ndizo zimeanza kukarabati kiwanda hiki, lakini pia kati ya fedha hizo zitatumika kuanza kununua pamba msimu huu mara baaada ya ukarabati kukamilika,” amesema Magembe.
Mwenyekiti wa SIMCU Lazaro Walwa amesema kuwa hadi kufikia Julai 14, 2022 kiwanda hicho kitakuwa kimeanza kufanya kazi ya kuchambua pamba na kuuza marobota kwani ukarabati unaoendelea utakuwa umemalizika.
Amesema kuwa mara baada ya kiwanda hicho kukamilika ukarabati wake, zaidi ya watu 300 wataajiliwa wakiwemo vibarua na kitawezesha kuinua uchumi wa wakulima wa pamba ambao watalipwa malipo ya pili mara baada ya chama hicho kuuza marobota ya pamba.
“ Iwe mvua, liwe jua, mwezi Julai, 2022 lazima kiwanda kianze kufanya kazi, fedha zipo na kazi inaendelea kwa kasi, wananchi na wakulima wajiandae viwanda vyetu vinarudi kama zamani,” amesema Walwa.
Mafundi wakiendelea na Shughuli za ukarabati wa mashine katika kiwanda cha kuchambua pamba Sola kilichopo katika Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, kiwanda hicho ambacho kilikuwa kinamilikiwa na SHIRECU sasa kinamilikiwa na Chama kikuu cha Ushirika mkoa wa Simiyu (SIMCU).
0 comments:
Post a Comment