Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji na Mahakimu watakaosikiliza mashauri yatakayotokana na uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu kuandika hukumu hizo katika lugha nyepesi, inayoeleweka na inayoelimisha wananchi.
Akifungua mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Maafisa 282 wa Mahakama wakiwemo waheshimiwa Majaji leo jijini Dodoma, Jaji Mkuu pia amewataka Wasajili kujitayarisha kutoa muhtasari wa hukumu husika kwa lugha nyepesi kila hukumu inaposomwa baada ya shauri la uchaguzi kukamilika ili wananchi waweze kujifunza.
“Katika mafunzo haya, kutakuwa na muwezeshaji atakayewaongoza katika uandishi wa hukumu katika mashauri ya uchaguzi (Judgment Writing for Election Petitions and Related Cases), hivyo tumieni wakati huu kujifunza uandishi wa mihutasari yenye kubeba mafunzo kwa wananchi bila kutumia maneno ya kisheria na kiufundi”, alisema.
Alisema Mahakama, inatakiwa kutenda haki, hivyo mafunzo hayo ni sehemu ya matayarisho yatakayowezesha kutimiza wajibu huo wa kutoa haki katika masuala ya Uchaguzi.
Aliongeza kuwa Ibara ya 113 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inawakumbusha Majaji, Mahakimu na Wasajili kutojiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa wanayo haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara
Aliongeza kuwa Ibara ya 113 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inawakumbusha Majaji, Mahakimu na Wasajili kutojiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa wanayo haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara
ya 5 ya Katiba.
“Katazo hili linatambua wajibu wetu Majaji, Wasajili na Mahakimu ili Mahakama isionekane kupendelea au kukandamiza upande wowote unaoshindana katika siasa na katika uchaguzi mkuu, lengo likiwa ni kuwatayarisha Majaji na Mahakimu kusikiliza mashauri ya uchaguzi kwa weledi, kwa wakati na kwa uwazi na haki”, alisema Jaji Mkuu.
Amewataka Majaji na Mahakimu kuamua mashauri ya uchaguzi kwa uwazi, utulivu, kujiamini na kuamini kile wanachokifanya kwa mujibu wa sheria na utaratibu ili kuongeza imani ya wananchi kwa Jaji au Hakimu husika na kwa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.
Alisema nafasi ya Mahakama katika kuisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwapa watanzania Uchaguzi huru na wa haki, usio na vitendo vya jinai ni kwa Mahakama kutimiza wajibu wake wa kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi katika mashauri ya jinai yatakayojitokeza katika hatua mbali mbali za uchaguzi kwa haraka na kuacha Kuahirisha kusiko na lazima.
Jaji Mkuu alisema kufunguliwa kwa mashauri ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani isichukuliwe kuwa ni kuonyesha udhaifu bali mashauri hayo yachukuliwe kuwa ni nafasi kwa wananchi kuhakikishiwa kuwa uchaguzi uliomalizika ulikuwa huru na wa haki kama Katiba ya Tanzania inavyotaka.
Alifafanua kuwa Katiba inampa Mwananchi haki ya kupiga kura, kugombea nafasi ya uongozi na pia inampa haki ya kufungua shauri mahakamani.
“Haki ya kupiga kura na kupigiwa kura hazitakuwa maana endapo hazitaambatana na haki ya kufungua shauri la uchaguzi pale mgombea anapoamini kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki’, alisema.
“Haki ya kupiga kura na kupigiwa kura hazitakuwa maana endapo hazitaambatana na haki ya kufungua shauri la uchaguzi pale mgombea anapoamini kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki’, alisema.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yanalenga kuwajengea uwezo maafisa wa Mahakama na kuwaandaa kutoa haki kwenye mashauri ya Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Awamu ya kwanza ya mafunzo yaliyoanza leo katika ukumbi wa mikutano wa Takwimu-Dodoma yanawahusisha Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu, Wasajili na Naibu Wasajili, na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi.
Aidha, awamu ya pili itawajumuisha waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na yatafanyika Septemba 2-4, 2020 mkoani Morogoro. Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya nao watapatiwa mafunzo hayo baadaye katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto-Tanga.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu waliopo na wastaafu, Naibu wasajili, Mahakimu pamoja na wawezeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Kurekebisha Sheria ambao ni wadau muhumu katika masuala ya Uchaguzi.
0 comments:
Post a Comment