Wednesday, 12 February 2020

Taarifa Toka CCM Kuhusu Maamuzi ya Kikao cha Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa Iliyoketi Leo

...
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wana CCM na watanzania kwamba Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imeketi leo Jijini Dar es Salaam chini ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikao cha Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kimeketi pamoja na mambo mengine kimepokea taarifa zifuatazo; -

Maandalizi ya Mwelekeo wa Sera za CCM kwa Mwaka 2020 – 2030 na Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Kamati Kuu imepokea taarifa ya Maendeleo ya Uandishi wa Waraka huu muhimu wa Kisera na kujiridhisha na kazi nzuri ambayo imekwisha kufanyika mpaka ngazi ya Rasimu. Kamati Kuu pia imepitia zoezi la uandishi wa Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na kuagiza maoni ya wadau mbalimbali kujumuishwa na kuzingatia ratiba ya kukamilisha uandishi wake ili vikao vya Chama vifanye uamuzi na kupitisha.

Maombi ya Kujiunga na uanachama wa CCM kutoka kwa Ndg. Fredrick Tluway Sumaye

Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imepokea taarifa ya Maombi ya kujiunga na CCM kutoka kwa Ndg. Fredrick Tluway Sumaye Waziri Mkuu Mstaafu na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Chama na Serikali ambayo imekiletea Chama heshima kubwa na ukubalifu kwa umma wa wananchi, wanachama na viongozi wa vyama vingine vya siasa. Kikao kimempongeza Ndg. Sumaye kwa uamuzi wake, kimeelekeza utaratibu wa kujiunga rasmi katika Chama ufuatwe kwa mujibu wa Katiba ya CCM.

Taarifa ya Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu
Kamati Kuu imepokea Taarifa ya Awali kutoka kwa Kamati ya Usalama na Maadili juu ya Utekelezaji wa Azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) katika Kikao chake cha Mwezi Disemba 2019 Jijini Mwanza kuhusu kuwaita na kuwahoji wanachama watatu, Ndg. Yusuph Makamba, Ndg. Abdulrahman Kinana na Ndg. Benard Membe ambao wote wameshafika mbele ya Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu inayoongozwa na Mzee Philip Mangula, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.

Kamati Kuu imetoa siku saba kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama hawa watatu na kuiwasilisha katika Vikao husika.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZ
Imetolewa na,

HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger