Monday, 17 August 2020

TAHARUKI YAIBUKA KAHAMA MJINI HARUSI KUAHIRISHWA HUKU WAALIKWA WAKIMININIKA UKUMBINI...MHASIBU, MAHARUSI WASEPA!!

...


 Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Ama Kweli! Ukistaajabu ya Musa uyataona ya Firauni. Katika hali  isiyotarajiwa wageni waalikuwa zaidi ya 150 katika Sherehe ya harusi ya Ephrahim Jonasi na Bisunga Nyabusani ambaye ni mtumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamepigwa na butwaa baada ya kuingia ukumbini usiku na kukuta hakuna wenyeji wao ambao ni (Maharusi) licha ya kuchangia fedha na kupewa kadi za Mwaliko.

Malunde  1 Blog ilifika katika ukumbi wa Niteshi uliopo Mjini Kahama Majira ya saa 2:00 usiku  A gosti 16,2020  ili kujua kwa undani wa tukio hilo baada ya kupata taarifa za sherehe hiyo kuahirihwa kimya kimya na kuzua taharuki kwa wageni waliochangia michango ya harusi hiyo.

Mmoja ya wageni waalikwa,Marco Jakson aliyefika katika ukumbi huo saa moja kamili usiku alisema kuwa yeye hakuwa na taarifa zozote za kuahirishwa kwa sherehe ya harusi hiyo kwani jana yake alipewa kadi ya mwaliko na waandaji ikimtaka kufika katika Ukumbi wa Niteshi kuanzia saa 12:00.

“Nimekaa hapa kwa muda wa masaa matatu lakini naona watu wanakuja na kuondoka hapa ukumbini ukiwauliza wanasema sherehe imeahirishwa sasa kama imeahirishwa viongozi wa sherehe hii wako wapi na kwanini wasije ukumbini kuwaomba watu radhi na kutuambia kunashida gani,”alisema Jackson akizungumza na Malunde 1 blog.

Alisema kitendo kilichofanywa na kamati ya harusi hiyo siyo cha kiungwana kwani watu wamechanga fedha zao na kisha kupatiwa kadi za mwaliko lakini sherehe ya harusi inaahirishwa kimya kimya bila taarifa rasmi huku watu wakiwa wameshafika ukumbini.

Zephania Kisandu ni mgeni mwalikwa katika sherehe hiyo alisema kuwa kitendo kilichofanywa na maharusi hao sio cha kiungwana na wanapaswa kurejesha michango ya fedha za watu waliowachangisha ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa na tija kutokana na kuwasababishia usumbufu usiokuwa na tija.

“Haiwezekani mimi nichangie 50,000/=,nifike ukumbini ndiyo nipate taarifa za sherehe kuahirishwa tena na waalikwa wenzangu,kwanini kamati ya harusi haijafika hapa ukumbini au maharusi wasije hapa ili tupate muafaka ninachotaka ni kupatiwa fedha zangu,”alisema Musa.

Mpishi mkuu katika harusi hiyo,Aziza Haji alisema kuwa mpaka saa 12 jioni alikuwa hajapewa taarifa yeyote rasimi ya kusitisha sherehe hiyo licha ya kupewa fedha za awali (advance) kwa ajili ya kuwapikia wageni waalikwa 150 ambao chakula chote kilikuwa tayari ukumbini tangu saa mmoja usiku.

“Nimeleta chakula tangu saa mmoja kamili usiku lakini Maharusi walionipa kazi na kamati yake hawaonekani ukumbini nilipika chakula cha watu 150 na hivi sasa ni saa sita usiku naanza kupata wasiwasi nani atakula chakula hiki na fedha ninazo wadai ntazipata wapi,”alisema Aziza.

Aliongeza kuwa anadai shilingi laki nane na hamsini kwa kamati ya harusi hiyo ambayo walimpa kazi ya kuaandaa chakula hicho na kuwaomba viongozi wa jeshi la Polisi waliofika katika ukumbi huo kuhakikisha usalama unakuwepo wanamsaidia ili apate haki zake.

Malunde 1 Blog ilizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya harusi hiyo Josephat Bukwimba aliyefika baada ya kupigiwa simu na Viongozi wa jeshi la Polisi waliofika katika ukumbi huo ili kuhakikisha usalama wa watu waliofika kwaajili ya sherehe hiyo unakuwepo.

Alisema Sherehe ya harusi hiyo ililazimika kuahirishwa kutokana na Mhasibu wa kamati hiyo ambaye alikuwa ni kaka wa bwana harusi kutokomea kusikojulikana na baadhi ya fedha,tangu juzi na tayari tumeshatoa taarifa Kituo cha Polisi Kahama ili kuendelea kumtafuta.

“Hatujui ndugu yetu kapatwa na nini simu yake ya mkononi haipatikani na baadhi ya fedha alikuwanazo tumetoa taarifa kwa watu kwa njia mbalimbali ikiwemo simu na ujumbe mfupi lakini kwa wale ambao hajapata taarifa tunamuomba radhi kwani hata sisi hatukupenda yatokee haya.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger