Thursday, 7 November 2019

Tanzania Na Malawi Wasaini Makubaliano Ya Kibiashara

...
Serikali ya Tanzania na Malawi zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa kuimarisha na kuongeza biashara, mahusiano ya kijamii na miundombinu hususani ya bandari, barabara na ndege.

Makubaliano hayo yamelenga pia kuingiza sheria mpya ili kufanya mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara baina ya mataifa hayo na kuyaingizia pato la Taifa.

Amesema hayo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe, mara baada ya kupitia makabalinao ya awali baina ya nchi hizo mbili yaliofanyika toka mwaka 1987 na kufafanua namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kufungua nchi yetu na nchi jirani kwa miundombinu bora.

“Nchi ya Tanzania na Malawi imekuwa ikishirikiana kwa muda mrefu katika masuala ya kijamii, na kiuchukuzi na hivyo makubaliano mapya yaliyosainiwa ni kuona namna bora zaidi ambavyo tutashirikiana hasa katika masuala ya kibiashara kwa kuzingatia miundombinu yetu” amefafanua Waziri Kamwelwe.

Akielezea uboreshaji wa miundombinu yetu nchini, Waziri Mhandisi Kamwelwe
ameeleza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Mpemba – Isongole yenye urefu wa (km 50.3) inayounganisha nchi yetu na mpaka wa Malawi kupitia Wilaya ya Chitipa hivyo ikikamilika itasaidia sana katika masuala ya usafirishaji wa bidhaa na mizigo.

Aidha, ameongeza kuwa katika mpaka wa Kasumulu ambao pia unaunganisha nchi hizo mbili, Serikali imeshaanza ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha (One Stop Border Post – OSBP) ambayo itasaidia katika kurahisisha biashara za Malawi na Tanzania.

Mhandisi Kamwelwe ameeleza uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam ikiwemo kuongeza kina cha maji na gati zake kuanzia Namba 1 hadi 7 ambazo zitaiwezesha bandari hiyo kuhudumia meli kubwa zenye uwezo wa kubeba makasha 5,000 kwa wakati mmoja.

Waziri Kamwelwe asema kuwa katika kujenga mahusiano mazuri kati ya nchi hizo, Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA), ilichukua hatua ya kutembelea nchi ya Malawi na kukutana na kuzungumza na wafanyabishara kwa lengo la kuainisha maeneo ya ushirikiano na kuboresha maisha ya Tanzania na Malawi.

Amefafanua kuwa sasa TPA ipo katika hatua za usimikaji wa(Flow Meter) za kisasa katika Bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ili kurahisisha upakuaji wa mafuta kutoka kwenye meli.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Malawi Mhe. Ralph Jooma,
amesema kuwa mkataba wa makubaliano waliosaini utatekelezwa kwa ufanisi na tija.

Pia Malawi itashirikiana vyema na Bandari ya Dar es Salaam kuwa bandari ya wafanyabishara na hivyo kusaidia kuongeza uchumi wa mataifa yote mawili.
 
Makubaliano ya kibishara kati ya nchi hizo yamefanywa kati ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Malawi Mhe. Ralph Jooma.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger