Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Machi 19, 2021 katika Ikuru ya Magogoni Mkoa wa Dar es Salaam. Ameapishwa leo baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kufariki Dunia Machi 17, 2021.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu amesema mazishi ya Dk John Magufuli yatafanyika Machi 25, 2021 Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Ametangaza siku ya mazishi muda mfupi baada kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania akichukua nafasi ya Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.
Akielezea ratiba nzima ya mazishi amesema Machi 20,2021 mwili utatolewa hospitali ya Lugalo na kupelekwa Kanisa la St. Peters kwa ibada na kisha kupelekwa uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kuagwa na viongozi.
Machi 21 mwili utaagwa na wakazi wa Dar es Salaam katika uwanja huo huo na baadaye utasafirishwa kuelekea Dodoma.
Machi 22 mwili utaagwa Dodoma kuanzia saa tatu asubuhi na siku hiyo itakuwa ya mapumziko.
Machi 23, 2021 mwili utaagwa Mwanza na kisha kusafirishwa kuelekea Chato ambako utaagwa siku ya Jumanne ya Machi 24, 2021.
“Machi 25 mazishi yatafanyika baada ya misa takatifu itakayofanyika katika kanisa katoliki Chato na siku hii itakuwa ya mapumziko,” amesema Samia.
0 comments:
Post a Comment