Nsekela amesema mwitikio huo wa wakimbiaji wa kimataifa unatokana na kuvutiwa na lengo la mbio hizo la kusaidia jamii pamoja na kusajiliwa kimataifa kwa mbio hizo na Chama cha Usajili na Upimaji wa Mbio za Kimataifa (AMIS) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Riadha (World Athletics).
“Mbio zetu sasa hivi zimeorodheshwa katika tovuti ya mbio za kimataifa ya AIMS. Huko ndipo wakimbiaji wengi wa kimataifa wamekuwa wakiziona na kuvutiwa na kujitoa kwetu kuhamasisha jamii kuchangia gharama za upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya moyo, ujenzi wa kituo cha mawasiliano katika hospitali ya Ocean Road na kuchangia katika utunzaji wa mazingira kupitia kampeni yetu ya Pendezesha Tanzania,” alisema Nsekela.
Akielezea maandalizi ya mbio hizo kuelekea Jumapili ya tarehe 15 Agosti 2021, Nsekela alisema maandalizi yamefikia hatua nzuri na kuahidi washiriki wote kupata uzoefu wa kimataifa. Alisema wataalamu wa usimamizi wa mbio za kimataifa kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Riadha wanatarajiwa kufika nchini mapema wiki ijayo kwa ajili ya maandalizi ya mwisho. Katika mkutano huo na Waandishi wa habari, Benki ya CRDB pia ilitambulisha vifaa vitakavyotumika mwaka huu ikiwamo medali, fulana, bib, mfuko wa kuwekea vifaa (back-pack).
Aidha Nsekela alitumia fursa hiyo kumtambulisha rasmi mgeni rasmi katika mbio hizo ambaye anategemewa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa. Aliongezea kuwa viongozi mbalimbali wanatarajiwa kushiriki mbio hizo ikiwamo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Mheshimiwa Tulia Ackson ambaye ataambatana na Waheshimiwa Wabunge, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa Serikali.
“Nitumie fursa hii kipekee kabisa kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi siku hiyo. Amenitumia salamu kuwa yeye muda huu uliobaki anajifua tutakutana naye hiyo Agosti 15,” alisema Nsekela. Aliongezea kuwa tayari Benki hiyo imeshapata muongozo wa jeshi la polisi juu ya kuhakikisha usalama siku hiyo, na kulishukuru jeshi hilo kwa ushirikiano mkubwa ambao wamewapatia.
Katika siku hizi chache zilizobaki, Nsekela amewataka Watanzania kuendelea kujisajili CRDB Bank Marathon kwani pamoja na kuwa mbio hizo sasa hivi ni za kimataifa lengo kubwa ni kukuza uzalendo miongoni mwa Watanzania kwa kuwaleta pamoja kutatua changamoto katika jamii. “Tungependa zaidi kuona Watanzania wakishiriki kwa wingi kwani hii ni marathon yetu na tungependa pia kuona zawadi hizi zikibaki nyumbani,” aliongezea.
Akiongea kwa niaba ya makampuni washirika wa CRDB Bank Maratho, Mkurugenzi wa Mkuu wa kampuni ya bima ya Sanlam, Julius Magabe alisema kampuni yao inajivunia kuwa washirika wa CRDB Bank Marathon kutokana na mbio hizo kujikita zaidi katika kuhamasisha watu kusaidia jamii. “Tunaishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizi zinazowaleta Watanzania kushiriki katika kutatua changamoto katika jamii. Sanlam ni kampuni ambayo inajali afya na mazingira ya watu wake hivyo tunakila sababu ya sisi kushiriki katika mbio hizi ikiwa ni sehemu yetu ya kusaidia jamii,” alisema Magabe huku akihamasisha Watanzania kushiriki kwa wingi siku hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt. Julius Mwaiselege aliishukuru Benki ya CRDB kwa kutambua changamoto ambazo taasisi yake pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete zinakumbanazo katika kutoa huduma bora za afya kwa Watanzania. Alisema ujenzi wa Kituo cha Mawasiliano cha Saratani kitasaidia sana katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kuhusu maradhi hayo na kupata matibabu kwa wakati. “Niwakaribishe Watanzania tuungane kwa pamoja kushiriki CRDB Bank Marathon na kuchangia ili tuweze kufikia lengo lililowekwa la kukusanya Shilingi 5oo,” alisisitiza Dkt. Mwaiselege.
Mbali na mashindano ya mbio siku hiyo pia kutakuwa na burudani za ngoma za asili kutoka mikoa mbalimbali, burudani kutoka wasanii maarufu wa ikiwamo Ben Pol, Mimi Marz, Dullah Makabila na MC Kinata, burudani kutoka wasanii wa kimataifa, pamoja na burudani ya vyakula na vinywaji. “Siku hiyo itakuwa ni siku ya kusambaza Tabasamu, leo tumetaja wasanii wanne tu lakini tuna orodha ya zaidi ya wasanii 23. Mbio hizi pia zitaonyweshwa mubashara kupitia TVE hivyo kutoa fursa ya kuitangaza nchi yetu na utamaduni wetu,” aliongezea Tully Mwambapa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB.
Kujisali na kuchangia katika CRDB Bank Marathon washiriki wanatakiwa kutembelea katika tovuti rasmi ya mbio hizo www.crdbbankmarathon.co.tz ambapo mtu binafsi anatakiwa kuchangia shilingi 30,000 na washiriki kupitia vikundi ni shilingi 25,000. Malipo yanaweza kufanyika kupitia matawi ya Benki ya CRDB, CRDB Wakala, SimBanking App, mitandao ya simu na kupitia kadi ambazo zinawawezesha hadi watu wa nje ya nchi kufanya malipo.QuoteReply
0 comments:
Post a Comment