Thursday, 15 April 2021

MAWAZIRI WAKETI KUWEKA MAMBO SAWA KUHUSU MAAGIZO YA RAIS YA ONLINE TV

...

Na Faraja Mpina, WMTH, Dodoma
***
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wamefanya kikao cha pamoja na Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu pamoja na wataalamu kujadili hoja mbalimbali zinazohusu utekelezaji wa majukumu ya Sekta ya Mawasiliano na Utangazaji nchini hasa wakiangazia suala la Online TV katika vipengele vya usajili, kanuni, sheria, miongozo pamoja na tozo.

Kikao hicho kimefanyika tarehe 14.04.2021 Jijini Dodoma kikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi kuhusu kufanya marekebisho ya kanuni na sheria zinazosimamia vyombo vya habari nchini hususani Televisheni Mtandao (Online TV).

Miongoni mwa maazimio yaliyoafikiwa na pande zote mbili ni pamoja na kuangaliwa upya muundo mzima wa uwajibikaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa Wizara zote mbili pasipo kuathiri utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo katika Sekta ya Mawasiliano na Utangazaji nchini.

Aidha, mawaziri hao walikubaliana kuzipitia upya kanuni, sheria na miongozo mbalimbali kuhusu Online TV ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo rafiki ya usajili na malipo kuangalia uwezekano wa kupunguza tozo na kufanya uchambuzi yakinifu wa nani anatakiwa kulipia kuendana na matumizi husika.

Katika hatua nyingine TCRA ilipewa maelekezo ya kuongeza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu usajili, kanuni, sheria na taratibu zote za Online TV ili ziwe wazi kwa wananchi na elimu hiyo iambatane na elimu ya matumizi sahihi ya mtandao kwa lengo la kuongeza uwazi na uwajibikaji wa pamoja.

Pamoja na mambo mengine mawaziri hao walipitia hoja mbalimbali zinazotakiwa kufanyiwa mapitio na maboresho ikiwa ni pamoja na chaneli za runinga zinazotakiwa kuonekana katika visimbuzi bila malipo (FTA), kanuni za maudhui na utoaji wa adhabu kwa vituo vya redio na runinga uwekewe ukomo kwa mujibu wa kanuni na adhabu ziwe zenye lengo la kulea na si vinginevyo.

Mawaziri hao kwa pamoja na watendaji wao wakuu wamejipanga kuhakikisha Sekta wanazozisimamia hasa katika maeneo ambayo yana muingiliano katika utendaji wao yanafanyiwa maboresho makubwa kuendana na hali halisi ya sasa ya kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano na kuhakikisha malalamiko ya wananchi yanafanyiwa kazi na wao kama watendaji wanazungumza lugha moja kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Tekbnolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na Naibu wake Dkt. Jim Yonazi, Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hasaan Abbas.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger