Serikali imewahakikishia Ushirikiano Wanunuzi Wakubwa wa Madini ya Tanzanite kutoka nchi za Marekani na Canada ambao Novemba 6, 2019, walihitimisha ziara ya siku tano nchini.
Ziara ya wanunuzi hao wakubwa ililenga kuona eneo ambalo madini hayo adhimu yanapozalishwa, kuona namna shughuli za uchimbaji zinavyofanyika, uzalishaji, uthamini, shughuli za uongezaji thamani madini hayo zinavyofanyika pamoja na masuala mengine yanayohusu madini ya tanzanite.
Akizungumza katika halfa fupi ya kuuaga ujumbe huo iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa KIA, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kuwa, ujumbe huo ndiyo wanunuzi wakubwa wa mwisho wa tanzanite yote duniani ambapo wananunua asilimia 75 hadi 80.
Ameongeza kwamba, wizara kwa upande wake imefurahishwa na ujio wa ujumbe huo kwa kuwa ni fursa ambayo itasaidia kutangaza madini ya tanzanite na mahali inapotoka na hivyo kuliwezesha taifa kupata wanunuzi zaidi wa tanzanite.
“Tumepata watu wakubwa na wameahidi kuendelea kuja, hii itatusaidia kupata wanunuzi wazuri wa tanzanite, watatusaidia kutangaza madini yetu”.
Aidha, Waziri Biteko amesema Tanzania ndiyo mahali salama pa kuwekeza katika sekta ya madini na hivyo wizara kwa upande wake, inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza nchini ikiwemo wanunuzi wa tanzanite.
Pia, amekipongeza Chama Cha Wafanyabishara wa Madini ya Vito (TAMIDA) kwa hatua hiyo ya kuwezesha wanunuzi hao kuja nchini na kueleza “TAMIDA mmethibitisha bila shaka mnaweza kufanya kazi na serikali’’.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMIDA Sam Mollel amesema kuwa ziara ya wanunuzi hao ililenga katika kuitangaza Tanzania kama nchi pekee inayozalisha madini ya tanzanite duniani, kuona eneo ambalo madini hayo yanapozalishwa, ikiwemo kuona namna shughuli za uchimbaji wa madini hayo unavyofanywa , uthamini unavyofanywa katika eneo la mirerani pamoja na udhibiti wa Tanzanite unaofanywa na serikali.
‘’ Tumepata watu watakao simama na sisi kutangaza madini ya tanzanite, suala ambalo litawezesha pia bei ya tanzanite kupanda. Hata wao wanataka yasipite kwingine yakishaongezwa thamani hapa yaende moja kwa moja kwao.’’amesema Mollel.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe huo, Ken Oschipok kutoka kampuni ya Diamond International amesema ni mara yake ya kwanza kufika Afrika na amevutiwa na mazingira yote kuhusu tanzanite, ukarimu wa watanzania na mazingira ya kibiashara na hivyo kuahidi kutumia fursa hiyo kutoa elimu kuhusu Madini hayo na uhalisia wake kwa watu wengine.
Mbali ya kutembelea migodi ya tanzanite Mirerani na kujionea shughuli za uzalishaji wa madini hayo, pia, ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko nchini.
Aidha, hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mhugwila, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Issa Nchasi na viongozi waandamizi wa Uwanja wa KIA.
0 comments:
Post a Comment