Sunday, 29 August 2021

TAASISI YA IBRAHIM HAJJ, JUMUIYA KSIJ WACHANGIA DAMU DAR ES SALAAM

...

:Mtaalam wa Maabara kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Mashariki, Gisbert Ruseneka, akimtoa damu, mmoja wa waumini wa Juimuiya ya Khoja Shia Ithnasheri Jamaat (KSIJ), wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kiongozi wa dhehebu hilo Imamu Hussein, kwenye msikiti wa KSIJ jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa waumini wa Juimuiya ya Khoja Shia Ithnasheri Jamaat (KSIJ) akishiriki katika zoezi la uchangiaji damu wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kiongozi wa dhehebu hilo Imamu Hussein, kwenye msikiti wa KSIJ jijini Dar es Salaam.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi la uchangiaji damu lilioandaliwa na Jumuiya Khoja Shia kwa kushirikiana na Taasisi ya Ibrahim Hajj.

 ***
WANACHAMA wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithna-Asheri Jamaat (KSIJ) kwa kushirikiana na Taasisi ya Ibrahim Hajj, wamejitolea kuchangia damu kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Imamu Hussein.


Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, alihudhuria hafla hiyo ya uchangiaji damu, iliyofanyika Msikiti wa KSIJ katikati ya jiji, ambako aliwapongeza Wana Jumuiya hao kwa kudumisha utamaduni chanya wa kusaidia wenye uhitaji ikiwemo uchangiaji damu huo.


Meya Kumbilamoto alibainisha kuwa, KSIJ na Ibrahim Hajj, wameionesha jamii ya Watanzania namna wanavyopaswa kujitoa kwa ustawi wa maisha wenye uhitaji, na kwamba damu iliyochangwa na Wana Jumuiya hao, inaenda kuokoa maisha Wengi miongoni mwa wahanga wa ajali, wamama wajawazito na wagonjwa wa kansa ya damu.


Kumbilamoto aliwapongeza KSIJ na Ibrahim Hajj na kuzitaka taasisi zingine na jamii kuiga utamaduni chanya unaofanywa na wanachama hao, ambao unalenga sio tu kuakisi yalivyokuwa maisha ya kiongozi wao Imamu Hussein, bali kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wake.


"Nitoe wito kwa jamii, kuiga mfano wa KSIJ na Ibrahim Hajj, ambao wamekuwa wakijitolea damu kila mwaka. Awali walikuwa wakitoa mara moja kwa mwaka kila wanapokuwa na maadhimisho haya, lakini Sasa wamekuwa wakichangia damu kila wanapoombwa kufanya hivi.


"KSIJ na Ibrahim Hajj, wameenda mbali zaidi kwa Sasa kwa kujitosa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali, hasa zinazoikabili sekta ya Elimu na Afya nchini, walikotoa vifaa tiba, vifaa vya elimu na hata ujenzi na maboresho ya miundombinu kwenye Sekta hizo muhimu kwa maendeleo ya jamii," alisisitiza Meya Kumbilamoto.


Akizungumza kwa niaba ya KSIJ, Ain Sharrif, ambaye ni Mwanachama Mwandamizi Jumuiya hiyo, alisema utamuduni huo wa kuchangia damu wamekuwa wakiufanya kila (Mwezi Muharram) wanapoadhimisha kifo cha kiongozi wao Sayyidina Hussein (Imamu Hussein), aliyekufa kwa kujitoa mhanga yapata miaka 1400 iliyopita.


"Tumekuwa tukifanya hivi tangu mwaka 2008, lengo likiwa ni kuyaishi maisha ya Imamu Hussein, ambaye alisimama imara katika kujitolea kwa ustawi wa maisha ya aliowaongoza na jamii iliyomzunguka. Nasi tunafanya haya na mengineyo ili kufuata nyayo zake na kutii wosia zake.


"Leo tunavyo vituo vitatu vinavyochangia damu jijini Dar es Salaam, ambapo pia kupitia Hospitali ya Ibrahim Hajj tumekuwa tukisaidia mamia ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa kuwapatia misaada mbalimbali kulingana na mahitaji yao, sambamba na huduma za matibabu," alisema Sharrif.


Naye Mtaalamu wa Maabara ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Samuel Mluma, aliishukuru KSIJ na Taasisi ya Ibrahim Hajj kwa kuthamini na kuijali jamii ya wenye uhitaji na kujitolea kuchangia damu, ambayo mahitaji yake ni makubwa.


"Kila mwaka KSIJ na Ibrahim Hajj wamekuwa wakichangia zaidi ya Unit 400 za damu kupitia maombolezo yao haya ama tunapowahitaji.


"Mahitaji nchini ni makubwa, takribani chupa 250,000 kwa mwaka, kwahiyo tunapowapata watu na Taasisi za mfano wa Kama KSIJ na Ibrahim Hajj, tunakuwa na uhakika wa makusanyo ya kutosha kukidhi mahitaji," alisema Mluma
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger