Saturday, 29 August 2020

DK.JOHN MAGUFULI AAHIDI KUENDELEA KUIMARISHA SEKTA YA NISHATI YA UMEME

...
Na Said Mwishehe,Michuzi Tv-Dodoma

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28,2020 Dk.John Magufuli amesema katika miaka mitano ijayo iwapo Chama Cha Mapinduzi(CCM) kitapata ridhaa ya kushika dola wataendelea kuimarisha sekta ya nishati.

Akizungumza leo Agosti 28, mwaka2020 katika Uwanja wa Jamhuri wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM ,Dk.Magufuli amesema wataingiza megawati 5000 za nishati ya umeme katika gridi ya Taifa ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na umeme wa uhakika.

Dk.Magufuli amesema kumekuwepo na mkakati kabambe wa kuimarisha sekta ya nishati ya umeme na licha ya uwepo wa miradi mikubwa ya umeme iliyotekelezwa, kazi inayoendelea sasa ni ujenzi wa bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere.

Kwa upande wa sekta ya afya,Dk.Magufuli amesema kwa kipindi cha miaka mitano wamefanikiwa kujenga zahanati 1,198, Hospitali za Wilaya tisa, vituo vya afya 487, Hospitali za Mikoa 10, Hospitali za Rufaa katika kanda tatu huku pia watumishi wa sekta hiyo 14,479 wakiongezwa.

Amefafanua kwamba bajeti ya imeongezeka kutoka Sh.bilioni 31 hadi Sh.bilioni 270 na tumenunua magari mapya ya wagonjwa 117.Pia amesema wamepunguza safari za rufaa nje ya nchi kwa wagonjwa wa moyo, figo, ubongo na saratani.

“Katika kuimarisha sekta ya afya nchini tuliamua kusomesha madaktari bingwa katika fani mbalimbali ndani na nje ya nchi.Hivyo tunayo sababu ya kuomba miaka mitano mingine ili tuendelee na kazi ambayo tulianza miaka mitano iliyopita,” amesisitiza.

Kuhusu sekta ya madini, Dk.Magufuli amefafanua usimamizi mzuri uliopo umeiwezesha  sekta hiyo kukua kwa asilimia 17.7.”Mapato yatokanayo na madini yameongezeka kwa kiwango kikubwa kwani hapo awali yalikuwa Sh.bilioni 168 katika mwaka 2014 hadi mwaka 2015 na sasa yamefikia Sh.bilioni 528.

“Tumeendelea kuboresha sheria kwani sheria mpya ya madini inaeleza kwa kila mgodi ambao utaanzishwa nchini kwetu serikali itakuwa na hisa ya 16,”amesema Dk.Magufuli na kufafanua kutokana na usimamizi mzuri Watanzania wamekuwa wakinufaika na madini yaliyoko katika nchi yao.

Ametumia nafasi hiyo kuzungumzia sekta ya elimu ambapo amegusia elimu bure ambayo inatolewa na Serikali na kufafanua kuwa Sh. Trilioni 1.09 zimetumika kusomesha watoto.

 Pia amesema katika kipindi cha miaka wamejenga shule mpya za msingi 905,  sekondari 228,wamekarabati shule kongwe 73, mabweni 253 na wameongeza madawati na  walimu sambamba na kuangalia maslahi yao.

Ametumia nafasi hiyo kuwaambia Watanzania kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu, wagombea wengi watapita kwa wananchi kunadi sera zao , kikubwa ni kuwasikilisa na kisha kufanya uamuzi sahihi Oktoba 28 mwaka huu ambayo ndio siku ya kupiga kura.

“Niwaombe tu wasikilizeni wagombea wote wataokuja kwenu na baada ya hapo mfanye uamuzi sahihi kwa kuchagua viongozi ambao wataleta maendeleo ya nchi yetu.CCM tunayo sababu ya kupewa dhamana ya kuongoza nchi kwasababu nia yetu ni kuendelea kuleta maendeleo.”


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger