Na Faraja Mpina – WMTH, Dodoma
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewakutanisha wadau mbalimbali ambao ni wataalamu wa TEHAMA kutoka katika Wizara, taasisi za Serikali na sekta binafsi ili kujadili mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya TEHAMA kwa lengo la kupata maoni ya wadau hao na kuyafanyia kazi kabla ya kupeleka mapendekezo hayo katika Sektetarieti ya Baraza la Mawaziri.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika tarehe 16.03.2021 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa kuna uhitaji mkubwa wa kuwepo kwa Sheria ya TEHAMA nchini kutokana na kukua kwa kasi kwa teknolojia hiyo nchini yenye msukumo mkubwa kibiashara.
Amesema kuwa Serikali imewekeza katika kukuza matumizi ya TEHAMA nchini ili kuendana na mahitaji ya mapinduzi ya nne ya viwanda, hivyo ni muhimu kuwa na Sheria itakayohakikisha inatoa mwongozo wa matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA na wananchi waweze kushiriki ipasavyo kwenye uchumi wa kidijitali.
“Ili mambo yaende vizuri ni lazima tuwe na Sheria mahsusi ya TEHAMA itakayotoa mwongozo na kusaidia kusimamia na kutambua nani anafanya nini, wapi, muda gani na kwa utaratibu upi”, alizungumza Dkt. Chaula
Ameongeza kuwa Sheria hiyo itaweka utaratibu wa mifumo rafiki na madhubuti katika uendelezaji na usimamizi wa matumizi ya TEHAMA nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya taasisi za umma kwa maendeleo ya Taifa.
“Kupitia Sheria hii natamani tutoke na dawa ya kumfanya kila mtu awe mtiifu na mzalendo badala ya kuwatafuta wahalifu wa mitandaoni tutengeneze elimu jamii itakayowafanya watu wawe na matumizi sahihi badala ya kutumia mifumo ya TEHAMA badala ya kuitumia kuchafua taswira ya nchi na kudhalilisha wengine”, alizungumza Dkt. Chaula
Aidha, Dkt Chaula ametoa rai kwa wadau hao kupeleka mrejesho kwa taasisi wanazoziwakilisha na kama kuna kitu ambacho kimesahaulika kitumwe katika Wizara hiyo kwa maandishi ili kuondoa sintofahamu ya wadau mbalimbali kuja kusema hawakushirikishwa.
Dkt. Chaula ameongeza kuwa mchakato wa kutungwa kwa Sheria hiyo ni wa muda mrefu na tayari maoni ya watu wengi katika maeneo tofauti tofauti yamekusanywa na kufanyiwa kazi
Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria wa Wizara hiyo Lugano Rwetaka amesema kuwa Sheria ya TEHAMA ni jambo la msingi kwa sababu soko la TEHAMA linakuwa kwa kasi nchini na duniani pote na kuleta uhitaji wa kuwa na matumizi ya TEHAMA kwa mujibu wa Sheria.
Amesema kuwa kuna sheria mbalimbali zinazosaidia kukuza na kuleta ulinzi katika TEHAMA lakini bado kuna vitu vingi ambavyo havijaainishwa katika sheria hizo hivyo kuna umuhimu wa kuwa na Sheria maalumu ya kusimamia TEHAMA nchini ambayo itaenda kubuni mbinu mbalimbali za kuimarisha ulinzi katika mtandao
“Moja ya malengo ya Sheria hii ni kuhakikisha bidhaa za TEHAMA zinatengenezwa hapa hapa nchini kwa matumizi ya nchi lakini hata pia tuweze kuziuza katika nchi nyingine za nje ya Tanzania”, Alizungumza Rwetaka
Naye Dkt. Nkundwe Mwasaga Mhadhiri kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) amesema kuwa kuna umuhimu wa kuwa na Sheria ya TEHAMA ambayo itatengeneza mazingira ya kuweza kufanya tafiti, ubunifu na uwekezaji katika TEHAMA.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
0 comments:
Post a Comment