CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeanzisha utaratibu wa kuwasomesha
wanafunzi wasiojiweza kifedha, wakiwamo wanaoshindwa kulipia ada na
malazi baada ya wazazi au wategemezi wao kufariki dunia.
Hayo yalielezwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Rwekeza Mukandala
alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe ofisini kwake
chuoni hapo jana.
Prof. Mukandala (64), alisema kuna wakati mwanafunzi hujiunga na chuo
hicho na kujitegemea kwa ada na malazi, lakini katikati ya masomo wazazi
au walezi wake wakafariki dunia, hivyo kushindwa kumudu gharama za
elimu ya juu.
Kutokana na changamoto hiyo, alisema UDSM kupitia baraza lake la chuo
imekuwa na utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi hao wachache wanaopatwa na
majanga hayo.
"Kunakuwa na wanafunzi wanakuwa na shida sana, labda alikuja
anajitegemea, wazazi wake ghafla wanakufa, Chuo kupitia baraza lake
kimekuwa na utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi hao wachache wenye shida
kubwa ya kujikimu juu ya maisha," alisema Prof. Mukandala.
Alisema baraza hilo liliamua kwa mwanafunzi halali ambaye ameshadahiliwa
kila kitu na baadaye baadhi ya majanga yakamtokea katika maisha yake na
kumuathiri kimasomo, ili asiathirike zaidi kwa kushindwa kupata chakula
na huduma nyingine, chuo kitampa msaada.
"Haswa pale mwanafunzi anakuja analia, sijala, baba mama wamekufa,
wengine wanakuja hapa wazazi wao wamekufa kwenye ajali, wengine wamepata
matatizo mbalimbali," alisema na kufafanua zaidi:
"Huko nyuma tulikuwa na uwezo wa kuwasaidia kwa kutoa fedha zangu
mfukoni, lakini kwa sasa chuo kina utaratibu uliopitishwa na baraza kwa
kuwasaidia wanafunzi waliopata shida ambazo haziwezi kutafutiwa ufumbuzi
kwa haraka na kwa muda mfupi."
Alisema fedha wanazopewa wanafunzi hao na chuo kikuu hicho kikongwe
zaidi nchini ni msaada na hivyo hazirejeshwi na wahusika hawawekwi
kwenye orodha ya watu wanaopaswa kurejesha mikopo ya Bodi ya Wanafunzi
wa Elimu ya Juu (HESLB).
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na mtaalamu huyo wa sayansi ya siasa:
SWALI: Usumbufu katika kupata mikopo ndiyo tatizo namba moja la
wanafunzi wa elimu ya juu kwa sasa. Kwa uzoefu wako kama mkufunzi lakini
pia kama mtawala, ni vigezo gani vinaweza kuwa mwarobaini na
mkanganyiko uliopo?
Prof. Mukandala: Nchi nyingi duniani ikiwamo Tanzania zinatambua haja ya kutoa elimu kwa wananchi wake.
Serikali ya Tanzania kwa awamu mbalimbali imeliona hilo, kwamba baada ya
matatizo mbalimbali yaliyokuwa yanajitokeza ikaleta sera ya mikopo,
msingi wake ukiwa ni wanafunzi wapewe mkopo kisha watarejesha baadaye
wakishahitimu.
Baada ya kuanzisha sera hiyo, kulikuwa na changamoto nyingi mojawapo ni
wanafunzi waliokuwa wanahitaji mkopo kuwa wengi, huku fedha kuwagawia
wanafunzi ziakiwa ni kidogo
Hapo mwanzo wa sera hiyo kulikuwa na tatizo kubwa la mchakato wa namna ya kuwapata wanafunzi halisi wenye shida ya mkopo.
Walengwa ambao ni watoto wa maskini na wasio na wazazi ndiyo
walihitajika wapate mikopo. Hapo ndipo matatizo yakaanza, hapo ndipo
kulikuwa na mtafaruku na kutoelewana na uzembe.
Kwa serikali ya awamu ya tano hatua zimeshachuliwa za kuongeza pesa. Pia
serikali imeshapitia vigezo kuhakikisha wale walengwa ambao ni watoto
wa maskini na yatima wanapata mikopo.
Kitu ambacho wananchi wanapaswa kufahamu ni kwamba, serikali haisaidii
elimu kupitia utoaji wa mikopo tu. Kwa vyuo vya umma serikali
inagharamia pia kulipa mishahara yote ya watumishi, majengo makubwa yote
ya vyuo vikuu yanajengwa na serikali, aidha kupitia mikopo au pesa ya
moja kwa moja.
Kwa mwaka uliopita vijana wengi walipata mikopo kwa kozi zilizopewa
kipaumbele, hata zile ambazo hazikuwa katika kipaumbele wanafunzi wake
walipewa mikopo kwa asilimia mbalimbali.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) nayo imefanya
makusanyo kwa wadaiwa, hali itakayosaidia serikali kutoa zaidi mikopo
kwa wanafunzi wengine.
SWALI: UDSM ndiyo chuo kikuu namba moja kwa ubora wa elimu ya juu
nchini. Matatizo yanayozunguka elimu hiyo kwa sasa, ikiwamo usumbufu
katika upatikanaji wa mikopo, yanatishia nafasi hiyo kwa kiasi gani?
Prof. Mukandala: Masuala ya uwezo wa kulipia gharama za masomo kwa wanafunzi ni changamoto iliyopo dunia nzima.
Hata kampeni za urais Marekani zilizofanyika hivi karibuni walikuwa
wanazungumzia masuala ya namna ya kutoa elimu kwa watu binafsi na
taasisi za serikali.
Chuo ni lazima kiwe na mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo kwa
kushirikiana na wadau wote serikali na vyama vya wanafunzi. Serikali
wanatoa miongozo na vigezo, bodi ya mikopo wanatekeleza hilo.
Sisi kama uongozi wa chuo tunajaribu kufuatilia na kuhakikisha kwamba
huo utekelezaji unakwenda vizuri na hakuna mtu anayeonewa na kila mtu
anayestahili anapatiwa mkopo.
Kwa wanafunzi ambao wanajilipia wenyewe chuo kina utaratibu wa
kuwawezesha kulipa kidogo kidogo, lengo likiwa ni kuwawezesha kumaliza
masomo yao.
Imeandikwa na Gwamaka Alipipi na Sanula Athanas >>NIPASHE
0 comments:
Post a Comment