Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
**
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole amesema chama hicho kinajiandaa kufanya mkutano mkuu maalum ili kumpendekeza na kumthibitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, kufuatia kifo cha Dkt John Magufuli aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Taarifa hiyo imetolewa jana jijini Dar es salaam na Katibu wa Iitikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba.
Kuhusu ratiba kamili ya kuaga mwili wa Dkt Magufuli Kichama, Polepole amesema kwa kuwa Dkt Magufuli aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge watapata nafasi ya kutoa heshima za mwisho kabla ya Wananchi wa mkoa wa Dodoma na maeneo jirani kupata nafasi hiyo.
“Pale Dodoma zitafanyika shughuli mbili, Kamati Kuu imeielekeza Serikali kwa kutambua ya kwamba Ndugu John Magufuli aliwahi kuwa sehemu ya Bunge, Wabunge wake wapate nafasi kwa desturi ya kibunge ya kumuaga mpendwa wao na Mbunge mwenzao kwa mujibu wa Katiba”, amesema Polepole.
Amewaomba WanaCCM na Wakazi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi tarehe 23 mwezi huu, kuaga mwili wa Dkt Magufuli.
“Tunatoa rai tarehe 23, kwa wana CMM wote, Watanzania wote na wazanzibari wote kujitokeza kwa wingi pale Zanzibar na tufuatilie matangazo ya Serikali kujua pahala palipoandaliwa tukatoe heshima zetu za mwisho na kumuaga mpendwa wetu John Joseph Pombe Magufuli”-amesema Polepole.
Tarehe 24 mwezi huu WanaCCM wote na Wakazi wa Kanda ya Ziwa watapata nafasi ya kuaga mwili wa Dkt Magufuli, shughuli itakayofanyika mkoani Mwanza.
Tarehe 25 itakuwa ni nafasi kwa wakazi wa Geita watakaoaga wilayani Chato na tarehe 26 ni siku ya mazishi.
Polepole ametoa rai kwa WanaCCM kujitokeza kwa wingi kumuaga Dkt Magufuli na siku ya mazishi ya kiongozi huyo.
0 comments:
Post a Comment