Saturday, 15 August 2020

Waziri Hasunga atoa siku 5 Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kukamilisha malipo ya wakulima wa Korosho Kibiti na Mkuranga

...
Na Innocent Natai, Pwani
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ametoa siku Tano kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania(CPB), Viongozi wa Vyama vya Ushirika pamoja na Benki ya Kilimo, kuhakikisha wanakutana na wakulima wa Korosho Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani ambao fedha zao za mauzo ya Korosho hazijalipwa mpaka sasa ili kuwalipa haraka iwezekanavyo.

Amewataka kukagua taarifa zao na kuwalipa fedha zao mara moja kwani serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ilishatoa fedha zote kwa ajili ya kufanyika kwa malipo hayo, "Nasikitika kwanini mpaka sasa malipo hayajakamilika" Aliuliza Waziri Hasunga

Akizungumza mbele ya Wakulima na Maafisa ugani Waziri Hasunga amesema kuwa inasikitisha kuona bado kuna wakulima wanaidai serikali angali serikali kupitia kwa Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imekwisha kutoa fedha kwa ajili ya kuwalipa kwa muda mrefu kitendo kinachowafanya wakulima kuichukia serikali na kukata taama ya kufanya kilimo.

Amesema kuwa kumekuwa na kisingizio cha muda mrefu kuwa baadhi ya wakulima taarifa zao za kibenki zina makosa hivyo kusababisha kushindwa kufanyiwa malipo kwa njia ya kibenki jambo hili siwezi kukubaliana nalo.

“Nilitoa siku 14 kuhakikisha kuwa wakulima wa Korosho Wilaya ya Mkuranga wawe wamemaliza kulipwa fedha zao lakini mpaka sasa bado natoa siku tano Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania(CPB), viongozi wa Vyama vya Ushirika pamoja na Benki ya Kilimo kuhakikisha hili suala linamalizika” Alisema Hasunga

Aidha, Hasunga ametoa siku mbili kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania CPB kuhakikisha wanabandika majina ya Wakulima waliolipwa fedha zao za Korosho kuanzia Mwezi Januari 2020 kwenye mbao za matangazo ili kuwasaidia wakulima kutambua walikwisha kulipwa fedha zao na ambao bado ili pia serikali kuweza kubaini udanganyifu unaofanywa katika malipo.

Pia amesema serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga imewakamata na itaendelea kuwakamata viongozi wa vyama vya ushirika wanaofanya ubadhilifu wa mali za wanaushirika, pia na waliofanya ubadhilifu na wizi kwenye uuzaji wa Korosho msimu uliopita

Hivyo, Hasunga amewataka wakulima kuendelea  kuvumilia wakati  serikali ikiendelea kuwafuatilia na kuwakamata waliofanya wizi wa kuuza korosho za wakulima bila kufuata utaratibi na kuwalipa Wakulima hao.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga mbali na kutembelea, kusikiliza na kutatua kero za Wakulima wa Korosho Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani alifika pia kuzungumza na wakulima Wilayani Kibiti Mkoani hapo huku akiendelea kutoa maagizo ya kuhakikisha wakulima wa Korosho wanalipwa stahiki zao kwa wakati na waliofanya udanganyifu na kuuza korosho za wakulima kuchukuliwa hatua za Kisheria.

Mwisho


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger